Chanjo inaweza kusaidia kuzuia ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Ushahidi umekuwa ukijikusanya kimya kimya kwa zaidi ya muongo mmoja. Sasa wataalamu wanaamini haupaswi tena kupuuzwa.

Mapambano dhidi ya ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu (dementia) ni miongoni mwa changamoto kubwa zaidi zinazoukabili ulimwengu wa afya. Hivi sasa zaidi ya watu milioni 55 duniani wanaishi na ugonjwa huo, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa kasi katika miongo ijayo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wazee.

Kufikia mwaka 2050, wataalamu wanatarajia zaidi ya watu milioni 140 watakuwa wanaishi na aina mbalimbali za ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu. Mbali na athari zake kwa wagonjwa na familia zao, gharama ya huduma na matibabu inatarajiwa kufikia kiwango kikubwa sana katika uchumi wa dunia.

Licha ya miongo ya utafiti, mafanikio katika matibabu yamekuwa madogo. Dawa nyingi zinazopatikana kwa sasa husaidia kupunguza baadhi ya dalili au kuchelewesha kupungua kwa uwezo wa kufikiri kwa muda mfupi, lakini haziwezi kuzuia au kusimamisha maendeleo ya ugonjwa.

Tatizo kubwa ni kwamba dalili zinapoanza kuonekana, mara nyingi tayari kunakuwa na uharibifu mkubwa wa ubongo ambao hauwezi kurekebishwa.

Hata hivyo, sasa kuna dalili kwamba jibu linaweza kuwa limekuwepo muda wote katika mahali ambapo hakuna aliyekuwa akitarajia kulipata: chanjo.

Jaribio ambalo halikukusudiwa

Mwaka 2013, serikali ya Wales ilianzisha mpango wa kitaifa wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa shingles (upele wa moto). Chanjo hiyo ilitolewa kwa watu waliokuwa na umri wa miaka 70 na zaidi.

Uamuzi huo haukulenga kabisa ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu. Lengo lilikuwa kupunguza madhara ya shingles, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya varicella-zoster, virusi vilevile vinavyosababisha tetekuwanga.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini namna mpango huo ulivyotekelezwa ndiyo iliyokuja kuwa muhimu.

Wale waliokuwa wametimiza miaka 70 kuanzia Septemba 1, 2013 walistahili kupata chanjo, huku waliokuwa wametimiza umri huo muda mfupi kabla ya tarehe hiyo wakikosa nafasi hiyo.

Kwa watafiti, hali hii iliunda kile kinachoitwa "jaribio la asili" (natural experiment). Makundi mawili ya watu yaliyokuwa karibu kufanana kwa kila hali yalijikuta yamegawanywa kwa msingi wa tarehe ya kuzaliwa pekee.

Profesa Pascal Geldsetzer, mtaalamu wa magonjwa kutoka Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani, anasema hali hiyo iliwapa watafiti fursa adimu ya kulinganisha afya za makundi mawili yanayofanana karibu kwa kila kitu.

"Ni sawa na kujaribu bahati," anasema.

Ikiwa watu elfu moja waliozaliwa wiki moja na watu elfu moja waliozaliwa wiki inayofuata wanaishi mazingira yanayofanana na wana tabia zinazofanana, basi tofauti yoyote kubwa inayojitokeza baadaye inaweza kuhusishwa kwa urahisi zaidi na chanjo.

.

Chanzo cha picha, Alamy

Matokeo yaliyowashangaza watafiti

Mwaka 2025, Geldsetzer na wenzake walichambua taarifa za afya za maelfu ya watu nchini Wales.

Waligundua jambo ambalo halikutarajiwa.

Watu waliokuwa wamepewa chanjo ya shingles walikuwa na uwezekano mdogo kwa takribani asilimia 20 wa kupata ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu ikilinganishwa na wale ambao hawakupokea chanjo hiyo.

Katika taaluma ya utafiti wa dementia, tofauti ya asilimia 20 inachukuliwa kuwa kubwa sana.

Athari hiyo ilionekana kuwa kubwa kuliko nyingi za hatua za mtindo wa maisha ambazo kwa muda mrefu zimehusishwa na kupunguza hatari ya ugonjwa huo.

Tafiti za ufuatiliaji zilionyesha pia kwamba chanjo hiyo inaweza kuwa na uwezo wa kupunguza kasi ya kuendelea kwa ugonjwa kwa baadhi ya watu ambao tayari walikuwa wameanza kupata dalili.

Iwapo matokeo haya yatathibitishwa zaidi katika tafiti zijazo, yanaweza kubadilisha kabisa namna wataalamu wanavyofikiria kuhusu kinga dhidi ya ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.

Uthibitisho kutoka nchi nyingine

.

Chanzo cha picha, National Institute on Aging, NIH

Katika sayansi, ugunduzi mmoja pekee hautoshi.

Hata hivyo, tangu matokeo ya Wales kuchapishwa, watafiti wameona mwelekeo unaofanana katika nchi nyingine kadhaa.

Taarifa kutoka Uingereza, Scotland, Canada na Australia zimeonyesha kwamba watu waliopata chanjo ya shingles wanaonekana kuwa na hatari ndogo zaidi ya kupata ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu baadaye maishani.

"Kinachofurahisha sana ni kwamba tunaendelea kuona matokeo haya katika seti tofauti za data," anasema Geldsetzer.

"Kila mara tunapoangalia taarifa kutoka eneo jingine, tunaona mwelekeo unaofanana."

Hali hiyo imeimarisha imani ya watafiti kwamba huenda kuna uhusiano wa kweli ambao unastahili kuchunguzwa zaidi.

Je, virusi vya herpes vina nafasi gani?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Ugunduzi huo umerejesha mjadala wa muda mrefu kuhusu uwezekano wa virusi kuwa na mchango katika ugonjwa wa Alzheimer.

Virusi vya herpes ni kundi la virusi vinavyojulikana kwa uwezo wake wa kubaki mwilini kwa muda mrefu baada ya maambukizi ya awali.

Kwa miaka kadhaa, tafiti zimekuwa zikionyesha kuwa watu waliopata maambukizi makubwa ya herpes wanaweza kuwa katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa Alzheimer.

Aidha, baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa wagonjwa waliotibiwa kwa dawa za kuzuia virusi walionekana kuwa na hatari ndogo ya kupata ugonjwa huo baadaye.

Halafu kulikuja ushahidi unaohusisha virusi vya herpes zoster, vinavyosababisha shingles.

Ingawa ushahidi haujathibitisha kwamba virusi hivyo ndiyo chanzo cha moja kwa moja cha ugonjwa wa Alzheimer, umeongeza hamasa ya kutafuta maelezo ya kina zaidi kuhusu uhusiano kati ya maambukizi, mfumo wa kinga na afya ya ubongo.

Siyo chanjo ya shingles pekee

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Jambo lingine lililowashangaza watafiti ni kwamba si chanjo ya shingles pekee iliyohusishwa na kupungua kwa hatari ya kupata dementia.

Mwaka 2019, watafiti waligundua kwamba chanjo ya BCG, inayotumika dhidi ya kifua kikuu, pia ilihusishwa na hatari ndogo ya kupata ugonjwa wa Alzheimer.

Kisha ikaja chanjo ya mafua

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Uchambuzi mkubwa wa mwaka 2023 uliounganisha matokeo ya tafiti kadhaa ulibaini kuwa watu wazee waliopata chanjo ya mafua walikuwa na uwezekano mdogo kwa takribani asilimia 31 wa kupata ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.

Baadhi ya tafiti zimeonyesha pia kwamba watu wanaochanjwa mafua mara kwa mara kila mwaka hupata ulinzi mkubwa zaidi.

Kwa maneno mengine, kadiri mtu anavyopokea chanjo hizo kwa muda mrefu, ndivyo faida inavyoonekana kuongezeka.

Kuna jambo la kipekee kuhusu chanjo

Mwaka 2022, David Lathe na wenzake kutoka Edinburgh waliamua kuchunguza jambo hili kwa mtazamo tofauti.

Walitathmini dawa 744 zinazotolewa kwa maelekezo ya daktari ili kuona kama kuna dawa ambazo zinaweza kupunguza hatari ya kupata dementia.

Matokeo yalikuwa ya kushangaza.

Ingawa dawa nyingi zilionyesha athari fulani, nyingi zilionekana kuongeza hatari.

Dawa nne pekee zilionyesha uwezo wa kupunguza hatari ya ugonjwa huo, na zote zilikuwa chanjo.

Ugunduzi huo ulizua swali muhimu: kwa nini chanjo zinaonekana kulinda ubongo dhidi ya ugonjwa ambao hazikulengwa kuuzuia?

Mfumo wa kinga unaweza kuwa ufunguo

Moja ya maelezo yanayojadiliwa sana ni kile kinachojulikana kama "kinga iliyofunzwa" (trained immunity).

Kwa mujibu wa nadharia hii, chanjo hazifundishi tu mwili kupambana na kimelea maalumu.

Badala yake, zinaweza kuboresha namna mfumo wa kinga unavyofanya kazi kwa ujumla wake kwa muda mrefu.

Lathe anasema chanjo huonekana kupunguza uvimbe sugu mwilini na kufanya seli za kinga kufanya kazi kwa ufanisi zaidi hata miaka baada ya mtu kuchanjwa.

Kwa mtazamo huo, chanjo zinaweza kusaidia kulinda ubongo kutokana na michakato ya uchochezi na uvimbe ambayo imekuwa ikihusishwa na maendeleo ya ugonjwa wa Alzheimer.

Je, tumekuwa tukielewa vibaya Alzheimer?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa miongo kadhaa, nadharia kuu imekuwa kwamba ugonjwa wa Alzheimer unasababishwa na mkusanyiko wa protini mbili muhimu: amyloid-beta na tau.

Protini za amyloid hujikusanya kati ya seli za ubongo na kutengeneza mabonge yanayojulikana kama plaques. Kwa upande mwingine, protini za tau hujikusanya ndani ya seli na kuvuruga mfumo wake wa kawaida wa kazi.

Kwa muda mrefu, protini hizi zimeonekana kuwa chanzo kikuu cha ugonjwa.

Lakini baadhi ya watafiti sasa wanaanza kuhoji iwapo protini hizo ni chanzo au ni matokeo ya tatizo jingine linalotokea mapema zaidi.

"Hakuna anayebisha umuhimu wa amyloid na tau katika ugonjwa wa Alzheimer," anasema Geldsetzer.

"Swali ni iwapo ndizo chanzo halisi cha ugonjwa huo."

Nadharia mpya inaeleza kwamba matatizo ya mfumo wa kinga, uvimbe wa muda mrefu au maambukizi yanaweza kuwa yanachochea ugonjwa mapema kabla ya protini hizo kujikusanya.

Iwapo nadharia hiyo ni sahihi, basi chanjo zinaweza kuwa zinazuia hatua za mwanzo kabisa za mchakato wa ugonjwa.