Vigogo watano wa CCM waliioondoka katika nyadhifa zao chini ya Rais Samia

Chanzo cha picha, CCM
Wanasiasa hustaafu, kujiuzulu au kuondoka madarakani kutokana na sababu mbalimbali za kibinafsi, kisiasa na kisheria. Baadhi hujiuzulu au kuachia ngazi ili kulinda umoja wa chama, kupisha damu mpya, au kupisha safu mpya ya uongozi inapotakiwa na Mkuu wa Nchi au chama.
Wengine huchagua kustaafu kwa hiari kutokana na umri mkubwa au changamoto za kiafya zinazowazuia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Migogoro ya maadili, tuhuma za rushwa, au matamshi yanayozua mjadala mkubwa na kukosa uungwaji mkono wa kijamii au kiserikali husababisha wanasiasa wengine kulazimika kuondoka katika nafasi zao.
Jambo jengine linalowaondoa wanasiasa katika nafasi zao ni kuamua kurejea kwenye maisha ya uraia, kilimo, au taaluma zao baada ya kutimiza malengo yao ya utumishi wa umma.
Tangu rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, kuna wanasiasa kadhaa cha Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao wameondoka kwa hiari au kwa shinikizo katika nafasi zao.
Emmanuel John Nchimbi

Chanzo cha picha, daily news
Dkt. Emmanuel John Nchimbi ni mwanasiasa mzoefu nchini Tanzania aliyepitia ngazi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikalini. Alianza kupata umaarufu mkubwa alipokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na baadaye kuhudumu kama Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini kwa vipindi kadhaa.
Alihudumu katika baraza la mawaziri chini ya Serikali ya Awamu ya Nne (Rais Jakaya Kikwete), akishika nyadhifa za Uwaziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mambo ya Ndani ya Nchi, na Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Baada ya kutumikia nafasi za kibalozi nchini Brazil na Misri, alirejea nchini na kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM mapema mwaka 2024.
Agosti 2025, aliteuliwa na kuapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Tarehe 25 Agosti 2026, Dkt. Nchimbi alitangaza rasmi kujiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais pamoja na kustaafu siasa na utumishi wa umma, uamuzi unaoanza kutumika rasmi tarehe 4 Septemba 2026.
Katika taarifa yake, alieleza kuwa alichukua hatua hiyo kutimiza ahadi aliyompa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiingia madarakani. kwamba angepisha bila kusita pale Rais atakapoona inafaa kuwa na mabadiliko katika safu yake ya uongozi. Alibainisha kujiridhisha kuwa Rais anahitaji mabadiliko hayo. Baada ya matukio hayo CCM imetangaza kumvua uwanachama.
Philip Mpango

Chanzo cha picha, ikulu
Dkt. Philip Isdor Mpango ni mchumi na mwanasiasa nchini Tanzania. Kabla ya kuingia kwenye siasa, alihudumu katika nafasi mbalimbali za kiserikali na kimataifa, ikiwemo Benki ya Dunia, Tume ya Mipango, na Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA.
Mwaka 2015, aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mbunge na baadaye Waziri wa Fedha na Mipango, nafasi aliyoitumikia kwa mafanikio hadi Machi 2021. Mnamo Machi 31, 2021, alichaguliwa na kuapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Mapema mwaka 2025, Dkt. Mpango alitangaza nia yake ya kustaafu utumishi wa umma na siasa mara baada ya kukamilisha muhula wake. Alieleza kuwa uamuzi huo ulilenga kutoa fursa kwa vijana kuongozana na Rais Samia, huku yeye akipanga kurejea kwenye shughuli za kilimo. Alihitimisha rasmi utumishi wake kama Makamu wa Rais mnamo Novemba 2025.
Job Ndugai

Chanzo cha picha, Tanzania Presidency/X
Job Yustino Ndugai ni mwanasiasa mzoefu nchini Tanzania aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma tangu mwaka 2000 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Safari yake ya uongozi wa Bunge ilianza rasmi mwaka 2010 alipochaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Spika Anne Makinda.
Mnamo Novemba 2015, alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kudumu katika nafasi hiyo kwa miaka sita, ambapo alirejeshwa tena madarakani kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Mnamo Januari 6, 2022, Ndugai alitangaza rasmi kujiuzulu nafasi ya Uspika. Uamuzi huo ulijiri siku chache baada ya kutokea kwa mkanganyiko na maneno ya ukosoaji aliyoyatoa hadharani kuhusu mikopo ya Serikali, jambo lililozua mjadala mkubwa wa kisiasa na kumfanya amwombe msamaha Rais Samia Suluhu Hassan kabla ya kuamua kuachia ngazi kwa hiari yake.
Tulia Ackson

Chanzo cha picha, tz
Dkt. Tulia Ackson ni mwanasheria na mwanasiasa nchini Tanzania. Alianza safari yake ya kisheria kama mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2015. Baadaye mwaka huo huo, aliteuliwa kuwa Mbunge na kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nafasi aliyoitumikia hadi mwaka 2022.
Mnamo Januari 2022, alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge kufuatia kujiuzulu kwa Job Ndugai. Katika kipindi chake cha uongozi, alipata pia heshima ya kimataifa kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Muungano wa Mabunge Duniani (IPU) mwaka 2023.
Mnamo Novemba 7, 2025, Dkt. Tulia alishangaza wengi kwa kutangaza kujiondoa katika kinyang'anyiro cha kutetea kiti cha Uspika kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alieleza kuwa uamuzi huo ulitokana na tafakari ya kina na lengo la kulinda umoja, mshikamano na amani ndani ya chama chake wakati kikitayarisha safu mpya ya uongozi.
Kassim Majaliwa

Chanzo cha picha, daily
Kassim Majaliwa Majaliwa ni mwanasiasa na mwalimu nchini Tanzania. Alianza safari yake ya uongozi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), akihudumu kama Mkuu wa Wilaya ya Rufiji na Kilwa kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ruangwa mwaka 2010. Baadaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI).
Mnamo Novemba 2015, Rais John Magufuli alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuendelea kushikilia nafasi hiyo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kurejeshwa tena madarakani mwaka 2020. Alikuwa mmoja wa Mawaziri Wakuu waliohudumu kwa muda mrefu zaidi nchini.
Baada ya kuwatumikia wananchi wa Ruangwa na taifa kwa zaidi ya miaka kumi na tano katika ngazi za juu, Majaliwa alitangaza rasmi kustaafu siasa na kutogombea tena Ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akilenga kupumzika na kupisha damu mpya katika uongozi wa umma.















