Gwiji wa muziki wa country Dolly Parton afariki dunia akiwa na miaka 80

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanamuziki mashuhuri wa muziki wa country, Dolly Parton, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80, familia yake imetangaza kupitia mitandao yake ya kijamii.
"Maumivu yako kwetu, si kwa Dolly," alisema mpwa wake, Brian Seaver, katika video iliyotangaza kifo chake.
Parton, aliyekulia katika Milima ya Smoky katika jimbo la Tennessee, atakumbukwa kwa nyimbo zake zilizokuwa zikisimulia hadithi za maisha, zikiwemo Coat of Many Colors, Jolene na I Will Always Love You.
Gwiji huyo wa muziki wa country aliuza zaidi ya rekodi milioni 100 duniani kote na aliandika zaidi ya nyimbo 3,000.
Parton aliuchukulia uandishi wa nyimbo kwa uzito mkubwa na alijitambulisha zaidi kama mtunzi wa nyimbo.
"Ni njia yangu ya kujieleza. Ni tiba yangu," aliwahi kusema.
Mbali na muziki, Parton alikuwa mfanyabiashara mahiri. Ucheshi na haiba yake vilimsaidia kudumu katika tasnia ya burudani kwa zaidi ya miaka 60.
"Dolly aliishi katika mwanga na sasa yuko mikononi mwa Yesu, bila shaka," alisema mpwa wake.
Dolly Parton alizaliwa mwaka 1946 katika familia maskini ya wakulima iliyokuwa ikiishi katika nyumba ndogo yenye chumba kimoja kando ya Mto Little Pigeon huko Tennessee.
Alikuwa wa nne kati ya watoto 12. Baba yake, Robert Lee Parton, alikuwa mkulima wa tumbaku na alilipa misionari kwa gunia la unga wa mahindi ili amsaidie kumleta duniani.
Parton alisema mama yake, Avie Lee, alikuwa akiimba nyimbo za jadi mara kwa mara. Pia alipewa msukumo na shangazi yake, aliyekuwa akipiga gitaa na kutunga nyimbo.
