Lifahamu Kombora la 'Kheibar Sheikan' linalotumika na Iran dhidi ya kambi za Marekani

.

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Usaid Siddiqui
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kheibar Shekan, kombora la Iran lenye masafa ya kati, linasemekana kuwa na nafasi muhimu katika kuchochea ongezeko la mvutano kati ya Marekani na Israel.

Kwa mujibu wa Al Jazeera, kombora la Iran la Kheibar Shekan{ Castle Breaker} , jina linalomaanisha "Mvunja Ngome" katika lugha ya Kiajemi, limeibuka kuwa mojawapo ya silaha zinazozungumziwa zaidi katika mzozo kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Kombora hilo la balistiki lenye masafa ya kati limetumiwa na Iran katika mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi na miundombinu ya Marekani Mashariki ya Kati wiki hii, huku Tehran ikilenga kuonyesha kuwa akiba yake ya makombora bado ni imara na ya kutosha licha ya mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa Marekani na Israel katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Vita hivyo viliingia katika awamu mpya wiki hii kufuatia kipindi cha utulivu wa mapigano kilichodumu kwa mwezi mmoja, pale vikosi vya Marekani viliposhambulia mifumo ya kurushia roketi kwenye Kisiwa cha Larak cha Iran katika Mlango bahari wa Hormuz,karibu na bandari muhimu ya kimkakati ya Bandar Abbas,siku ya Jumatatu. Hatua hiyo ilisababisha Iran kulipiza kisasi kwa kushambulia maeneo na vifaa vya kijeshi vya Marekani nchini Jordan.

Tangu wakati huo, Marekani imefanya mashambulizi zaidi dhidi ya maeneo mbalimbali ya Iran, huku Tehran nayo ikijibu mashambulizi hayo kwa kushambulia kambi kadhaa za Marekani katika eneo hilo, ikiwemo zile zilizopo Jordan na Falme za Kiarabu (UAE).

Basi, "Castle Breaker" ni nini, ina uwezo gani, na ni yapi ya hivi punde kuhusu vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran?

Je, kombora la Kheibar Shekan au "Vunja-Ngome" ni nini?

Hili ni kombora la balistiki la masafa ya kati lililotengenezwa na Kikosi cha jeshi la Iran (IRGC) kama sehemu ya safu yake pana ya makombora.

Ni mojawapo ya mifumo mipya ya makombora ya masafa ya kati ya Iran, yenye uwezo wa kufikia umbali wa takriban kilomita 1,450 (maili 901), na uwezo wa kubeba mzigo (mizani ya kichwa cha kombora) kati ya kilo 449 na kilo 590 (pauni 990 hadi 1,300).

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa kulinganisha, Marekani imezindua kombora la *Precision Strike Missiles* (PrSM) wakati wa mzozo huo, makombora ambayo mtengenezaji wake, Lockheed Martin, anayaelezea kuwa ni makombora ya masafa marefu yenye usahihi wa hali ya juu, yanayoweza kulenga shabaha zilizopo umbali wa kuanzia kilomita 60 (maili 37) hadi zaidi ya kilomita 499 (maili 310).

Marekani pia imetumia makombora ya kusafiri kwa meli ya Tomahawk, ambayo ni silaha za masafa marefu, zinazoongozwa kwa usahihi ambazo zinaweza kuruka katika miinuko ya chini na kulenga shabaha hadi kilomita 2,500 (maili 1,550).

Kombora la Kheibar Shekan lilizinduliwa mwaka wa 2022 na limepata jina lake kutoka Khaybar, neno linalomaanisha makazi yenye ngome yanayohusiana na historia ya awali ya Kiislamu. Shekan inamaanisha kivunja au mharibifu.

Moja ya sifa muhimu za kombora ni msukumo mkubwa wa kupaa kwa mafuta yake, ambao huruhusu kuzinduliwa ndani ya dakika chache wakati wa mgogoro. Makombora ya mafuta ya aina hii hujazwa mafuta mapema, kwa hivyo hayahitaji kuongezwa mafuta kabla tu ya kuzinduliwa,mchakato ambao unaweza kuchukua saa kadhaa. Hii inayafanya yawe rahisi na salama zaidi kuyaendesha, hayana uwezekano mkubwa wa kugunduliwa, na yanahitaji usaidizi mdogo wa vifaa kwa ajili ya usafirishaji wa mafuta.

Mafuta ni mazito na huchomwa haraka, na kutoa msukumo mfupi lakini wenye nguvu. Inaweza pia kuhifadhiwa kwa muda mrefu bila kuharibika au kuvunjika, tofauti na mafuta ya kioevu, ambayo yanaweza kuharibika zaidi.

.

Chanzo cha picha, Aljazeera

Iran imetumia wapi kombora lake la "Castle Breaker" (Kheibar Shekan)?

Iran imesema mara kwa mara kuwa imekuwa ikitumia makombora ya Kheibar Shekan dhidi ya ngome za kijeshi za Marekani katika eneo hilo tangu mgogoro wa miezi sita ulipoanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Tehran na maeneo mengine nchini Iran mnamo tarehe 28 Februari.

Shirika la utangazaji la serikali, IRIB, liliripoti kuwa vikosi vya Iran vilitumia kombora hilo katika mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya maeneo na rasilimali za Marekani nchini Jordan wiki hii.

Mnamo tarehe 20 Julai, Jeshi la Iran la (IRGC) lilitoa picha zinazoonyesha kombora la Kheibar Shekan likiwa pamoja na makombora ya balistiki ya aina ya Fateh-110, Zolfaghar, Emad na mengine yakitumika kushambulia shabaha za kijeshi za Marekani.

Siku nne kabla ya hapo, IRGC ilisema kuwa ilishambulia kituo cha kutengenez ndege za kivita za Marekani na kituo kipya cha amri na udhibiti huko Azraq, Jordan, kwa kutumia makombora ya Kheibar Shekan.

Je, Iran ina mifumo mingine gani ya makombora?

Iran ina mchanganyiko wa makombora yenye masafa mafupi, ya kati na marefu.

Makombora ya balistiki yenye masafa mafupi, ambayo yana uwezo wa kufikia umbali wa takriban kilomita 150 hadi 800 (maili 93-500), yameundwa kufikia shabaha za kijeshi zilizo karibu kupitia mashambulizi ya haraka ya kikanda.

Mifumo mikuu inajumuisha aina mbalimbali za Fateh:

Zolfaghar, Qiam-1 na makombora ya zamani zaidi ya Shahab-1/2.

Masafa yake mafupi yanaweza kuwa faida wakati wa mgogoro kwani yanaweza kurushwa kwa mfululizo wa haraka, jambo linalopunguza muda wa tahadhari na kufanya iwe vigumu kwa adui kuyazuia kabla hayajafika shabaha.

Makombora ya balistiki yenye masafa ya kati, yenye uwezo wa kufikia umbali wa takriban kilomita 1,500 hadi 2,000 (maili 900-1,200), yanajumuisha mifumo kama vile Shahab-3, Emad, Ghadr-1, aina mbalimbali za Khorramshahr na Sejjil, pamoja na miundo mipya zaidi kama vile Kheibar Shekan na Haj Qassem.

Makombora haya yana uwezo wa kufikia shabaha za Israel na maeneo yanayohusiana na Marekani katika nchi za Ghuba.

Iran pia ina akiba ya makombora ya aina ya 'cruise' kama vile Soumar, Ya-Ali, matoleo ya Quds, Hoveyzeh, Paveh na Ra'ad. Kombora la Soumar lina uwezo wa kufikia umbali wa kilomita 2,500 (maili 1,553).

Kiongozi wa Juu wa zamani wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, hapo awali aliweka kikomo cha umbali wa makombora ya Iran kufikia kilomita 2,200 (maili 1,367), lakini aliondoa kikomo hicho kufuatia vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran mwezi Juni 2025.

.

Chanzo cha picha, Aljazeera

Ni yapi ya hivi punde kuhusu mzozo kati ya Marekani na Iran?

Kuzidi kwa uhasama hivi karibuni kumemaliza kipindi cha utulivu wa kiasi.

Marekani ilianza upya mashambulizi dhidi ya maeneo ya Iran mnamo Agosti 31, huku Kamandi Kuu ya Marekani ikisema kuwa ilishambulia maeneo ya Jeshi la Iran (IRGC) kusini mwa Iran.

Iran ilijibu kwa makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya vikosi na vifaa vya kijeshi vya Marekani vilivyoko katika eneo hilo. Siku ya Jumanne, jeshi la Marekani lilisema kuwa limemaliza wimbi jingine la mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Iran.

Tehran iliripoti kuwa Marekani pia ilishambulia maeneo ya raia, ikiwemo nyumba iliyolipuliwa wakati wa sherehe ya harusi katika mji wa Kuhestak, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua watano na majeraha kwa watu 68, wakiwemo wanawake na watoto.

Jeshi la Iran lilisema kuwa lilifanya mashambulizi dhidi ya kambi na vifaa vya Marekani nchini Jordan, Bahrain, Kuwait na Erbil nchini Iraq kama hatua ya kulipiza kisasi.

Rais wa Marekani Donald Trump hapo awali alitishia kufanya mashambulizi zaidi iwapo Iran ingelipiza kisasi, huku Tehran ikisema nayo ingejibu mashambulizi ya Marekani.

Mapigano hayo mapya pia yamerudisha mlango bahari wa Hormuz katika kiini cha mzozo huo, huku vikosi vya Iran na Marekani vikipigania udhibiti wa njia hiyo muhimu ya maji.

Bei ya mafuta ilipanda kwa kasi wiki hii huku masoko yakijibu mapigano hayo mapya kati ya Marekani na Iran pamoja na hatari kwa usafirishaji wa nishati kupitia njia hiyo muhimu, ambayo katika nyakati za amani hupitisha asilimia 25 ya mafuta na bidhaa za petroli duniani.

Mashambulizi hayo ya Marekani yanajiri muda mfupi baada ya Washington kutangaza kampeni ya shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran, ikitangaza kuwa ingelenga maslahi yake ya kifedha kote duniani.