Dhehebu la vijana watanashati lililoambiwa dunia itaisha mwaka 1999

Chanzo cha picha, (Credit: HBO)
Wakati wa miaka ya 1980, mhitimu wa chuo kikuu cha Princeton, Hoyt Richards alikuwa akiishi maisha mawili tofauti: Machoni mwa watu, alikuwa "mwanamitindo wa kiume," akitangaza kampuni za kifahari kama Ralph Lauren na Donna Karan.
Hata hivyo, nyuma ya pazia, alikuwa mwanachama wa Eternal Values, kundi au dhehebu la siri lililpongozwa na msosholaiti kutoka Manhattan, Marekani anayeitwa Frederick von Mierers.
Makala kuhusu asili ya kundi hilo na kupotea kwake baadaye, inapatikana katika mtandao wa HBO kwa jina la Bring Me the Beauties: A Model CultVon Mierers, aliyezaliwa kwa jina la Fred Meyers katika familia ya wafanyakazi huko Brooklyn, Marekani.
Mierers alidai kuwa yeye ni "kiumbe" kutoka sayari ya Arcturus ambaye amechukua umbo la mwanadamu ili kueneza maarifa duniani. Aliwaambia wafuasi wake kwamba dhamira yake ni kuajiri viongozi kutoka nje ya sayari ya dunia kabla ya janga ambalo litaharibu sayari ya dunia mwaka 1999.
Uajiri, Ushawishi, na Unyonyaji wa Kifedha

Chanzo cha picha, HBO
Von Mierers aliwalenga vijana wenye kuvutia, waliofanikiwa, na wenye malengo ili kuinua sifa yake na hali yake ya kifedha. Alimshawishi Richards tangu akiwa na umri wa miaka 16, kwa mara ya kwanza alishawishi kwenye ufuo katika hoteli ya kifahari ya Nantucket.
Von Mierers alitumia mbinu za kisaikolojia kumnasa kijana huyo, akimsifu sana Richards kwa kumwambia alikuwa "ana akili" na "wa kipekee," jambo ambalo lilimfanya kutohoji kuhusu mafundisho yake ya ajabu.
Baada ya muda, Von Mierers alifanikiwa kumuweka mbali Richards kutoka kwa marafiki zake na familia yake, utengano ambao ulidumu kwa miaka 12.
Richards alipohamia Princeton, Von Mierers alitumia nyumba yake ya Manhattan kwa sherehe ili kuongeza ushawishi wake. Hatimaye alimtambulisha Richards kwa mtu mashuhuri katika Kampuni ya Wanamitindo ya Ford, na kuingia katika kazi hiyo ambayo ilimpa faida kubwa.
Kwa kutumia hatia ya ndani ya Richards kuhusu kufuata kazi isiyo ya kiroho, Von Mierers alifanikiwa kumshawishi arudishe mapato yake kwenye kundi hilo. Richards anakadiria alitoa kati ya dola milioni 4 na dola milioni 5 kwa kundi la Eternal Values.
Mwanamitindo mwingine maarufu, Jacki Adams, naye pia alinaswa, na kumpa Von Mierers zaidi ya $100,000 kwa ajili ya vito vya thamani na ukarabati wa vyumba.
Kundi hilo lilifadhili shughuli zake hasa kwa kuuza "vitabu juu ya maisha" kwa gharama kubwa, ambavyo vilikuwa vimerikodiwa kwenye kaseti na vito maalum, ambavyo Von Mierers alidai vina sifa za uponyaji.
Matendo ya kundi

Chanzo cha picha, HBO
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ingawa kundi hilo lilibaki kuwa dogo kwa kiasi fulani, chini ya wanachama 100, hadhi yake iliimarika na kuwa dhehebu mwaka 1985. Mwaka huo, mwandishi Ruth Montgomery alichapisha kitabu kilichouzwa sana cha Aliens Among Us, ambacho kilithibitisha historia ya ajabu ya Von Mierers kwa kudai kwamba kweli alikuwa kiumbe wa nje ya dunia.
Hali hii ya umaarufu ilisaidia kikundi kujenga biashara ya kimataifa, kikipokea barua kutoka nchi 45.
Katika maisha ya kila siku ya wananchama, walilala katika sakafu ya nyumba ya Von Mierers. Mwanzoni, Von Mierers aliamuru mtindo wa maisha wa useja. Hata hivyo, baadaye alibadilisha mbinu, akiwaamuru wanachama kufanya ngono wao kwa wao.
Mtaalamu wa madhehebu Dkt. Steven Hassan anabainisha kuwa kutumia hisia za mapenzi za wafuasi ni njia maarufu sana ya kuunda utegemezi na utii kwa kiongozi.
Mtu yeyote aliyepinga agizo hilo aliaibishwa hadharani na Von Mierers. Na baadaye ilibainika kwamba Von Mierers mara kwa mara aliwaajiri wafanyakazi wa ngono wa kiume wakati wa enzi zake za useja, akiwashawishi wafuasi wake aliowapotosha kwamba alikuwa akiwaleta kwenye nyumba hiyo kwa ajili ya msaada wa kiroho tu.
Kilichofuata baadaye

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na Dkt. Hassan, Von Mierers alikuwa na udhibiti kwa kutumia mbinu kadhaa, akibadilisha kati ya ukosoaji mkali, wa kinidhamu na sifa za ghafla na malezi ili kuwaweka wafuasi wake kuwa watiifu.
Von Mierers alifariki mwaka 1990 kutokana na UKIMWI, na kufanya kundi hilo kufikia mwisho. Hata hivyo, wanachama wasio na mwelekeo, akiwemo Richards, waliendelea kuishi katika kivuli chake.
Richards hakujiondoa kundini hadi mwaka 1999, mwaka ambao ilitabiriwa kuwa dunia ingeisha, ndipo alipokimbia kundi hilo kwa msaada wa mwanamitindo mwenzake wa kiume Fabio Lanzoni.
Sasa akiwa na umri wa miaka 64, Richards ametumia miaka 25 akikumbuka maisha hayo, akiungana tena na familia yake, na kuzungumza hadharani kuwaonya wengine.
Anaiona hadithi yake kama hadithi ya kutisha kuhusu "madhehebu," ambayo anaifafanua kama mabadiliko yasiyofaa ambapo mtu bila kujua husalimisha nguvu zake binafsi kwa mtu ambaye humpa sifa na muwa mwingi.















