Zaidi ya Wajapani 100,000 wafikisha umri wa miaka 100

Chanzo cha picha, Getty Images
Idadi ya watu walio na umri wa miaka 100 au zaidi nchini Japan imevuka watu 100,000 kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo, kwa mujibu wa Wizara ya Afya.
Takwimu zinaonyesha kuwa Japan sasa ina watu 107,677 waliofikisha umri wa miaka 100 au zaidi, idadi kubwa zaidi duniani. Kati yao, asilimia 88 ni wanawake.
Mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi nchini humo ni Kishimoto Fuyo mwenye miaka 114 kutoka mji wa Kyoto, huku mwanaume mwenye umri mkubwa zaidi akiwa Kato Hikaru, mwenye miaka 112 kutoka Kumamoto.
Waziri wa Afya, Kenichiro Ueno, alisema anafurahishwa na ukweli kwamba watu wengi zaidi wanaishi maisha marefu, yenye afya njema na yenye shughuli za kujenga jamii. Alieleza kuwa maendeleo katika sekta za tiba na teknolojia yamechangia ongezeko hilo.
Hata hivyo, alionya kuwa kuongezeka kwa idadi ya wazee kunaleta changamoto kwa mfumo wa hifadhi ya jamii na huduma za ustawi wa wananchi.
Wataalamu wanasema maisha marefu ya Wajapani yanachangiwa na sababu kadhaa, ikiwemo lishe bora na mtindo wa maisha unaohusisha shughuli za mwili. Mlo wa kawaida nchini humo unajumuisha samaki, mboga na wali, huku ukiwa na kiwango kidogo cha mafuta ikilinganishwa na nchi nyingi za Magharibi.
Aidha, watu wengi wazee nchini Japan huendelea kutembea kwa miguu, kutumia usafiri wa umma, kuendesha baiskeli na kufanya mazoezi mepesi ya kujinyoosha.
Japan imekuwa ikikabiliwa na ongezeko la idadi ya wazee kwa miaka mingi. Katika ishara ya mabadiliko hayo ya demografia, mauzo ya nepi za watu wazima yamekuwa yakizidi yale ya nepi za watoto kwa zaidi ya muongo mmoja.



























