Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani yatangaza silaha yake ya kwanza katika obiti ya Dunia
- Author, Bernd Debusmann Jr
- Author, Chris Graham
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Marekani imethibitisha kwa mara ya kwanza kuwa imepeleka silaha angani katika obiti ya Dunia, hatua ambayo ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kukiri rasmi kuwa inamiliki silaha zenye uwezo huo wa kushambulia kutoka angani.
Waziri wa Jeshi la Anga la Marekani, Troy Meink, amesema silaha hiyo iliyoko kwenye mzingo wa dunia ama obiti ni muhimu kwa ajili ya kulinda majeshi ya Marekani dhidi ya vitisho au mashambulizi kutoka kwa maadui.
Akizungumza katika mkutano maalumu wa masuala ya anga, Meink alisema Marekani iko tayari kukabiliana na "vitisho vinavyoendelea kubadilika", lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu uwezo wa silaha hiyo wala wakati ilipopelekwa kwenye obiti.
Maafisa wakuu wa kijeshi wa Marekani walikuwa wameeleza hapo awali mipango ya kupanua uwezo wa kijeshi wa nchi hiyo angani, wakitaja mipango ya Urusi na China ya kutengeneza njia za kushambulia au kuvuruga satelaiti za Marekani iwapo kutatokea mzozo wa kijeshi siku zijazo.
China yaonya kuhusu mashindano ya silaha
China imekosoa hatua hiyo na kuonya dhidi ya kuanzishwa kwa "mashindano ya silaha angani."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema Marekani inapaswa kusitisha kupanua uwezo wake wa kijeshi na maandalizi ya vita angani.
Hata hivyo, mamlaka za Marekani bado hazijaweka wazi namna silaha hiyo inavyofanya kazi.
Msemaji wa Jeshi la Anga la Marekani amesema uwezo wa kudhibiti anga unahusisha shughuli zinazolenga kuhakikisha nchi inaweza kushindana na kudhibiti nafasi yake angani, kwa kutumia njia za kimwili na zisizo za kimwili kuvuruga, kudhoofisha au hata kuharibu uwezo wa wapinzani inapobidi.
Bleddyn Bowen, mtaalamu wa matumizi ya kijeshi ya anga za juu, amesema taarifa kuhusu teknolojia hiyo ni chache sana hadharani.
Amesema kuna uwezekano silaha hiyo kuwa ya aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mfumo wa vita vya kielektroniki au kifaa cha kuvuruga mawasiliano ya redio.
Silaha ya aina hiyo inaweza kutumika kuvuruga mawasiliano ya redio, ikiwa ni pamoja na yale yanayohusisha satelaiti.
Uwezekano mwingine, kwa mujibu wa Bowen, ni kifaa kinachoweza kuharibu satelaiti kwa kugonga satelaiti nyingine kwa kasi kubwa.
Hata hivyo, amesema aina hiyo ya silaha ina uwezekano mdogo kwa sababu inaweza kusababisha kiasi kikubwa cha mabaki ya vyuma na vifaa kuzunguka Dunia, jambo linaloweza kuhatarisha satelaiti nyingine.
Silaha angani na mkataba wa kimataifa
Utawala wa Rais Donald Trump umesema uwezo wa kijeshi angani, pamoja na makombora ya kuzuia mashambulizi, ni sehemu muhimu ya mfumo wa ulinzi wa Golden Dome, unaolenga kuilinda Marekani dhidi ya makombora na vitisho vingine vya angani.
Mkataba wa mwaka 1967 ulipiga marufuku kuwekwa kwa silaha za maangamizi makubwa katika obiti ya Dunia.
Hata hivyo, tangu wakati huo, mataifa yenye nguvu kijeshi, yakiwemo Marekani, Urusi na China, yameendelea kutengeneza uwezo mwingine wa kijeshi angani ambao haujapigwa marufuku na mkataba huo.
Miongoni mwa uwezo huo ni kushambulia satelaiti za wapinzani, ambazo ni muhimu kwa mawasiliano ya kijeshi na ufuatiliaji.
Mwaka jana, Rais Trump alisaini amri ya kiutendaji iliyosisitiza nafasi ya Jeshi la Anga la Marekani si tu katika kulinda mali za Marekani angani, bali pia kama nguvu ya kushambulia.
Jeshi la Anga la Marekani lilianzishwa mwaka 2019 na ni tawi jipya zaidi la majeshi ya Marekani katika kipindi cha zaidi ya miaka 70. Liliundwa kulinda mali za Marekani angani, zikiwemo mamia ya satelaiti zinazotumika kwa mawasiliano na ufuatiliaji.
Urusi na China
Mapema Februari, iliripotiwa kuwa satelaiti mbili za Urusi huenda zilinasa mawasiliano kutoka kwa angalau satelaiti 12 za Ulaya tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka 2022.
Ujasusi huo huenda uliwezesha maafisa wa kijasusi wa Urusi kusoma taarifa nyeti zilizokuwa zikitumwa kupitia satelaiti hizo au, kinadharia, hata kuzidhibiti.
Mwaka 2024, Marekani ilidai kuwa Urusi ilikuwa imepeleka angani satelaiti ambayo Marekani iliamini ilikuwa na uwezo wa kushambulia satelaiti nyingine. Urusi haijatoa maelezo ya hadharani kuhusu madai hayo.
Jeshi la Anga la Marekani linasema China inaendeleza na kutumia uwezo wa kijeshi na wa kukabiliana na mifumo ya angani, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuboresha jeshi.
Pia linasema Urusi inaiona anga za juu kama eneo la vita na inaamini kuwa uwezo wa kuitawala anga utakuwa na umuhimu mkubwa katika migogoro ya kijeshi ya siku zijazo.