Silaha gani hatari za urani zinazotumiwa na Urusi?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Ripoti zinaeleza kuwa Urusi imetumia ndege zisizo na rubani zilizobeba urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi katika mashambulizi yake dhidi ya Ukraine.

Kuna takribani matukio 10 yanayojulikana ya matumizi ya droni hizo. Zote ni droni za upelelezi za Urusi zilizopatikana baada ya kuanguka nchini Ukraine.

Kila moja ilikuwa imebeba kombora la R-60 la kutoka angani, lililokuwa na vijiti vya urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi.

Nyenzo hii ina kiwango cha mionzi kilicho chini sana ikilinganishwa na urani ya asili, na silaha zinazotumia nyenzo hiyo huainishwa kama silaha za kawaida, si silaha za nyuklia.

Kwa ujumla, hatari zinazotokana na mionzi ya urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi huchukuliwa kuwa ndogo.

Idara ya Usalama ya Ukraine (SBU) inasema makombora hayo yaliundwa kulenga ndege za Ukraine zinazotumika kuzuia mashambulizi, ambazo huruka wakati wa mashambulizi ya anga ya Urusi.

Shirika hilo limesema kuwa hadi sasa limebaini droni tisa zilizokuwa na makombora yenye nyenzo zenye mionzi. Droni zote zilipatikana kaskazini mwa Ukraine kati ya Aprili na Julai 2026; saba zilipatikana katika mkoa wa Chernihiv, na mbili katika mkoa wa Sumy.

Hata hivyo, taarifa ya kwanza kuhusu droni ya aina hiyo ilichapishwa Januari 2026. Taarifa hiyo ilitolewa na Sergey Beskrestov, mtaalamu maarufu wa droni nchini Ukraine, anayejulikana pia kwa jina la "Flash."

Baadaye, Beskrestov aliwahi kuwa mshauri wa Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, na baadaye akawa mshauri wa Rais Volodymyr Zelensky.

R-60 ni aina gani ya makombora?

Makombora ya R-60 yalitengenezwa katika Umoja wa Kisovieti katika miaka ya 1970 kwa ajili ya mapambano ya angani ya masafa mafupi kati ya ndege za kivita.

Toleo la R-60M, ambalo linaweza kutumia vichwa vya vita vyenye urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi, lilikuwa tayari linatumika katika jeshi muda mrefu kabla ya kuanza kwa vita vya Ukraine.

Hili ni kombora la zamani sana lililotengenezwa na Umoja wa Kisovieti, ambalo kichwa chake cha vita kina vijiti maalumu vilivyotengenezwa kwa urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi , alisema Sergei Beskrestenov katika mahojiano.

Aliongeza kuwa madhumuni makuu ya kombora hilo ni kuangusha ndege, si kusababisha uchafuzi wa mazingira.

"Kombora hili halina kichwa cha nyuklia," aliiambia shirika la habari la Ukraine la Union.

Urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi ni nyenzo yenye msongamano mkubwa sana. Kwa sababu hiyo, matumizi yake ya kijeshi yanayojulikana zaidi ni katika silaha za kuharibu magari yenye kinga nzito .

Robert Tolstoy wa taasisi ya utafiti ya Royal United Services Institute (RUSI) mjini London anasema kwamba nyenzo hiyo inapotumika katika makombora ya angani, inaweza kuongeza ufanisi wa kombora kwa kutengenezwa kuwa vipande vidogo lakini vizito.

"Msongamano mkubwa huwezesha kutumika vipande vidogo, na hivyo kuwa vingi zaidi, kuzunguka vilipuzi. Hii inaweza kuongeza umbali wa kufikia na uwezo wa kusababisha uharibifu," aliiambia BBC.

Hilo ni muhimu wakati silaha inakusudiwa kusababisha uharibifu mkubwa bila kulenga moja kwa moja, kwa mfano pale silaha inapotumia kifaa cha kulipuka kinachowashwa inapokaribia shabaha kama ilivyo kwenye R-60.

Urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi ni hatari kiasi gani?

Robert Tolstoy wa Taasisi ya Royal United Services Institute (RUSI) anasema kwamba urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi inapotumika katika silaha za kutoboa kinga nzito au ikiwa imehifadhiwa kama sehemu ya silaha, kwa ujumla huchukuliwa kuwa salama kusafirisha na kutumia.

Hata hivyo, chembechembe za urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi zinaweza kuingia mwilini kama vumbi baada ya silaha hizo kuharibika, kwa mfano zinapogonga shabaha. Watafiti wanasema kuna uwezekano mdogo kwamba watu watavuta au kumeza chembechembe hizo kwa kiasi kikubwa kiasi cha kusababisha matatizo makubwa ya kiafya.

Makala ya kisayansi kuhusu athari za urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi, iliyochapishwa katika Journal of Environmental Radioactivity, inasema kwamba hakutarajiwi kuwa na athari zinazoonekana kwa afya ya binadamu, na makadirio ya hatari iliyobaki ya saratani yanategemea zaidi nadharia za kisayansi.

Kwa mujibu wa makala hayo, hatari hiyo inaonekana kuwa ndogo sana katika mazingira yote baada ya vita, ikiwa ni sehemu ndogo tu ya hatari inayotarajiwa kutokana na mionzi ya asili.

Hata hivyo, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limesema kwamba kiasi cha mionzi ambacho mtu anaweza kupokea kutokana na kugusana na silaha zenye urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi ni kiasi ambacho kinahitaji muda wa kugusana na kushughulikia nyenzo hizo uwe mfupi iwezekanavyo. Pia linashauri kutumia vifaa vya kujikinga, ikiwa ni pamoja na glovu.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) kuhusu madhara ya vita nchini Ukraine pia inasema kwamba urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi inaweza kusababisha muwasho wa ngozi, kushindwa kufanya kazi kwa figo na kuongeza hatari ya saratani.

Mzozo kuhusu urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi

Matumizi ya silaha zenye urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi yamekuwa yakizua mzozo na mabishano kwa miaka mingi. Nyenzo hiyo ilitumika katika silaha za kutoboa vifaru wakati wa Vita vya Ghuba mwaka 1991, baadaye Kosovo mwaka 1999, na Iraq mwaka 2003.

Urusi ilionesha ghadhabu yake mwezi Machi 2023 baada ya ripoti kuibuka kwamba Uingereza ilikuwa inapanga kuipa Ukraine mabomu ya kutoboa vifaru yenye urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi kwa ajili ya vifaru vyake vya Challenger 2.

"Magharibi kwa pamoja imefika hatua ya kuanza kutumia silaha zenye sehemu ya nyuklia," Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema wakati huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, pia aliishutumu Uingereza kwa kukiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.

Hata hivyo, hakuna mkataba wa kimataifa unaopiga marufuku matumizi ya silaha zenye urani iliyopunguzwa kiwango cha mionzi, na Urusi yenyewe hutumia mabomu ya kutoboa vifaru yenye nyenzo hiyo, ikiwa ni pamoja na silaha aina ya Svinets.