Ruto afichua mradi mwingine wa Dangote baada ya kiwanda cha kusafisha mafuta cha Lamu
Tajiri nambari moja barani Afrika, Aliko Dangote, yuko katika mazungumzo na serikali ya Kenya kwa ajili ya ujenzi wa bomba la mafuta ghafi litakalounganisha Lamu na Turkana, ikiwa ni sehemu ya mipango ya kufungua fursa za rasilimali ya mafuta nchini humo.
Rais William Ruto alibainisha hayo wakati wa mkutano na vyombo vya habari katika Ikulu Ndogo ya Kisumu siku ya Jumanne, Septemba 15, akisema bomba hilo linalopendekezwa litakuwa sehemu ya mradi wa kiwanda cha kusafisha mafuta ambacho Dangote anapanga kukijenga Lamu.
"Kama sehemu ya mradi huo wa kiwanda cha kusafisha mafuta huko Lamu, tunafanya mazungumzo na Dangote kuhusu ujenzi wa bomba la kuelekea Turkana ili tuweze kufaidika na mafuta tuliyonayo Turkana," alisema Ruto.
Rais pia alitangaza kuwa ujenzi wa kiwanda hicho utazinduliwa rasmi tarehe 30 Septemba, huku Dangote na viongozi wengine wa mataifa wakitarajiwa kuhudhuria hafla hiyo ya kuweka jiwe la msingi.
Bomba hilo linalopendekezwa litatoa njia ya kuunganisha visima vya mafuta vya Turkana na pwani ya Kenya, na hivyo kuruhusu mafuta ghafi yanayozalishwa katika eneo hilo kusafirishwa hadi Lamu kwa ajili ya kusafishwa.
Hatua hii inakuja wakati Dangote akijiandaa kuwekeza katika kiwanda cha kusafisha mafuta chenye thamani ya Shilingi trilioni 2.59 (dola bilioni 20) huko Lamu, ambacho kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku kitakapokamilika mwaka 2030.