Rubani wa F-15 wa Marekani asimulia alivyohangaika kwa saa 50 kwenye milima ya Iran

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Mmoja wa maafisa wawili wa Jeshi la Anga la Marekani ambaye ndege yao ya kivita aina ya F-15E ilidunguliwa juu ya Iran mwezi Aprili, amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu tukio hilo.

Kanali wa Jeshi la Anga la Marekani ambaye jina lake halijawekwa wazi kwa sababu za kiusalama, amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu tukio la kuangushwa kwa ndege yake ya kivita juu ya Iran.

Afisa huyo, anayefahamika kwa jina la utambuzi wa kijeshi "Dude 44 Bravo" au "Bravo", alikuwa afisa wa mifumo ya silaha katika ndege ya kivita ya viti viwili aina ya F-15E Strike Eagle, akikaa kwenye chumba cha nyuma cha rubani.

Akizungumza na kipindi cha 60 Minutes cha CBS, Bravo alisema kombora lilipoigonga ndege hiyo, athari yake ilikuwa "kama kugongwa na treni ya mizigo".

Ndege hiyo ya Marekani ilidunguliwa asubuhi ya Aprili 3 katika eneo la milima kusini mwa mji wa Isfahan nchini Iran. Wafanyakazi wa ndege walijulikana kwa majina ya kioperesheni "Alpha" na "Bravo", ambapo Alpha alikuwa rubani huku Bravo akiwa afisa wa mifumo ya silaha.

Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, operesheni ya kuwaokoa wahudumu wa ndege hiyo ilihusisha kupelekwa kwa takribani wanajeshi 100 ndani ya ardhi ya Iran.

Awali, Bravo ameeleza jinsi alivyonusurika baada ya kutoka kwenye ndege iliyokuwa imeharibiwa, akitumia parachuti iliyokuwa imeathirika, kupata majeraha kadhaa na kujaribu kukwepa vikosi vya Iran kabla ya kuokolewa na timu ya uokoaji ya Marekani.

Lengo la operesheni lilikuwa lipi?

Kamanda wa Uongozi wa Jeshi la Marekani (Centcom), Admirali Brad Cooper, amesema ndege ya kivita aina ya F-15E ilikuwa kwenye operesheni ya kushambulia "vituo vya viwanda vinavyohusishwa na programu za Iran za droni na makombora."

Alisisitiza kuwa operesheni hiyo "haikuhusiana kwa namna yoyote na kituo cha nyuklia cha Isfahan."

Kwa mujibu wa Cooper, kufikia wakati huo Marekani ilikuwa imefanya takribani safari za kijeshi za anga 13,000 katika vita dhidi ya Iran. Alisema Marekani ilikuwa na udhibiti mkubwa wa anga, lakini akaongeza kuwa mazingira ya operesheni yalikuwa hatari.

Ndege hiyo ya F-15E ilidunguliwa kwa kombora la ardhini kwenda angani la kubebwa begani na mwanajeshi mmoja. Kulingana na taarifa za CBS, ndege hiyo ina thamani ya karibu dola milioni 30 za Marekani, huku kombora lililoitungua likigharimu takribani dola 100,000.

Afisa anayejulikana kwa jina la utambulisho wa kijeshi "Bravo" alisema yeye na mwenzake walijaribu kuiokoa ndege baada ya kushambuliwa, lakini muda mfupi baadaye ilidhihirika kuwa haingeweza kuendelea kuruka.

Baada ya kuruka kutoka kwenye ndege, upepo uliwatenganisha wawili hao walipokuwa wakishuka kwa parachuti. Walitua umbali wa karibu maili tano kutoka kwa kila mmoja, sawa na takribani kilomita nane.

Bravo alisema parachuti yake ilikuwa imeharibika kutokana na athari ya shambulio la kombora.

"Niliangalia juu wakati mmoja na kugundua kwamba sikuwa na parachuti," alisema. "Ilikuwa ni taswira ya kutisha zaidi niliyowahi kuona maishani mwangu."

Alieleza kuwa alijaribu kufungua sehemu za parachuti zilizokuwa zimejikunja huku akikaribia kuanguka kwa kasi kubwa.

Wataalamu wa kijeshi walikadiria kuwa, kutokana na majeraha aliyopata, huenda aligonga ardhi kwa kasi ya kati ya maili 70 na 100 kwa saa, sawa na kilomita 113 hadi 161 kwa saa.

Athari ya kuanguka ilisababisha kuvunjika kwa mifupa ya mgongo, mkono na bega. Pia aliteguka kifundo cha mguu huku akiwa na majeraha ya kukatwa kichwani na usoni yaliyokuwa yakivuja damu.

Licha ya majeraha hayo, alisema aliondoka mara moja eneo alipotua ili kuepuka kukamatwa.

"Tumefundishwa kuendana na mazingira na kushinda changamoto. Licha ya majeraha yangu, niliondoka eneo nilipotua haraka iwezekanavyo," alisema.

Kupanda juu ili kutoroka

Bravo alisema alijikuta usiku wa manane katikati ya bonde lenye miamba mikali, akiwa amejeruhiwa na bila uhakika wa usalama wake. Aliamua kupanda kuelekea maeneo ya juu zaidi na kufanikiwa kufika kwenye mwinuko wa takribani futi 7,000 (zaidi ya mita 2,100).

Alipoulizwa jinsi alivyoweza kupanda mlima huo akiwa na majeraha, alisema hakutaka kukamatwa na kuonyeshwa kwenye televisheni ya Iran.

Kwa mujibu wa CBS, baada ya ajali hiyo vyombo vya habari vya Iran vilitangaza zawadi kwa yeyote ambaye angewasaidia kuwapata wanajeshi hao wawili wa Marekani, huku picha za watu wenye silaha wakifanya msako zikioneshwa hewani.

Maafisa wa Marekani wanadai kuwa wanajeshi wapatao 1,500 wa Iran walishiriki katika msako huo na wakati mmoja walifika karibu sana na eneo alipokuwa amejificha. Hata hivyo, madai hayo hayajathibitishwa na vyanzo huru.

Mwenyekiti wa Jopo la Wakuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Dan Keene, alisema hofu kubwa ya makamanda wa Marekani ilikuwa uwezekano wa wanajeshi hao kukamatwa na kuonyeshwa hadharani mjini Tehran.

Takribani saa sita baada ya ndege kudunguliwa, vikosi vya Marekani vilifanikiwa kumpata rubani mwenzake, Alpha, na kuanza operesheni ya uokoaji.

Kulingana na CBS, operesheni ya uokoaji ilihusisha ndege 21 za Marekani zilizokuwa zimeingia katika anga ya Iran, zikiwemo ndege 12 za kivita, nne za vita vya kielektroniki na tano za utafutaji na uokoaji.

Helikopta mbili zilitumwa kumuokoa rubani Alpha, lakini zilikumbana na mashambulizi ya risasi. Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alisema kulikuwa na mashambulizi ya risasi wakati wote wa operesheni hiyo, ingawa vikosi hivyo vilifanikiwa kumtoa Alpha salama.

Helikopta moja ya HH-60 iliharibiwa na risasi za silaha ndogo na baadhi ya wahudumu wake walijeruhiwa, lakini ilifanikiwa kurejea salama. Wakati huo huo, ndege ya mashambulizi ya A-10 pia iliharibiwa na rubani wake akalazimika kujinusuru kwa kuruka nje ya ndege juu ya Ghuba ya Uajemi. Naye alinusurika.

Licha ya mafanikio ya kumuokoa Alpha, vikosi vya Marekani havikufanikiwa kumpata Bravo katika operesheni hiyo na vililazimika kuondoka eneo hilo. Alpha, ambaye hakutaka kuzungumza na CBS, amerejea katika majukumu yake ya kawaida ya urubani ndani ya Jeshi la Anga la Marekani.

Ujumbe wa Bravo

Usiku ulipoingia, Bravo alipata eneo la kujificha na kufanikiwa kutuma ujumbe wa siri kwa vikosi vya Marekani kusema: "Nimejeruhiwa, niko safarini." Katika ujumbe mwingine mfupi lakini wenye uzito mkubwa, aliandika: "Mungu ni mwema."

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa baadaye, ujumbe huo uliwapa makamanda wa operesheni uthibitisho muhimu kwamba Bravo bado alikuwa hai, alikuwa huru na alikuwa akiendelea kutafuta njia ya kujiokoa.

Hegsett alisema kupokea ujumbe hizo kuliondoa hofu kwamba afisa huyo huenda alikuwa amekamatwa au kuuawa. Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa mipango ya kuanzisha operesheni ya uokoaji usiku huo, mazingira yaliyokuwepo yalionekana kuwa hatari mno kwa vikosi vya uokoaji kuendelea mara moja.

Akikumbuka majadiliano yaliyofanyika katika Chumba cha Kudhibiti Hali za Dharura (Situation Room) cha Ikulu ya Marekani, Hegsett alisema viongozi wa kijeshi na kisiasa walikubaliana kuahirisha operesheni hiyo kwa saa 24 zaidi.

"Ulikuwa uamuzi mgumu sana," alisema. "Ulimaanisha kwamba Bravo angelazimika kubaki huko kwa takribani saa nyingine 24."

Kwa Bravo, uamuzi huo ulimaanisha kuendelea kupambana na mazingira magumu akiwa peke yake katika eneo la milimani. Alilazimika kustahimili usiku mwingine wa baridi kali, akiwa na kiasi kidogo sana cha maji na karibu bila chakula.

Licha ya majeraha aliyokuwa amepata baada ya kuruka kutoka kwenye ndege iliyodunguliwa, afisa huyo aliendelea kujificha huku akijaribu kuepuka kugunduliwa na vikosi vya Iran, akisubiri kwa matumaini kuwasili kwa timu ya uokoaji ya Marekani. Hali hiyo iligeuka kuwa jaribio kubwa la uvumilivu, mafunzo ya kijeshi na uwezo wa kuishi katika mazingira hatari.

Bravo alinusurika kwa siku nyingine na usiku mwingine katika mazingira ya baridi kali ya milimani, akiwa na maji kidogo huku chakula kikikaribia kumuishia.

Kwa mujibu wa CBS, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) lilianzisha operesheni ya hadaa iliyolenga kupotosha vikosi vya Iran kuhusu mahali alikokuwa Bravo. Taarifa za uongo zilidai kuwa alikuwa akielekea mpaka wa Afghanistan, Bahari ya Caspian au kusini mwa Iran, wakati kwa siri maafisa wa Marekani walikuwa wakifuatilia eneo lake halisi.

Kabla ya kikosi cha uokoaji kufika, ndege za kivita na ndege zisizo na rubani za Marekani zilishambulia maeneo ya vikosi vya Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) yaliyokuwa karibu. CBS iliripoti kuwa Marekani ilitumia jumla ya silaha 339 katika operesheni hiyo iliyodumu takribani saa 50.

Awamu ya pili ya operesheni ilihusisha zaidi ya ndege 150 za kijeshi. Miongoni mwa hizo kulikuwa na ndege 64 za kivita, ndege nne za mashambulizi, ndege 48 za kuongeza mafuta angani, ndege 13 za utafutaji na uokoaji, pamoja na ndege 26 za ujasusi na vita vya kielektroniki.

Admirali Brad Cooper alisema takribani wanajeshi 92 wa Marekani walishiriki operesheni hiyo wakiwa ardhini, huku mamia ya wengine wakifanya kazi angani na maelfu zaidi wakitoa msaada katika sekta mbalimbali.

Cooper aliitaja operesheni hiyo kuwa "operesheni ndani ya operesheni", akisema ilikuwa mara ya kwanza kwa vikosi vya Marekani kuendesha operesheni ya aina hiyo ndani ya Iran katika kipindi cha miaka 46.

Ndege za usafirishaji kutua katika ardhi ya kilimo

Pentagon ilizingatia mbinu nne za kumuokoa Bravo, lakini hatimaye ikaamua kutumia ndege mbili maalumu za usafiri za MC-130 zilizotua kwenye uwanja wa muda uliotengenezwa katika eneo la mashamba, karibu kilomita 16 kutoka alipokuwa amejificha.

Ndege hizo zilibeba helikopta nne ndogo za MH-6 "Little Bird" zilizokuwa zimekunjwakunjwa kwa ajili ya usafirishaji. Wanajeshi walizikusanya ndani ya dakika 15 tu, na safari kutoka uwanja huo wa muda hadi mahali alikokuwa Bravo ilichukua takribani dakika saba.

Kwa mujibu wa CBS, vikosi maalumu vililinda uwanja huo huku timu za uokoaji za Jeshi la Anga la Marekani zikielekea kumchukua Bravo.

Bravo alielezea kuwasili kwa kikosi hicho kama moja ya nyakati muhimu zaidi maishani mwake. Hakutaka kueleza mazungumzo yao, lakini alisema maneno yake ya kwanza yalikuwa mafupi:

"Twende."

Hata hivyo, hatari haikuisha mara baada ya kuokolewa. Magurudumu ya ndege mbili za MC-130 yalikwama kweny udongo laini wa uwanja huo wa muda, na kuzifanya zishindwe kuruka.

Kutokana na hali hiyo, zaidi ya wanajeshi 90 wa Marekani waliokuwa ndani ya operesheni hiyo walihitaji kuondolewa haraka kweny ardhi ya Iran. Pentagon ilitekeleza mpango mbadala na kuwahamisha kwa kutumia ndege nyingine.

Marekani iliacha ndege mbili za MC-130 pamoja na helikopta nne za Little Bird katika eneo hilo, kabla ya kuziharibu kwa mashambulizi ya anga ili kuzuia teknolojia na vifaa vyake kuangukia mikononi mwa Iran.

Hatimaye Bravo aliwasili salama akiwa mikononi mwa vikosi vya Marekani tarehe 5 Aprili, takribani saa 50 baada ya ndege yake ya kivita kudunguliwa.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi