Mambo 10 kuhusu kufika kileleni ambayo wataalamu wanataka ujue

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Kufika kileleni, kuwa na mwisho mzuri, kufikia mshindo, kuna misamiati mingi sana ya kuelezea hali ya kupata upeo war aha ya ngono.

Lakini tunajua nini hasa kuhusu kufika kileleni, zaidi ya yale tuliyofundishwa shuleni kuhusu ngono, mazungumzo ya hapa na pale, na nakala za zamani za majarida?

Kisayansi, Kufika kileleni hufafanuliwa kama mikazo ya mwili inayotokea kwa mfululizo kwa tofauti ya takriban sekunde 0.8, na muda kati ya mikazo hiyo huongezeka hatua kwa hatua hadi inapoisha. Mara nyingi, hali hii huambatana na hisia za furaha na raha kubwa.

Hata hivyo, upeo wa ngono unaweza kufanya mengi zaidi ya kukupa hisia za raha kwani pia unaweza kuimarisha uhusiano kati yako na mwenzi wako, kupunguza maumivu kwa muda mfupi, na hata kubadilisha hali yako ya ufahamu.

Wafaransa huita kufika kileleni "la petite mort", au "kifo kidogo".

Hata hivyo, kufika kileleni kunaweza pia kukufanya ujisikie vibaya. Kwa baadhi ya matatizo ya kiafya, kufikia kileleni kunaweza kusababisha changamoto ulionayo kuendelea au hata maumivu.

Na hayo ni kwa kuangalia tu tafiti zinazohusu kufika kileleni kwa binadamu. Uchunguzi zaidi katika ulimwengu wa wanyama unaonyesha kwamba kufika kileleni ni sehemu ndogo tu ya taratibu za kujamiiana.

Haya hapa ni mambo yote ambayo huenda hukuwahi kuyajua kuhusu kufika kileleni na baadhi yake huenda yakakushangaza.

1. Ubongo wako unaweza kutofautisha aina mbalimbali za msisimko

Kwa kawaida, kufika kileleni huhusishwa na msisimko wa sehemu za siri na maeneo kama kisimi na mkundu.

Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kuwa takriban asilimia 12 ya wanawake wanaweza kufika kileleni kupitia msisimko wa maeneo mengine yenye hisia za kimapenzi, yakiwemo midomo, chuchu na hata ngozi ya kichwa.

Kinachovutia zaidi ni kwamba ubongo wako unaweza kutambua kwa usahihi wakati maeneo mbalimbali ya mwili yanapochochewa kihisia au kimapenzi.

Utafiti wa mfumo wa neva uliofanywa mwaka wa 2016, uliotumia picha za ubongo, unaonyesha kuwa kufika kileleni kunatokana na aina tofauti za msisimko huamsha njia za neva zinazofanana kwa kiasi fulani, lakini pia zikiwa na tofauti katika baadhi ya maeneo.

Sehemu ya ubongo inayohusika na uchakataji wa hisia za mwili, inayojulikana kama sensory cortex, inaonekana kuwa na ramani tofauti za maeneo haya ya mwili. Hivyo, ikiwa mwenzi wako ana uwezo wa kuchochea maeneo yote kwa wakati mmoja, huenda hilo likasababisha mshindo mkali zaidi.

"Kila moja ya maeneo hayo ya mwili hutuma ishara katika sehemu tofauti ya ubongo, na kila eneo linaweza, lenyewe, kusababisha aina tofauti ya msisimko na kufika kileleni," anaeleza Dkt Barry Komisaruk, mtafiti wa masuala ya kufika kileleni katika Chuo Kikuu cha Rutgers, Newark, nchini Marekani.

"Nadharia yangu ni kwamba ikiwa maeneo yote yanachochewa kwa wakati mmoja, husababisha kufika kileleni wenye utofauti mkubwa zaidi na mkali zaidi.

"Kwa sababu kila eneo hutuma ishara katika sehemu tofauti ya ubongo, kila moja husababisha mwitikio wake wa kufika kileleni. Kwa hiyo, unapochanganya yote pamoja, unapata kufika kileleni kwa kishindo na raha Zaidi.

2. Watu walio na majeraha ya uti wa mgongo bado wanaweza kufikia kileleni

Uti wa mgongo hufanya kazi kama njia ya mawasiliano ya pande mbili kati ya ubongo na sehemu nyingine za mwili. Uti wa mgongo unapokatika, kwa kawaida mtu hupoteza kabisa uwezo wa kuhisi hisia katika maeneo yaliyoathirika, ikiwemo hisia za ngono.

Hata hivyo, utafiti uliofanywa na Dkt Barry Komisaruk ulibaini kuwa wanawake waliokuwa na uti wa mgongo ulioathirika bado waliweza kufika kileleni

3. Kufika kileleni hupunguza dopamine na kuongeza testosterone

Unapofikia kileleni, mwili hutoa homoni na kemikali mbalimbali za neva. Inajulikana kwamba ubongo hutoa oxytocin, homoni inayohusishwa na kuimarisha ukaribu na uhusiano, wakati wa kufikia kileleni.

Hali hiyo pia inaweza kuongeza homoni ya dopamine

"Dopamine hufanya kazi kama kichocheo cha hamu na motisha," anaeleza Dkt Nicole Prause, mwanasayansi wa neva na mtafiti wa saikolojia ya mwitikio wa mwili na ngono katika Chuo Kikuu cha Michigan.

"Dopamine huongezeka wakati wa msisimko wa ngono, lakini hupungua baada ya kufikia kileleni. Hii ni kwa sababu mwili hutoa prolactin, ambayo huzuia dopamini. Prolactin hupunguza hamu ya kuendelea kufanya ngono na pia ndiyo sababu unaweza kuhisi uchovu baada ya kufanya ngono."

Hadithi nyingine kuhusu mshindo wa ngono ambayo mara nyingi huenezwa kana kwamba ni ukweli hasa na baadhi ya washawishi wa mitandaoni wanaohamasisha kujizuia kufanya ngono au kujichua ni kwamba kujichua na kumwaga manii hupunguza kiwango cha testosterone.

Baadhi yao hudai kwamba kujizuia kumwaga manii ni njia ya "kurudisha" nguvu za kiume, nidhamu na umakini. Hata hivyo, madai hayo hayana msingi wa kisayansi.

4. Kufikia kileleni kunaweza kupunguza maumivu kwa muda

Kufanya ngono na kufikia kileleni kunaweza kusaidia kupunguza maumivu kwa muda na kwa kiwango kikubwa.

Moja ya vitu vinavyotolewa na mwili wakati wa kufikia kileleni ni vasoactive intestinal peptide (VIP).

"Katika utafiti wangu, tuligundua kwamba wakati wa kufikia kileleni, neva ya nyonga hutoa peptidi ya vasoactive, ambayo hufanya kazi kama dawa kali ya kupunguza maumivu kwa kuzuia ishara za maumivu katika ubongo na uti wa mgongo," anaeleza Komisaruk.

5. Si kila kufikia kileleni huwa na hisia za raha

Kwa kawaida tunahusisha upeo wa ngono na raha na starehe, lakini kwa baadhi ya watu, kufikia kileleni kunaweza kuwa na maumivu.

"Hii inaweza kutokea kwa sababu mbalimbali," anaeleza Dkt Sara Nasserzadeh,

"Wakati wa mshindo, mwili hufanya mikazo. Ikiwa misuli ya nyonga au misuli ya coccygeal katika nyonga imekaza kupita kiasi, mikazo hiyo inaweza kuhisiwa kwa nguvu zaidi, na si lazima kila mara ilete raha.Hii inaweza kuwa dalili ya tatizo la kiafya lililopo, kama vile prostatitis, endometriosis au fibroids. Ikiwa maumivu haya yanaathiri maisha yako ya ngono, unapaswa kushauriana na daktari."

Nasserzadeh anaongeza kwamba baadhi ya maumivu yanayotokea baada ya kufanya ngono yanaweza kuwa ya kisaikolojia: "Kunaweza kuwa na sababu za kina za kihisia na kisaikolojia zinazokufanya uhisi maumivu baada ya ngono, ambazo zinaweza kuhusishwa na matukio ya awali ya kiwewe."

6. Baadhi ya dawa zinaweza kuzuia kabisa kufikia kileleni

Dawa zinazojulikana kama SSRIs (selective serotonin reuptake inhibitors), ambazo mara nyingi hutumika kutibu msongo wa mawazo na matatizo ya wasiwasi, zinaweza kusababisha mabadiliko ya muda katika utendaji wa ngono.

Hii hutokana na dawa za SSRI kuongeza kiwango cha serotonin mwilini, jambo ambalo huathiri kwa mfululizo homoni na kemikali nyingine za neva.

Dalili hizo huchangia kupungua kwa hamu ya ngono kwa ujumla na kufa ganzi katika sehemu za siri.

7. Msisimko wa ngono unaweza kusogeza viungo vya ndani

Ikiwa umewahi kuhisi kana kwamba viungo vyako vya ndani vimebadilisha nafasi baada ya kufanya ngono kwa nguvu au kwa muda mrefu, huenda hisia hiyo isiwe ya kufikirika.

Kwa wanawake, mchakato huu wakati wa msisimko wa ngono hujulikana kama "tenting", na hutokea ili kutoa nafasi zaidi kwa ajili ya kuingia kwa uume kwa kina zaidi.

"Unapokuwa umesisimuliwa na sehemu za siri za mwanamke kujaa damu, mfuko wa uzazi huinuka na shingo ya kizazi huvutika nyuma, hivyo kutengeneza nafasi zaidi," anaeleza Nasserzadeh.

8. Sokwe na nyani wengine hutumia 'vifaa' kuchochea msisimko

Lengo kuu la ngono ni uzazi, lakini binadamu si viumbe pekee wanaofanya ngono kwa ajili ya raha.

Pomboo aina ya bottlenose wameonekana kujichua, kushiriki ngono na wenzao wa jinsia moja na kufanya ngono isiyolenga uzazi.

Wakati huo huo, tafiti zilizofanywa kwa panya wa kike zimeonyesha kwamba hurudi mara kwa mara katika maeneo yanayohusishwa na kujamiiana, jambo linaloashiria kwamba tendo hilo linaweza kuwa na hisia ya raha.

Hata hivyo, ni wanyama wachache wenye tabia mbalimbali za ngono kama bonobo, aina ya nyani mkubwa ambaye ameonekana kutumia ngono kama nyenzo muhimu ya kijamii.

"Bonobo wana akili sana," anaeleza Komisaruk. "Tafiti zimeonyesha kwamba hutumia ngono kupunguza mvutano au kupatana baada ya kupigana.

"Pia tunaona bonobo wakiwa na mahusiano ya jinsia moja. Wana kiwango cha chini cha uzazi ikilinganishwa na baadhi ya nyani wengine, jambo linaloashiria kwamba kujamiiana hutumiwa kwa ajili ya raha au sababu nyingine mbali na kuzaa."

Wakati huo huo, vifaa vya kuchezea wakati wa ngono si vya binadamu pekee. Baadhi ya tafiti zimeonyesha kwamba nyani wa kike aina ya Japanese macaque hutumia vijiti, matawi madogo na mawe kuchochea msisimuko.

"Wanyama wanaojihusisha na tabia hizi wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipa raha na kujizawadia, " anasema Komisaruk.

9. Nguruwe wana mfumo wa kipekee wa kisaikolojia wakati wa ngono

Si nyani pekee wanaohusika katika tabia za kuvutia za ngono, tabia za nguruwe dume na jike pia zimewavutia watafiti.

Nguruwe wana mshindo wa ngono wa muda mrefu sana. Kwa wastani, nguruwe dume mwenye uwezo mkubwa wa uzazi anaweza kutoa manii mfululizo kwa muda wa dakika tano hadi saba, na kutoa takriban mililita 200 hadi 250 za manii katika kila tendo.

Nguruwe wana rekodi ya Guinness kwa kuwa miongoni mwa wanyama wenye mshindo mrefu zaidi, ambao unaweza kudumu hadi dakika 30.

Hata hivyo, kinachovutia zaidi ni mchakato wa kujamiiana kati ya nguruwe dume na jike.

"Nguruwe dume anapomng'ata au kumkazia meno nguruwe jike aliye katika kipindi cha joto, husababisha jike huyo kutulia kabisa na kushindwa kusogea.

10. Kufikia kileleni kunaweza kuathiri hali yako ya ufahamu

Hata kama wewe si nguruwe, si jambo la kushangaza kuhisi kama umechanganyikiwa au umepigwa na bumbuazi baada ya kufikia kileleni, kwa sababu ubongo huwa umepitia tukio kubwa la kinyurolojia.

Kwa mfano, unapofikia kileleni, tafiti zimeonyesha kwamba sehemu ya orbitofrontal cortex inayohusika na kufanya maamuzi hupunguza shughuli zake. Hali hii inaweza kukufanya uhisi kama umepoteza udhibiti kwa muda.

Hii inaweza kusababisha hisia au matendo yanayoonekana kutokea bila hiari, kama vile kupiga mayowe kwa sauti kubwa kutokana na raha unapokuwa katika kilele cha tendo.