Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, CBS yachapisha picha mpya za uharibifu katika kambi za Marekani Mashariki ya Kati

Picha hizo za kipekee zinaonyesha uharibifu mkubwa katika baadhi ya kambi za kijeshi za Marekani, ambapo majengo, magari ya kijeshi na miundombinu mingine iliharibiwa katika mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. Raia wa Uingereza atekwa nchini Malawi

    Polisi nchini Malawi wanaendelea na uchunguzi wa tukio la kutekwa nyara kwa raia wa Uingereza katika mji wa Blantyre, kitovu cha biashara cha nchi hiyo.

    Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, Nusrat Osman, mwenye umri wa miaka 47, alitekwa na watu wanne majira ya mchana siku ya Ijumaa. Inadaiwa kuwa watekaji hao walikuwa wakitumia gari la rangi ya kijivu aina ya Nissan Dualis.

    Mamlaka zimeahidi kutoa zawadi ya zaidi ya dola 17,000 za Marekani (takriban pauni 12,600) kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa za kuaminika zitakazosaidia kupatikana kwa Osman na kuwafikisha wahusika wa tukio hilo mbele ya sheria.

    Osman, ambaye ni mama wa watoto wawili wadogo, anaripotiwa kufanya kazi katika kampuni ya ukaguzi wa hesabu nchini Malawi.

    Vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti kuwa mume wake ameeleza hofu na majonzi makubwa kufuatia kutoweka kwake.

    "Sijui alipo wala hali yake ikoje. Mke wangu ni mkaguzi wa hesabu na sina ugomvi na mtu yeyote," alinukuliwa akisema na gazeti la Nyasa Times.

    Polisi wamesema hadi sasa chanzo cha utekaji huo hakijafahamika. Pia wameeleza kuwa watekaji bado hawajawasiliana na familia ya Osman wala mamlaka za serikali.

    Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imesema inafahamu taarifa za kutekwa kwa raia wake nchini Malawi na inaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka za Malawi katika kufuatilia tukio hilo.

  2. Marekani yabana viza za maafisa wa Afrika Kusini kwa madai ya ubaguzi dhidi ya wazungu

    Marekani imetangaza vikwazo vya usafiri dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuwabagua wazungu walio wachache nchini Afrika Kusini, katika hatua mpya ambayo huenda ikachangia kuongezeka kwa mvutano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

    Utawala wa Rais Donald Trump umeendelea kuikosoa Afrika Kusini kuhusu sera zake za kushughulikia ukosefu wa usawa wa rangi, ukidai kuwa baadhi ya hatua hizo zinawabagua Waafrikaans, ambao wengi wao ni wazao wa walowezi wa Uholanzi na Ufaransa.

    Hata hivyo, serikali ya Afrika Kusini imekuwa ikikanusha mara kwa mara tuhuma hizo.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema serikali ya Afrika Kusini haijatoa majibu ya kuridhisha kuhusu wasiwasi uliowasilishwa hapo awali na Washington.

    Uhusiano kati ya Marekani na Afrika Kusini umeendelea kudorora tangu Donald Trump alipoingia tena madarakani mapema mwaka jana.

    Utawala wake umepunguza baadhi ya misaada kwa Afrika Kusini, kumfukuza balozi wa nchi hiyo nchini Marekani, na kutangaza kuwa utawapa hifadhi baadhi ya wazungu wa Afrika Kusini wanaodai kukabiliwa na mateso nchini mwao.

    Hata hivyo, serikali ya Afrika Kusini imeendelea kupinga madai kuwa inawalenga au kuwatesa raia weupe, pamoja na tuhuma za kunyang'anya ardhi yao.

    Imeeleza kuwa madai ya kuwepo kwa kile kinachoitwa "mauaji ya kimbari dhidi ya wazungu" nchini humo yamepuuzwa na wataalamu na hayana msingi wowote.

    Hata hivyo, takwimu za hivi karibuni za uhalifu nchini Afrika Kusini hazioneshi kuwa wazungu wanakabiliwa na tishio kubwa la kuvamiwa ikilinganishwa na makundi mengine ya wananchi nchini humo.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Zaidi ya Wajapani 100,000 wafikisha umri wa miaka 100

    Idadi ya watu walio na umri wa miaka 100 au zaidi nchini Japan imevuka watu 100,000 kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo, kwa mujibu wa Wizara ya Afya.

    Takwimu zinaonyesha kuwa Japan sasa ina watu 107,677 waliofikisha umri wa miaka 100 au zaidi, idadi kubwa zaidi duniani. Kati yao, asilimia 88 ni wanawake.

    Mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi nchini humo ni Kishimoto Fuyo mwenye miaka 114 kutoka mji wa Kyoto, huku mwanaume mwenye umri mkubwa zaidi akiwa Kato Hikaru, mwenye miaka 112 kutoka Kumamoto.

    Waziri wa Afya, Kenichiro Ueno, alisema anafurahishwa na ukweli kwamba watu wengi zaidi wanaishi maisha marefu, yenye afya njema na yenye shughuli za kujenga jamii. Alieleza kuwa maendeleo katika sekta za tiba na teknolojia yamechangia ongezeko hilo.

    Hata hivyo, alionya kuwa kuongezeka kwa idadi ya wazee kunaleta changamoto kwa mfumo wa hifadhi ya jamii na huduma za ustawi wa wananchi.

    Wataalamu wanasema maisha marefu ya Wajapani yanachangiwa na sababu kadhaa, ikiwemo lishe bora na mtindo wa maisha unaohusisha shughuli za mwili. Mlo wa kawaida nchini humo unajumuisha samaki, mboga na wali, huku ukiwa na kiwango kidogo cha mafuta ikilinganishwa na nchi nyingi za Magharibi.

    Aidha, watu wengi wazee nchini Japan huendelea kutembea kwa miguu, kutumia usafiri wa umma, kuendesha baiskeli na kufanya mazoezi mepesi ya kujinyoosha.

    Japan imekuwa ikikabiliwa na ongezeko la idadi ya wazee kwa miaka mingi. Katika ishara ya mabadiliko hayo ya demografia, mauzo ya nepi za watu wazima yamekuwa yakizidi yale ya nepi za watoto kwa zaidi ya muongo mmoja.

    Soma zaidi:

  4. Lissu apendekezwa kuwania Tuzo ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Ulaya

    Kundi la Chama cha Watu wa Ulaya (EPP) katika Bunge la Ulaya limemteua mwanasheria, mwanaharakati wa haki za binadamu na mwanasiasa wa Tanzania, Tundu Lissu, kuwa miongoni mwa wanaowania Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo.

    Katika taarifa yake, EPP ilisema uteuzi wa Lissu unatambua mchango wake katika kutetea demokrasia, utawala wa sheria na haki za msingi za raia, licha ya changamoto mbalimbali za kisiasa na binafsi alizokumbana nazo kwa miaka kadhaa.

    Kundi hilo lilikumbusha kuwa Lissu alinusurika jaribio la mauaji mwaka 2017 kabla ya kurejea Tanzania kuendelea na kampeni za kudai mageuzi ya kidemokrasia. EPP ilieleza kuwa baadaye alikabiliwa na kukamatwa, mashtaka ya uhaini na kuzuiwa kushiriki uchaguzi wa urais wa mwaka 2025, huku chama chake kikiondolewa kwenye mchakato wa uchaguzi.

    Kwa mujibu wa EPP, matukio hayo yanaibua maswali kuhusu hali ya ushindani wa kisiasa na demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania.

    Kundi hilo lilisema Lissu anaashiria ujasiri, msimamo wa kidemokrasia na dhamira ya kutetea uhuru wa kisiasa, likiongeza kuwa uteuzi wake unaonyesha mshikamano wa Ulaya na watu wanaopigania demokrasia ya kikatiba na uhuru wa kisiasa barani Afrika pamoja na nchi washirika wa Umoja wa Ulaya.

    Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo ndiyo tuzo ya juu zaidi inayotolewa na Umoja wa Ulaya (EU) kwa watu au makundi yaliyotoa mchango mkubwa katika utetezi wa haki za binadamu na uhuru wa msingi duniani.

    Maelezo zaidi:

  5. Edward Rukidi kutawazwa Mfalme wa Tooro Septemba 29

    Mwanamfalme Edward Rukidi Kijanangoma, ambaye hivi karibuni alitangazwa kuwa mfalme mpya wa Ufalme wa Tooro magharibi mwa Uganda, anatarajiwa kutawazwa rasmi Septemba 29, 2026.

    Hatua hiyo inafuatia kuidhinishwa kwake na Baraza Kuu la Kifalme la Tooro baada ya kutambulishwa kama mrithi wa marehemu Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi IV.

    Hata hivyo, uteuzi wake umeibua mvutano ndani ya familia ya kifalme kuhusu suala la urithi wa kiti cha enzi. Baadhi ya wanafamilia wa karibu wa marehemu mfalme, akiwemo mama yake na dada yake, wamepinga uamuzi huo.

    Wanaopinga uteuzi huo wanadai kuwa mtoto wa marehemu mfalme ndiye anayestahili kurithi ufalme huo kwa mujibu wa wosia wa marehemu. Hata hivyo, mtoto huyo anayehusishwa na madai hayo hajawahi kutambulishwa rasmi mbele ya taasisi za ufalme.

    Mvutano huo umeendelea hata baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Uganda kuripotiwa kuishauri serikali kuzingatia matakwa ya wosia wa marehemu mfalme katika mchakato wa kumpata mrithi. Lakini viongozi wa ukoo wa kifalme walikataa msimamo huo, wakisisitiza kuwa masuala ya urithi wa ufalme yanapaswa kuamuliwa kwa kuzingatia taratibu na mila za ufalme, si kwa maelekezo ya serikali.

    Licha ya upinzani huo, viongozi wa ukoo wa kifalme wameendelea na maandalizi ya sherehe ya kutawazwa kwa Prince Edward kama ilivyopangwa.

    Wakati huohuo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda (UPDF), Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, amemuunga mkono hadharani Prince Edward Rukidi Kijanangoma, akimtaja kuwa mrithi halali wa marehemu Mfalme Oyo.

  6. Tetesi za Soka Ulaya Jumatano: Barcelona yawanyatia Kane & Haaland

    Barcelona inaendelea kutathmini chaguo mbalimbali ili kuimarisha safu yao ya mashambulizi, huku majina ya Harry Kane wa Bayern Munich na Erling Haaland wa Manchester City yakitajwa kama mbadala endapo mpango wa kumsajili Julian Alvarez wa Atletico Madrid hautafanikiwa.

    Bayern Munich inatajwa kumfuatilia mshambuliaji wa kimataifa wa Ujerumani Nick Woltemade, anayemilikiwa na Newcastle United lakini anayekipiga kwa mkopo Juventus. Mabingwa hao wa Bundesliga wanamwona kama chaguo la baadaye la kuziba nafasi ya Kane.

    Nchini England, Manchester United wamefufua nia yao ya kumsajili beki wa Everton Jarrad Branthwaite, baada ya mchezaji huyo kurejea uwanjani kufuatia kipindi cha majeraha.

    Kwa upande wa vijana, Arsenal wameonyesha kuvutiwa na winga chipukizi wa Liverpool Rio Ngumoha, mwenye umri wa miaka 18. Hata hivyo, Liverpool wanaripotiwa kufanya kila juhudi kuhakikisha wanamfunga kwa mkataba mpya wa muda mrefu.

    Tottenham Hotspur nao bado hawajakata tamaa katika harakati za kumsajili kiungo wa Nottingham Forest Morgan Gibbs-White. Spurs walijaribu kumpata mwaka 2025, lakini Forest wameweka wazi kuwa hawana mpango wa kuuza nyota huyo.

    Naye mshambuliaji wa Real Madrid Endrick anaweza kuwa mmoja wa majina makubwa yatakayopatikana katika dirisha la usajili la Januari. Manchester United ni miongoni mwa klabu zinazofuatilia kwa karibu maendeleo ya Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 20.

    Kwingineko, kiungo wa Hispania Rodri amefichua kuwa alimwasiliana na kocha wa Real Madrid Jose Mourinho kumshukuru kwa hamu yake ya kutaka kumsajili, kabla ya yeye kuamua kujiunga na Barcelona akitokea Manchester City majira ya joto yaliyopita.

    Barcelona pia wanaendelea na mipango ya kuhifadhi nyota wao muhimu, huku mkurugenzi wa michezo Deco akifanya mazungumzo na mshambuliaji wa Brazil Raphinha kuhusu kuongeza muda wa mkataba wake, ambao kwa sasa unamalizika mwaka 2028.

    Nchini Italia, AC Milan wana nafasi ya kugeuza uhamisho wa mkopo wa mshambuliaji wa England Omari Hutchinson kutoka Nottingham Forest kuwa wa kudumu, kwa ada inayokadiriwa kufikia euro milioni 50.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Wasanii wasusia tamasha la Ed Sheeran kupinga kuondolewa kwa Macklemore.

    Wasanii wote waliokuwa wamepangwa kutumbuiza katika tamasha la Ed Sheeran nchini Marekani wamejiondoa, wakipinga uamuzi wa kuondolewa kwa rapa Macklemore kufuatia kauli zake za kuunga mkono Palestina alizotoa jukwaani.

    Miongoni mwa waliojiondoa ni Finneas, kaka wa mwimbaji nyota Billie Eilish, ambaye alisema wasanii hawapaswi kuzuiwa au kunyamazishwa wanapotumia majukwaa yao kuzungumzia mateso ya watu wanaokandamizwa.

    Pia waliojitenga na ziara hiyo ni mwimbaji na mtunzi wa nyimbo kutoka Ireland Aaron Rowe, bendi ya Denmark Lukas Graham, pamoja na bendi ya muziki wa folk ya Ireland Beoga, ambayo imekuwa ikitumbuiza pamoja na Sheeran katika maonesho ya ziara hiyo.

    Hatua ya wasanii hao ilikuja saa chache baada ya Sheeran kueleza hadharani kuwa hatahusika katika mjadala kuhusu vita vya Gaza. Mwimbaji huyo alisisitiza kuwa hakuwa na nafasi yoyote katika uamuzi wa kumuondoa Macklemore.

    Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye Instagram, Sheeran alisema kuondolewa kwa Macklemore kulikuwa uamuzi wa waandaaji wa ziara, na si wake binafsi.

    Aliongeza kuwa hangeweza kufuta au kuondoka kwenye ziara hiyo kwa sababu ya wajibu wake kwa mashabiki, wafanyakazi na wanamuziki wanaotegemea maonesho hayo kwa ajira na kipato.

    Mapema mwezi huu, Macklemore, ambaye jina lake halisi ni Benjamin Haggerty, alitoa wito wa "Palestina Huru" na kuonyesha picha za uharibifu wa Gaza wakati wa maonesho mawili ya muziki yaliyofanyika New Jersey.

    Kauli hizo zilisababisha ukosoaji kutoka kwa baadhi ya makundi ya Wayahudi. Baada ya hapo, baadhi ya kumbi za maonesho ziliripotiwa kuweka shinikizo kwa waandaaji wa ziara hiyo, wakitaka rapa huyo aondolewe kwenye orodha ya watumbuizaji.

  8. Saudi Arabia yazuiwa droni ya Wahouthi karibu na Makka

    Vikosi vya ulinzi wa anga vya Saudi Arabia vimesema viliizuia na kuiangamiza droni iliyokuwa imerushwa na waasi wa Wahouthi kutoka Yemen kabla haijaingia katika eneo la anga lililowekewa marufuku ya kuruka ndege karibu na mji mtakatifu wa Makka.

    Kwa mujibu wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen, tukio hilo limetokea wakati wa ongezeko la mashambulizi ya makombora na droni yanayolenga maeneo mbalimbali ndani ya ufalme huo.

    Msemaji wa muungano huo, Turki al-Maliki, amesema katika taarifa kwamba hii ni mara ya pili kwa Wahouthi kujaribu kushambulia Makka. Alisema jaribio la kwanza lilitokea Julai 2017, wakati kombora la masafa marefu lilirushwa kuelekea eneo hilo.

    Wakati huohuo, tahadhari ya kiusalama ilitolewa kwa muda mfupi Jumanne, tarehe 15 Septemba, katika miji ya Makka, Jeddah na Taif. Hata hivyo, mamlaka za ulinzi wa raia baadaye zilitangaza kuwa hali ilikuwa salama na kwamba "hatari imedhibitiwa".

    Tahadhari hiyo iliyotolewa mjini Makka imezua taharuki, kwani mji huo haujawahi kushuhudia tukio la aina hiyo katika kipindi cha hivi karibuni cha mvutano na mashambulizi kati ya Wahouthi na Saudi Arabia.

    Siku moja kabla, mashambulizi ya makombora na droni yaliyotekelezwa na Wahouthi dhidi ya miji mitatu nchini Saudi Arabia yaliwajeruhi raia 13, kwa mujibu wa muungano huo. Muungano huo pia ulisema nyumba saba na magari mawili yaliharibiwa katika mashambulizi hayo.

    Wahouthi hawajatoa kauli yoyote kuhusiana na madai hayo ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.

    Soma zaidi:

  9. CBS yachapisha picha za uharibifu katika kambi za Marekani

    Mtandao wa habari wa Marekani, CBS, ambao ni mshirika wa BBC nchini humo, umechapisha kwa mara ya kwanza picha mpya zinazoonyesha kile unachosema ni uharibifu mkubwa uliosababishwa na mashambulizi ya Iran dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani Mashariki ya Kati.

    Kwa mujibu wa CBS, picha hizo za kipekee zinaonyesha uharibifu mkubwa katika baadhi ya kambi za kijeshi za Marekani, ambapo majengo, magari ya kijeshi na miundombinu mingine iliharibiwa katika mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani.

    Mmoja wa wanajeshi walioko katika kambi hizo alinukuliwa na CBS akisema kuwa ukubwa wa uharibifu uliosababishwa na mashambulizi hayo haujawekwa wazi kikamilifu kwa umma wa Marekani.

    "Hii ni hasara kubwa kwa kambi zetu ambayo wananchi wa Marekani hawajafahamishwa kikamilifu. Tumekuwa tukikabili mashambulizi mfululizo huku tukionekana kutokuwa na uwezo wa kujibu kwa ufanisi," alisema.

    Miongoni mwa picha zilizosambazwa ni moja inayodaiwa kupigwa katika Kambi ya Jeshi la Anga ya Prince Sultan nchini Saudi Arabia. Picha hiyo inaonyesha kile kinachodaiwa kuwa athari ya shambulio la moja kwa moja kwenye sehemu ya nyuma ya ndege ya kijeshi ya Boeing A-3 Sentry yenye injini nne.

    Katika picha hiyo, mkia wa ndege unaonekana kuwa umetenganishwa na sehemu kuu ya mwili wa ndege, huku mabaki yake yakionyesha dalili za kuungua. Uharibifu pia unaonekana kuathiri sehemu iliyobeba mfumo wa rada unaozunguka, unaotumiwa kufuatilia na kukusanya taarifa kuhusu shughuli za angani.

    Maelezo zaidi:

  10. Natumai hujambo.