Siri ya Kenya kupata nafasi ya kuandaa Mashindano ya Dunia ya Riadha 2029

    • Author, Rob Stevens
    • Nafasi, BBC Sport Africa
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Rais wa Kenya, William Ruto, amesema kuwa Mashindano ya Dunia ya Riadha "yanarudi nyumbani", baada ya Nairobi kuchaguliwa kuandika historia kama jiji la kwanza barani Afrika kuandaa tukio hilo kubwa mwaka 2029.

"Ruto alisema ushindi huo ni 'ushindi kwa vizazi vya wanariadha' ambao wameifanya Kenya kuwa kinara wa ubora katika mbio za uwanjani na barabarani.

Jiji la Nairobi lilizishinda London ya Uingereza na Rome ya Italia katika kinyang'anyiro cha kupewa haki za kuandaa mashindano hayo, huku Munich ya Ujerumani ikichaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2031.

Baada ya kupoteza zabuni ya kuandaa Mashindano ya Dunia ya 2025 yaliyokwenda Tokyo, Kenya ilirejea kwa nguvu zaidi na safari hii ikafanikiwa kuzizidi nguvu nchi zake washindani kutoka Ulaya.

Mchezo uliokita mizizi katika maisha ya Wakenya

Rais wa Shirikisho la Riadha Duniani, Lord Coe, alipotangaza uamuzi huo mjini Budapest siku ya Jumanne, alisema ombi la Kenya lilikuwa na hoja nzito na pia lililogusa hisia.

Kenya, taifa la Afrika Mashariki linalotamba duniani kwa mafanikio ya riadha, ndiyo nchi ya pili iliyofanikiwa zaidi katika historia ya Mashindano ya Dunia ya Riadha, ikiwa imekusanya medali 72 za dhahabu, ikitanguliwa na Marekani pekee.

Mafanikio mengi hayo, pamoja na medali 38 za dhahabu za Olimpiki, yamepatikana katika mbio za masafa ya kati na marefu.

Lord Coe alisema riadha "imejikita katika maisha ya taifa hilo", na kwamba Wakenya wamechangia "kuandika historia" ya mchezo huo.

Aliwataja kwa majina wanariadha kadhaa, akiwemo bingwa wa Olimpiki mara mbili Eliud Kipchoge, ambaye alihusika katika kampeni ya kuishawishi World Athletics kuipa Kenya nafasi hiyo; David Rudisha, anayeshikilia rekodi ya dunia ya mbio za mita 800 kwa wanaume; na Faith Kipyegon, mshindi wa medali nyingi za dunia na Olimpiki.

Shauku kubwa ya Wakenya kwa riadha pia ni miongoni mwa mambo yanayoipa Kenya nguvu

Kwa mujibu wa utafiti wa Rais wa Shirikisho la Riadha Duniani, takriban asilimia 68 ya Wakenya waliohojiwa walisema wana shauku kubwa ya kufuatilia riadha, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 39 duniani.

Riadha ni mchezo wa pili unaofuatiliwa zaidi nchini Kenya baada ya soka. Katika tathmini yake ya kurasa za mitandao ya kijamii, Shirikisho hilo lilibaini kuwa Kenya ilikuwa nchi ya nne duniani kwa idadi kubwa ya wafuasi.

Safari ya kuandaa Mashindano ya Dunia

Zabuni ya awali ya Kenya kuandaa mashindano ya mwaka 2025 ilikwama kwa kiasi kikubwa kutokana na changamoto za miundombinu na vifaa vya michezo nchini.

Safari hii, Uwanja wa Kasarani utafanyiwa ukarabati mkubwa wa miundombinu kabla ya wanariadha bora duniani kuwasili Nairobi.

Uwanja huo wenye uwezo wa kuwa na watazamaji 48,000 pia utatumika Kenya itakapokuwa mwenyeji mwenza wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027, litakalofanyika Juni na Julai mwakani pamoja na Tanzania na Uganda.

Tulijifunza kutokana na zabuni ya mwaka 2025 kwa sababu kulikuwa na maeneo ambayo hatukufanya vizuri," Barnaba Korir, aliyeshiriki katika maandalizi ya zabuni iliyofanikiwa, aliiambia BBC World Service.

"Kutokana na hilo, tuliweza kuyafanyia maboresho maeneo hayo."

"Ninafurahi kwamba miundombinu ambayo tayari tumeijenga pia itafikia viwango ambavyo tumeviona katika maeneo mbalimbali duniani."

Upatikanaji wa hoteli hauonekani kuwa tatizo, kwani Nairobi mara kwa mara huwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kimataifa.

"Kenya pia inajulikana kwa sekta yake ya utalii na ukarimu," Elijah Mwangi, Katibu Mkuu katika Idara ya Michezo, aliiambia BBC.

Tuna mbuga ya wanyama ndani ya jiji lenyewe, hivyo tunasubiri kwa hamu kuwakaribisha wageni wote."

Rais Ruto alitoa dhamana za kifedha na kiusalama zilizohitajika ili Kenya ipewe nafasi ya kuwa mwenyeji wa Mashindano hayo.

Tunawashukuru Shirikisho la Riadha Duniani kwa imani waliyoweka kwa Kenya," Ruto alisema.

Tutaitunza imani hiyo kwa kuhakikisha tunaandaa mashindano yatakayokumbukwa, yanayostahili wanariadha wetu, nchi yetu na bara letu.

Kenya yaweka Afrika katikati ya jukwaa la riadha duniani

Mwanariadha wa mbio fupi wa Kenya, Ferdinand Omanyala, aliyepigwa picha akishiriki mashindano katika Uwanja wa Kasarani mwaka 2023, alisema imekuwa "ndoto ya muda mrefu" kwake kuiona Kenya ikiandaa mashindano makubwa ya kimataifa.

Lord Coe alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Riadha Duniani, ambalo wakati huo lilijulikana kama IAAF, mwaka 2015 na ameahidi kuendelea kukuza riadha duniani kote.

Katika kipindi chake kama rais, Mashindano ya Dunia ya Riadha yamefanyika Qatar mwaka 2019, Marekani mwaka 2022 na Tokyo, huku Beijing, China, ikitarajiwa kuwa mwenyeji mwaka 2027.

Kenya imewahi kuandaa kwa mafanikio mashindano ya vijana mjini Nairobi na Mashindano ya Dunia ya Riadha za Nchi Kavu mjini Mombasa. Aidha, Mashindano ya Dunia ya Relay yalifanyika Gaborone, mji mkuu wa Botswana, mnamo mwezi Mei.

Huku muhula wa tatu wa Coe ukitarajiwa kumalizika mwakani, mmoja wa maafisa walioshiriki katika zabuni ya Kenya alisema kabla ya kutangazwa kwa mwenyeji kwamba haikuwa rahisi kufikiria Nairobi ikikosa nafasi hiyo.

"Kutokana na uamuzi huu, tunaendelea kutekeleza dhamira yetu ya kukuza riadha duniani kote," Coe alisema.

Ilikuwa muhimu Mashindano ya Dunia ya Riadha kufanyika barani Afrika wakati ambapo tulikuwa na mwenyeji anayefaa, zabuni yenye ushindani na mazingira stahiki.

Coe alisifu "ubora, dhamira na kujitolea" kwa miji yote minne iliyowania nafasi hiyo.

London, Munich na Roma zote zimewahi kuwa wenyeji wa Michezo ya Olimpiki. London pia iliandaa Mashindano ya Dunia ya Riadha mwaka 2017, lakini nafasi ya kufungua ukurasa mpya kwa kupeleka mashindano hayo barani Afrika ilionekana kuwa na mvuto mkubwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa UK Athletics, Jack Buckner, alisema timu yake "imekatishwa tamaa sana" baada ya London kukosa nafasi hiyo

Nini kinahitajika sasa?

Kenya sasa inakabiliwa na changamoto za maandalizi na uratibu katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, huku ikijiandaa kuandaa Mashindano ya Dunia ya Riadha kwa mara ya kwanza barani Afrika.

Huku Afcon 2027 ikikaribia, Nairobi itapata fursa ya kufanya majaribio ya jinsi ya kuwaingiza na kuwatoa mashabiki katika Uwanja wa Kasarani, uliopo takriban nusu saa kwa gari kutoka katikati ya jiji.

Uwanja huo hauna huduma ya usafiri wa reli, lakini Korir anasema maafisa wa Shirikisho la Riadha Duniani "waliridhishwa sana" na mpango wa Kenya wa usafiri.

Kulikuwa na matukio ya msongamano wakati Uwanja wa Kasarani ulipoandaa mechi za Kenya katika Mashindano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) mwaka jana, hali iliyosababisha idadi ya mashabiki kupunguzwa katika baadhi ya mechi.

Kuchelewa kwa maandalizi ya Afcon kumeibua wasiwasi, huku gharama zote za kuandaa Mashindano ya Dunia zikitarajiwa kugharamiwa na serikali ya Kenya.

Mwangi alisema kwa sasa serikali inakadiriwa kuchangia dola milioni 78 (£58.5m), huku mikataba ya udhamini pia ikitarajiwa kuchangia katika ufadhili wa mashindano hayo.

"Tumejiandaa kuhakikisha kwamba fedha zote zinazopaswa kulipwa zitalipwa kwa wakati unaostahili," aliongeza.

Msongamano wa mashabiki katika Uwanja wa Kasarani ulionekana wazi wakati wa baadhi ya mechi za Kenya katika Mashindano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024.

Uchaguzi mkuu wa Kenya unatarajiwa kufanyika mwaka ujao, lakini mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Dunia ya Riadha 2029, Jackson Tuwei Korir, amesema ana imani kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya maandalizi hayo zitaendelea kupatikana hata kama kutakuwa na mabadiliko ya uongozi wa kisiasa.

Korir amesema ahadi zilizotolewa na serikali ya sasa zina hadhi ya makubaliano ya kimataifa, na hivyo zinapaswa kuheshimiwa na serikali yoyote itakayochukua madaraka baada ya uchaguzi.

Hata hivyo, changamoto si fedha pekee. Waandalizi pia wanapaswa kupata uwiano kati ya kuweka bei za tiketi zinazoweza kufikiwa na wananchi wengi na kuhakikisha viwanja vinajaa watazamaji wakati wa mashindano.

Uzoefu wa mashindano yaliyopita unaonyesha ugumu wa kufikia lengo hilo. Katika Mashindano ya Dunia ya Riadha kwa Vijana chini ya umri wa miaka 18 yaliyofanyika Nairobi mwaka 2017, tiketi za bei ya chini ziliuzwa kwa shilingi 200 za Kenya, lakini mahudhurio yalibaki chini hadi pale kiingilio kilipofanywa kuwa bure.

Kwa upande wake, Shirikisho la Riadha Duniani (World Athletics) linaamini kuwa kuandaa mashindano hayo Nairobi kutasaidia kueneza mchezo huo katika masoko mapya. Hata hivyo, kiwango cha mahudhurio kitakuwa mojawapo ya maeneo yatakayofuatiliwa kwa karibu, hasa baada ya viwanja kushuhudia idadi ndogo ya watazamaji katika baadhi ya vipindi vya Mashindano ya Dunia yaliyofanyika Doha mwaka 2019.

Licha ya wasiwasi huo, Korir ana matumaini kuwa Uwanja wa Kasarani utajaa mashabiki katika kila siku ya mashindano, ikiwemo vipindi vya asubuhi, ikiwa mauzo ya tiketi yataanza mapema na kampeni za uhamasishaji kuendeshwa kwa ufanisi.

Wakati huo huo, Kenya inaendelea kukabiliwa na changamoto ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni. Katika miaka ya karibuni, wanariadha kadhaa kutoka taifa hilo wamefungiwa kwa kukiuka kanuni za kupambana na matumizi ya dawa hizo.

Kutokana na hali hiyo, Kenya itakuwa chini ya uangalizi mkubwa katika miaka ya maandalizi kuelekea 2029, ikilazimika kutimiza ahadi zake za maandalizi, kuhakikisha mashindano yanaendeshwa kwa ufanisi na kudumisha viwango vya juu vya uadilifu katika mchezo wa riadha.

Taarifa hii imeandaliwa kwa msaada wa taarifa kutoka kwa Ian Williams na Celestine Karoney.