Ubingwa umerudi senegal, lakini bomu jingine lalipuka! Morrocco watilia shaka uamuzi wa CAS!

Chanzo cha picha, Getty Images
Saa chache tu baada ya Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo, CAS, kutoa uamuzi uliorejesha ubingwa wa AFCON 2025 kwa Senegal, sasa Morocco wamefungua ukurasa mwingine wa mgogoro huu ambao tayari umeitikisa soka la Afrika!
Safari hii, mjadala hauhusu tena bao la Pape Gueye, penalti iliyokoswa na Brahim Diaz, wala kitendo cha wachezaji wa Senegal kutoka uwanjani wakati wa fainali iliyochezwa Januari 18 mwaka huu mjini Rabat.
Sasa macho yameelekezwa kwenye mchakato wa kisheria uliotumika kutoa uamuzi huo, baada ya Shirikisho la Soka la Morocco, FRMF, kuibua madai ya kuwepo kwa mawasiliano ya simu kati ya rais wa Shirikisho la Soka la Senegal, Abdoulaye Fall, na mmoja wa wasuluhishi waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo.
Lakini madai haya yameibuka vipi, nani anahusika na je, yanaweza kubadilisha chochote kuhusu hukumu iliyotolewa leo?
Kwa mujibu wa taarifa za Shirikisho la Soka la Kifalme la Morocco (FRMF), Morocco iliiarifu CAS kuhusu kile ilichokitaja kama tukio linalohitaji kuchunguzwa wakati kesi ya Senegal ikiwa bado inasubiri uamuzi.
Kwa mujibu wa madai hayo, Abdoulaye Fall, rais wa Shirikisho la Soka la Senegal, alidaiwa kuzungumza kwa simu siku ya Jumapili, Novemba 22, na Ulrich Haas, mtaalamu wa sheria kutoka Ujerumani aliyekuwa mmoja wa wasuluhishi watatu waliounda jopo la CAS lililosikiliza rufaa ya Senegal.
Hiyo ilikuwa takribani saa 48 kabla ya kutangazwa kwa hukumu ya kesi hiyo.
Morocco waliona kuwa madai hayo yalikuwa na uzito mkubwa, hasa kwa kuzingatia kwamba Haas alikuwa sehemu ya jopo lililopaswa kusikiliza hoja za pande zote mbili na kutoa uamuzi bila upendeleo.
Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kwamba madai hayo hayajathibitishwa kwa ushahidi huru. Reuters ilisema haikuweza kuthibitisha kama mawasiliano hayo yalifanyika wala kujua kilichozungumzwa.
Na sasa, nini kilitokea ndani ya CAS?
Morocco waliwasilisha pingamizi rasmi dhidi ya msuluhishi Ulrich Haas chini ya saa moja kabla ya kutangazwa kwa hukumu ya mwisho.
Pingamizi hilo lilifanyiwa mapitio na kamati ya CAS inayoshughulikia changamoto zinazowasilishwa dhidi ya wasuluhishi.
Hata hivyo, kamati hiyo iliona kuwa ushahidi uliokuwepo wakati huo haukutosha kuhalalisha kucheleweshwa kwa kutangazwa kwa uamuzi wa kesi hiyo.
Na hatimaye CAS ikatoa hukumu yake kwa kauli moja, ikibatilisha uamuzi wa bodi ya rufaa ya CAF na kurejesha matokeo ya fainali yaliyokuwa yameipa Senegal ushindi wa bao 1-0.
Lakini Morocco hawakuridhishwa na hatua hiyo.
Katika taarifa yake baada ya hukumu, Shirikisho la Soka la Morocco lilionyesha kushangazwa na kutoridhishwa na namna pingamizi lake lilivyoshughulikiwa.
FRMF ilisema kuwa inatilia shaka uadilifu na uaminifu wa mchakato wa usuluhishi, hasa kutokana na mawasiliano hayo yanayodaiwa kufanyika kati ya Fall na Haas.
Morocco pia ilipinga namna CAS ilivyotafsiri kanuni za mashindano kuhusu timu zinazotoka uwanjani bila ruhusa ya mwamuzi.
Shirikisho hilo likatangaza kuwa litachukua hatua zote za kisheria zinazopatikana ili kupinga uamuzi wa CAS.
Lakini upande wa Senegal umejibu nini?

Chanzo cha picha, Supersport
Shirikisho la Soka la Senegal limekanusha vikali madai hayo.
Msemaji wake aliiambia Reuters kwamba madai hayo si ya kweli, akisisitiza kuwa hakukuwa na mawasiliano yoyote ya simu kati ya Fall na msuluhishi huyo siku ya Jumapili au siku nyingine yoyote.
Na si Senegal pekee waliokanusha.
CAS yenyewe ilieleza kuwa Ulrich Haas amekanusha vikali kuwahi kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na upande wowote uliohusika katika kesi hiyo.
Hivyo, kwa sasa kuna madai ya Morocco, kukanusha kwa Senegal na msimamo wa msuluhishi mwenyewe. Hakuna uthibitisho huru uliowekwa hadharani unaothibitisha kwamba mawasiliano hayo yalifanyika.
Sasa swali kubwa ni je, Morocco wanaweza kuufuta tena ubingwa wa Senegal?
Kisheria, Morocco wanaweza kujaribu kupeleka pingamizi lao katika Mahakama Kuu ya Shirikisho la Uswisi, Swiss Federal Supreme Court, ambayo ndiyo mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza maombi ya kubatilisha tuzo za usuluhishi za CAS.
Hata hivyo, kuna jambo muhimu: mahakama hiyo haisikilizi upya kesi kama ilivyokuwa katika CAS, wala haibadilishi matokeo kwa sababu tu upande mmoja haujaridhishwa na hukumu.
Inahitaji kuwepo kwa sababu maalumu za kisheria, kama vile dosari kubwa katika utaratibu wa usuluhishi, suala la mamlaka ya mahakama au ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa kwa upande husika.
Kwa hiyo, Morocco italazimika kuwasilisha hoja na ushahidi unaokidhi vigezo hivyo vya kisheria.
Wakati huo huo, CAF imesema inaheshimu uamuzi wa CAS na itachukua hatua zinazohitajika kuutekeleza.
Hii ina maana kwamba kwa sasa Senegal wanaendelea kutambuliwa kama mabingwa wa AFCON 2025, huku uwezekano wa Morocco kuanzisha hatua nyingine za kisheria ukiwa bado ni suala la kufuatilia.
Na hapo ndipo tunapojiuliza: Je, madai haya mapya yataishia kuwa sehemu nyingine ya mgogoro wa AFCON 2025, au yatafungua kesi nyingine itakayoweza kuhoji uhalali wa mchakato uliorejesha ubingwa kwa Senegal?
Jambo moja ni wazi: baada ya vita ya uwanjani, vita ya CAF na vita ya CAS, sasa macho yanaelekezwa kwenye hatua inayofuata ya kisheria.
Senegal wameurejesha ubingwa wao, lakini Morocco bado hawajafunga ukurasa wa mgogoro huu!






























