Zelensky athibitisha Ukraine kushambulia meli za Urusi karibu na Libya
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amethibitisha kuwa vikosi vya nchi hiyo vilishambulia meli mbili za Urusi karibu na pwani ya Libya kwa kutumia ndege zisizo na rubani za majini.
Muhtasari
- Mhubiri maarufu wa Zimbabwe akamatwa kwa tuhuma za unyanyasaji wa kingono
- Uingereza kuandaa Kombe la Dunia la Wanawake 2035
- Hisa za Nvidia zaongezeka kwa kasi baada ya Jensen Huang kurejeshwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji
- Mwili wa Angel Wariael wafikishwa nyumbani kwao Arusha
- Jensen Huang arejeshwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Nvidia
- Samia: Takwimu za vifo vya wajawazito Afrika zinatisha
- Waziri Mkuu wa Qatar kukutana na Marco Rubio Washington
- Korea Kusini yasema uwepo wa wanajeshi wake Ghuba ya Aden haumaanishi inashiriki vita dhidi ya Iran
- Moto Nungwi: Wizara ya Utalii na Urithi Zanzibar yasema jiko la kuokea mikate huenda ndiyo chanzo
- FBI yachunguza uwezekano kwamba ilidukuliwa kanzidata yake yenye taarifa za uhalifu
- Pochettino aanza vibaya, akabiliana na ukubwa wa changamoto Manchester United
- Zelensky athibitisha Ukraine kushambulia meli za Urusi karibu na Libya
- Mlango wa Hormuz utafunguliwa iwapo Marekani itatekeleza ahadi zake - Iran
- Trump aunga mkono kurejea kwa Jensen Huang katika kampuni ya Nvidia
- AFCON 2027: Viwanja sita vyateuliwa kuandaa mechi Kenya, Tanzania na Uganda
- Mataifa yashindwa kufikia makubaliano katika mkutano wa COP31
- Trump aituhumu Iran kwa kuongeza mashambulizi ya droni
- Mvulana wa miaka saba aokolewa baada ya saa 14 chini ya vifusi Ukraine
- Meli ya Urusi yashambuliwa kwa droni katika bandari ya Libya
- Tetesi za usajili Ulaya: Manchester United yamtaka Ivan Toney
- Rais Ruto akutana na Rais Tshisekedi
Moja kwa moja
Beldeen Waliaula & Faidha Ngaga
Mhubiri maarufu wa Zimbabwe akamatwa kwa tuhuma za unyanyasaji wa kingono

Chanzo cha picha, H-Metro
Maelezo ya picha, Uebert Angel bado yuko polisi kufuatia kukamatwa kwake mwishoni mwa juma Mhubiri maarufu nchini Zimbabwe amekamatwa kwa tuhuma za makosa ya kingono, polisi nchini humo wamethibitisha.
Uebert Angel, ambaye anaongoza kanisa la kimataifa la Kipentekoste lenye matawi katika mataifa mbalimbali duniani, alikamatwa Jumapili wakati wa ibada ya kanisa jijini Harare. Picha na video za tukio hilo la kukamatwa kwake zimekuwa zikisambaa mitandaoni.
Katika moja ya video hizo, msafara wa magari unaonekana ukimsindikiza mhubiri huyo, ambaye anajitambulisha kama nabii, akiwa ameketi nyuma ya gari la polisi huku akizungukwa na maafisa wa polisi waliokuwa na silaha.
Angel, mwanzilishi mwenye utata wa kanisa la Spirit Embassy, aliteuliwa mwaka 2021 kuwa mjumbe maalumu wa rais wa Zimbabwe na balozi maalumu anayeshughulikia masuala ya Ulaya na Amerika.
Hadi sasa, hajatoa tamko lolote kuhusu tuhuma zinazomkabili.
Mwaka 2023, alijikuta kwenye vichwa vya habari baada ya uchunguzi wa siri uliofanywa na kituo cha televisheni cha Al Jazeera kudai kuwa alitoa pendekezo la kutumia hadhi yake ya kidiplomasia kufanikisha utakatishaji wa kiasi kikubwa cha fedha kupitia mpango wa magendo ya dhahabu nchini humo.
Kwa mujibu wa kituo hicho chenye makao yake makuu nchini Qatar, Angel, mwenye umri wa miaka 48, aliwaambia waandishi wa habari waliofanya uchunguzi huo kwa kujificha kuwa mpango huo ulikuwa umeidhinishwa na Rais Emmerson Mnangagwa.
Polisi nchini Zimbabwe walitoa taarifa fupi kuthibitisha kukamatwa kwake kwa tuhuma za unyanyasaji wa kingono na kufanya vitendo vya ngono kinyume cha sheria.
Mmoja wa washirika wake aliliambia kundi la waandishi wa habari kuwa Angel, ambaye ana uraia wa Uingereza na Zimbabwe, bado alikuwa mikononi mwa polisi na haikuwa wazi ni lini angefikishwa mahakamani.
"Inaweza kuwa mchana au kesho [Jumanne]. Bado tuko ndani ya muda unaoruhusiwa kisheria kwa ajili ya kufikishwa kwake mahakamani," alisema Profesa Lovemore Madhuku katika mahojiano na shirika la utangazaji la serikali la ZBC, katika kipande cha video kilichowekwa mtandaoni.
Hii si mara ya kwanza kwa mhubiri huyo maarufu kukabiliwa na tuhuma za tabia zisizofaa.
Ripoti iliyochapishwa mwaka 2021 na chombo cha habari cha mtandaoni cha nchini Zimbabwe, ZimLIVE, ilisema Angel alikuwa amewahi kukabiliwa na tuhuma za utovu wa maadili ya kingono kutoka kwa wanawake kadhaa, ambapo angalau watano kati yao walikuwa nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa chombo hicho cha habari wakati huo, mhubiri huyo amekanusha tuhuma hizo.
Kanisa lake lina matawi nchini Zimbabwe, Afrika Kusini na Uingereza. Pia anafahamika kwa uhusiano wake na wahubiri wengine maarufu, akiwemo mchungaji wa televisheni kutoka Malawi, Shepherd Bushiri.
Unaweza pia kusoma:
Uingereza kuandaa Kombe la Dunia la Wanawake 2035

Chanzo cha picha, Getty Images
Uingereza imethibitishwa kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia la Soka la Wanawake mwaka 2035, itakayoshirikisha timu 48 na jumla ya mechi 104 zitakazochezwa kwa siku 39.
Uamuzi huo umetangazwa katika mkutano maalumu wa FIFA uliofanyika kwa njia ya mtandao mjini Zurich, Uswisi, Jumatatu.
Michuano hiyo itakuwa tukio kubwa zaidi la mchezo mmoja kuwahi kufanyika nchini Uingereza, na pia Kombe la Dunia la FIFA la kwanza kuandaliwa nchini humo tangu mwaka 1966.
Zabuni ya Uingereza imependekeza viwanja 22 katika miji 16, vikiwemo viwanja 16 nchini England, vitatu Wales, viwili Scotland na kimoja Ireland Kaskazini. Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika katika majira ya kiangazi mwaka 2035.
Mashirikisho manne yatashirikiana kuandaa michuano hiyo ambayo ni Chama cha Soka cha England (FA), Chama cha Soka cha Ireland (Irish FA), Chama cha Soka cha Scotland (Scottish FA) na Chama cha Soka cha Wales (FA of Wales).
Zabuni hiyo iliwasilishwa kwa kaulimbiu ya “All Together” (Sote Pamoja), yenye dhamira ya kuwaunganisha watu kupitia soka, kuwawezesha wanawake na wasichana duniani kote na kuleta mabadiliko ya kudumu katika mchezo huo hata baada ya mwaka 2035.
Mbali na kukuza soka, mashindano hayo yanalenga kutoa jukwaa kubwa zaidi kuwahi kutolewa kwa michezo ya wanawake nchini Uingereza, kuendeleza usawa wa kijinsia katika michezo na jamii, pamoja na kuchochea ukuaji wa michezo ya wanawake kwa kizazi kijacho.
FIFA inatarajiwa kuthibitisha baadaye miji itakayokuwa mwenyeji, viwanja vitakavyotumika pamoja na vituo vya mazoezi ya timu zitakazoshiriki.
Unaweza pia kusoma:
Hisa za Nvidia zaongezeka kwa kasi baada ya Jensen Huang kurejeshwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Hisa za kampuni ya teknolojia ya Nvidia zimepanda kwa kasi soko la hisa lilipoanza biashara leo, kufuatia taarifa za kurejeshwa kwa Jensen Huang katika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji (CEO).
Hisa za kampuni hiyo zilifunguliwa kwa ongezeko la takriban asilimia 30.
Awali, thamani ya hisa za Nvidia ilikuwa imeshuka kwa kiasi kikubwa, huku zikifunga biashara siku ya Ijumaa zikiwa zimepungua kwa karibu asilimia 14.
Kushuka huko kulifuatia taarifa za shirika la habari la Reuters kwamba kampuni hiyo ilikuwa inachunguzwa na Tume ya Usalama na Masoko ya Hisa ya Marekani (SEC) kuhusu taratibu zake za uhasibu.
Masoko mengine ya hisa pia yameanza biashara yakiwa katika hali nzuri, ingawa ni muhimu kuzingatia kuwa fahirisi za masoko ya Marekani zilikuwa tayari zimeanza kupanda katika biashara za awali kabla ya soko kufunguliwa, kufuatia kushuka kwa kasi kwa masoko siku ya Ijumaa.
Unaweza pia kusoma:
Mwili wa Angel Wariael wafikishwa nyumbani kwao Arusha

Chanzo cha picha, The Chanzo
Huzuni imetanda nyumbani kwao Angel Wariael, baada ya mwili wake kuwasili katika makazi ya familia yake yaliyopo Nkoasenga, Kata ya Leguruki, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha.
Angel, mwenye umri wa miaka 13, alipigwa risasi akiwa nyumbani kwao Manzese wakati wa matukio ya Oktoba 29, nchini Tanzania. Na alifariki dunia Novemba 18, 2026, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikokuwa akipatiwa matibabu kufuatia kujeruhiwa katika tukio hilo.
Mwili wake sasa umefikishwa nyumbani kwao Arusha, ambako ataagwa na ndugu, jamaa na marafiki kabla ya kuzikwa.
Matukio ya Oktoba 29 yalihusisha vurugu na matumizi ya silaha katika maeneo mbalimbali, huku baadhi ya wananchi wakiripotiwa kujeruhiwa kwa risasi.
Angel alikuwa miongoni mwa walioathirika, baada ya kupigwa risasi akiwa nyumbani kwao Manzese, Dar es Salaam, majeraha yaliyosababisha kukatisha masomo yake.
Unaweza pia kusoma:
Jensen Huang arejeshwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Nvidia

Chanzo cha picha, Getty Images
Bodi ya kampuni ya teknolojia ya Nvidia imepiga kura kwa kauli moja kumrejesha Jensen Huang katika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji (CEO), ikisema anaamini ndiye mtu anayefaa kuiongoza kampuni hiyo.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Nvidia, mwenyekiti wa bodi amesema uamuzi huo umefikiwa kwa kauli moja na kwamba kurejeshwa kwa Huang ni kwa manufaa ya wanahisa, wafanyakazi, washirika na wateja wa kampuni hiyo.
Baada ya uamuzi huo, Huang ameeleza heshima yake kwa kurejea kuiongoza Nvidia, akisema kampuni hiyo ni miongoni mwa taasisi muhimu zaidi za teknolojia duniani wakati huu wa mwanzo wa mapinduzi mapya ya viwanda.
Katika taarifa yake, Huang amesema anapokea jukumu hilo kwa unyenyekevu mkubwa na dhamira mpya ya kuendelea kuiongoza kampuni hiyo.
Pia ametoa shukrani kwa bodi ya wakurugenzi kwa kumwamini, akimtaja mwenyekiti Harvey Jones kwa uongozi wake, pamoja na Colette Kress na timu ya viongozi waandamizi kwa kuisimamia Nvidia katika kipindi hicho.
Aidha, amewashukuru wafanyakazi, wanahisa, viongozi wa sekta ya teknolojia na washirika wa kampuni hiyo duniani kote kwa kumuunga mkono, huku akitaja familia yake kuwa chanzo muhimu cha upendo na msaada.
"Ninashukuru zaidi kwa upendo na msaada wa familia yangu. Ninashauku kubwa ya kurejea kazini," amesema Huang.
Unaweza pia kusoma:
Samia: Takwimu za vifo vya wajawazito Afrika zinatisha

Chanzo cha picha, IKULU MAWASILIANO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema mustakabali wa Afrika unategemea afya na ustawi wa wananchi wake, akisisitiza umuhimu wa kulinda afya ya wajawazito, watoto na kuwekeza kwa vijana.
Akizungumza katika mkutano wa Kimataifa wa Afya ya Umma (CPHIA 2026) mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Samia amesema kulinda afya ya mama na mtoto pamoja na kuwawezesha vijana ni majukumu ya msingi ya viongozi wa Afrika.
Amesema takwimu rasmi zinaonesha kuwa mwaka 2023 takriban wanawake 180,000 walifariki kutokana na sababu zinazohusiana na uzazi barani Afrika, huku vifo vingi katika maeneo ya vijijini vikikosa kurekodiwa rasmi, hali inayoweza kufanya idadi halisi kuwa kubwa zaidi.
Rais Samia ameonya kuwa iwapo mwenendo huo utaendelea, Afrika inaweza kurekodi takriban vifo 300 vya wajawazito kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ya lengo la Malengo ya Maendeleo Endelevu la kupunguza vifo hivyo hadi chini ya 70.
Amesema takwimu hizo zinatia wasiwasi mkubwa na zinahitaji hatua za haraka, dhamira thabiti ya kisiasa, uwekezaji endelevu na uwajibikaji.
Ameongeza kuwa dira ya Afrika inayotaka kujenga bara lenye maendeleo, kama ilivyoainishwa katika Agenda 2063, haiwezi kufikiwa huku vifo vya wajawazito na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika vikiendelea kutokea.
Mkutano huo wa CPHIA 2026 unajadili afya, usalama na mamlaka ya Afrika katika masuala ya afya, ukilenga kuhamisha bara hilo kutoka utegemezi na mazingira ya hatari katika sekta ya afya na kwenda kwenye umiliki wa mifumo yake na uwezo wa kujitegemea na kustahimili changamoto.
Waziri Mkuu wa Qatar kukutana na Marco Rubio Washington

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Qatar ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani, mjini Washington leo.
Mkutano huo unafanyika wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukiongezeka katika siku za hivi karibuni.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema mkutano huo utafanyika mchana wa leo kwa saa za Washington.
Waziri Mkuu wa Qatar alikutana na Rais wa Marekani, Donald Trump, mjini Washington mapema mwezi huu. Katika mkutano huo, Trump alisema kuwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vilikuwa vinakaribia kumalizika.
Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdel Ati, amesema alijadili masuala ya kikanda na Bw. Al Thani pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al Saud.
Abdel Ati, aliyeandika kwenye mtandao wa X, amesema lengo la mazungumzo hayo ni kupunguza mvutano na kufanya juhudi za upatanishi katika eneo hilo.
Qatar ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika juhudi za upatanishi kati ya Marekani na Iran, kwa lengo la kumaliza vita vilivyoanza mwishoni mwa Februari.
Mkuu wa Kamandi Kuu ya Marekani, Brad Cooper, na ujumbe wake walikutana na Waziri wa Ulinzi wa Qatar, Saud bin Abdulrahman Al Thani, pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, mjini Doha siku ya Ijumaa.
Ujumbe wa Qatar ulikuwa Tehran Ijumaa usiku kwa mazungumzo yaliyodumu kwa saa mbili.
Unaweza pia kusoma:
Korea Kusini yasema uwepo wa wanajeshi wake Ghuba ya Aden haumaanishi inashiriki vita dhidi ya Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini Kang Shin-chul amesema kuongeza muda wa operesheni ya kikosi cha kupambana na uharamia katika Ghuba ya Aden hakumaanishi nchi hiyo inashiriki katika vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Kang Shin-chul aliliambia Bunge la Korea Kusini kuwa kupelekwa kwa wanajeshi hao hakumaanishi "ushiriki wa kijeshi usio wa moja kwa moja" katika mzozo kuhusu Mlango-Bahari wa Hormuz.
Kwa mujibu wa Kang, vitendo vya uharamia katika eneo hilo vimeongezeka zaidi ya mara tatu katika mwaka uliopita.
Alisema lengo la operesheni hiyo ni kulinda meli za Korea Kusini na raia wake wanaosafiri kupitia njia hiyo ya baharini.
Unaweza pia kusoma:
Moto Nungwi: Wizara ya Utalii na Urithi Zanzibar yasema jiko la kuokea mikate huenda ndiyo chanzo

Chanzo cha picha, Getty Images
Wizara ya Utalii na Urithi Zanzibar imesema jiko la kuokea (oven) mikate katika Hoteli ya Makofi linashukiwa kuwa chanzo cha moto ulioteketeza eneo la Nungwi Jumamosi, Novemba 21.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, moto huo ulisambaa na kuathiri jumla ya hoteli sita, migahawa inayohudumia watalii pamoja na takribani maduka 40.
Hoteli zilizoathirika ni Makofi, Nungwi Garden Inn, Sandies Nungwi Beach, Pasha, Z Hotel na Bravo.
Kutokana na tukio hilo, wageni 183 walihamishwa na kupangiwa makazi katika hoteli nyingine. Hata hivyo, Hoteli ya Bravo haikuwa na wageni waliohitaji kuhamishwa.
Wizara imesema moto huo ulidhibitiwa ndani ya saa tatu kutokana na juhudi za pamoja za wazima moto, vyombo vya usalama, jamii za eneo hilo na wadau wa utalii.
Waziri wa Utalii, Nasra Nassor Omar, ameelekeza kufanyika kwa tathmini ya uharibifu uliosababishwa na moto huo na kuimarishwa kwa hatua za kuzuia majanga kama hayo.
Miongoni mwa hatua zilizotajwa ni kupitia upya matumizi ya mapaa ya makuti katika hoteli na kuhakikisha njia za dharura hazizuiwi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za uokoaji.
Unaweza pia kusoma:
FBI yachunguza uwezekano kwamba ilidukuliwa kanzidata yake yenye taarifa za uhalifu

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) linachunguza uwezekano kwamba kanzidata yake inayohifadhi taarifa za uhalifu ilidukuliwa. Hii ni kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Marekani vilivyonukuu watu wawili waliofahamishwa kuhusu suala hilo.
Kanzidata hiyo inayojulikana kama National Crime Information Center (NCIC), hutumiwa na vyombo vya usalama vya serikali kuu na vya maeneo mbalimbali nchini Marekani kubadilishana taarifa kuhusu hati za kukamatwa kwa washukiwa na ukaguzi wa historia za watu.
Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa wadukuzi kulenga FBI, chombo cha Marekani kinachohusika na upelelezi wa ndani na usalama wa taifa. Shirika hilo halikujibu ombi la BBC la kutoa maoni kuhusu tukio hilo.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kanzidata hiyo kudukuliwa katika mahojiano na kituo cha Fox News Jumamosi, Rais Donald Trump alisema alikuwa "amesikia tu" kuhusu shambulizi hilo.
"Nitasema kuwa hilo si jambo zuri. Silipendi," alisema Trump.
"Hata hivyo, huenda tukajifunza mambo ambayo tusingeweza kuyajua kwa njia nyingine," aliongeza.
Uwezekano huo wa kudukuliwa kwa kanzidata ya FBI unajiri baada ya mfululizo wa hitilafu za kiteknolojia zilizoathiri sekta za benki, udhibiti wa safari za ndege na sekta nyingine nchini Marekani wiki iliyopita.
Maafisa wamesema hitilafu hizo hazikusababishwa na mashambulizi ya mtandao, lakini zimeibua uchunguzi na maswali kutoka kwa wabunge.
Mkurugenzi wa Usalama wa Mtandao wa Ikulu ya Marekani, Sean Cairncross, alitimuliwa kazi wiki hii, huku Trump akisema hakuwa na uwezo wa kutosha.
Dan Lorhmann, mchambuzi wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA), aliiambia Idhaa ya Habari ya BBC kuwa taarifa zilizohifadhiwa katika kanzidata ya NCIC zinajumuisha "taarifa muhimu zinazohusiana na shughuli za uhalifu kote nchini" na zinapaswa kulindwa.
Aliongeza kuwa ingawa vyombo vya usalama vya Marekani, ikiwemo FBI, vina "uwezo wa kipekee" wa kulinda taarifa hizo na vinaheshimika duniani, kiwango cha mashambulizi ya mtandao kinaongezeka duniani kote.
"Kuna sababu nyingi tofauti zinazosababisha hali hiyo, lakini nina imani na wataalamu wetu serikalini," alisema Lorhmann.
Mwezi Septemba, FBI ilisema ilikuwa inachunguza uwezekano wa kudukuliwa kwa mifumo yake na kundi la wahalifu wa mtandao linalojulikana kama ShinyHunters.
Kundi hilo lilidai kuwa limeiba taarifa nyeti za wafanyakazi wote wa shirika hilo, ambao wanakadiriwa kuwa takribani 38,000.
Unaweza pia kusoma:
Pochettino aanza vibaya, akabiliana na ukubwa wa changamoto Manchester United

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mauricio Pochettino ni kocha wa nane wa kudumu wa Manchester United tangu Sir Alex Ferguson alipoondoka madarakani. Kocha mpya wa Manchester United, Mauricio Pochettino, ameanza kazi yake kwa hali mbaya baada ya timu yake kufungwa vibaya na wapinzani wao Liverpool na kubaki katika eneo la kushuka daraja la Ligi Kuu ya England.
Karibu kila kitu kilikwenda kombo kwa Manchester United ndani ya dakika 13 za mwanzo, ambapo ilifungwa mabao mawili na beki wake Leny Yoro akatolewa kwa kadi nyekundu. Hali hiyo iliifanya Liverpool kutawala mchezo na kupata ushindi kwa urahisi kuanzia wakati huo.
Hii ilikuwa mara ya kwanza tangu mwaka 1937 kwa Manchester United kufika katika uwanja wa Anfield ikiwa miongoni mwa timu tatu za mwisho kwenye msimamo wa ligi. Wakati huo, Mashetani Wekundu walifungwa na Liverpool katika msimu ambao baadaye walishuka daraja.
Inaonekana vigumu kufikiria Manchester United ya sasa inaweza kukumbwa na hatima kama hiyo, lakini kiwango cha timu hiyo na matokeo ya mchezo huo yameonyesha ukubwa wa changamoto inayomkabili Pochettino katika jitihada zake za kuipandisha timu hiyo kwenye msimamo wa ligi.
Yoro alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya nane baada ya mwamuzi kubaini kuwa alimchezea vibaya Alexander Isak nje kidogo ya eneo la hatari.
Dominik Szoboszlai alichukua jukumu la kupiga mpira wa adhabu na kuutumbukiza wavuni katika kona ya chini kushoto ya lango.
Unaweza pia kusoma:
Zelensky athibitisha Ukraine kushambulia meli za Urusi karibu na Libya

Chanzo cha picha, getty
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema meli ya kivita ya Urusi ilizamishwa na ndege zisizo na rubani za majini za Ukraine karibu na pwani ya Libya siku ya Jumapili.
Shambulizi hilo pia lililenga meli nyingine ya Urusi ya mizigo iliyokuwa ikitumika kusafirisha silaha, kwa mujibu wa madai ya Waziri Mkuu wa Ukraine.
Mapema Jumapili, serikali inayodhibiti maeneo ya mashariki mwa Libya ilisema mlipuko ulitokea kwenye meli hiyo ya kivita katika bandari ya Benghazi, wakati ikiwa imetia nanga kwa ajili ya kujaza mafuta na kupata mahitaji mengine kabla ya kurejea Urusi.
Wakati huo huo, Wizara ya Afya ilisema ilipokea watu waliojeruhiwa kutoka kwenye meli ya kibiashara iliyoshambuliwa karibu na pwani ya bandari hiyo. Haijafahamika iwapo hiyo ni meli hiyo hiyo ambayo Ukraine imedai kuishambulia.
Moscow bado haijatoa maoni kuhusu shambulizi hilo.
Katika taarifa yake ya Jumatatu, Zelensky alisifu kile alichokiita "operesheni ya mfano ya Ukraine katika kukabiliana na vita vya Urusi".
Zelensky aliandika kuwa ndege saba zisizo na rubani za majini zilitumika kuilenga na kuizamisha meli ya kivita aina ya Corvette Merkury, mojawapo ya meli mpya zaidi za Urusi.
Ameongeza kuwa helikopta ya kijeshi aina ya Ka-27 pia iliharibiwa.
Rais huyo wa Ukraine amesema meli ya pili iliyolengwa ni MV ANGARA, meli ya Urusi ya kubeba makontena.
Unaweza pia kusoma:
Mlango wa Hormuz utafunguliwa iwapo Marekani itatekeleza ahadi zake - Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Iran, Esmail Baghaei, amesema kuwa iwapo Marekani itatekeleza ahadi zake, usalama utarejea katika Mlango Bahari wa Hormuz na maeneo jirani kwa muda mfupi iwezekanavyo.
Akizungumza katika mkutano wake wa kila wiki na wanahabari, Baghaei alisema masharti ya Iran ni kuondolewa kwa vikwazo anavyovitaja kuwa haramu na kusitishwa kwa mzingiro wa baharini.
Baghaei amesisitiza kuwa iwapo Marekani itatekeleza ahadi zake, usalama utarejea katika Mlango Bahari wa Hormuz na eneo hilo kwa muda mfupi iwezekanavyo.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz, alisema Tehran inaweza kuchukua hatua haraka sana.
Soma pia:
Trump aunga mkono kurejea kwa Jensen Huang katika kampuni ya Nvidia

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Jensen Huang na Donald Trump Rais wa Marekani Donald Trump ameunga mkono kurejea kwa Jensen Huang katika kampuni ya Marekani ya kutengeneza chipu za kompyuta, Nvidia.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump alisema: "Natumai bodi ya wakurugenzi ya Nvidia itamrejesha Jensen Huang. Huo utakuwa uamuzi bora kwa kampuni hiyo na Marekani."
Matamshi hayo yanajiri baada ya Jensen Huang kujiuzulu kutoka wadhifa wake wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Nvidia mapema mwezi huu.
Kuondoka kwa Huang kulifuatia utata kuhusu maisha yake binafsi, uliohusisha madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa na mwanamke anayedaiwa kuwa jasusi wa China.
Nvidia ni mojawapo ya kampuni zinazoongoza duniani katika utengenezaji wa chipu za kisasa zinazotumika katika teknolojia ya akili unde (AI).
Soma pia:
AFCON 2027: Viwanja sita vyateuliwa kuandaa mechi Kenya, Tanzania na Uganda

Chanzo cha picha, online
Viwanja sita vimeteuliwa kuandaa mechi za fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka ujao, ambazo zitaandaliwa kwa pamoja nchini Kenya, Tanzania na Uganda.
Viwanja vitakavyotumika kwa mashindano hayo vilitangazwa wakati wa mkutano wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Nigeria.
Mjini Nairobi, mechi zitachezwa katika Uwanja mpya wa Talanta wenye uwezo wa kuchukua watazamaji elfu 60,000, ambao unatarajiwa kufunguliwa mwezi Januari.
Tanzania itakuwa na viwanja vitatu vitakavyotumika katika miji ya Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar.
Uganda itatumia Uwanja wa Taifa wa Mandela ulioko Kampala pamoja na Uwanja mpya wa Hoima City, ambao timu ya taifa ya Uganda imekuwa ikiutumia katika mechi zake za hivi karibuni za kimataifa.
Uwanja utakaotumika kuandaa fainali ya mashindano hayo ya timu 24, yatakayofanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, bado haujaamuliwa.
Fainali za mwisho za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), zilizofanyika Morocco kuanzia Desemba 2025 hadi Januari 2026, zilichezwa katika viwanja tisa vilivyoko katika miji sita.
Soma pia:
Mataifa yashindwa kufikia makubaliano katika mkutano wa COP31

Chanzo cha picha, Reuters
Nchi mbalimbali zimeshindwa kufikia makubaliano mapya muhimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kufuatia mivutano kuhusu matumizi ya nishati ya kisukuku na ufadhili katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi ya COP31 nchini Uturuki.
Mazungumzo hayo yaliyopaswa kukamilika siku ya Ijumaa ila yaliendelea hadi Jumapili huku wanaoshiriki wakijaribu kufikia mwafaka, na hivyo kuwa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi uliochukua muda mrefu zaidi katika historia.
Hata hivyo, mapendekezo ya mwisho hayakukubalika na Umoja wa Ulaya, mataifa ya visiwa vya Pasifiki na nchi nyingine kwa sababu hayakutaja moja kwa moja matumizi ya nishati ya kisukuku, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha ongezeko la joto duniani.
Wakati huohuo, nchi nyingi maskini zilipinga kutokuwepo kwa ahadi zozote za wazi za kifedha kutoka kwa mataifa tajiri za kuzisaidia kukabiliana na athari za ongezeko la joto duniani.
Mara ya mwisho makubaliano makuu ya kisiasa katika mkutano wa COP kushindwa kufikiwa kwa aina hii ilikuwa mwaka 2009 mjini Copenhagen, Denmark.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ambaye huu ulikuwa mkutano wake wa mwisho wa COP kabla ya kuondoka madarakani, alisema amesikitishwa sana na matokeo hayo.
Aliyashutumu makundi yenye ushawishi mkubwa katika sekta ya nishati ya kisukuku, akisema yanatumia mbinu zinazofanana na zile za kampuni kubwa za tumbaku.
Alisema makundi hayo yanapotosha sayansi, kuchelewesha sera, kuzuia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kujikusanyia faida kubwa huku watu kote duniani wakilipa gharama.
Trump aituhumu Iran kwa kuongeza mashambulizi ya droni

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa Iran imerusha ndege zisizo na rubani na makombora mengi zaidi, ndani ya wiki moja iliyopita kuliko wakati mwingine wowote katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja tangu vita kuanza.
Trump hakutaja ripoti wala chanzo chochote cha takwimu kuthibitisha madai yake, lakini alihusisha kuongezeka kwa mashambulizi hayo na ushindi wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa katikati ya muhula Marekani.
"Kwanza, nilisema kuwa iwapo chama cha Democratic kingeshinda, masoko ya hisa yangeshuka, jambo ambalo limetokea. Pili, nilisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo hadi sasa imewaua waandamanaji 81,000, ingeongeza mashambulizi yake, jambo ambalo pia limetokea."
Rais huyo wa Marekani aliongezea kuwa,
"Iran imefyatua ndege zisizo na rubani na makombora mengi zaidi katika wiki moja iliyopita kuliko wakati mwingine wowote katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja. Msijali, yote yamenaswa na kudunguliwa, bila kusababisha uharibifu wowote."
Soma pia:
Mvulana wa miaka saba aokolewa baada ya saa 14 chini ya vifusi Ukraine

Chanzo cha picha, Ukraine State Emergency Service
Mvulana mwenye umri wa miaka saba ameokolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo la makazi lililoporomoka katika mji wa Dymer, baada ya kunaswa humo kwa saa 14 kufuatia mashambulizi ya usiku ya Urusi katika eneo la Kyiv, yaliyosababisha vifo vya watu tisa, kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine.
Shambulizi hilo lilitokea mapema Jumapili. Mkuu wa utawala wa eneo la Kyiv, Tymur Tkachenko, alisema pia mwanamke mwenye umri wa miaka 79 aliokolewa akiwa hai kutoka kwenye jengo hilo lililoporomoka.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pia amesema watu watatu waliuawa na wengine 13 kujeruhiwa katika shambulizi tofauti lililotokea katika mji wa Vyshneve, pia katika eneo la Kyiv,hapo jana. Shambulizi hilo lililenga duka la bidhaa za vyakula.
Mamlaka za Ukraine zimesema mvulana aliyeokolewa katika mji wa Dymer anaendelea vizuri kiafya na alikimbizwa hospitalini.
Soma pia:
Meli ya Urusi yashambuliwa kwa droni katika bandari ya Libya

Chanzo cha picha, Reuters
Serikali ya Libya imesema mlipuko uliotokea ndani ya meli ya Urusi iliyokuwa imetia nanga katika kituo cha wanamaji kilichoko Benghazi,ulisababishwa na shambulizi linaloshukiwa kutekelezwa na ndege isiyo na rubani.
Mlipuko huo ulitokea mapema Jumapili wakati meli hiyo ilipowasili bandarini kwa ajili ya kuongeza mafuta na kupokea bidhaa kabla ya kuendelea na safari yake ya kurejea Urusi.
Taarifa ya serikali hiyo imesema hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo. Hadi kufikia sasa, Moscow haijatoa tamko lolote kuhusu shambulizi hilo.
Baadaye hapo jana, Wizara ya Afya ya Libya ilisema kuwa imepokea watu waliojeruhiwa kutoka katika meli nyingine ya kibiashara ambayo pia ililengwa katika shambulizi lililotokea karibu na pwani ya Benghazi.
Wizara hiyo ilisema majeraha ya waliojeruhiwa yalikuwa madogo na hali zao za afya zilikuwa imara.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ulieleza wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi hayo, huku ukitaka uchunguzi wa haraka, huru na wa wazi kufanyika.
"Libya haiwezi kumudu, wala hairuhusiwi kuwa uwanja wa mapambano ya migogoro ya kigeni," Umoja wa Mataifa uliandika kwenye mtandao wa X
Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa kijiografia na kitengo cha BBC Verify zinaonyesha meli iliyoshambuliwa ikiwa imezingirwa na moto na moshi.
Picha za setilaiti kutoka kampuni ya Planet Labs PBC pia zinaonyesha meli ikiwa inawaka moto katika bandari ya Benghazi.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNS) inayotawala mashariki mwa Libya ilisema meli hiyo ya Urusi, ambayo haikutajwa jina wala kutambuliwa rasmi, ilikuwa ikitumia bandari ya Benghazi chini ya makubaliano yaliyopo ya usafiri wa baharini.
Soma pia:
