Tanzania inataka Katiba mpya au marekebisho?

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kauli ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwamba ifikapo mwaka 2028 au 2029 nchi itakuwa na Katiba iliyorekebishwa au Katiba mpya, imeibua mjadala kuhusu aina ya Katiba inayotarajiwa kupatikana na namna itakavyopatikana.

Akizungumza Novemba 20, 2026, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi, Rais Samia alisema serikali inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2028 au 2029 Tanzania inakuwa na Katiba mpya au iliyorekebishwa.

Alisema: "Kama tulivyoahidi kwenye ilani, ikifika 2028/2029, tayari tutakuwa na Katiba iliyorekebishwa au jina lolote linalopendwa kuitwa Katiba mpya. Katiba iliyorekebishwa tutakuwa tayari tuko nayo mkononi."

Rais Samia alieleza kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho za kuunda na kutangaza Tume ya Maridhiano ya Kitaifa, itakayolenga kuimarisha umoja wa kitaifa, kusikiliza hoja za wananchi na kubaini masuala yanayopaswa kubadilishwa kwenye Katiba.

Kwa kauli hiyo, matarajio ya kupata Katiba nyingine kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030 yanaonekana kuwekwa katika ratiba ya serikali. Sio siri tena kwamba Tanzania itakuwa na Katiba nyingine, lakini itakuwa Katiba ya aina gani: mpya kabisa au ile ya mwaka 1977 iliyofanyiwa marekebisho?

Kauli zinazobadilika kuhusu aina ya Katiba

.
Maelezo ya picha, Rais Samia akiteta na Nchimbi aliyekuwa Makamu wa Rais kabla ya kuondolewa

Kwa zaidi ya miongo mitatu, madai ya kupata Katiba mpya yamekuwa sehemu ya mijadala ya kisiasa na kijamii nchini humo. Lakini matumizi ya maneno tofauti katika kauli za viongozi yanaibua mjadala mpya kuhusu maana ya mabadiliko yanayotarajiwa.

Kabla ya mwaka 2010, hoja iliyokuwa ikisikika zaidi kutoka kwa wananchi, wanaharakati na baadhi ya viongozi ilikuwa ni hitaji la kupata Katiba mpya. Kauli ilikuwa moja: tunataka Katiba mpya, si Katiba iliyorekebishwa, iliyoboreshwa au kufanyiwa mabadiliko ya vipengele kadhaa.

Hata mchakato ulioanzishwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, mwaka 2011, chini ya Tume iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba, ulilenga kupata Katiba mpya.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014. Rais Samia, alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo.

Hata hivyo, Bunge hilo lilifanya mabadiliko katika mapendekezo yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Warioba, jambo lililozua kutokubaliana na kusababisha baadhi ya wajumbe wa upinzani na makundi mengine kususia mchakato huo. Hatimaye, mchakato ulisimama kabla ya Katiba Inayopendekezwa kupelekwa kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni.

Baada ya John Pombe Magufuli kuingia madarakani mwaka 2015, suala la Katiba mpya liliendelea kuwa sehemu ya mijadala ya kisiasa, lakini mchakato haukuendelea hadi mwisho.

Tangu Rais Samia aingie madarakani mwaka 2021, amekuwa akitoa kauli mbalimbali kuhusu suala hilo. Akizindua Bunge la 13, alisema mchakato wa Katiba mpya ni miongoni mwa ahadi zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 na kwamba utaanza kutekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Katika kauli nyingine ya miaka iliyopita, aliwahi kusema: "Katiba ni mali ya Watanzania, ambayo tukifanya marekebisho yatuchukue muda, kitabu chetu kile kiende."

Hapa kuna matumizi ya maneno mawili tofauti: Katiba mpya na marekebisho ya Katiba.

Mjadala huo ulipata msukumo zaidi baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kutoa wito kwa Watanzania waipambanie Katiba mpya. Kauli yake ilizua maswali kwa baadhi ya watu kuhusu tofauti kati ya msimamo huo na lugha iliyokuwa ikitumiwa na viongozi wengine kuhusu mchakato wa Katiba.

Je, Nchimbi alimaanisha kuwa Watanzania wanapaswa kudai Katiba mpya ambayo bado haijahakikishwa kupatikana? Au alikuwa akisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika kuhakikisha Katiba itakayopatikana inakidhi matarajio yao?

Katika maelezo yake, Nchimbi alisisitiza kuwa Katiba inayohitajika ni ile yenye makubaliano ya wadau wote, inayojenga muafaka wa kitaifa, inayoheshimu haki za wananchi na inayoweza kuliongoza taifa kwa miongo ijayo.

Je, Katiba ya sasa inaweza kurekebishwa?

Mmoja wa wadau waliozungumza na Sauti Digital, Jeremia Maganga, anaamini kuwa Katiba ya sasa haiwezi kurekebishwa kwa kiwango kinachohitajika.

Anarejea ripoti za tume mbalimbali zilizochunguza masuala ya utawala na Katiba nchini, zikiwemo Tume ya Jaji Nyalali, Tume ya Jaji Kisanga, Tume ya Jaji Warioba na Tume ya Jaji Chande, ambazo zimebainisha changamoto mbalimbali katika mfumo wa kisheria na kikatiba wa Tanzania.

Kwa mtazamo wake, changamoto hizo zinaonyesha kuwa marekebisho ya vipengele vichache hayawezi kutoa majibu ya kina kwa matatizo yaliyopo.

Katika mjadala ulioibuliwa kwenye mtandao wa JamiiForums, Pascal Mayalla, mmoja wa wadau wanaofuatilia kwa karibu siasa za Tanzania, pia alihoji matumizi ya maneno Katiba mpya na marekebisho ya Katiba katika kauli za viongozi.

Aliandika: "Kwa vile Watanzania walitaka Katiba mpya, taarifa hii inazungumzia marekebisho ya Katiba, tungeomba mtufafanulie inawezekana ni lugha tu kuwa neno 'Katiba Mpya' na 'Kurekebisha Katiba' ni neno hilo hilo moja lenye maana ile ile?"

Mjadala huo unaenda sambamba na kauli ya Waziri wa Mipango, Profesa Kitila Mkumbo, aliyoitoa bungeni Juni 23, 2026, akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Alisema: "Ilani imejumuisha wazi ahadi ya kuhuisha na kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya, kama sehemu ya sera rasmi zilizoidhinishwa na wananchi kupitia uchaguzi mkuu."

Kwa Mayalla, maneno muhimu katika kauli hiyo ni "kuhuisha na kukamilisha", akieleza kuwa yanaweza kumaanisha kufufuliwa kwa mchakato ulioanza mwaka 2011 chini ya Jaji Warioba, uliozaa Rasimu ya Katiba ya mwaka 2014 na kujadiliwa na Bunge Maalumu la Katiba.

Hata hivyo, bado haijawekwa wazi sana kama serikali inakusudia kuendeleza rasimu hiyo, kuanza mchakato mwingine wa kukusanya maoni au kutumia utaratibu tofauti wa kufanya marekebisho ya Katiba iliyopo.

Watanzania wanataka Katiba ya aina gani?

.
Maelezo ya picha, Jaji Warioba aliongoza Tume na mchakato wa kupata katiba mpya 2011-2014

Ukisikiliza hoja za wadau mbalimbali kuhusu suala la Katiba, jambo linalojitokeza ni hitaji la kuwa na Katiba itakayokubalika kwa upana na kuakisi matarajio ya Watanzania. Ndiyo maana baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa kauli ya aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, haipaswi kutazamwa kwa kuzingatia matumizi ya maneno "Katiba mpya" pekee, bali pia kile alichokieleza kuhusu Katiba wanayoihitaji Watanzania.

Nchimbi alisisitiza umuhimu wa kuwa na Katiba yenye makubaliano ya wadau wote, inayojenga muafaka wa kitaifa, inayoheshimu haki za wananchi na inayoweza kuliongoza taifa kwa miongo ijayo.

Kwa maana hiyo, mjadala hauishii katika suala la kuitaja Katiba kuwa mpya au iliyorekebishwa. Muhimu zaidi ni maudhui yake, namna itakavyopatikana na kama wananchi wataridhika nayo.

Iwe ni kwa kufanya marekebisho, kuiboresha Katiba iliyopo au kuandaa mpya kabisa, changamoto kubwa itakuwa kuhakikisha mchakato huo unawashirikisha wananchi na kupata makubaliano mapana. Hilo ni muhimu hasa ikizingatiwa kuwa mchakato wa kwanza chini ya Rais Jakaya Kikwete, licha ya kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Jaji Warioba, haukukamilika baada ya kutokea tofauti kubwa kuhusu maudhui ya Katiba iliyopendekezwa.

Sasa, Rais Samia anasema hatua inayofuata ni kuunda Tume ya Maridhiano. Katika kauli yake ya Novemba 20, alisema: "Kinachofuata sasa tunaunda Tume ya Maridhiano kuelekea uundaji wa Katiba. Sasa Tume ya Maridhiano tutaitangaza hivi karibuni."

Alizungumza kuhusu Katiba kwa ujumla na kueleza kuwa kuundwa kwa Tume ya Maridhiano ni miongoni mwa hatua zinazofuata.

Hivyo, wakati serikali ikiweka mwaka 2028 au 2029 kama muda wa kuwa na Katiba, bado kuna maswali yanayohitaji majibu: Je, Watanzania watapata Katiba mpya au Katiba ya mwaka 1977 itafanyiwa marekebisho? Na zaidi ya yote, Katiba itakayopatikana itakuwa imeakisi kwa kiwango gani matakwa ya wananchi?