Moja kwa moja , Israel yaishutumu Iran kwa kutengeneza silaha za kemikali, yataka Marekani kuanzisha mashambulizi mapya

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ameishutumu Iran kwa kuendeleza mpango wa kutengeneza silaha za kemikali, lakini akasisitiza kuwa Tehran bado haijafikia uwezo wa kuzitumia kuishambulia Israel.

Muhtasari

Israel yaishutumu Iran kwa kutengeneza silaha za kemikali, yataka Marekani kuanzisha mashambulizi mapya

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Bajeti ya kuendeleza vita dhidi ya Iran ipo - Trump

    .

    Rais wa Marekani Donald Trump, amesema kuwa bajeti ya kuendesha vita dhidi ya Iran inajitosheleza hadi mwisho wa Januari 2027.

    Katika mahojiano na gazeti la New York Post, Trump alisema kuwa wanachama wa Democrat katika bunge la Congress,wanaweza kugeuza ‘ushindi’ wao kuwa ‘kushindwa’ iwapo watajaribu kusitisha vita dhidi ya Iran.

    Trump aliongezea kuwa wameliharibu jeshi la wanamaji la Iran Pamoja na mifumo yake ya ulinzi wa anga.

    "Tunaweza kumaliza vita hivi wakati wowote tunapotaka,"alisema Trump.

    Wiki iliyopita, Seneti ya Marekani ilipinga mswada uliolenga kuweka mipaka kwa mamlaka ya Trump ya kuendeleza vita dhidi ya Iran.

    Mswada huo ungehitaji Rais wa Marekani ama kusitisha vita dhidi ya Iran au kupata idhini ya Congress ili kuendelea na operesheni za kijeshi.

    Soma pia:

  2. Thomas Markle akabiliwa na mashtaka ya kumiliki picha za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto

    .

    Thomas Markle, babake Meghan Markle, amefunguliwa mashtaka na baraza kuu la mahakama mjini Los Angeles, Marekani, kwa tuhuma za kumiliki picha na video za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.

    Markle, ambaye bado anazuiliwa katika jimbo la Florida, anadaiwa kumiliki kanda hizo zilizojumuisha angalau picha moja ya mtoto ambaye hajafikia umri wa kubaleghe na mwingine mwenye umri wa chini ya miaka 12, kwa mujibu wa nyaraka za mahakama zilizowasilishwa California.

    Markle mwenye umri wa miaka 82 amekanusha kumiliki picha za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani mjini Los Angeles katika wiki zijazo ili kujibu mashtaka hayo.

    Wiki iliyopita, mahakama ya Florida ilitangaza kuwa baba mkwe wa Prince Harry ana uwezo wa kiakili wa kuelewa mashtaka yanayomkabili na kushiriki katika kesi yake.

    Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) lilimkamata Markle tarehe 6 Novemba, katika makazi ya wazee katika jimbo la Florida.

    Wakili wa serikali ya Marekani, Bill Essayli, alisema kuwa iwapo atapatikana na hatia, Markle anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 20 jela kwa kila shtaka.

  3. Takriban wanajeshi laki tano wa Urusi wameuawa vitani Ukraine

    .

    Takriban wanajeshi 490,334 wa Urusi wamefariki tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine mwaka wa 2022, hii ni kulingana na takwimu za serikali ya Urusi zilizochambuliwa na BBC.

    Takwimu zilizovuja kutoka shirika la takwimu la Urusi, Rosstat, zinaonesha jinsi uvamizi wa Ukraine ulivyobadilisha kwa kiasi kikubwa mwenendo wa vifo nchini humo, na kufichua gharama kubwa ya maisha ya binadamu katika vita ambavyo Rais Vladimir Putin alidhani vingedumu kwa siku chache, lakini sasa vinakaribia kutimiza miaka mitano.

    BBC Russian imepata zaidi ya rekodi milioni 11 za vifo kuanzia mwaka 2021 hadi Septemba 2026, baada ya udukuzi wa mtandao uliofanywa na makundi ya Belarus ya Cyber Partisans BY na Silent Crow ya Ukraine.

    Shirika la takwimu la Urusi lilikiri kuwa lilidukuliwa, lakini likakanusha madai kwamba taarifa zozote zilivuja.

    Kwa kushirikiana na chombo huru cha habari cha Urusi, Mediazona, BBC Russian ililinganisha takwimu za Rosstat na orodha yake ya wanajeshi waliothibitishwa kufariki, ambayo imekuwa ikiandaliwa kwa kutumia taarifa kutoka vyanzo vya wazi tangu kuanza kwa uvamizi huo.

    Ulinganisho huo umebaini kuwa asilimia 90 ya rekodi hizo zinaendana na taarifa za vifo vya wanajeshi zilizokusanywa na BBC na Mediazona.

    Soma pia:

  4. Israel yaishutumu Iran kwa kutengeneza silaha za kemikali

    .
    Maelezo ya picha, icha ya Israel Katz

    Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ameishutumu Iran kwa kuendeleza mpango wa kutengeneza silaha za kemikali, lakini akasisitiza kuwa Tehran bado haijafikia uwezo wa kuzitumia kuishambulia Israel.

    Katika taarifa iliyochapishwa na chama cha Likud kupitia mtandao wa Telegram, Katz amesema Iran imeanza kutengeneza silaha za kemikali lakini bado haina uwezo wa kuzitumia kuishambulia Israel.

    "Hatupaswi kuruhusu hali hii kuendelea,"alisema Katz.

    Matamshi ya Katz yanajiri siku chache baada ya kituo cha televisheni cha CNN kuripoti, kikirejelea taarifa za kijasusi za Marekani, kwamba Iran imekuwa ikiandaa mipango ya kuwalenga maafisa katika utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump kwa kulipua kile kinachojulikana kama “bomu chafu” au dirty bomb, mjini Washington DC.

    CNN ilinukuu vyanzo ambavyo hawakuvitaja majina, vikisema mipango hiyo ya Iran ni ya tahadhari, lakini haimaanishi kwamba shambulio linakaribia kutekelezwa.

    Waziri huyo wa Ulinzi alidokeza uwezekano wa Israel kuishambulia Iran akisema hawatasubiri kushambuliwa kwanza.

    “Jeshi linaweza kuamrishwa kuchukua hatua mapema ili kuzuia tishio hilo iwapo itabainika kuwa Iran inapanga kuishambulia Israel.”

    Kauli hizo zinajiri wakati Israel inakabiliwa na changamoto za kisiasa, baada ya Waziri Mkuu wa mpito Benjamin Netanyahu na mpinzani wake mkuu Gadi Eisenkot kushindwa kupata wingi wa viti katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi uliopita.

    Rais wa Israel Isaac Herzog alimpa Eisenkot jukumu la kujaribu kuunda serikali, huku Netanyahu akizidisha matamshi yake kuhusu tishio la Iran na kusisitiza umuhimu wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayojumuisha chama chake cha Likud.

    Ripoti zingine zimeelezea kuwa Netanyahu amekuwa akimhimiza Rais wa Marekani Donald Trump, kuanzisha tena vita dhidi ya Iran.

    Soma pia:

  5. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumatano ya leo