Moja kwa moja, Iran yakanusha madai ya Trump, na kusema hakuna makubaliano yaliyoafikiwa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Iran,Esmail Baghaei, amesema taarifa za kuafikiwa kwa makubaliano na Marekani, si za kweli na mazungumzo bado hayajakamilika.

Muhtasari

Skip Video and continue reading
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Beldeen Waliaula

  1. Iran yakanusha kuwa karibu kuafikia makubaliano na Marekani

    Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Iran, Esmail Baghei

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Iran, Esmail Baghei

    Iran imesisitiza kuwa bado haijaafikia makubaliano ya kumaliza mzozo kati yao na Marekani, licha ya Rais Trump kutangaza tena kuwa makubaliano hayo yanatarajiwa kutiwa saini hivi karibuni.

    Trump alikuwa ametangaza kwamba Marekani ingeishambulia Iran "kwa nguvu kubwa" siku ya Alhamisi, lakini baadaye akasema amesitisha mashambulizi hayo baada ya "kuafikia makubaliano mazuri" na Iran.

    Trump aliwaambia wanahabari kuwa huenda makubaliano hayo yakatiwa siku chache zijazo.

    Aidha msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Iran,Esmail Baghaei, amesema taarifa za kuafikiwa kwa makubaliano si za kweli na mazungumzo bado hayajakamilika.

    Hii si mara ya kwanza kwa Trump kudai kuwa makubaliano na Iran yako karibu kuafikiwa bila matokeo yoyote kuonekana baadaye.

    Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi dhidi ya Iran tarehe 28 mwezi Februari. Iran ilijibu mashambulio hayo kwa kushambulia Israel na mataifa washirika wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi, na kufunga mlango bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na gesi.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Somaliland yafungua ubalozi wake Taiwan

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Eneo la Somaliland limesema lina haki ya kuchagua washirika wake, huku shinikizo kutoka Beijing na Mogadishu zikifeli kusambaratisha uhusiano wa Somaliland na kisiwa kinachojitawala cha Taiwan.

    Balozi wa Somaliland mjini Taipei alitangaza kuwa eneo hilo litakuwa linafungua ubalozi wake katika kisiwa hicho cha Taiwan.

    Eneo la Somaliland limekuwa likijitawala kuanzia mwaka wa 1991, baada ya kujitenga na Somalia kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe.

    Akizungumza na wanahabari, mwakilishi wa Somaliland eneo la Taiwan, Mahmoud Adam Jama Galaal, alisema kuwa kisiwa hicho ni mshirika mkubwa wa Somaliland.

    Hadi mwishoni mwa mwaka uliopita, Somaliland ilikuwa haitambuliwi kama taifa huru, ila mwezi Disemba, Israel ilitangaza kuitambua Somaliland kama taifa huru, hatua iliyokashifiwa vikali ya Somalia.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Kundi la kigaidi la JNIM, latangaza zawadi ya Euro millioni 2 kwa yeyote mwenye taarifa kumhusu rais wa Mali

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kundi la kigaidi nchini Mali, Jama’at Nusrat al-Islam wal Muslimin (JNIM) lenye uhusiano na Al- Qaeda, limetangaza zawadi ya mamilioni ya euro kwa yeyote atakayetoa taarifa kuhusu aliko rais wa taifa hilo, na maafisa wakuu wa jeshi la taifa hilo, wakitaja serikali ya taifa hilo kuwa si halali.

    Taarifa ya kundi hilo la kigaidi la JNIM limekuja siku moja tu, baada ya serikali ya Mali, kutangaza zawadi ya mamilioni ya pesa kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu watu walioishambulia serikali, miundombinu na raia.

    Hii inajiri baada ya kundi hilo lenye uhusiano na Al-Qaeda kutekeleza mashambulizi mwezi Aprili na kumuua Waziri wa Ulinzi wa taifa hilo na kuwajeruhi maafisa wengine.

    Serikali ya Mali ilikuwa imetangaza zawadi ya dola millioni 3.55 kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu Lyad Ag Ghaly, kiongozi wa JNIM.

    Kundi la JNIM limetangaza zawadi ya Euro million mbili kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu rais wa taifa hilo Assimi Goita, aliyechukua madaraka baada ya mapinduzi mwaka wa 2020, na Euro million moja kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu maafisa wakuu wa jeshi Kanali Lassina Diallo na Jenerali Malik Dicko.

    Pia unaweza kusoma:

  4. “Msitumie muziki wangu,” Ariana Grande aiambia Ikulu ya Marekani

    Ariana Grande

    Chanzo cha picha, Noam Galai/Getty Images for MTV

    Muimbaji maarufu wa muziki wa pop kutoka Marekani, Ariana Grande, ameomba Ikulu ya Marekani isitumie muziki wake baada ya kufanya hivyo katika video ya mitandao ya kijamii iliyokuwa ikitangaza sera za uhamiaji za serikali.

    Video hiyo ya TikTok iliyochapishwa Jumatatu inaonesha maafisa wa ulinzi wa mipaka wakiwafunga pingu watu mbalimbali, huku wimbo wa Ariana Grande wa mwaka 2024, Bye, ukitumika kama muziki wa video hiyo.

    Video hiyo ilikuwa na maelezo yaliyosema:

    "Bye-bye... Rais Trump ametoa mpaka salama zaidi katika historia."

    Grande alijibu kwenye chapisho hilo kwa kuandika:

    "Tafadhali msitumie muziki wangu kuhusishwa na upuuzi huu wa kikatili, usio wa kibinadamu na wa kutisha."

    Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Abigail Jackson, alijibu kwa vyombo vya habari vya Marekani akisema:

    "Kilicho cha kikatili, kisicho cha kibinadamu na cha kutisha ni wahamiaji haramu wahalifu ambao wamejeruhi na kuwaua raia wasio na hatia wa Marekani."

    Video hiyo ilikuja baada ya Rais Donald Trump kutia saini sheria iliyotenga zaidi ya dola bilioni 70 kwa ajili ya mashirika ya uhamiaji katika kipindi kilichobaki cha muhula wake wa urais.

    Video hiyo inaonesha maafisa wakiwafunga watu pingu, kuwaingiza kwenye magari na baadaye kuwapeleka katika vituo vya kuzuiliwa.

    Baada ya Ariana Grande kutoa maoni yake, sauti ya wimbo huo iliondolewa kwenye video na maoni yake kufutwa. Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii walibaini kuwa maoni yake yalikuwa yameondolewa na kwamba video hiyo ilikuwa imezimwa sauti.

    Muigizaji wa filamu ya Wicked amejiunga na orodha inayoongezeka ya wasanii ambao wameitaka timu ya Trump kutotumia muziki wao kutangaza sera au ajenda za kisiasa za rais huyo.

    Mwaka jana, mwimbaji Sabrina Carpenter aliandika:

    “Msinijumuishe mimi au muziki wangu kamwe ili kuunga mkono ajenda yenu isiyo ya kibinadamu”, baada ya video ya Ikulu ya Marekani kutumia sehemu ya wimbo wake wa 2024 Juno katika mkusanyiko wa video zilizoonesha operesheni za Idara ya uhamiaji ya Marekani.

    Wanamuziki wa kundi ABBA, pamoja na Celine Dion na Beyoncé, pia walisisitiza kuwa timu ya kampeni ya Rais Donald Trump isitumie muziki wao wakati wa kampeni yake ya 2024 ya uchaguzi, ikiwemo katika mikutano ya kampeni.

  5. Rais wa zamani wa Korea Kusini aliyeko gerezani ahukumiwa miaka 30 zaidi kwa kutuma droni Korea Kaskazini

    Yoon

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mahakama nchini Korea Kusini imemhukumu rais wa zamani, Yoon Suk Yeol, kifungo cha miaka 30 jela kwa kuhusika na operesheni ya kutuma droni ndani ya Korea Kaskazini.

    Waendesha mashtaka walidai kuwa Yoon aliamuru operesheni hiyo mwezi Oktoba 2024 kwa lengo la kuichokoza Pyongyang na kuunda mazingira ya dharura ambayo yangetoa sababu ya kutangaza sheria ya kijeshi baadaye mwaka huo.

    Yoon alipotangaza sheria ya kijeshi tarehe 3 Desemba, alidai kuwa alikuwa akilinda nchi dhidi ya "vikosi vinavyopinga taifa" ambavyo vinaunga mkono Korea Kaskazini.

    Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa hatua hiyo ilichochewa zaidi na matatizo ya kisiasa ya ndani, na alilazimika kufuta amri hiyo baada ya maandamano makubwa ya wananchi.

    Yoon tayari alikuwa ameondolewa madarakani kupitia mchakato wa kura ya kutokuwa na imani naye na alikuwa akitumikia kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya uasi kufuatia jaribio lake la kutangaza sheria ya kijeshi.

    Mawakili wa Yoon Suk Yeol walidai kwamba hatua zake zilikuwa "halali" na zilikuwa jibu la uchokozi wa Korea Kaskazini kupitia kile walichokiita "maputo ya taka".

    Hii ilikuwa ikirejelea tukio la mwaka 2024 ambapo Korea Kaskazini ilirusha mamia ya maputo kuvuka mpaka kuelekea Korea Kusini.

    Baadaye iligundulika kuwa maputo hayo yalikuwa yamebeba taka, uchafu mbalimbali na kinyesi.

    Nchi hizi mbili zimekuwa zikitumia mbinu ya "maputo ya propaganda" tangu wakati wa Vita vya Korea, ambapo ujumbe wa kisiasa au propaganda huwekwa ndani ya maputo hayo na kurushwa kuvuka mpaka kuelekea upande mwingine.

    Kwa miaka mingi, maputo hayo yametumiwa kusambaza ujumbe wa kisiasa, vipeperushi, habari na propaganda kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini kama sehemu ya vita vya kisaikolojia kati ya nchi hizo mbili.

    Unaweza kusoma;

  6. Mabaharia watatu wa India wauawa katika shambulio la Marekani dhidi ya meli ya mafuta

    CENTCOM ilichapisha kile ilichosema kuwa ni video ya shambulio dhidi ya chumba cha injini cha meli hiyo.

    Chanzo cha picha, Centcom

    Mabaharia watatu wa India wamethibitishwa kufariki dunia baada ya jeshi la Marekani kushambulia meli ya mafuta ya MT Settebello katika Ghuba ya Oman, ambayo Marekani ilidai ilikuwa imekiuka zuio lake dhidi ya bandari za Iran.

    Meli hiyo ilishambuliwa Jumatano ikiwa na wafanyakazi 24 wa India. Kati yao, watu 21 waliokolewa. Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Waziri wa Usafirishaji wa India, Sarbananda Sonowal, alisema miili ya mabaharia hao watatu itarejeshwa nchini India hivi karibuni.

    Siku ya Ijumaa, kampuni inayoendesha meli hiyo, iOS Marine, ilisema katika taarifa kwamba “haina uhusiano wowote na Iran au mafuta ya Iran.”

    Marekani imeshambulia meli tatu katika eneo la Ghuba wiki hii, zote zikiwa na wafanyakazi wa India.

    Siku ya Alhamisi, serikali ya India ilisema wafanyakazi wote 20 wa meli ya Jalveer walikuwa salama baada ya meli hiyo kushambuliwa karibu na Oman.

    Siku tatu kabla ya hapo, wafanyakazi 24 wa India waliokuwa kwenye meli ya mafuta Marivex, ambayo ilikuwa imewekewa vikwazo, waliokolewa kabla ya meli hiyo kuzama.

    Marekani ilithibitisha kuwa ilizishambulia meli zote mbili.

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, CENTCOM ilisema kuwa moja ya ndege zake ilirusha “silaha za usahihi wa hali ya juu” kwenye chumba cha injini cha meli hiyo baada ya wafanyakazi wake “kushindwa mara kwa mara kufuata maelekezo.”

    Hata hivyo, katika taarifa yake, iOS Marine ilikanusha madai ya CENTCOM kwamba meli hiyo ilipuuza maonyo na mawasiliano ya onyo yaliyotolewa na vikosi vya Marekani.

    Unaweza kusoma;

  7. Shambulio la droni nchini Sudan lalenga msafara wa mazishi na kuua watu kadhaa

    Mji wa El-Obeid umekuwa ukilengwa katika mashambulizi kadhaa ya droni, ikiwa ni pamoja na wakati picha hii ilipopigwa mwezi Machi.

    Chanzo cha picha, Los Angeles Times via Getty Images

    Shambulio la ndege isiyo na rubani lililolenga msafara wa mazishi katika makaburi ya mji wa El-Obeid nchini Sudan limeua takribani watu wanne na kuwajeruhi wengine kadhaa, kwa mujibu wa makundi mawili ya kutetea haki za binadamu na huduma za afya, Sudan Doctors Network na Emergency Lawyers.

    Makundi yote mawili yamelilaumu kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF) kwa kuhusika na shambulio hilo. Kundi la Emergency Lawyers limesema kuwa shambulio hilo ni sehemu ya mfululizo wa mashambulizi ya droni yaliyoanza Jumatano jioni, ambapo kwa jumla watu wasiopungua 23 wameuawa.

    RSF haijatoa tamko lolote kuhusu madai hayo.

    Mji wa El-Obeid, ambao kwa sasa unadhibitiwa na jeshi la Sudan, ni moja ya maeneo muhimu ya mapigano katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan vilivyoanza miaka mitatu iliyopita baada ya viongozi wa jeshi na RSF kutofautiana kuhusu mustakabali wa nchi hiyo.

    Mapigano hayo yamesababisha kile kinachotajwa kuwa janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani kwa sasa, ambapo zaidi ya watu milioni 11 wamelazimika kuyahama makazi yao na watu milioni 28 wanakabiliwa na njaa kali.

    Hakuna takwimu rasmi na za kuaminika kuhusu idadi kamili ya waliopoteza maisha tangu vita hivyo vianze, lakini inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 50,000 wamefariki dunia.

    Unaweza kusoma;

  8. Tetesi za soka Ijumaa: Lewis Hall wa Newcastle ana nia ya kuondoka

    Lewis Hall

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Manchester United inaonesha nia ya kumsajili mlinzi wa Newcastle United na timu ya taifa ya England, Lewis Hall (21), ambaye anaripotiwa kutaka kuondoka klabuni hapo.

    Mlinzi wa kushoto wa Fulham na timu ya taifa ya Marekani, Antonee Robinson (28), pia anatazamwa na Manchester United kama usajili wao kwa msimu ujao.

    Barcelona haitalingana na ofa kubwa za kifedha zinazotolewa kwa kiungo wa Ureno Bernardo Silva (31) na Atletico Madrid pamoja na Real Madrid, ambazo zote zinataka kumsajili mkataba wake na Manchester City utakapoisha mwishoni mwa Juni.

    Real Madrid inaonekana kuwa mbele katika mbio za kumsajili Bernardo Silva na tayari ipo kwenye mazungumzo ya hatua za mwisho kuhusu makubaliano binafsi ya mchezaji huyo.

    Beki wa Croatia wa Manchester City, Josko Gvardiol (24), ameibuka kuwa chaguo kuu la Jose Mourinho kwa ajili ya kuimarisha safu ya ulinzi ya Real Madrid.

    Kocha wa zamani wa Manchester United, Ruben Amorim (41), anawindwa na AC Milan, ambao wanaamini anaweza kuleta nguvu mpya katika timu hiyo.

    Barcelona inatarajiwa kukataa fursa ya kumsajili mshambuliaji wa Manchester United Marcus Rashford (28) kwa ada yake ya kuachiliwa ya pauni milioni 26, huku kipengele hicho kikitarajiwa kuisha muda wake Jumatatu.

    Manchester United pia inaweza kuelekeza nguvu zake kwa kiungo wa Lens, Mamadou Sangare (23), baada ya kushindwa kumudu gharama za kumsajili kiungo wa England Elliot Anderson (23) kutoka Nottingham Forest.

    Beki wa Borussia Dortmund na Ujerumani, Nico Schlotterbeck (26), ameweka pembeni mawazo ya kuhamia Real Madrid ili kuzingatia kwanza FIFA World Cup.

    Trabzonspor inataka kukamilisha usajili wa moja kwa moja wa mlinda lango wa Cameroon wa Manchester United, Andre Onana (30), msimu huu wa kiangazi.

    Manchester United pia inatafuta kuwaondoa mlinda lango Altay Bayindir (28) wa Uturuki na Radek Vitek (22) wa Czech Republic, ambaye alikuwa kwa mkopo katika Bristol City msimu uliopita.

    Sunderland imejiunga na mbio za kumsajili mshambuliaji chipukizi wa Bosnia, Kerim Alajbegovic (18), kutoka Red Bull Salzburg.

    Wolverhampton Wanderers inaweza kuvutiwa kumrejesha mshambuliaji wa West Ham United, Pablo (22), kufanya kazi tena na kocha mpya Cesar Peixoto, ambaye aliwahi kufanya naye kazi Gil Vicente FC.

    Real Madrid inatafuta kumtoa kwa mkopo mshambuliaji wa Argentina Franco Mastantuono (18) kwenda Juventus.

    Unaweza kusoma;

  9. Vance asema Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu ‘amekosea katika baadhi ya mambo’

    Vance

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema kwamba Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, "bila shaka amekosea katika baadhi ya mambo", huku uhusiano kati ya washirika hao wawili katika vita dhidi ya Iran ukionekana kuwa na msukosuko katika wiki za hivi karibuni.

    Ingawa Vance hakutoa mifano maalumu, aliiambia CBS News kwamba Netanyahu "anapigania kwa nguvu maslahi ya nchi yake", lakini maslahi hayo si mara zote yanalingana na yale ya Marekani.

    Kauli zake zinaashiria waziwazi zaidi kwamba uhusiano kati ya washirika hao wa muda mrefu umekuwa ukikabiliwa na changamoto hivi karibuni.

    Hivi karibuni, Rais wa Marekani Donald Trump anaripotiwa kutofautiana na Netanyahu kuhusu hatua za kijeshi za Israel nchini Lebanon, ambazo zilisababisha mashambulizi mapya na kutishia juhudi za mazungumzo ya amani na Iran.

    Marekani na Iran zilirushiana mashambulizi kwa siku ya pili mfululizo usiku kucha, jambo lililoongeza shinikizo kwenye makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyokuwepo tangu mwezi Aprili.

    Hali hiyo ilikuja baada ya Trump kusema kwamba Tehran ilikuwa imechukua "muda mrefu sana kufikia makubaliano" ya kumaliza vita. Hata hivyo, kuongezeka kwa mapigano kulichochewa na matukio nchini Lebanon, ambako Israel imeendelea na operesheni dhidi ya Hezbollah, kundi linaloungwa mkono na Iran.

    Wiki iliyopita, Trump alimwambia mwandishi wa habari wa Axios kwamba alimwita Netanyahu "mwendawazimu kabisa" katika mazungumzo ya simu, akisema alikuwa amekerwa na "kupigana kwake mara kwa mara na Lebanon."

    Katika mahojiano yanayotarajiwa kurushwa hewani Jumapili, Vance alisema:

    "Waziri Mkuu Netanyahu, anaongoza nchi ambayo kwa hakika imekuwa mshirika wa karibu sana wa Marekani."

    Hata hivyo, aliongeza kuwa Marekani na Israel si lazima zikubaliane katika kila suala la sera au hatua za kijeshi, licha ya ushirikiano wao wa muda mrefu.

    Unaweza kusoma;

  10. SpaceX ya Elon Musk yapata dola bilioni 75 kabla ya kuanza kuuzwa katika soko la hisa

    Space X

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Space X imepata uwekezaji wa dola bilioni 75 (takribani pauni bilioni 56) kutoka kwa taasisi za kifedha kabla ya kuanza kuuzwa katika soko la hisa kwa umma siku ya Ijumaa, katika kile kinachotarajiwa kuwa uorodheshaji wa hisa wenye thamani kubwa zaidi katika historia.

    Katika nyaraka zilizowasilishwa kwa U.S. Securities and Exchange Commission (SEC), kampuni hiyo ya safari za anga za juu na akili mnemba imeuza hisa zenye thamani ya dola bilioni 75 kwa bei ya dola 135 kwa kila hisa.

    Bei hiyo ya hisa inalingana na makadirio ambayo SpaceX ilitoa wiki iliyopita, jambo linaloweka thamani ya awali ya kampuni hiyo sokoni kufikia karibu dola trilioni 1.8.

    Kwa thamani hiyo, mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, Elon Musk, ambaye tayari ndiye mtu tajiri zaidi duniani, anatarajiwa kuwa mtu wa kwanza duniani kufikia utajiri wa dola trilioni moja.

    Mara tu hisa zitakapoanza kuuzwa sokoni, thamani yake inaweza kupanda au kushuka kulingana na idadi ya hisa zitakazopatikana kwa ajili ya kuuzwa na kiwango cha mahitaji kutoka kwa wanunuzi.

    Ikiwa hisa za kampuni zitauzwa kwa dola 135 au zaidi wakati biashara itakapoanza siku ya Ijumaa, SpaceX itakuwa mara moja miongoni mwa kampuni zenye thamani kubwa zaidi duniani zinazouzwa hadharani katika soko la hisa.

    Hata hivyo, ni jukumu la wawekezaji kuamua kama wanaamini hisa hizo zina thamani hiyo.

    Maslahi ya kununua sehemu ya umiliki wa SpaceX miongoni mwa mifuko ya uwekezaji na wawekezaji binafsi (wanaojulikana kama retail investors) yanatarajiwa kuwa makubwa sana.

  11. Trump asema makubaliano ya kumaliza vita na Iran yako karibu baada ya kusitisha mashambulizi

    Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amedai kuwa makubaliano ya awali yanayolenga kumaliza vita na Iran yako karibu kufikiwa, baada ya kutangaza kuwa amefuta mashambulizi yaliyokuwa yamepangwa dhidi ya nchi hiyo.

    "Ndiyo kwanza tumefikia makubaliano mazuri kuhusu vita na Iran," aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake siku ya Alhamisi.

    Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, aliiambia televisheni ya taifa kwamba taarifa za kuwepo kwa makubaliano ni "za kubahatisha" na kwamba "hakuna jambo lolote lililokamilishwa."

    Trump amewahi kutoa madai kama hayo hapo awali kwamba Marekani na Iran ziko karibu kufikia makubaliano ya kumaliza mzozo huo. Saa chache kabla ya tangazo hilo, alikuwa ametishia kuishambulia Iran "kwa nguvu kubwa sana."

    Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Iran tarehe 28 Februari. Iran ilijibu kwa kushambulia Israel na mataifa washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba, na kwa kiasi kikubwa kufunga mlango bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na gesi asilia duniani.

    Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Aprili, Marekani na Iran zimeendelea kurushiana mashambulizi mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na duru mbili za mashambulizi ya kulipizana kisasi wiki hii. Wakati huohuo, Trump ameendelea kuzungumzia uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano na Iran.

    Unaweza kusoma;

  12. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo