"Kujiua kwa hofu ya kubakwa": Tahadhari za kimataifa kuhusu madhara ya ukatili wa kingono nchini Sudan

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani na ya kimataifa yameonya kuhusu madhara makubwa ya kuenea kwa ubakaji na aina nyingine za ukatili wa kijinsia nchini Sudan, hususan athari zake katika afya ya akili ya waathirika na walionusurika.
Tangu Aprili 2023, Sudan imekuwa ikikumbwa na vita kati ya jeshi la serikali na kikosi cha Rapid Support Forces, ambavyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kuwahamisha takriban watu milioni 11, kulingana na shirika la habari la AFP. Hali hii imeambatana na ongezeko kubwa la ukatili wa kijinsia.
Katika ripoti iliyotolewa mwishoni mwa Machi yenye kichwa "Kuna kitu ningependa kukuambia...",Shirika la Madaktari wasio na mipaka, Médecins Sans Frontières lilisema kuwa kati ya Januari 2024 na Novemba 2025, angalau manusura 3,396 wa ukatili wa kijinsia walipata huduma za afya katika vituo vinavyosaidiwa na shirika hilo Kaskazini na Kusini mwa Darfur, na karibu wote walikuwa wanawake na wasichana.
Shirika hilo lilieleza kuwa uhalifu huu umekuwa "alama" ya mzozo unaoendelea nchini Sudan, huku World Health Organization likionya kuwa takwimu zilizopo huenda zinaonyesha tu "ncha ya barafu".
"Majeshi yalinibaka mbele ya watu wote, akiwemo mume wangu," alisema mwanamke mmoja kutoka mji wa Tawila, Kaskazini mwa Darfur, katika ushuhuda uliorekodiwa na Shirika la Médecins Sans Frontières mwezi Novemba 2025.
"Tunataka haki"
Akizungumza na BBC, mwanamke mmoja alisema kwamba alibakwa na kikundi cha wanamgambo wa Rapid Support Forces.
Aliongeza: "Wallahi, wanamgambo wametuchosha, wametudhuru na wametusababisha kuhama makazi yetu… Wamechukua kila kitu tulichokuwa nacho, wametutishia kwa silaha, na wamekiuka heshima yetu. Tunataka haki na tunaomba jumuiya ya kimataifa itusaidie kufanikisha hilo na si kitu kingine."
Mwanamke mwingine, kutoka kijiji kilichopo katika Jimbo la Al-Jazirah, alisema naye pia "alitendewa vibaya na RSF."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Aliendelea kusema: "Hali zetu zilikuwa ngumu sana na walitutishia kwa silaha. Tumeishi katika janga kubwa. Tunadai haki zetu kwa sababu wametudhuru vibaya sana."
Ripoti ya shirika la Médecins Sans Frontières inaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 95 ya walionusurika Kaskazini mwa Darfur walisema walishambuliwa na mtu mwenye silaha. Kusini mwa Darfur, idadi hiyo ilikuwa asilimia 68.
Shirika hilo pia lilibaini kuwa manusura 1,395 katika Kusini mwa Darfur, sawa na asilimia 59.8, walishambuliwa na zaidi ya mtu mmoja katika shambulio lilelile.
Mkurugenzi Mkuu wa Médecins Sans Frontières Netherlands, Vicky Hawkins, alisema: "Tunajua kuwa ukatili wa kijinsia umefanywa na pande zote zinazopigana katika mzozo huu. Lakini kuendelea kwake Darfur kunatokana na miongo ya migogoro na kushindwa mara kwa mara kulinda raia na kuwawajibisha wahalifu."
Aliongeza: "Kuanguka kwa El Fasher mnamo Oktoba 2025 kulikuwa moja ya matukio ya kushtua zaidi, yakionyesha ukatili usiofikirika. Katika ripoti hii, wanawake na wasichana waliofanikiwa kutoroka mji huo walielezea mateso ya kutisha zaidi ambayo hakuna mtu anayepaswa kuyapitia."
"Hakuna usalama kabisa"
Avni Amin, mkuu wa kitengo kinachoshughulikia ukatili wa kijinsia katika Shirika la Afya Duniani (World Health Organization), alisema kuwa kupata huduma baada ya kubakwa ni jambo "gumu sana".
Alitoa kauli hiyo wakati wa hafla iliyofanyika Jumanne katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, ikijadili hali ya dharura ya kibinadamu na kiafya nchini Sudan.
Amin alitaja vikwazo kadhaa vinavyowazuia waathirika kupata huduma, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa usalama, ugumu wa kufikia vituo vya afya vinavyofanya kazi, unyanyapaa mkali unaowakumba waathirika, pamoja na uhaba wa wahudumu wa afya waliopata mafunzo ya kushughulikia kesi hizo.
Alisema: "Kwa kila mwanamke anayezungumza, kuna uwezekano wa wanawake wengine wanane au tisa ambao wamebakwa na wataendelea kuteseka kimya kimya."
Nimat Ahmadi kutoka Darfur Women's Action Group alielezea hali wanayopitia waathirika wakati wanatafuta matibabu kuwa ya kutisha, hasa baada ya kushambuliwa kwa ukatili unaosababisha madhara makubwa ya kiafya.
Ahmadi alisema kuwa hata wakati wa amani, kulikuwa na idadi ndogo sana ya madaktari Darfur wanaoweza kushughulikia kesi hizo, akiongeza: "Leo hii hawapo kabisa."
Alisisitiza kuwa wale wanaolazimika kuhama kwenda vituo vya matibabu hawana "usalama wowote," akibainisha kuwa waathirika husita kwenda hospitali zilizobaki kwa sababu mara nyingi ziko chini ya udhibiti wa pande zinazopigana.
Ahmadi alieleza tukio ambalo alisema wapiganaji wa Rapid Support Forces walivamia hospitali moja Darfur na kumbaka na kumuua mfanyakazi wa afya mwanamke.
Shoko Arakaki, mkurugenzi wa kitengo cha majibu ya kibinadamu katika United Nations Population Fund, alisema ni "muhimu sana" waathirika wa ukatili wa kijinsia kupata matibabu ndani ya saa 72.
Aliongeza: "Lakini hatuna huduma wala dawa" nchini Sudan, akisisitiza haja ya msaada wa kisaikolojia na kijamii kutokana na ongezeko la matatizo ya afya ya akili.
Arakaki alikiri kuwa "viwango vya kujiua ni vya juu".
Ingawa kupata takwimu rasmi ni ngumu, Nemat Ahmadi alisema anafahamu wanawake wengi waliojiua katika Jimbo la Al-Jazirah, kusini mashariki mwa Khartoum, kwa hofu ya kubakwa.
Avni Amin alisema msaada wa afya ya akili "lazima ujumuishwe" katika msaada kwa waathirika, akionya kuhusu "athari za muda mrefu" za uhalifu huo.
Aliongeza: "Tunajua kutoka migogoro mingine kwamba athari sio za muda mrefu tu, bali hupitishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Lazima tujiandae kwa hilo."













