Mtoto wa miaka sita mwenye Ebola aliyekuwa ametoweka DRC apatikana

Chanzo cha picha, Reuters
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka sita aliyekuwa akitibiwa ugonjwa wa Ebola na ambaye mamlaka za DRC zilikuwa zikimtafuta baada ya watu wenye silaha kuvamia hospitali aliyokuwa amelazwa, amepatikana na anaendelea vizuri, kwa mujibu wa afisa wa afya wa eneo hilo.
Siku ya Jumatano, Dk. Lubambo Maboko Gaston alisema kuwa mtoto huyo pamoja na mama yake walichukuliwa kutoka hospitalini katika mji wa mashariki wa Butembo na wanaume waliokuwa na hasira kali siku mbili kabla.
Haijulikani ikiwa wanaume hao walikuwa wanafahamiana na mtoto huyo, lakini hofu na mashaka kuhusu vituo vya matibabu ya Ebola vimekuwa vikienea katika kipindi cha mlipuko huu wa ugonjwa huo.
Siku ya Ijumaa, Dk. Gaston alisema mtoto huyo na mama yake walijitokeza katika kituo kingine cha matibabu ya Ebola kilichopo takribani kilomita 18 kutoka Butembo.
Akizungumzia hali ya mtoto huyo, alisema:
"Hali yake kwa sasa ni nzuri."
Vituo vya matibabu ya Ebola vimekuwa vikishambuliwa mara kadhaa wakati wa mlipuko huu unaoendelea. Kufikia sasa, zaidi ya watu 230 wamefariki dunia huku visa zaidi ya 890 vya Ebola vikithibitishwa.
Mamlaka za afya zinaendelea kuhimiza wananchi kushirikiana na wahudumu wa afya ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo na kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu kwa usalama.
Unaweza kusoma;




























