Shuti kali la Saibari laihakikishia Morocco ushindi muhimu

Chanzo cha picha, PA Media
Morocco ilipata bao la mapema dhidi ya Scotland katika Uwanja wa Boston na haikuangalia nyuma tena. Bao pekee la Atlas Lions lilifungwa na Ismael Saibari, ambaye alipenya nyuma ya safu ya ulinzi ya Scotland, akautuliza mpira uliopigwa kwa ustadi na Brahim Diaz, kisha akaupiga kwa nguvu ukampita Angus Gunn na kutinga juu ya nyavu.
Bao la Saibari liliweka rekodi mpya: lilikuwa bao la haraka zaidi hadi sasa katika Kombe la Dunia la FIFA 2026, na pia bao la haraka zaidi kuwahi kufungwa na Morocco katika mashindano hayo ya dunia.
Ushindi huo unaifanya Morocco kufikisha pointi nne na kuongoza Kundi C kabla ya mechi ya Brazil huko Philadelphia.
Baada ya mapumziko, mchezo uliendelea kuwa wa kasi na mashambulizi ya pande zote mbili. Saibari alikaribia kufunga bao la pili baada ya shuti lake lililopata mguso wa mchezaji wa Scotland kugonga mwamba wa juu, kufuatia Bilal El Khannouss kuvamia upande wa kushoto na kutoa pasi ya chini ndani ya eneo la hatari.
Morocco ilikaribia tena kufunga muda mfupi baadaye wakati El Khannouss alipokaribia kugeuza kona ya karibu iliyopigwa na Achraf Hakimi kuwa bao, lakini Angus Gunn aliokoa tena kwa ustadi.
Scotland iliongeza presha katika dakika 15 za mwisho. John McGinn, Ben Doak na Scott McTominay waliongoza mashambulizi mfululizo. Hata hivyo, muda uliisha kabla hawajafanikiwa, na Atlas Lions wakang'ang'ania ushindi muhimu.
Soma zaidi:


















