Mabaharia watatu wa India wauawa katika shambulio la Marekani dhidi ya meli ya mafuta

Chanzo cha picha, Centcom
Mabaharia watatu wa India wamethibitishwa kufariki dunia baada ya jeshi la Marekani kushambulia meli ya mafuta ya MT Settebello katika Ghuba ya Oman, ambayo Marekani ilidai ilikuwa imekiuka zuio lake dhidi ya bandari za Iran.
Meli hiyo ilishambuliwa Jumatano ikiwa na wafanyakazi 24 wa India. Kati yao, watu 21 waliokolewa. Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Waziri wa Usafirishaji wa India, Sarbananda Sonowal, alisema miili ya mabaharia hao watatu itarejeshwa nchini India hivi karibuni.
Siku ya Ijumaa, kampuni inayoendesha meli hiyo, iOS Marine, ilisema katika taarifa kwamba “haina uhusiano wowote na Iran au mafuta ya Iran.”
Marekani imeshambulia meli tatu katika eneo la Ghuba wiki hii, zote zikiwa na wafanyakazi wa India.
Siku ya Alhamisi, serikali ya India ilisema wafanyakazi wote 20 wa meli ya Jalveer walikuwa salama baada ya meli hiyo kushambuliwa karibu na Oman.
Siku tatu kabla ya hapo, wafanyakazi 24 wa India waliokuwa kwenye meli ya mafuta Marivex, ambayo ilikuwa imewekewa vikwazo, waliokolewa kabla ya meli hiyo kuzama.
Marekani ilithibitisha kuwa ilizishambulia meli zote mbili.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, CENTCOM ilisema kuwa moja ya ndege zake ilirusha “silaha za usahihi wa hali ya juu” kwenye chumba cha injini cha meli hiyo baada ya wafanyakazi wake “kushindwa mara kwa mara kufuata maelekezo.”
Hata hivyo, katika taarifa yake, iOS Marine ilikanusha madai ya CENTCOM kwamba meli hiyo ilipuuza maonyo na mawasiliano ya onyo yaliyotolewa na vikosi vya Marekani.
Unaweza kusoma;
















