Milio ya risasi yasikika katika uwanja wa ndege wa mji mkuu wa Niger

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Milipuko na milio ya risasi imesikika ikitokea uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Niger, Niamey, wakazi wameiambia BBC.
"Nilisikia milio ya kwanza ya risasi saa 06:00 (05:00 kwa saa za hapa) nilipokuwa msikitini. Lakini hali sasa imedhibitiwa," mtu mmoja alisema.
Milio ya risasi iliodumu kwa saa mbili, ilitoka kwenye mlango wa kuingia uwanja wa ndege, aliyeshuhudia aliambia shirika la habari la AFP.
Niger imekuwa ikipambana na uasi wa wanamgambo wa Kiislamu kwa muongo mmoja na mwezi Januari washukiwa wa jihadi walianzisha shambulio kwenye uwanja huo wa ndege.
Kama majirani zake, Burkina Faso na Mali, Niger inaongozwa na kikosi cha kijeshi ambacho kiliingia madarakani kwa sababu ya serikali kushindwa kushughulikia vurugu.
Wakazi wameiambia BBC kwamba shambulio la Alhamisi lilizuiwa na jeshi, ambalo sasa linawasaka washambuliaji waliokimbia ambao inasemekana waliacha silaha zao.
Mamlaka bado haijatoa maoni na hakuna kundi lililokiri kuhusika na shambulizi hilo. Lakini mshirika mmoja wa kundi la Islamic State alisema ndilo lililofanya shambulio la Januari.
























