Marekani na Uingereza zawakumbuka waathiriwa wa ghasia za uchaguzi Tanzania
Haya yanajiri wakati familia za waathiriwa zikiendelea kudai ukweli, uwajibikaji na haki kufuatia vifo vilivyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Muhtasari
- Ghasia za uchaguzi Tanzania: CHADEMA yatangaza siku saba za maombolezo
- Rais wa Nigeria Bola Tinubu aelekea Makka kuiombea nchi yake
- Watu 13 wafariki baada ya Urusi kushambulia kituo cha reli Ukraine
- KNCHR yataka mamlaka za Kenya kubaini aliko mwanaharakati wa Tanzania anayedaiwa kutekwa nyara
- Meli tatu za mafuta zaripotiwa kulipuka katika Mlango Bahari wa Hormuz
- Raia 27 wa Uganda wanaopigana Urusi wanahofiwa kufariki
- Mashirika ya kijamii Tanzania zataka waliohusika na vifo vya Oktoba 29 kuwajibishwa
- Marekani na Uingereza zawakumbuka waathiriwa wa ghasia za uchaguzi Tanzania
- Ethiopia yapokea ndege 12 za kivita za Su-35 kutoka Urusi
- Mchungaji amtambulisha mke wa pili kanisani, akidai Biblia inaruhusu wake wawili
- Hispania yaanza siku tatu za maombolezo baada ya ajali ya treni kuua watu 68
- Netanyahu adai vyama vya Kiarabu viliiba uchaguzi Israel
- Taarifa za maelfu ya maafisa wa uhamiaji Marekani zavujishwa baada ya udukuzi
- Tetesi za soka Alhamisi: Everton yafikiria kumsajili Marcus Rashford
- Maandamano Hispania baada ya ajali ya treni kuua watu 68
- Flávio Bolsonaro ajitangaza kuwa rais halali wa Brazil baada ya kuwasili Marekani
- Netanyahu kuendelea kuwa Waziri Mkuu wa mpito baada ya uchaguzi wa Israel kukosa mshindi wa wazi
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Beldeen Waliaula
Ghasia za uchaguzi Tanzania: CHADEMA yatangaza siku saba za maombolezo

Chanzo cha picha, Getty Images
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa wito kwa watu kuungana kuadhimisha siku saba za maombolezo, kuwakumbuka mamia ya watu waliofariki wakati wa maandamano yaliyotokea tarehe 29 mwezi Oktoba 2025 nchini Tanzania.
Katika taarifa iliyotolewa na Amani Golugwa Naibu katibu mkuu Chadema Bara, chama hicho kinawataka watu kuvaa nguo nyeusi, ili kuadhimisha maombolezo hayo.
“Itakuwa ni siku saba kuanzia leo tarehe 29 mwezi wa Oktoba hadi tarehe 4 mwezi Novemba kwa ajili ya kuwaenzi Watanzania wenzetu waliopoteza maisha yao,na kuwafariji waliojeruhiwa katika matukio ya Oktoba 29.”
Chama hicho kimewataka raia wote wa Tanzania kushiriki katika maombolezo hayo, kama ishara ya kuleta mshikamano.
“Tunaomba Watanzania wote wavae nguo nyeusi kipindi hiki, au kama umevaa nguo yenye rangi nyingine, ufunge kitambaa cheusi katika mkono wako wa kushoto kama ishara ya majonzi, kumbukumbu na mshikamano na familia zilizofiwa”
Aidha bendera zilizoko katika ofisi zote za chama cha CHADEMA zitapeperushwa nusu mlingoti, katika wa maombelezo kuwaenzi waliopoteza Maisha yao.
Soma pia:
Rais wa Nigeria Bola Tinubu aelekea Makka kuiombea nchi yake

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Rais wa Nigeria, Bola Tinubu Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, amesafiri kwenda mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia, kutekeleza ibada ya Umra, ambapo anatarajiwa kuiombea Nigeria, kulingana na taarifa iliyotolewa na ikulu ya taifa hilo.
Msemaji wa Rais huyo , Bayo Onanuga, amesema ziara hiyo itampa rais huyo mwenye umri wa miaka 74 fursa ya kutafakari kiroho, kujitolea katika ibada na kuiombea Nigeria kuwa na amani, umoja, utulivu na maendeleo endelevu.
Tinubu, ambaye ni Muislamu kutoka kusini mwa Nigeria, alisafiri mara ya mwisho kwenda Saudi Arabia kutekeleza ibada ya Umra mwaka 2022, alipokuwa akiwania urais wa nchi hiyo.
Safari ya Tinubu inakuja wakati Nigeria inatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwezi Januari, mwaka ujao, huku Nigeria ikiwa inakabiliwa na ukosefu wa usalama hasa kaskazini mwa taifa hilo.
Soma pia:
Urusi yashambulia reli Ukraine, 13 wafariki

Chanzo cha picha, State Emergency Service Of Ukraine
Watu 13 wameuawa nchini Ukraine, baada ya ndege isiyo na rubani kugonga eneo lililokuwa na watu wengi katika kituo cha reli cha Dnipro, kaskazini mwa nchi hiyo.
Kulingana na kiongozi wa eneo la Dnipropetrovsk, Oleksandr Hanzha, watu wasiopungua 10 wamejeruhiwa katika shambulio hilo, akiwemo mvulana wa miaka 11.
Kampuni ya reli ya Ukraine, Ukrzaliznytsia, imesema treni moja iliyokuwa ikielekea eneo la Zaporizhzhia ilikuwa kwenye kituo cha Dnipro wakati shambulizi hilo lilipotokea.
Urusi imekuwa ikilenga mara kwa mara mtandao mkubwa wa reli nchini Ukraine, lakini imekuwa ikikanusha kulenga raia kimakusudi.
Katika tukio jingine nchini Ukraine, wasichana wawili wenye umri wa miaka 15 waliuawa katika shambulio la kombora la Urusi katikati ya jiji la Chernihiv, kaskazini mwa nchi hiyo.
Soma pia:
KNCHR yahoji kutoweka kwa mwanaharakati wa Tanzania

Chanzo cha picha, Mitandaoni
Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu nchini Kenya (KNCHR) imeitaka mamlaka za Kenya kuchukua hatua za haraka kujua aliko mwanaharakati wa kisiasa kutoka Tanzania, Twaha Salim Mwaipaya, ambaye anadaiwa kutekwa katika Kaunti ya Machakos.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, tume hiyo imesema Mwaipaya alikuwa akisafiri kutumia teksi kwenda kuwatembelea marafiki zake eneo la Kamulu, siku ya Jumapili, Oktoba 25, wakati watu wasiojulikana waliposimamisha gari hilo na kumchukua kwa nguvu.
Kulingana na taarifa iliyopokelewa na tume hiyo, tukio hilo lilitokea takriban saa nane mchana, huku watu wanaodaiwa kumteka wakiwa katika msafara wa magari matatu.
KNCHR imesema mwanaharakati huyo bado hajulikani aliko, na kuongeza kuwa Mwaipaya alikimbilia Kenya mwaka wa 2025 kutoka Tanzania kwa kuhofia maisha na usalama wake.
Tume hiyo imeeleza wasiwasi wake kuhusu kile ilichokitaja kuwa mwenendo wa watu kupotezwa, kutekwa nyara na kuhamishwa kuvuka mipaka kinyume cha sheria, wakiwemo watu wanaoishi Kenya au waliokimbilia nchini humo kutafuta hifadhi.
Tume hiyo imesema Kenya inawajibu ya kuwalinda watu waliokatika hatari chini ya sheria za kimataifa na haki za kibinadamu.
Meli tatu za mafuta zaripotiwa kulipuka Hormuz

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Iran (IRGC) limesema meli tatu za mafuta zilizokiuka kanuni za Iran ziliwaka moto, baada ya kugonga mabomu yaliyotegwa baharini katika mlango bahari wa Hormuz.
Katika taarifa iliyotolewa na jeshi hilo, meli hizo zilizima mifumo yake ya rada na urambazaji na kupuuza maonyo yaliyotolewa jeshi hilo.
Meli hizo zinasemekana zilikuwa zikijaribu kuondoka kupitia njia ya kusini ya Mlango Bahari wa Hormuz ambayo Iran inasema haijaidhinishwa, na hapo ndipo ziligonga mabomu yaliyotegwa baharini na kulipuka.
Majina ya meli hizo, bendera za nchi zilizosajiliwa, wamiliki wake na hali za wahudumu wake bado hazijafahamika.
Hapo jana, Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani (CENTCOM) ilitaja madai ya maafisa wa Iran kwamba meli za kibiashara zilikuwa zikigonga mabomu katika Mlango Bahari wa Hormuz kuwa hayana msingi, na si ya kweli.
CENTCOM ilisema kuwa wameondoa mabomu yote ya baharini katika njia zote kuu za kimataifa katika mlango bahari wa Hormuz.
Soma pia:
Raia 27 wa Uganda wanaopigana Urusi wanahofiwa kufariki

Chanzo cha picha, Getty Images
Raia 27 wa Uganda waliojisajili na kujiunga na jeshi la Urusi kupigana vita vya Ukraine, wameripotiwa kuuawa, hii ni kulingana na barua iliyotolewa na ubalozi wa Uganda mjini Moscow.
Kulingana na shirika la habari la Reuters, barua hiyo ilikuwa na majina 11 ya raia wa Uganda waliothibitishwa kufariki huku wengine 16 miili yao bado haijaweza kupatikana.
Taarifa za wanaume kutoka Afrika kushawishiwa kwenda Urusi kwa ahadi za ajira na baadaye kujikuta katika mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine, zimekuwa zikiongezeka katika mataifa ya Afrika Mashariki.
Mwaka uliopita, Ukraine ilisema zaidi ya raia 1,400 kutoka nchi takribani 36 za Afrika walikuwa wakipigana pamoja na vikosi vya Urusi.
Mamlaka za Urusi zimekanusha kuwasajili raia wa Afrika kinyume cha sheria ili kupigana nchini Ukraine.
Soma pia:
Mashirika ya kijamii Tanzania yataka waliohusika na vifo vya Oktoba 29 kuwajibishwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Asasi za kiraia nchini Tanzania zinataka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote watakaothibitishwa kuhusika na vifo na ukiukwaji wa haki za binadamu wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka 2025.
Mashirika hayo yamesema kuwa mwaka mmoja baadaye baada ya maandamano ya Oktoba 29, bado hakuna uwazi wa kutosha kuhusu hatua za kuwawajibisha waliohusika.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa mapema leo, asasi hizo zimesema bado kuna maswali ambayo hayajajibiwa kuhusu mazingira ya vifo, watu waliopotea na miili ambayo familia zinasema hazikuweza kuzipata.
Kulingana na taarifa hiyo, Tume ya Jaji Chande iliripoti vifo vya watu 518, huku ikieleza kuwa takribani watu 700 hawakujulikana walipo. Tume hiyo pia ilieleza kuhusu miili takribani 39 ambayo ndugu waliripoti kuitambua katika vituo vya afya lakini baadaye hawakuweza kuzipata.
Hata hivyo, asasi hizo zinasema ripoti ya tume hiyo haikuwataja wazi watu au mamlaka waliohusika na vifo hivyo, walioamuru au kuruhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi, wala kutoa mwelekeo wa kutosha kuhusu namna ushahidi ulivyokusanywa, na utakavyotumika katika uchunguzi na mashtaka.
Asasi hizo zimeeleza kutoridhishwa na uamuzi wa kuunda Tume ya Jaji Lila baada ya Tume ya Jaji Chande kukamilisha kazi yake, zikisema hatua hiyo inaweza kusababisha kurudiwa kwa kazi, matumizi ya muda na rasilimali zaidi za umma, huku hatua za moja kwa moja za uwajibikaji wa kisheria zikicheleweshwa.
Badala yake, mashirika hayo ya kutetea haki za kibinadamu, zimetaka ripoti ya Tume ya Jaji Chande na ushahidi uliokusanywa kuwasilishwa kwa mamlaka husika za kikatiba na kisheria ili hatua zinazostahili zichukuliwe kwa haki na bila upendeleo.
Hata hivyo, asasi hizo zimesisitiza kuwa maridhiano haifai kuchukua nafasi ya uwajibikaji.
Taarifa hiyo ya pamoja imetolewa na mashirika mbalimbali, yakiwemo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Twaweza, Foundation for Civil Society, JamiiAfrica, Msichana Initiative, Tanganyika Law Society na Internet Governance Tanzania Working Group.
Soma pia:
Marekani na Uingereza zawakumbuka waathiriwa wa ghasia za uchaguzi Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images
Balozi za Marekani na Uingereza nchini Tanzania zimetoa ujumbe wa kumbukumbu na pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao katika ghasia zilizohusishwa na uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, balozi wa Marekani alisema jumuiya ya ubalozi imeungana kuwakumbuka waliopoteza maisha na kutoa pole kwa familia ambazo bado zinaomboleza huku zikiendelea kutafuta majibu kuhusu kilichosababisha vifo vya wapendwa wao.
“Tunawakumbuka waathiriwa hao na familia ambazo bado zinaomboleza na kutafuta majibu,” aliandika.
Balozi huyo alisisitiza kuwa vifo hivyo na mazingira yaliyozunguka ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi havipaswi kusahaulika. Akirejea kauli aliyoitoa wakati wa kusikilizwa na Seneti ya Marekani kabla ya kuthibitishwa rasmi kuwa balozi, alisema suala hilo halitapuuzwa.
“Jambo hili halitafagiliwa chini ya zulia,” alisema.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Uingereza nchini Tanzania alitoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao katika ghasia hizo, akieleza kuguswa na majonzi yanayoendelea kuzikabili familia zilizoathirika.
Kauli za wanadiplomasia hao zinakuja wakati familia za waathiriwa zikiendelea kudai ufafanuzi kuhusu mazingira ya vifo vya wapendwa wao na hatua za kuwawajibisha waliohusika na matukio hayo yaliyofuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Maelezo zaidi:
Ethiopia yapokea ndege 12 za kivita za Su-35 kutoka Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Abiy Ahmed Ethiopia imepokea ndege 12 za kivita aina ya Su-35 kutoka Urusi, huku mapigano yakiendelea katika eneo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo, karibu na mpaka wa Eritrea.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ambaye kwa sasa anahudhuria mkutano wa kilele wa Urusi na Afrika mjini Moscow, amesema kuwasili kwa ndege hizo ni hatua muhimu itakayoisaidia Ethiopia kuimarisha ulinzi wake.
Abiy aliongezea kuwa Ethiopia na Urusi zilitia Saini mktaba wa ulinzi miaka kadhaa iliyopita, na kwamba ndege hizo zimewasili mapema kabla ya muda ulioratibiwa.
Waziri huyo Mkuu pia aliongezea kuwa Ethiopia inapanga kununua mifumo minne ya ulinzi wa anga aina ya S-400 kutoka Moscow.
Kiongozi huyo wa Ethiopia amesema vifaa hivyo vya kijeshi ni muhimu katika kuilinda nchi yake dhidi ya vitisho vya nje.
Abiy, ambaye amemtaja Rais wa Urusi Vladimir Putin kama “rafiki wa karibu wa Ethiopia”, amesema Ethiopia sasa imekuwa nchi ya kwanza katika Kusini mwa Jangwa la Sahara kumiliki teknolojia hiyo ya kisasa ya kivita.
Urusi na Ethiopia zimetia saini mikataba kadhaa ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo mkataba wa mwaka 2021 wa kutoa mafunzo kwa wanajeshi na kuboresha teknolojia ya kijeshi.
Soma pia:
Saudi Arabia yaonya kuhusu hatari inayoweza kutokea Najran na mashariki mwa nchi

Chanzo cha picha, getty
Mamlaka ya Ulinzi wa Raia nchini Saudi Arabia imetoa tahadhari kuhusu hatari inayoweza kutokea katika eneo la Najran, kusini-magharibi mwa nchi hiyo, pamoja na maeneo ya mashariki.
Mamlaka hiyo imewataka wakazi wa maeneo hayo kujisitiri katika sehemu salama iliyo karibu nao.
Tahadhari hiyo inatolewa wakati mashambulizi ya waasi wa Houthi kutoka Yemen dhidi ya Saudi Arabia yakiendelea, yakilenga viwanja vya ndege, bandari na miundombinu ya mafuta.
Wakati huohuo, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umetangaza kuzuia na kuharibu kombora la balistiki lililorushwa na Houthi kutoka Yemen kuelekea mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa upande mwingine, vyombo vya habari vya Iran, vikirejea vyanzo vya Kiarabu, vimeripoti milipuko kadhaa katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Ras Tanura, mashariki mwa Saudi Arabia, vikihusisha milipuko hiyo na mashambulizi ya Houthi.
Vyombo hivyo pia vimedai kuwa shughuli katika kiwanda hicho zilisitishwa na safari za ndege katika Uwanja wa Ndege wa King Fahd zikakatizwa. Hata hivyo, madai hayo yanahitaji kuthibitishwa na vyanzo huru.
Oman yaonya kuhusu uwezekano wa vita vipya Mashariki ya Kati

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Busaidi, ameonya kuwa kuna uwezekano wa kuzuka kwa vita vingine Mashariki ya Kati.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha Channel 4 cha Uingereza, Busaidi amesema nchi za Ghuba zinapaswa kuendelea kuchukua nafasi ya uongozi katika masuala ya usalama wa Mashariki ya Kati.
Ametaka kuundwa kwa mfumo mpya wa usalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi, akisema nchi za eneo hilo zinapaswa kushiriki zaidi katika kulinda usalama wao badala ya kutegemea kwa kiwango kikubwa Marekani.
Kabla ya vita vya hivi karibuni, Oman ilikuwa ikipatanisha mazungumzo kati ya Iran na Marekani.
Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia alionya kuwa vita vipya au shambulizi la Israel dhidi ya Iran vinaweza kusababisha changamoto zaidi, zikiwemo athari kwa biashara ya kikanda na kimataifa.
Iran pia imeitaka Qatar kuheshimu masharti ya upatanishi na kudumisha msimamo wa kutopendelea upande wowote. Hata hivyo, msemaji wa Qatar aliwahi kusema kuwa Iran inapaswa kusitisha vitisho dhidi ya nchi za eneo hilo.
Wakati huohuo, ripoti zinaeleza kuwa Qatar imewasilisha rasimu mpya ya makubaliano kwa Iran, ingawa maelezo zaidi kuhusu pendekezo hilo hayajawekwa wazi.
Mchungaji amtambulisha mke wa pili kanisani, akidai Biblia inaruhusu wake wawili

Chanzo cha picha, LifeWorks Church
Mchungaji mmoja katika jimbo la Ohio, Marekani, amezua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii na miongoni mwa waumini baada ya kumtambulisha mke wake wa pili kwa waumini wa kanisa lake, huku mke wake wa kwanza akiunga mkono hatua hiyo.
Israel T. Ford, mwanzilishi na mchungaji mkuu wa kanisa la LifeWorks Church lililoko Wickliffe, karibu na mji wa Cleveland, alimtambulisha mke wake wa pili, Shakayla Ford, wakati wa ibada ya Jumapili hivi karibuni.
Katika video iliyorekodiwa wakati wa tukio hilo na kusambaa sana mtandaoni, mke wake wa kwanza ambaye pia ni mchungaji mwenza, Lydia Ford, alisimama madhabahuni kumkaribisha Shakayla, akimtaja kama “dada yangu katika ndoa.”
Baadaye, Shakayla alilihutubia kanisa na kufichua kuwa yeye na Mchungaji Ford walikuwa wameoana kwa siri kwa karibu miaka mitatu.
Utetezi wa kibiblia na ukosoaji
Baada ya tangazo hilo, Mchungaji Ford alitumia mitandao ya kijamii kutetea ndoa hiyo, akidai kuwa msimamo wa mwanamume kuwa na mke mmoja pekee ni mtazamo uliobuniwa na binadamu, wala si sharti la Biblia.
Akinukuu vifungu vya Agano la Kale, ikiwemo Kutoka 21:10, alisema kuwa mwanamume kuwa na wake wengi kunaruhusiwa kwa mujibu wa maandiko.
“Tumezoeshwa kama jamii kuamini kuwa mwanamume anaweza kuwa na mke mmoja tu. Hilo halipatani na mafundisho ya Biblia,” alisema Ford katika video aliyochapisha mtandaoni akijibu utata ulioibuka. Naelewa kuwa ukweli huu hauwapendezi watu wengi na kwamba viongozi wengi huepuka kuuzungumzia. Lakini jukumu langu si kuwapendeza watu, bali kufuata yale ambayo yamefunuliwa.”
Ford alikiri kuwa msimamo wake unaweza kuwafanya baadhi ya waumini kuondoka kanisani, akisema yuko tayari kupoteza waumini kutokana na uamuzi huo.
Mwitikio wa umma na masuala ya kisheria
Tangazo hilo limeibua hisia tofauti kwenye mitandao ya kijamii. Wasomi wa Kikristo na wakosoaji wamepinga tafsiri ya Ford ya maandiko, wakirejelea mafundisho ya Agano Jipya, hususan 1 Timotheo 3:2, ambayo inasema kuwa kiongozi wa kanisa anapaswa kuwa “mume wa mke mmoja.”
Pia, maswali yameibuka kuhusu uhalali wa mpango huo kisheria. Sheria za jimbo la Ohio zinakataza mtu kufunga ndoa na mtu mwingine wakati bado yuko kwenye ndoa halali na mtu mwingine.
Hata hivyo, haijabainika iwapo ndoa ya pili ya Ford ilisajiliwa rasmi kwa kupata leseni ya ndoa kutoka kwa mamlaka za serikali au ni makubaliano ya kidini pekee ndani ya kanisa lake.
Kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya watu walionyesha mshangao kuhusu tukio hilo, hasa kutokana na namna mke wa kwanza alivyomkaribisha mke wa pili madhabahuni. Wengine walimshutumu Ford kwa kutafsiri maandiko ya Biblia kwa namna inayolingana na maisha yake binafsi.
Pia unaweza kusoma:
Polisi, jeshi wenye silaha za moto watanda katika jiji la Dar es Salaam

Chanzo cha picha, Getty Images
Usalama unaendelea kuimarishwa kwenye miji mikubwa nchini Tanzania ambapo kumeshuhudiwa maafisa wa polisi na jeshi wenye silaa wakifanya doria, huku Serikali ikionya kuwa itachukua hatua dhidi ya mtu yeyote atakayehamasisha vurugu Alhamisi ya Oktoba 29.
Maafisa hao wameonekana kwa wingi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye mizunguko ya barabara na mitaa katika jiji kuu la kibiashara la Dar es Salaam na miji mingine.
Hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii, wanaharakati wamekuwa wakihamasisha kufanyika maandamano siku ya Jumanne, kushinikiza kuwepo kwa uhuru wa kisiasa na uwajibikaji kufuatia matukio ya mauaji yaliyotokea kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetangaza kufanyika kwa misa maalumu leo, kwa ajili ya kuwaombea na kuwakumbuka watu waliouawa, kujeruhiwa au kuathiriwa na matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu nchini humo.
Viongozi wa Chadema, chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, wamesema watahudhuria misa hiyo. Kwa upande wake, serikali imesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na kuwataka wananchi kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu nchini.
Misa hiyo inafanyika mwaka mmoja tangu ghasia zilizoshuhudiwa wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania. Hata hivyo, mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti kuhusu matukio hayo bado hayajaanza kutekelezwa.
Soma Pia:
Iran, Pakistan, Saudi Arabia na Uturuki zajadiliana kuhusu umoja wa kikanda

Chanzo cha picha, IRNA
Iran imesema mkutano wa mataifa manne uliofanyika mjini Tehran umekubaliana kuwa usalama wa kikanda unapaswa kusimamiwa na nchi za eneo hilo zenyewe, bila kuingiliwa na mataifa ya nje.
Kauli hiyo imetolewa na Mohsen Rezaei, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, baada ya kushiriki mkutano uliofanyika Jumatatu mjini Tehran, uliowahusisha maafisa waandamizi wa kijeshi na kijasusi kutoka nchi wanachama wa kile kinachoitwa Mkataba wa Mecca Pakistan, Saudi Arabia na Uturuki pamoja na Iran.
Akizungumza na Shirika la Habari la Iran la Sadavism, Rezaei amesema washiriki wamekubaliana kuwa usalama wa kikanda unapaswa kusimamiwa ndani ya eneo hilo, bila kuingiliwa na mataifa ya nje, yakiwemo nchi nyingine za eneo hilo.
Aidha, amesema washiriki walisisitiza kuwa Israel inapaswa kuondoka kusini mwa Lebanon, kusini mwa Syria, Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Rezaei ameelezea ziara ya maafisa waandamizi wa kijeshi na kijasusi kutoka Pakistan, Saudi Arabia na Uturuki nchini Iran kuwa ishara kuwa vitisho vya Marekani dhidi ya Iran havijafanikiwa.
Amesema pia ana matumaini kuwa mkutano huo utakuwa mwanzo wa hatua za vitendo kuelekea umoja wa kikanda.
Hispania yaanza siku tatu za maombolezo baada ya ajali ya treni kuua watu 68

Chanzo cha picha, 1vanta3 / X via Anadolu / Getty Images
Hispania imeanza siku tatu za maombolezo kufuatia ajali ya treni iliyoua watu 68 na kujeruhi wengine kadhaa, katika mojawapo ya ajali mbaya zaidi za reli barani Ulaya katika miaka ya hivi karibuni.
Waokoaji walifanya kazi usiku kucha wakikata mabaki ya mabehewa yaliyobondeka kuwatafuta wahanga. Baadhi ya waliofariki bado hawajatambuliwa.
Mamlaka zinaendelea kuchunguza chanzo cha ajali hiyo iliyotokea Jumatano asubuhi, wakati treni iliyokuwa ikisafiri kutoka Madrid kuelekea Seville ilipogonga treni nyingine iliyokuwa imesimama kwenye reli.
Waziri Mkuu Pedro Sánchez amesema taifa lote la Hispania linaomboleza, akieleza kuwa familia zimevunjika moyo na maumivu ni makubwa.
Wizara ya Mambo ya Ndani imesema mamia ya wafanyakazi wa uokoaji wamepelekwa eneo la ajali, huku ndege zisizo na rubani na helikopta zikitumika kutafuta wahanga na kuondoa vifusi.
Waziri wa Uchukuzi Óscar Puente amesema treni iliyokuwa imesimama, inayoendeshwa na kampuni binafsi ya Iryo, ilikuwa na abiria 147 na ilisimama kwenye reli kutokana na hitilafu ya mfumo wa kompyuta.
Soma Pia:
Netanyahu adai vyama vya Kiarabu viliiba uchaguzi Israel

Chanzo cha picha, Reuters
Chama cha Likud cha Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kimevituhumu vyama vya Kiarabu nchini humo kwa kuiba uchaguzi kupitia rushwa, vitisho, vurugu na udanganyifu wa kura.
Katika taarifa yake, Likud imesema imewasilisha mamia ya ushahidi kwa polisi, shirika la usalama wa ndani la Israel, Shin Bet, pamoja na maafisa wa uchaguzi.
Netanyahu amesema: “Uchaguzi katika Taifa la Israel uliibiwa na vyama vya Kiarabu vinavyounga mkono ugaidi na kuondolewa kwa taifa la Wayahudi.”
Aidha, Netanyahu amedai kuwa vyama hivyo vilitumia vitisho, rushwa, vurugu, kughushi nyaraka na programu zilizopigwa marufuku kuwahamasisha wapiga kura.
Hata hivyo, madai hayo ni ya chama cha Likud na bado hayajathibitishwa kama ukweli na mamlaka husika.
Kura zinaendelea kuhesabiwa nchini Israel huku matokeo yakitangazwa kwa kasi. Hata hivyo, miungano miwili mikuu ya kisiasa inayowania kuunda serikali inaonekana kukosa wingi wa viti bungeni unaohitajika kupata ushindi wa wazi.
Ushiriki wa wapiga kura umefikia rekodi ya zaidi ya asilimia 77, lakini kama ilivyotarajiwa, uchaguzi huo unaelekea kuacha mkwamo wa kisiasa.
Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa vyama vinavyoongozwa na Waarabu vinaweza kupata takriban viti 19 bungeni. Hali hiyo inaweza kuvipa vyama hivyo nafasi muhimu katika kuamua ni upande gani utakaopata uungwaji mkono wa kutosha kuunda serikali.
Soma Pia:
Taarifa za maelfu ya maafisa wa uhamiaji Marekani zavujishwa baada ya udukuzi

Chanzo cha picha, Reuters
Taarifa za zaidi ya wafanyakazi 41,000 wa Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani (DHS), wakiwemo maelfu ya maafisa wanaotekeleza sheria za uhamiaji, zimevujishwa na kuwekwa hadharani baada ya udukuzi mkubwa.
Taarifa hizo zinajumuisha majina, anwani za kazini na nambari za simu za wafanyakazi wa wizara hiyo, wakiwemo maafisa wa Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE) na Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka (CBP). Pia zinaeleza majukumu yao katika idara husika.
Taarifa hizo zilivujishwa Jumatano, ikiwa ni mara ya tatu katika wiki za hivi karibuni kwa taasisi ya serikali ya Marekani kukumbwa na uvujaji wa taarifa au udukuzi.
Msemaji wa DHS amesema wizara hiyo inafahamu kuhusu uwezekano wa ukiukaji wa usalama wa taarifa na inachukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo.
“Tunachukulia kwa uzito vitisho vyote vya usalama vinavyolenga wafanyakazi na maafisa wetu, na tutahakikisha wanalindwa ipasavyo,” alisema msemaji huyo, akiongeza kuwa umma utaarifiwa zaidi taarifa zitakapopatikana.
Uvujaji huo ulitangazwa kupitia mtandao baada ya kundi linalojiita Department of Peace kupata taarifa hizo kutoka kwa DHS.
Mtafiti wa usalama wa mtandao na mwanahabari Maia Crimew, kwa kushirikiana na tovuti ya Distributed Denial of Secrets, waliweka taarifa hizo hadharani.
Taarifa hizo ziliwekwa katika hifadhidata iliyopewa jina la Icepick.
Soma Zaidi:
Tetesi za soka Alhamisi: Everton yafikiria kumsajili Marcus Rashford

Chanzo cha picha, Getty Images
Everton inafikiria kumsajili mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, mwenye umri wa miaka 28.
Winga wa England, Jadon Sancho, amekataa ofa ya kujiunga na Getafe ya La Liga nchini Hispania, lakini ana ofa kutoka Saudi Arabia. Sancho mwenye umri wa miaka 26 amekuwa mchezaji asiye na klabu tangu alipoondoka Manchester United majira ya kiangazi.
Mshambuliaji wa Ufaransa, Désiré Doué, mwenye umri wa miaka 21, yuko kwenye mazungumzo na Paris Saint-Germain kuhusu kuongeza mkataba wake. PSG inalenga kuhakikisha inaendelea kuwa na huduma yake kwa muda mrefu, huku Arsenal, Chelsea na Manchester City zikionyesha nia ya kumsajili.
Liverpool imewasiliana na Monaco kuhusu kiungo wa Senegal, Lamine Camara, mwenye umri wa miaka 22. Camara alikaribia kujiunga na Chelsea katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
Chelsea bado inamfuatilia beki wa Everton, Jarrad Branthwaite, mwenye umri wa miaka 24, lakini inakabiliwa na ushindani kutoka Manchester United.
Everton pia inamfuatilia mshambuliaji wa Real Sociedad na timu ya taifa ya Iceland, Orri Óskarsson, mwenye umri wa miaka 22, huku klabu hiyo ikitafuta kuimarisha safu yake ya ushambuliaji.
Chelsea inafikiria kumsajili kiungo wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Fermín López. Hata hivyo, Paris Saint-Germain pia inamuwania mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23.
Leeds United itajaribu kumsajili beki wa kushoto wa Porto na timu ya taifa ya Nigeria, Zaidu Sanusi, mwenye umri wa miaka 29, katika dirisha la usajili la Januari.
Arsenal, Manchester United na Chelsea ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kiungo wa Como, Nico Paz. Hata hivyo, klabu hiyo ya Serie A haina nia ya kumuuza mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 22.
Soma pia:
Maandamano Hispania baada ya ajali ya treni kuua watu 68

Chanzo cha picha, EPA
Maandamano yamezuka mjini Madrid, Hispania, kufuatia ajali mbaya zaidi ya treni nchini humo katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja, huku waandamanaji wakitaka serikali iwajibike.
Waandamanaji wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia wanamtaka Waziri wa Uchukuzi, Oscar Puente, ajiuzulu, wakiishutumu serikali kwa kushindwa kuhakikisha usalama wa safari za treni.
Takriban waandamanaji 500 walikusanyika nje ya Wizara ya Uchukuzi mjini Madrid, wakielekeza hasira zao kwa mamlaka. Polisi wa kutuliza ghasia waliwatawanya waandamanaji kwa kurusha mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya.
Takriban watu 68 wamefariki baada ya treni ya mwendo kasi kugongana na treni iliyokuwa imesimama karibu na mji wa Adamuz.
Wachunguzi wanaendelea kuchunguza chanzo cha ajali hiyo, ikiwemo taarifa za uwezekano wa hitilafu katika mfumo wa ishara za reli.
Ajali hiyo inatokea baada ya ajali nyingine mbaya ya treni mwezi Januari iliyosababisha vifo vya watu 46 katika njia hiyo hiyo ya reli ya mwendo kasi.
Maafa hayo yameibua maswali kuhusu usalama wa usafiri wa reli nchini Hispania na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuzuia ajali nyingine.



















