Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi IV wa Ufalme wa Tooro magharibi mwa Uganda, ambaye alifariki mwezi uliopita baada ya kupambana na saratani, amezikwa katika Makaburi ya Kifalme ya Karambi magharibi mwa Uganda.
Mfalme huyo, ambaye alitawazwa tarehe 12 Septemba 1995 kufuatia kifo cha baba yake, alizikwa katika tarehe hiyo hiyo aliyotawazwa kuwa mfalme miaka 31 iliyopita.
Shughuli ya kumuaga ilifanyika katika hafla ya faragha kabisa kulingana na mila za kifalme za Tooro, huku marafiki wachache wa karibu na familia wakihudhuria.
Kwa kuzingatia taratibu za muda mrefu za mazishi ya kifalme, wananchi na vyombo vya habari hawakuruhusiwa kushuhudia dakika hizo za mwisho za faragha, na hakuna kamera zilizoruhusiwa eneo la kaburi.
Mnamo saa 3:16 asubuhi kwa saa za eneo hilo, jeneza lililobeba mwili wake, likiwa limefunikwa kwa rangi rasmi za Ufalme wa Tooro za njano na bluu, liliondoka Ikulu ya Karuziika mjini Fort Portal kwa mara ya mwisho.
Maelfu ya waombolezaji walikusanyika katika Kanisa Kuu la St. John, kanisa lililojengwa na babu yake Mfalme Oyo, Omukama Rukidi III, na ambapo mfalme huyo marehemu alibatizwa.
Miongoni mwa waliohudhuria walikuwa maafisa wa serikali, viongozi wa ngazi za juu, na wawakilishi wa falme na utawala wa machifu wa jadi kutoka Uganda, Kenya, Sudan Kusini, Nigeria na Eswatini.
Kwa kuzingatia mila za Tooro, ‘Omusuna’ msimamizi mkuu wa masuala ya kifalme mwenye jukumu la kuzika wafalme, ndiye aliyeongoza taratibu za mazishi.
Miongoni mwa desturi zilizotekelezwa ni kitendo cha mfalme mpya kutupa punje tisa za kahawa kaburini kama ishara maalum.
Kifo cha Mfalme Oyo kimezua mzozo wa kurithi kiti cha ufalme ndani ya familia ya kifalme.
Mama yake na baadhi ya wanafamilia ya kifalme wamepinga uteuzi wa Edward Rukidi Kijanangoma, ambaye ni mwandishi wa habari wa televisheni, kuwa mrithi wa kiti hicho, wakisisitiza kuwa mwana wa marehemu mfalme ndiye anayepaswa kumrithi.
Hata hivyo, Baraza la Wazee wa Tooro limeunga mkono uamuzi wa ukoo wa kifalme wa kumteua Mwana wa Mfalme Edward Rukidi Kijanangoma kuwa kiongozi ajaye wa Ufalme wa Tooro.
Wakati wa ibada ya mazishi, Mkuu wa Ukoo wa Kifalme, Omusuuga Charles Kamurasi, alisisitiza kuwa uamuzi wa ukoo huo hautabadilika.
"Tunaye mfalme mpya, Edward Rukidi Kijanangoma. Kila hatua tuliyochukua imezingatia sheria na kuongozwa na mila na desturi za Tooro. Tudumishe amani na tutulie," alisema Kamurasi.
Serikali ya Uganda ilimfanyia Mfalme Oyo mazishi ya kitaifa na kutangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa heshima yake.
Kama sehemu ya taratibu za mazishi ya kitaifa, marehemu mfalme alipewa heshima ya kupigwa mizinga tisa, ishara ya heshima inayotolewa kwa viongozi na watu mashuhuri wa taifa.
Safari ya mwisho ya Mfalme kuelekea Makaburi ya Kifalme Mamia ya waombolezaji walikusanyika kando ya barabara inayoelekea kwenye Makaburi ya Kifalme ya Karambi, wakiwa na huzuni huku wakimsindikiza Mfalme wao hadi mahali pake pa kupumzikia pa mwisho.
Mazishi hayo yalihitimisha kipindi cha utawala ambacho kilimfanya Mfalme Oyo kuwa mmoja wa wafalme waliodumu kwa muda mrefu zaidi barani Afrika, akiwa amevishwa taji hilo akiwa na umri wa miaka mitatu.