Raia wa kigeni waliobaki Kenya waeleza wasiwasi kuhusu usalama wao

Chanzo cha picha, BBC/Brian Khisa
Kwa Ndaikech Ali, ambaye amekuwa akizunguka mitaa ya mji mkuu wa Kenya akijipatia riziki kama dereva wa tuk-tuk kwa miaka tisa iliyopita, msongamano wa magari jijini Nairobi, na si chuki dhidi ya wageni, ndilo limekuwa suala linalompa wasiwasi mkubwa zaidi.
Raia huyo wa Burundi anasema kuwa katika muda wake wote nchini humo, amekuwa akiwaona Wakenya kuwa watu wenye urafiki na ukarimu,hali iliyobadilika wiki iliyopita, wakati rais alipoagiza kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wageni wanaofanya biashara ndogondogo.
"Sasa wamegeuka dhidi yetu," aliambia BBC katika ubalozi wa Burundi jijini Nairobi, ambapo watu wengi wamekuwa wakipanga foleni wiki hii kupata nyaraka za kuwaruhusu kurejea nyumbani.
"Vitisho ni vingi... hata kutoka kwa watoto," alisema, na kuongeza, "Ni kana kwamba tumeshambuliwa na mbwa aliyeachiwa huru. Tumeumwa."
Rais William Ruto alitoa kauli hiyo wiki iliyopita alipokuwa akihutubia wafanyabiashara wa Kenya waliokusanyika Ikulu, akirejelea muswada uliopo bungeni unaolenga kuwazuia raia wa kigeni kufanya biashara ndogondogo na kuweka sheria ya kutumia vifaa vinavyopatikana nchini kwa shughuli mbali mbali.
Katika hotuba yake, alisema kuwa raia wote wa kigeni wanaofanya biashara ndogondogo walikuwa na muda hadi tarehe 7 Septemba kufunga biashara zao, akisisitiza kuwa kazi za aina hiyo zinapaswa kutengwa kwa ajili ya Wakenya pekee.
Ali, kama wengine, aliingiwa na hofu, akisema ilionekana kuwa tangazo la rais lilitafsiriwa na baadhi ya Wakenya kama ishara kwamba raia wa kigeni hawakaribishwi tena nchini humo.
"Tunakabiliwa na unyanyasaji na hatuwezi kufanya kazi," anasema. "Kazi zetu zikisimamishwa, tunapoteza kipato kinachotuwezesha kulipa kodi ya nyumba na kununua chakula. Kazi hizo zinapoondolewa, chaguo pekee lililosalia ni kurejea nyumbani."
Pia unaweza kusoma:




















