Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump aituhumu Iran kuhusika katika shambulio Saudi Arabia

Rais wa Marekani Donald Trump amesema huenda Iran ilihusika katika shambulio la anga lililolenga bomba kuu la mafuta la Saudi Arabia.

Moja kwa moja

Na Sarafina Robi & Mariam Mjahid

  1. Katika picha: Mamia ya waombolezaji waelekea atakapozikwa mfalme Oyo wa Tooro Uganda

  2. Raia wa kigeni waliobaki Kenya waeleza wasiwasi kuhusu usalama wao

    Kwa Ndaikech Ali, ambaye amekuwa akizunguka mitaa ya mji mkuu wa Kenya akijipatia riziki kama dereva wa tuk-tuk kwa miaka tisa iliyopita, msongamano wa magari jijini Nairobi, na si chuki dhidi ya wageni, ndilo limekuwa suala linalompa wasiwasi mkubwa zaidi.

    Raia huyo wa Burundi anasema kuwa katika muda wake wote nchini humo, amekuwa akiwaona Wakenya kuwa watu wenye urafiki na ukarimu,hali iliyobadilika wiki iliyopita, wakati rais alipoagiza kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wageni wanaofanya biashara ndogondogo.

    "Sasa wamegeuka dhidi yetu," aliambia BBC katika ubalozi wa Burundi jijini Nairobi, ambapo watu wengi wamekuwa wakipanga foleni wiki hii kupata nyaraka za kuwaruhusu kurejea nyumbani.

    "Vitisho ni vingi... hata kutoka kwa watoto," alisema, na kuongeza, "Ni kana kwamba tumeshambuliwa na mbwa aliyeachiwa huru. Tumeumwa."

    Rais William Ruto alitoa kauli hiyo wiki iliyopita alipokuwa akihutubia wafanyabiashara wa Kenya waliokusanyika Ikulu, akirejelea muswada uliopo bungeni unaolenga kuwazuia raia wa kigeni kufanya biashara ndogondogo na kuweka sheria ya kutumia vifaa vinavyopatikana nchini kwa shughuli mbali mbali.

    Katika hotuba yake, alisema kuwa raia wote wa kigeni wanaofanya biashara ndogondogo walikuwa na muda hadi tarehe 7 Septemba kufunga biashara zao, akisisitiza kuwa kazi za aina hiyo zinapaswa kutengwa kwa ajili ya Wakenya pekee.

    Ali, kama wengine, aliingiwa na hofu, akisema ilionekana kuwa tangazo la rais lilitafsiriwa na baadhi ya Wakenya kama ishara kwamba raia wa kigeni hawakaribishwi tena nchini humo.

    "Tunakabiliwa na unyanyasaji na hatuwezi kufanya kazi," anasema. "Kazi zetu zikisimamishwa, tunapoteza kipato kinachotuwezesha kulipa kodi ya nyumba na kununua chakula. Kazi hizo zinapoondolewa, chaguo pekee lililosalia ni kurejea nyumbani."

    Pia unaweza kusoma:

  3. Trump aituhumu Iran kuhusika na shambulio Saudi Arabia

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema huenda Iran ilihusika katika shambulio la anga lililolenga bomba kuu la mafuta la Saudi Arabia.

    Shambulio hilo lilisababisha kusitishwa kwa shughuli za bomba lakusafirisha mafuta, mojawapo ya njia kuu za Saudi Arabia kusafirisha mafuta bila kupitia Mlango wa Hormuz.

    Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dublin, Trump alipoulizwa iwapo Iran ilihusika, alisema:

    “Nadhani wanahusika, huenda wanahusika.”

    Rais Trump pia amesema amezungumza na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kuhusu hali hiyo.

    Hata hivyo, Iran haijazungumzia kuhusu shambulio hilo lililolenga mabomba ya kusafirishia mafuta duniani.

    Wakati huo huo, Trump amesema wapiganaji wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen wamewasiliana na utawala wake na kueleza kuwa hawataki Marekani kuingilia moja kwa moja mzozo huo.

    Kwa mujibu wa Trump, Houthi wameweka kizuizi dhidi ya meli za Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu, huku wakidhibiti eneo la mkondo wa Bab el Mandeb kutoka kwa serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia.

    Trump amesema Houthi wameashiria kuwa wako tayari kuruhusu meli nyingi kuendelea kupita katika eneo hilo.

    Rais huyo wa Marekani pia amerudia kauli yake kwamba vita dhidi ya Iran vinaweza kumalizika muda mfupi baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani mwezi Novemba.

    Amesema kumalizika kwa vita hivyo kutasababisha bei ya mafuta kushuka kwa kiasi kikubwa.

    Trump amesema, "Nadhani itakuwa hivi karibuni. Huenda ikawa mara tu baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula."

    Ameongeza kuwa Iran haiwezi kuruhusiwa kumiliki silaha za nyuklia.

  4. Wahouthi wasonga kwa kasi Tihama, wakiteka kilomita 130 za pwani ya Yemen

    Kusonga kwa kasi kwa Wahouthi katika eneo kubwa la tambarare ya pwani ya Tihama, kusini mwa Yemen, kunaonekana kuwashangaza wachunguzi wengi.

    Tihama ni eneo kame la tambarare ya pwani nchini Yemen. Hadi hivi karibuni, muungano unaopinga Wahouthi unaojulikana kama ‘National Resistance’ ulikuwa ukidhibiti eneo kubwa kando ya pwani ya Bahari ya Shamu, lakini ndani ya siku chache, sehemu kubwa ya eneo hilo imeangukia mikononi mwa Wahouthi.

    Kwa mujibu wa baadhi ya makadirio, vikosi vya Wahouthi vinavyoungwa mkono na Iran vimetwaa hadi kilomita 130 za pwani ya Yemen yenye umuhimu wa kimkakati.

    Hii ni mafanikio makubwa zaidi ya kijeshi ya Wahouthi katika miaka ya hivi karibuni, yakionyesha kuwa licha ya miaka 12 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, mashambulizi makali ya anga ya Saudi Arabia, pamoja na mashambulizi ya Marekani, Israel na Uingereza, Wahouthi bado ni nguvu inayopaswa kuzingatiwa.

    “Kwa kuwa sasa wamefika huko, wataimarisha udhibiti wao, na itakuwa gharama kubwa zaidi kuwaondoa,” Hisham al-Ameisi, mchambuzi mwandamizi katika Taasisi ya Ulaya ya Amani yenye makao yake Brussels, aliiambia BBC.

    Afisa mmoja aliambia mashirika ya habari ya Reuters na AFP kuwa boti zilizobeba wapiganaji wenye silaha wa Houthi zilifika katika Kisiwa cha Baryim/Miyun,ambacho hugawanya mlango bahari huo katika njia mbili za meli, baada ya vikosi vya serikali kuondoka eneo hilo siku ya Alhamisi.

    Afisa huyo, aliyeomba kutotajwa jina, aliongeza, "Wahouthi wametwaa udhibiti kamili wa eneo la Bab al-Mandab na Kisiwa cha Miyun kilicho katikati ya mlango bahari huo."

    Shahidi mmoja alisema kuwa wanamgambo wa Houthi "wamesambaa kando ya pwani ya Bab al-Mandab, na wanazunguka kwa kutumia magari ya kijeshi."

    Pia unaweza kusoma:

  5. Mfalme Oyo alikuwa kiongozi mwenye maono - Uhuru Kenyatta

    Rais wa zamani Uhuru Kenyatta ametoa rambirambi kufuatia kifo cha Mfalme Oyo wa Tooro, akielezea kifo chake cha ghafla kuwa pigo kubwa kwa Ufalme wa Tooro, Uganda na eneo zima la Afrika Mashariki.

    Kupitia mtandao wa X, katika ujumbe wake kwa Rais Yoweri Kaguta Museveni, rais huyo wa zamani alitoa pole kwa Rais Museveni, Mama Janet, familia ya kifalme ya Tooro na wananchi wa Uganda.

    Rais Kenyatta alimsifu Mfalme Oyo kwa maono yake, uongozi na kujitolea kwake kushirikiana na serikali kuu pamoja na serikali za mitaa ili kuendeleza ustawi na maisha bora ya watu wake.

    Alibainisha kuwa kifo cha Mfalme huyo kinaacha pengo kubwa litakalohisiwa kwa vizazi vijavyo, huku akionyesha mshikamano na Rais Museveni pamoja na familia ya kifalme katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Waziri Mkuu wa Ethiopia na Rais wa Iran wajadili usalama katika Bahari ya Shamu

    Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, amefanya mazungumzo na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, kuhusu usalama wa Bahari ya Shamu na utulivu wa eneo hilo, pembezoni mwa Mkutano wa BRICS.

    Katika ujumbe kupitia X, Abiy alisema mazungumzo hayo yalilenga maendeleo ya hali ya usalama katika Bahari ya Shamu na eneo kwa ujumla, huku wakisisitiza umuhimu wa mazungumzo na utulivu wa kikanda.

    Mkutano huo unafanyika wakati Bahari ya Shamu ikiendelea kuwa eneo muhimu la kiusalama, huku mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara, mivutano nchini Yemen na hali ya sintofahamu Mashariki ya Kati ikiendelea kuathiri njia za biashara za baharini.

    Nia ya Ethiopia ya kupata njia ya uhakika ya kufikia bahari imeongeza mvutano na nchi jirani ya Eritrea, huku masuala ambayo hayajatatuliwa kutokana na vita vya Tigray yakiendelea kutatiza uhusiano kati ya Addis Ababa na Asmara.

    Ethiopia na Iran ni miongoni mwa wanachama wa BRICS iliyopanuliwa, ambayo imezidi kuwa jukwaa la majadiliano kuhusu masuala ya kisiasa na kiusalama duniani, sambamba na ushirikiano wa kiuchumi.

    Abiy hakufichua iwapo suala la azma ya Ethiopia ya kupata ufikiaji wa bahari lilijadiliwa moja kwa moja katika mkutano huo.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Mfalme Oyo wa Tooro: Kutoka kutawazwa akiwa mtoto hadi kifo chake

    Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi IV alizaliwa Aprili 16, 1992, katika familia ya kifalme ya Ufalme wa Tooro, magharibi mwa Uganda.

    Alikuwa mwana wa kiume wa aliyekuwa Mfalme wa Tooro, marehemu Patrick David Mathew Rwamuhokya Kaboyo Olimu III, na mama yake ni Best Kemigisha.

    Oyo alitawazwa kuwa Mfalme wa Tooro Septemba 12, 1995, akiwa na umri wa miaka mitatu pekee, kufuatia kifo cha baba yake. Kutawazwa kwake kulimfanya kuwa mfalme mdogo zaidi duniani wakati huo, na kumuweka katika uangalizi wa kimataifa.

    Kutokana na umri wake mdogo, shughuli za ufalme ziliendeshwa na walezi pamoja na viongozi wakuu wa familia ya kifalme.

    Oyo alianza masomo katika Shule ya Msingi ya Aga Khan jijini Kampala, kabla ya kuendelea na masomo nje ya nchi, ambako alisomea Usimamizi wa Biashara na Mifumo ya Taarifa za Kibiashara.

    Alipokua na kufikia utu uzima, Mfalme Oyo alianza kushiriki kikamilifu zaidi katika masuala ya ufalme.

    Aliongoza na kuunga mkono mipango katika sekta za elimu, kilimo, uwezeshaji wa vijana, uhifadhi wa mazingira, utalii na afya. Pia alishiriki katika kampeni zilizolenga kuboresha maisha ya vijana.

    Mwaka 2016, Oyo aliteuliwa kuwa Balozi wa Hisani wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS). Kupitia nafasi hiyo, alihamasisha vijana kuhusu maambukizi ya VVU na UKIMWI katika Afrika Mashariki na Kusini.

    Mfalme Oyo pia alikuwa na shauku kubwa katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya utalii. Miongoni mwa juhudi zake ilikuwa kutangaza Milima ya Rwenzori na kuunga mkono mipango ya kulinda Mto Mpanga pamoja na mazingira kwa ujumla.

    Baada ya miaka 31 kwenye kiti cha ufalme, Mfalme Oyo alifariki Agosti 27, 2026, akiwa na umri wa miaka 34, baada ya kuugua saratani.

    Alifariki nchini Marekani, ambako alikuwa akipokea matibabu.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Mvua kubwa yashuhudiwa maeneo mengi pwani Kenya, msimu wa Elnino ukianza

    Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu, Idara ya Serikali ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na Mamlaka ya Hali ya Hewa Kenya zimesema katika utabiri wao wa jumla kuwa mvua inatarajiwa kunya katika kipindi cha siku saba, kuanzia Septemba 8 hadi 14, 2026. Baadhi ya maeneo katika Kaunti za Lamu, Kilifi, Tana River, Mombasa, Kwale, Narok na Bomet yanatarajiwa kupata mvua.

    Utabiri huo, uliotolewa Ijumaa, Septemba 11, unaonyesha kuwa mvua hizo zitanyesha zaidi wakati wa mchana, huku baadhi ya maeneo yakitarajiwa kupata mvua nyepesi asubuhi.

    Katika ukanda wa Pwani, Mombasa inatarajiwa kupata mvua ya kiwango cha chini kila asubuhi katika kipindi hicho, huku hali ya hewa ikitarajiwa kuwa ya jua wakati wa mchana, isipokuwa Jumanne.

    Joto la mchana linalozidi nyuzi joto 30 linatarajiwa katika kaunti kadhaa, zikiwemo Kilifi, Tana River, Lamu, Garissa, Wajir, Isiolo, Marsabit na Turkana.

    Kwa upande mwingine, baadhi ya maeneo katika Kaunti za Meru, Tharaka Nithi, Kirinyaga, Murang’a, Nyeri, Nyandarua, Laikipia, Nakuru, Narok, Taita-Taveta na Kajiado yanatarajiwa kuwa na wastani wa joto la chini ya nyuzi joto 10 wakati wa usiku.

    Wakenya wametakiwa kujiandaa kwa mvua za wastani hadi kubwa katika maeneo mbalimbali ya nchi katika kipindi cha siku tano, kuanzia Jumapili, Septemba 13 hadi Alhamisi, Septemba 17, 2026.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Gazeti la Financial Times: Marekani yataka meli za mafuta zinazopita Hormuz kusafiri wakati maalum

    Gazeti la Financial Times limeripoti kuwa Marekani imezitaka meli za mafuta zinazopita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz kusafiri wakati maalum pekee ili kuhakikisha zinapata ulinzi wa kijeshi.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ombi hilo lilikuja baada ya Iran kuongeza mashambulizi dhidi ya meli zinazosafiri nyakati za usiku.

    Ripoti hiyo inaeleza kuwa tangu mwezi Mei, Marekani imekuwa ikitoa ulinzi wa anga kwa meli zinazojaribu kupita katika njia iliyo kando ya pwani ya Oman, upande wa kusini wa mlango-bahari huo.

    Financial Times iliripoti, ikinukuu barua pepe zilizotumwa na Kituo cha Uratibu cha Jeshi la Wanamaji la Marekani kwa washauri wa masuala ya majini, kuwa muda wa kuzilinda meli hizo ulipunguzwa na kuwa vipindi viwili maalum kwa siku mwanzoni mwa mwezi Septemba.

  10. Jeshi la Yemen ladai kusababisha hasara kubwa katika mashambulizi dhidi ya ngome za Wahouthi

    Msemaji wa jeshi la serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa ametangaza kuwa ngome za kundi la Wahouthi la Ansar Allah zimeshambuliwa katika maeneo ya Mokha na Dhubab, magharibi mwa Yemen.

    Msemaji wa jeshi, Majid al-Nuzili, alidai katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa mashambulizi hayo yaliharibu shabaha kadhaa katika maeneo ya Mokha na Dhubab.

    Kulingana na yeye, magari na silaha ziliharibiwa kabisa katika operesheni hizo, huku wapiganaji wa Kihouthi waliokuwa karibu na bandari ya Mokha pia wakiuawa.

    Aliongeza kuwa wanachama wengine wa kundi la Wahouthi walilengwa pia katika sehemu mbalimbali za mji huo wa pwani.

    Kwa mujibu wake, kundi kubwa la wapiganaji wa Kihouthi lilishambuliwa karibu na kituo cha biashara katika mji wa Mokha, na kusababisha kuangamizwa kabisa kwa watu waliokuwepo hapo.

  11. Maziko ya Mfalme Oyo: Binti Mfalme Ruth Nsemere Komuntale amuomboleza kakake kama mtu aliyekuwa mcheshi

    Wakati akitoa hotuba yake ya mwisho ya kumuaga mdogo wake, Binti Mfalme Ruth Nsemere Komuntale alielezea miezi ya mwisho kabla ya kifo cha Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi IV.

    Kwa ufupi, alielezea wakati ambapo saratani ya Mfalme Oyo iligunduliwa na matibabu aliyopata baadaye.

    Kulingana na Binti Mfalme Ruth, "safari ya mapambano ya saratani ya mdogo wake ilianza katikati ya mwezi Oktoba mwaka 2025, alipogunduliwa kuwa na saratani ya *Angiosarcoma*aina ya saratani adimu na kali sana inayoweza kuenea kwa kasi kubwa."

    Anasema, "alitumia zaidi ya mwaka mmoja akifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu hapa nchini Uganda kwa ajili ya maumivu mbalimbali aliyokuwa akihisi. Kwa masikitiko, hakupata utambuzi sahihi wa tatizo lake."

    Aliongeza kuwa aliambiwa maumivu yake huenda yalisababishwa na "mazoezi makali au vidonda vya tumbo, na kufikia wakati alipopata utambuzi sahihi, saratani ilikuwa tayari imeenea sana na kuathiri viungo vingine vya mwili."

    Wakati akipata matibabu nchini Marekani baadaye, Mfalme aliomba hali yake iwekwe siri ili kuepuka kuleta hofu ndani ya familia na ufalme.

    Mbali na ugonjwa wake, Binti Mfalme Ruth alikumbushia utoto wake na mdogo wake, Mfalme Oyo, akisema: "Ingawa alikuwa mfalme, hakuwahi kupoteza kabisa ile hali ya utoto na kupenda kufurahia maisha."

    Alikumbuka kuwa "ingawa alivishwa taji akiwa na umri wa miaka mitatu tu, hakuacha kujifunza na alikuwa na hamu ya kufahamu mambo yanayomzunguka, hasa alipokutana na jambo ambalo hakuwa na ujuzi nalo."

    Alimwelezea kama mtu mwenye "imani, aliyewapenda watu, aliyejali wanyama, na aliyependa kufanya mazoezi pamoja na kwenda kutazama sinema." Akihitimisha hotuba yake, Binti Mfalme aliwataka "watu wote kuzingatia afya ya miili yao na kutafuta huduma sahihi za kimatibabu."

  12. Mkutano wa Delhi kuamua mustakabali wa muungano wa BRICS

    Viongozi wa dunia, akiwemo Rais wa Urusi Vladimir Putin, Rais wa China Xi Jinping, na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, wamekusanyika Delhi kwa ajili ya mkutano wa kilele wa BRICS.

    Kundi hilo liliundwa kwa lengo la kuwa na nguvu ya usawa dhidi ya Marekani na Ulaya Magharibi, lakini vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati vimeibua nyufa ndani yake.

    Mkutano huo ni fursa kwa BRICS kudhihirisha nafasi yake kama nguvu ya kisiasa na kiuchumi inayoweza kukabiliana na Magharibi, lakini pia ni jaribio kubwa kwa umoja wake.

    Migogoro ya kimataifa imefichua migawanyiko mikubwa, kwa mfano, Falme za Kiarabu zimekuwa zikilengwa na mashambulizi kadhaa ya ndege zisizo na rubani na makombora kutoka Iran mwaka huu.

    Mikutano ya BRICS katika kipindi cha miezi sita iliyopita haijazaa taarifa ya pamoja, jambo linalodaiwa kusababishwa na kutokubaliana sana kuhusu Iran na namna ya kushughulikia mizozo inayohusiana na Israel.

    Suala jingine ni Donald Trump, vitisho vyake vya ushuru wa biashara vinafanya iwe muhimu zaidi kwa wanachama wa BRICS kuungana ili kuleta uwiano, lakini wakati huo huo, kukabiliana naye kunaweza kuwa na gharama kubwa.

    Ikulu ya Marekani imeelezea baadhi ya mapendekezo ya BRICS kama yenye msimamo wa "kupinga Marekani," na nchi nyingi zitakuwa na tahadhari dhidi ya kumkasirisha rais huyo wa Marekani.

  13. Katika Picha: Ibada ya maziko ya Mfalme Oyo Nyimba katika kanisa la St John's Cathedral

    Ibada ya mazishi ya kumuaga Mfalme Oyo Nyimba yaanza rasmi katika kanisa la St. John's Cathedral nchini Uganda.

    Familia, jamaa na marafiki wamehudhuria katika ibada hiyo huku shughuli za misa zikianza rasmi.

    Maelfu ya waombolezaji walijipanga kando ya barabara wakati mwili wa Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi wa Nne, Omukama wa Tooro, ukisafirishwa katika safari yake ya mwisho kuelekea Ikulu ya Karuziika.

    Sherehe za kimila ziliambatana na kila hatua ya msafara huo, kwa heshima ya utawala wake wa takriban miaka 31.

  14. Saudi Arabia yasitisha kwa tahadhari shughuli za bomba la mafuta la Mashariki-Magharibi

    Bomba la mafuta la Mashariki-Magharibi la Saudi Arabia, ambalo limekuwa likilengwa na mashambulizi ya droni kutoka Iraq, limezidi kuwa muhimu tangu kuzuka kwa vita Mashariki ya Kati kati ya Marekani na Israel upande mmoja na Iran upande mwingine.

    Bomba hilo la Petroline linaanzia katika maeneo ya mafuta ya Abqaiq, katika Mkoa wa Mashariki wa Saudi Arabia, hadi bandari ya Yanbu, magharibi mwa nchi hiyo. Lina urefu wa takriban kilomita 1,200 na ni njia kuu mbadala ya kusafirisha mafuta ya Saudi Arabia kwenda katika masoko ya dunia, bila kupitia Mlango wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa kampuni za usafirishaji na wachambuzi, katika miezi michache iliyopita bomba hilo limekuwa likisafirisha mapipa milioni nne hadi tano ya mafuta kwa siku, sawa na asilimia nne hadi tano ya usambazaji wa mafuta duniani.

    Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA), mabomba hayo yana uwezo wa kusafirisha takriban mapipa milioni saba ya mafuta kwa siku.

    Saudi Arabia imetangaza mara kadhaa katika miezi ya hivi karibuni kuwa maeneo yake, hususan miundombinu ya nishati, yamelengwa katika mashambulizi ambayo inasema yalifanywa na makundi nchini Iraq yenye uhusiano na Tehran.

  15. Tetesi za soka Ulaya: Richarlison bado anaweza kuondoka Spurs

    Klabu kadhaa bado zinamuwania mshambuliaji wa Brazil, Richarlison, mwenye umri wa miaka 29, baada ya mpango wake wa kuondoka Tottenham na kujiunga na Vasco da Gama kuvunjika. (UOL - in Portuguese)

    Philippe Coutinho, aliyewahi kuichezea Brazil, amekubali kutumia miezi mitatu katika klabu ya Santos. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34, aliyewahi kucheza Liverpool na Aston Villa, anatafakari iwapo ataendelea na soka baada ya kuwa mchezaji huru tangu Februari, alipoondoka Vasco da Gama. (Globo - in Portuguese)

    Manchester United inamfuatilia kwa karibu beki wa kushoto wa Bournemouth na timu ya taifa ya Ufaransa, Adrien Truffert, mwenye umri wa miaka 24, ambaye thamani yake inakadiriwa kuwa pauni milioni 60.(Teamtalk)

    Liverpool bado inamtaka kiungo wa Inter Milan, Aleksandar Stankovic, mwenye umri wa miaka 21, baada ya kuulizia uwezekano wa kumsajili katika dirisha la usajili la majira ya joto. (Teamtalk)

    Crystal Palace bado haijakata tamaa ya kumsajili beki wa kati wa Brest, Raphael Le Guen, mwenye umri wa miaka 20, ambaye ilijaribu kumsajili katika dirisha la usajili lililopita. (Ouest-France via SportWitness)

    Liverpool bado inamuwania winga wa Ufaransa, Michael Olise, mwenye umri wa miaka 24, lakini Bayern Munich haina mpango wa kumuuza katika dirisha la usajili la Januari. (Christian Falk)

    Lamine Camara sasa ameelekeza nguvu zake katika klabu ya Monaco baada ya mpango wa siku ya mwisho wa usajili wa kiungo huyo wa Senegal, mwenye umri wa miaka 22, kujiunga na Chelsea kuvunjika. Camara amesema, “Labda fursa nyingine zitajitokeza.” (ESPN)

    Jadon Sancho hatarajiwi kujiunga na klabu mpya hivi karibuni, huku winga huyo wa zamani wa England, mwenye umri wa miaka 26, akiendelea kutathmini chaguo zake baada ya kuondoka Manchester United mwezi Juni. (Football Insider)

    Lazio na Parma zimejiunga na Everton katika kuonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Argentina, Mauro Icardi, mwenye umri wa miaka 33, ambaye ni mchezaji huru baada ya kuondoka Galatasaray mwishoni mwa msimu uliopita. (Corriere dello Sport - in Italian)

    Malaga inazingatia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Ufaransa, Anthony Martial, mwenye umri wa miaka 30, ambaye ni mchezaji huru baada ya kuondoka klabu ya Monterrey ya Mexico mwezi Juni. (Mundo Deportivo - in Spanish)

    Soma Zaidi Hapa:

  16. Mamia ya waombolezaji waelekea atakapozikwa mfalme Oyo wa Tooro Uganda

    Mwili wa marehemu Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi wa Nne, aliyefariki dunia mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 34, umesafirishwa kutoka Ikulu ya Karuzika hadi Kanisa Kuu la dayosisi ya St. John mjini Fort Portal.

    Maelfu ya waombolezaji,baadhi wakiwa wamevalia kanzu nyeupe na mavazi ya gome la mti, pamoja na viongozi wa taasisi za kitamaduni na watu mashuhuri wengine,wamekusanyika katika ikulu hiyo na kanisa kuu kuhudhuria shughuli ya kumuaga mfalme huyo kwa mara ya mwisho.

    Mfalme Oyo alifariki dunia nchini Marekani mwezi uliopita, ambako alikuwa akipatiwa matibabu ya saratani. Baadaye atazikwa leo Jumamosi katika eneo la makaburi ya kifalme huko Karambi.

  17. Hujambo na Karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja.