Serikali ya Kenya yakiri kwa mara ya kwanza kuwaweka watu karantini kutokana na tishio la Ebola

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Afya wa Kenya, Aden Duale, amekiri kwa mara ya kwanza kuwa kuna watu wengi waliowekwa kwa karantini kwa siku 21.
''Tumeweka watu wengi kwa karantini ikiwemo wafanyikazi wa Rais '', asema Waziri wa Afya Aden Duale.
Alipoulizwa na wanahabari kuhusu mustakabali wa vituo vya karantini kujengwa ili kuhifadhi wamarekani ameeleza kuwa serikali imesitisha ujenzi wa kituo cha karantini ya Ebola kilichokuwa kinajengwa Laikipia, kufuatia amri ya mahakama iliyosimamisha mradi huo.
''Tumeheshimu Mahakama na tumesitisha ujenzi wa kituo cha karantini cha Laikipia,'' asema Duale.
Duale alitoa kauli hiyo alipokuwa akipokea tani tano za vifaa vya matibabu kutoka India, vikiwemo vifaa vya kujikinga (PPE), vifaa vya uchunguzi, vipima joto vya miale ya infraredi na vifaa vingine vya dharura kwa ajili ya kuimarisha maandalizi ya Kenya dhidi ya Ebola.
Waziri huyo alisema kuwa hadi sasa hakuna kisa cha Ebola kilichothibitishwa nchini Kenya, lakini serikali inaendelea kuwa katika hali ya tahadhari.
Kauli yake inajiri wakati kukiwa na mjadala kuhusu kituo cha karantini kinachofadhiliwa na Marekani mjini Nanyuki, ambacho baadhi ya taarifa zinadai kinaendelea kufanya kazi licha ya amri ya mahakama iliyositisha ujenzi wake mwezi Mei.
Wiki iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilithibitisha kuwa wafanyakazi saba wa misaada wa Marekani waliokuwa wakishiriki kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanajitenga katika kituo kilichopo Kenya. Hata hivyo, haijawekwa wazi iwapo wanahifadhiwa katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Laikipia kilichopo Nanyuki.
Unaweza kusoma:




































