Jaji Mkuu wa zamani Kenya akamatwa katika maandamano ya kupinga kuhamishwa kwa Hifadhi ya Wanyama pori

Chanzo cha picha, EPA
Aliyekuwa Jaji Mkuu nchini Kenya amekamatwa katika maandamano ya kupinga mradi unaopendekeza uendelezaji wa miundombinu ndani ya Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi.
David Maraga alikuwa miongoni mwa wanaharakati kadhaa wa mazingira waliokamatwa Jumatatu asubuhi katika mji mkuu, Nairobi.
Vikundi vya uhifadhi na wanaharakati walikuwa wamekusanyika kupinga mradi wa Huduma ya Wanyamapori ya Kenya kutenga sehemu ya mbuga hiyo kwa maendeleo ya miundombinu.
Waandamanaji wanahoji kuwa mradi huo unaweza kutishia ardhi ya hifadhi na kuwa mwanzo wa kufanyika kwa miradi zaidi ya ujenzi ndani ya mbuga hiyo.
Jaji Mkuu huyo wa zamani na anayewania urais amekuwa akizungumza kuhusu ulinzi wa mazingira.
Waandamanaji wanadai takriban ekari 76 za makazi yaliyohifadhiwa zinaweza kuathiriwa na miradi ya miundombinu.
Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha polisi wakiwatawanya waandamanaji kabla ya kuwazuilia Maraga na wanaharakati wengine.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani, Maraga na waandamanaji wengine kwa sasa wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Langa'ta.
Shirika la Huduma la Wanyamapori nchini Kenya linakanusha madai ya unyakuzi wa ardhi, likisema mradi huo unahusisha kuhamisha na kuboresha Hifadhi hiyo ya Wanyama ya Nairobi ili kuboresha ustawi wa wanyama na huduma za uhifadhi.






















