Je mahakama kumsafisha Rigathi Gachagua?

Chanzo cha picha, EPA
Jumatatu Juni 8 ni siku muhimu kwa aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua almaarufu Riggy G, huku Mahakama Kuu ikitarajiwa kutoa uamuzi kuhusu iwapo kuondolewa kwake madarakani kupitia kura ya kutokuwa na imani naye, kulifuata katiba ya Kenya au la.
Majaji Eric Ogolla, Anthony Mrima na Fred Mugambi watatoa uamuzi baada ya miezi kadhaa ya kusikiliza kesi hiyo yenye mvutano mkubwa wa kisiasa nchini Kenya.
Gachagua aliondolewa rasmi madarakani Oktoba 17 mwaka 2024, baada ya bunge la taifa kupiga kura ya kumuondoa kwa zaidi ya wabunge 280 kuunga mkono hoja hiyo, kabla Seneti nayo kuidhinisha hatua hiyo.
Alikabiliwa na mashtaka matano makuu yakiwemo ukiukaji wa katiba, matumizi mabaya ya ofisi, ufisadi, utakatishaji fedha, utovu wa nidhamu kazini na kuendesha siasa za ukabila.
Miongoni mwa kauli zilizozua mjadala mkubwa ni ile aliyosema kuwa “wadau waliopiga kura ndio watanufaika zaidi serikalini,” kauli ambayo wakosoaji wake waliitafsiri kuwa serikali ya Kenya Kwanza ilikuwa ikibagua maeneo ambayo hayakumpigia kura Rais William Ruto.
Katika kesi yake, Gachagua amedai kuwa kuondolewa kwake madarakani kulikuwa mpango wa kisiasa uliopangwa baada ya uhusiano wake na Rais Ruto kuzorota ndani ya serikali ya Kenya Kwanza.
Pia aliiambia mahakama kuwa Bunge la Taifa na Seneti hazikumpa nafasi yakutosha kujitetea, akisema siku mbili pekee za kujiandaa zilikuwa chache mno kwa kesi nzito kama hiyo.
Aidha, mawakili wake waliiambia mahakama kwamba Seneti iliendelea na kesi hiyo hata baada ya Gachagua kulazwa hospitalini, huku Spika wa Seneti Amason Kingi akikataa ombi la kuahirisha vikao hadi.
Uamuzi wa leo unaweza kubadilisha kabisa siasa za Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Kama mahakama itakubaliana na Riggy G basi kiongozi huyo wa chama cha DCP atakuwa na nafasi ya kuwania tena uongozi katika uchaguzi mkuu mwakani.
Lakini Ikiwa mahakama itatupilia mbali ombi la Gashagua, basi atabakia kuwa ‘King Maker’ kwani sheria za uchaguzi hazimruhusu kiongozi aliyeondolewa madarakani kupitia ‘Impeachment’ kuwania tena kiti cha uongozi au iwapo tu wakati wa uchaguzi awe bado mahakamani na hajafikia mahakama ya upeo.
Je, mahakama itabatilisha kura ya kutokuwa na imani na Rigathi Gachagua au itaacha uamuzi wa Bunge na Seneti usimame?
Unaweza kusoma;




















