Kwa nini Wapalestina wanapeperusha bendera za Marekani juu ya nyumba zao?

Wapalestina wenye uraia wa Marekani katika mji wa Termesaya, kaskazini mashariki mwa Ramallah, wamepandisha bendera za Marekani juu ya nyumba zao. Hatua hiyo imechukuliwa kwa matumaini kwamba itazuia uvamizi wa jeshi la Israel na mashambulizi ya walowezi, au kuushawishi ubalozi wa Marekani kuingilia kati kwa ajili ya ulinzi wao.
Waandaaji wa mpango huo wanasema uzoefu wa awali katika mji huo umeonyesha kuwa ubalozi wa Marekani umekuwa ukijibu kwa haraka zaidi pale bendera ya Marekani inapopeperushwa kwenye nyumba zao. Hata hivyo, baadhi ya washiriki wana hofu kwamba hatua hiyo inaweza kusababisha majibu makali kutoka kwa jeshi la Israel au walowezi.
Balozi wa Marekani nchini Israel, Mike Huckabee, ambaye alitembelea eneo hilo baada ya kupokea maombi kutoka kwa wakazi, alisema ubalozi una wajibu wa kuchukua hatua kwa niaba ya raia wa Marekani na kutekeleza sera za Marekani.
"Tumepata taarifa kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo majumbani mwao na vitisho vinavyotolewa na watu ambao mimi ningewaita magaidi," aliiambia BBC.
Bendera za Marekani kama ngao ya ulinzi
Termesaiya iko umbali wa takriban kilomita 20 kaskazini mashariki mwa Ramallah. Yasser Al-Kahleh, mwanzilishi wa wazo la kutumia bendera za Marekani, aliiambia BBC kuwa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi hawana njia za kujilinda, na kwamba jaribio lolote la kujilinda linaweza kutafsiriwa kama shambulio, na hivyo kusababisha kukamatwa, kupigwa au hata kuuawa.
Al-Kahleh, ambaye ana uraia wa Palestina na Marekani na anaishi katika mji huo, alisema wazo hilo linahusisha kupandisha bendera za Marekani kwenye nyumba na majengo ya umma kwa matumaini kwamba zitatoa aina fulani ya uungaji mkono na ulinzi, na kuifanya serikali ya Marekani kuwajibika zaidi kwa usalama wao.
"Tunayo fursa halisi ya kuhoji mwenendo wa serikali ya Marekani kwa kupandisha bendera za Marekani juu ya nyumba zetu na majengo ya umma," alisema.
Tofauti ya nyumba yenye bendera na isiyo na bendera
Al-Kahleh anasimulia jinsi jeshi la Israel lilivyobadilisha nyumba moja jijini kuwa kambi ya muda ya kijeshi wiki chache zilizopita, likiwataarifu wakazi kuwa lingekuwepo hapo kwa saa 24, lakini baadaye likaongeza muda wa kukaa hapo kwa siku nyingine. Nyumba hiyo ilikuwa mali ya raia wa Marekani, lakini bendera ya Marekani haikupepea juu yake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Takriban saa 48 baadaye, Al-Kahleh alisema, askari hao walihamishiwa kwenye nyumba iliyo ng'ambo ya barabara, ambapo mmiliki alikuwa ameweka bendera ya Marekani kwa miaka mingi. Waliwaambia wakazi kuwa wangekuwepo hapo kwa saa 24, huku kukiwa na uwezekano wa kuongeza muda.
Aliongeza kuwa wakazi wa mji huo waliwasiliana na ubalozi wa Marekani wakati huo na kuuarifu ubalozi huo kuwa kuingia ndani ya nyumba hiyo "si changamoto tu kwa Wapalestina na Wapalestina wenye uraia wa Marekani, bali pia kwa serikali ya Marekani na ubalozi wa Marekani."
Al-Kahlah alisema jeshi liliondoka katika nyumba hiyo takriban saa nne baada ya kuwasiliana na ubalozi, akiongeza kuwa "Kwa kweli tuliona tofauti kati ya nyumba iliyokuwa na bendera ya Marekani ikipepea na nyumba ambayo haikuwa na bendera hiyo."
Kwa upande mwingine, jeshi la Israel, lilipoulizwa kuhusu maelezo ya tukio hilo linalohusu nyumba aliyoitaja Al-Kahla, lilisema kuwa "jeshi linafanya operesheni katika Ukingo wa Magharibi kulingana na mahitaji ya dharura ya kioperesheni ili kudumisha usalama wa wakazi wa eneo hilo."
Jeshi la Israel pia lilitangaza kuwa "operesheni hizi zinafanywa ili kuhakikisha usalama wa raia wa Taifa la Israel, huku likizingatia utu wa binadamu na matakwa ya kisheria."
Taarifa hiyo iliendelea kusema, "Katika hali ambapo mahitaji ya usalama yanahitajika, vikosi vya IDF vina mamlaka ya kuchukua udhibiti wa muda wa majengo, ikiwa ni pamoja na nyumba za watu binafsi, kwa muda maalum uliopangwa mapema. Katika hali kama hizo, agizo mwafaka litatolewa na kuwasilishwa kwa wakazi wa nyumba hiyo."

'Ilikuwa ni wakati wa mshtuko na huzuni'
Hassan Shukri, raia wa Marekani mwenye asili ya Palestina, anasema amewahi kukumbwa na hali kama hiyo licha ya kupeperusha bendera ya Marekani nyumbani kwake katika eneo la Turmus Ayya.
Alisema kuwa wakati mmoja jeshi la Israel liliingia nyumbani kwake wakati hakuna mtu aliyekuwapo, likavunja milango, likapekua nyumba hiyo na kisha kukaa humo kwa siku mbili.
Shukri alisema kuwa katika tukio jingine, alipokuwa nyumbani, vikosi vya Israel vilimtaka aondoke ndani ya saa moja kwa sababu za kiusalama bila kutoa maelezo zaidi.
"Ilikuwa ni wakati wa mshtuko na huzuni," alisema.
Aliongeza kuwa aliwasiliana na vyombo vya habari pamoja na Ubalozi wa Marekani, na saa chache baadaye vikosi hivyo viliondoka nyumbani hapo bila kueleza sababu za kuondoka kwao.
Shukri anaamini kuwa shinikizo kutoka kwa Ubalozi wa Marekani huenda lilichangia kuondoka kwa wanajeshi hao, lakini anasema matokeo hayo pia yameongeza huzuni yake kwa sababu Wapalestina wengi hawana uraia wa Marekani wala njia za kufikisha malalamiko yao kwa ubalozi au vyombo vya habari.
Aliongeza: "Lengo langu si kuzua utata, bali kusimulia kisa cha kibinadamu; kisa kuhusu nyumba, kumbukumbu na usalama ambavyo kila mwanadamu huvitamani."
Shukri alisema ujumbe wake ni kwamba, zaidi ya yote, ni lazima kuthamini utu wa mwanadamu na kwamba kila mtu anapaswa kuweza kuishi nyumbani kwake kwa usalama na heshima, bila hali hiyo kutegemea uraia wake.
Akijibu swali kuhusu tukio hilo, jeshi la Israel lilisema:
"Kama sehemu ya operesheni za kupambana na ugaidi katika Ukingo wa Magharibi, vikosi vya IDF vilitembelea nyumba hiyo husika na kumjulisha mmiliki kuhusu kuchukuliwa kwa muda kwa mali hiyo kwa sababu za kiutendaji. Raia hao hawakuondoka nyumbani hapo na waliruhusiwa kubaki, lakini baadaye iliamuliwa kutotumia nyumba hiyo."
Jeshi la Israel pia lilijibu madai kuhusu uharibifu wa nyumba na mali za wakazi, likisema:
"Iwapo kutakuwa na madai mahususi ya uharibifu wa mali au madhara ya kimwili kwa wakazi, madai hayo yatafanyiwa uchunguzi wa kina na, yakithibitishwa, yatashughulikiwa kwa uzito mkubwa."
Bendera ya Marekani ni ngao dhidi ya mashambulizi ya walowezi?
Samir Juma Hazmeh anaamini kuwa kupandisha bendera ya Marekani juu ya nyumba yake kulisaidia kukomesha unyanyasaji kutoka kwa mkazi wa eneo la walowezi anayeishi karibu na makazi yake.
"Ubalozi wa Marekani unaweza kulishinikiza jeshi kuwaondoa raia wa Marekani kutoka kwenye makazi yao ndani ya saa chache," alisema Hazmeh.
Alieleza kuwa nyumba yake iko umbali wa takriban mita 500 kutoka eneo la walowezi na kwamba unyanyasaji huo umekoma kwa takriban mwezi mmoja tangu alipopandisha bendera ya Marekani juu ya nyumba yake.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, angalau Wapalestina 81 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi na vikosi vya Israel au walowezi tangu kuanza kwa mwaka huu. Kati yao, angalau 23 walifariki kutokana na mashambulizi ya walowezi.
Umoja wa Mataifa pia umesema kuwa katika kipindi hicho hicho, Waisraeli watatu, wakiwemo maafisa wa usalama na raia, waliuawa na Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, jamii 127 za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi zilikumbwa na uhamisho wa kulazimishwa, kwa sehemu au kikamilifu, kuanzia Januari 2023 hadi Agosti mwaka huu. Kati ya jamii hizo, 47 zimeondoka kabisa katika maeneo yao ya makazi, hali iliyoathiri maisha ya zaidi ya Wapalestina 6,390.
Umoja wa Mataifa pia ulirekodi kuwa mwaka 2026, takriban Wapalestina 3,800, karibu nusu yao wakiwa watoto, walilazimika kuyahama makazi yao kutokana na vurugu za walowezi pamoja na operesheni za ubomoaji na kufukuzwa kutoka maeneo yao.
Hofu ya kulipiziwa kisasi
Hata hivyo, Shukri anasema hawezi kusema kwa uhakika kama bendera ya Marekani au uraia wake wa Marekani ndiyo iliyosababisha askari kuondoka haraka kutoka nyumbani kwake.
Pia anahoji iwapo jaribio hili linaweza kurudiwa katika miji na vijiji vingine vya Wapalestina ambapo raia wa Marekani wanaishi. Ana wasiwasi kwamba "kutumia bendera kama njia ya kushinikiza, kwa kuiaibisha serikali ya Israel, kunaweza kusababisha hatua za kulipiza kisasi kutoka kwa jeshi au walowezi."
Lakini Al-Bakhla anaamini kuwa kuna uwezekano mdogo kwamba kupeperusha bendera ya Marekani kutawachochea walowezi kufanya mashambulizi zaidi. Anaamini kuwa hatua hiyo inaweza kuzuia mashambulizi kama hayo, au angalau kupunguza ukali wake, na kuwalazimisha askari kuzungumza na wakazi wa nyumba wanazoingia "kwa upole na heshima."
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alilaani vurugu zinazofanywa na walowezi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, baada ya makumi ya walowezi wa Israel kushambulia mji wa Wapalestina wa Qasra mwishoni mwa mwezi wa Agosti. Alilaani kile alichokiita "vitendo vya uhalifu na vurugu" katika vijiji viwili vya Wapalestina na kuwataja walowezi waliohusika na mashambulizi hayo kama "kundi dogo la wahalifu wanaovunja sheria na kuzua fujo."
Rais wa Israel Isaac Herzog pia alilaani vurugu hizo, akisema kuwa ni "uvukaji wa mstari mwekundu uliofanywa na watu wanaovunja sheria, ambao wanatenda kinyume kabisa na sheria na maadili ya Taifa la Israel." Alielezea tukio hilo kama "doa katika sura ya Israel."
Herzog alitoa wito kwa serikali, vyombo vya usalama, idara ya mahakama, na vyombo vya kutekeleza sheria "kutumia njia zote zilizopo na kushirikiana kikamilifu ili kutokomeza jambo hili la aibu na kuwafikisha mbele ya sheria wale waliofanya vurugu hizo."
Kuwasiliana na ubalozi wa Marekani pamoja na watunga Sheria
Al-Kahleh anasema kuwa kampeni hiyo haikuishia tu kwenye kupandisha bendera, bali ilihusisha pia kuwasiliana na watunga sheria wa Marekani, akiwemo Seneta Chris Van Hollen.
Seneta Van Hollen aliweka video kwenye mitandao ya kijamii akimtaka Mike Huckabee, balozi wa Marekani nchini Israel, ajiuzulu. Aliongeza kuwa jukumu la balozi wa Marekani ni kulinda na kutetea maslahi ya Marekani, "jukumu ambalo Huckabee ameshindwa kulitekeleza."
Katika video hiyo, Van Hollen alizungumzia kuzuiliwa kwa baadhi ya Wapalestina ambao ni raia wa Marekani. Pia alisema kuwa yeye na maseneta wengine 31 walimtaka Huckabee, miezi michache iliyopita, kuifanya Israel iwajibike kwa vifo vya zaidi ya raia tisa wa Marekani katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Video hiyo iliyotolewa na seneta huyo ilionyesha picha za Wapalestina kadhaa wenye uraia wa Marekani, akiwemo mzee mmoja aliyelala chini huku damu ikimtoka kichwani baada ya shambulio la jeshi la Israel.
Ziara ya Huckabee katika Ukingo wa Magharibi
Siku ya Jumamosi, tarehe 5 Septemba 2026, Balozi wa Marekani nchini Israel, Mike Huckabee, alitembelea mji wa Termesaya, ulioko kaskazini mwa Ramallah katika eneo la katikati la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu, mji wenye idadi kubwa ya wakazi walio na uraia wa Marekani.
Aliambia mkutano na waandishi wa habari kuwa alikuja katika eneo hilo kusikiliza "malalamiko halali ya wananchi," akiongeza, "Ujumbe wetu uko wazi, uhalifu ni uhalifu na ugaidi ni ugaidi. Wale wanaofanya vitendo kama hivyo wanapaswa kutarajia kukabiliwa na matokeo makali."
"Nilieleza wazi kuwa ubalozi wa Marekani katika nchi nyingine una mipaka yake, hatuwezi kufanya uchunguzi kwa sababu hatuna mamlaka au uwezo wa kisheria wa kufanya hivyo, na hatuwezi kutoa maamuzi kuhusu kesi," Huckabee aliambia BBC.
"Lakini tunaweza kuleta mabadiliko na kuelekeza umakini kwenye masuala yanayohitaji kushughulikiwa, tunaweza pia kusisitiza ukweli kwamba si haki kwa maisha ya watu wengi wanaoishi kwa amani pande zote mbili za mipaka hii kuvurugwa kwa kiasi hiki kikubwa au kutishiwa. Masuala haya yote yanahitaji kushughulikiwa," aliongeza.















