Huenda unatupa sehemu muhimu zaidi ya tunda bila kujua

s
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Maganda, sehemu ya nje, mashina na mbegu za matunda na mboga mara nyingi huwa na kiwango kikubwa cha nyuzinyuzi za lishe (fiber) kuliko sehemu tunazokula kwa kawaida, kwa mujibu wa utafiti mpya uliofanywa na Chuo cha King's College London.

Watafiti walifanya uchunguzi kwa aina 12 za matunda na mboga mbichi na kubaini kuwa katika aina 10 za matunda na mboga hizo, mabaki yanayotupwa kama maganda, mbegu na mashina yalikuwa na viwango vya juu zaidi vya nyuzinyuzi za lishe kuliko sehemu zinazoliwa.

Utafiti huo unaonyesha kuwa sehemu nyingi tunazozitupa zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha afya ya mmeng'enyo wa chakula na lishe kwa ujumla.

Kwa mfano, watafiti walibaini kuwa ganda na kiini cha nanasi vilikuwa na kiwango cha nyuzinyuzi za lishe takriban mara tano zaidi ya sehemu laini ya tunda inayoliwa.

Wakati huo huo, ganda na mbegu za boga zilikuwa na gramu 9.25 za nyuzinyuzi kwa kila gramu 100, kiasi ambacho ni karibu theluthi moja ya kiwango cha nyuzinyuzi kinachopendekezwa kuliwa kwa siku.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa sehemu nyingi za matunda na mboga ambazo mara nyingi hutupwa zinaweza kuwa chanzo muhimu cha nyuzinyuzi zinazosaidia afya ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula.

s

Sehemu hizi za matunda na mboga kuanzia mizizi hadi ncha, ambazo mara nyingi hutupwa, zilichangia kati ya asilimia 25 na 48 ya uzito wote wa mazao hayo, alisema kiongozi wa mradi huo, Dk Rachel Gibson.

"Hii ina maana kwamba watu wanatupa sehemu kubwa ya matunda na mboga wanazonunua," alisema. "Huu si upotevu wa virutubisho pekee, bali pia ni hasara ya kifedha.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kimsingi, unakuwa unatupa sehemu kubwa ya bidhaa ambayo tayari umeilipia kwa fedha zako."

Hivyo ili kujua kama watu wako tayari kula maganda, ngozi za nje, mashina na mbegu za matunda na mboga, watafiti waliandaa orodha maalumu ya matunda na mboga maarufu kama "root-to-tip" katika Chuo cha King's College London, ambapo sehemu zote zinazoweza kuliwa za mazao zilitumika.

Washiriki waliulizwa ni nini kingewashawishi kujaribu vyakula hivyo. Matokeo yalionyesha kuwa faida za kiafya zinazotokana na nyuzinyuzi za ziada zilikuwa kivutio kikubwa zaidi kuliko faida zake kwa mazingira.

Hata hivyo, watafiti walionya kuwa si kila sehemu inayotupwa inapaswa kuanza kutumika jikoni mara moja.

Walisema kuna haja ya kufanya tafiti zaidi kuhusu mabaki ya viuatilifu (pesticides) na uchafu mwingine unaoweza kuwepo kwenye maganda na mboga.

Aidha, utafiti huo haukuchunguza moja kwa moja ikiwa kula sehemu hizo kunaleta maboresho ya afya kwa kiwango kinachoweza kuthibitishwa kisayansi, hivyo utafiti zaidi unahitajika kabla ya kutoa hitimisho kamili kuhusu manufaa yake kiafya.