Mchungaji amekutwa na hatia ya kuhusika na mauaji ya Rais wa Haiti

Chanzo cha picha, Police Nationale Haiti
Mchungaji mmoja kutoka jimbo la Florida nchini Marekani amepatikana na hatia ya makosa kadhaa yanayohusiana na mauaji ya aliyekuwa Rais wa Haiti, Jovenel Moïse.
Christian Emmanuel Sanon, raia mwenye uraia wa Marekani na Haiti, amepatikana na hatia ya mashtaka yote manane yaliyokuwa yakimkabili, yakiwemo ya kula njama ya kumuua au kumteka nyara mtu. Anakabiliwa na uwezekano wa kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Sanon, mwenye umri wa miaka 67, alishtakiwa kwa kuhusika katika mpango wa kumuondoa madarakani Moïse na kujichukua nafasi ya urais wa Haiti mwaka 2021. Inadaiwa kuwa alikusudia kufanya hivyo ili baada ya kushika madaraka, aweze kutoa mikataba yenye thamani kubwa kwa kampuni ya ulinzi yenye makao yake Florida.
Mauaji ya Moïse yameiacha Haiti bila kiongozi kwa kipindi cha miaka mitano. Pengo hilo la uongozi limechangia kuongezeka kwa machafuko yanayosababishwa na magenge ya uhalifu katika taifa hilo maskini la eneo la Caribbean.
Uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika mwaka ujao, huku mke wa Moïse, Martine, ambaye alijeruhiwa katika shambulio lililomuua mumewe, akitangaza wiki hii kuwa anakusudia kugombea urais.
Kwa mujibu wa CBS, mshirika wa BBC nchini Marekani, Sanon alipatikana na hatia siku ya Jumatano baada ya kesi iliyodumu kwa wiki nane katika mahakama ya shirikisho mjini Miami.
Wakili wake amesema Sanon bado anasisitiza kuwa hana hatia na anakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Waendesha mashtaka wamesema Sanon alikuwa na "matamanio ya kisiasa" nchini Haiti na kwamba mwezi Aprili 2021 alikutana na washirika wengine wa njama hiyo kupanga mpango wa kumuondoa Moïse madarakani kupitia shambulio la kutumia silaha katika kasri la rais mjini Port-au-Prince, mji mkuu wa nchi hiyo.
Miongoni mwa washirika hao walikuwa wakuu wa kampuni za Counter Terrorist Unit Federal Academy na Counter Terrorist Unit Security, ambazo kwa pamoja zilijulikana kama CTU.
Kampuni hizo zilitarajiwa kufadhili mapinduzi hayo kwa kubadilishana na kupata mikataba ya serikali ya kutekeleza miradi ya miundombinu, pamoja na kutoa vikosi vya ulinzi na vifaa vya usalama.





















