Sababu ya Ghuba ya Uajemi kuwa na mafuta na gesi zaidi kuliko mahali pengine popote duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Scott L. Montgomery
- Nafasi, The Conversation
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Inasemekana kwamba nchi za Ghuba ya Uajemi zimebarikiwa na kulaaniwa kwa kuwa na akiba kubwa ya mafuta na gesi. Eneo hilo lenye utajiri wa nishati, kwa sasa lina vita vinavyoendelea vinavyosababisha mgogoro wa nishati duniani.
Kama mtaalamu wa jiolojia ya mafuta ambaye nimechunguza eneo hilo, bado nashangazwa na ukubwa wa akiba yake ya hidrokaboni.
Kwa mfano, kuna zaidi ya maeneo 30 makubwa, kila moja likiwa na mapipa bilioni 5 au zaidi ya mafuta, katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Na visima katika eneo hilo hutoa mafuta mara mbili zaidi hadi tano kwa siku kuliko hata visima bora zaidi katika Bahari ya Kaskazini na Urusi.
Sayansi ya sasa ya jiolojia inatambua mambo kadhaa muhimu kuhusu miamba inayofanya eneo kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta, ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa kuzalisha na kuhifadhi hidrokaboni. Katika eneo la Ghuba ya Uajemi, mambo haya yako katika kiwango bora.
Kwa wingi na urahisi wa uzalishaji, hakuna eneo kama Ghuba ya Uajemi.
Historia

Chanzo cha picha, Central Intelligence Agency via Library of Congress
Wanadamu walijua kuhusu uwepo wa hidrokaboni katika eneo hilo muda mrefu kabla ya mafuriko yaliyounda Ghuba ya Uajemi kati ya miaka 14,000 na 6,000 iliyopita.
Mifereji ya asili ya mafuta na gesi ni ya kawaida kando ya mito na mabonde katika sehemu nyingi za eneo hilo. Maelfu ya miaka watu walitumia lami, mafuta mazito, kwa ajili ya kutengeneza chokaa ya kuziba kuta na kuziba majahazi yasipitishe maji.
Ugunduzi wa kwanza wa mafuta katika zama zetu ulikuja mwaka 1908 katika eneo la magharibi mwa Iran. Katika miaka ya 1950 na 60, wakati wa utafutaji wa mafuta na gesi, ikawa wazi kwamba hakuna eneo lingine duniani ambalo lina wingi wa rasilimali hiyo kuliko hapo.
Kuna maeneo mengine yenye kiasi kikubwa cha mafuta na gesi, kama vile Siberia Magharibi nchini Urusi na Bonde la Permian nchini Marekani, lakini hakuna eneo lolote kati ya hayo linaloweza kulinganishwa na kiwango cha akiba au viwango vya juu vya mafuta na gesi vinavyopatikana katika Ghuba ya Uajemi.
Mpangilio wa kijiolojia

Chanzo cha picha, NASA kupitia Flickr
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Eneo la Ghuba ya Uajemi liko katika eneo ambalo mabamba mawili ya bara yanagongana: Bamba la Arabia upande wa kusini-magharibi na Bamba la Eurasia upande wa mashariki na kaskazini.
Mgongano huu umekuwa ukitokea kwa takriban miaka milioni 35 na umesababisha mazingira yenye mabadiliko ambapo tabaka za miamba zimeunda milima na huko ndani kabisa, hubadilika kutokana na joto na mgandamizo.
Mazingira ya kijiolojia hutofautiana kati ya pande mbili za Ghuba. Kwa upande wa Iran, Milima ya Zagros imeenea maili 1,100 (kilomita 1,800) kutoka Ghuba ya Oman hadi mpaka wa Uturuki. Ni sehemu ya mfumo wa milima ya Alpine-Himalaya.
Zagros imeundwa na milima ambayo iliundwa katika kipindi cha miaka milioni 60 iliyopita kutokana na migongano ya bara la Afrika, Arabia na India na Eurasia.
Upande wa Ghuba ya Arabuni, aina hiyo ya miamba ya milima haikutokea. Badala yake, nguvu ya mgongano iliunda bonde la mfano wa kuba katika makumi hata mamia, ya maili za mraba.
Chini ya Ghuba ya Uajemi kuna bonde lililojaa uchafu uliomomonyoka kutokana na kupanda kwa Milima ya Zagros. Katika sehemu zake za ndani zaidi, bonde lina halijoto ya kiwango cha juu na ndio joto linalohitajika kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta na gesi.
Kwa ujumla, ni mahali pazuri pa kuzalisha hidrokaboni kwa kiwango kikubwa.
Miamba inayotengeneza mafuta

Chanzo cha picha, Picha ya AP/Vahid Salemi
Mafuta na gesi huundwa kutokana mabaki ya mimea, wanyama, na vijidudu, yaani viumbe hai vilivyooza kama vile zooplankton wa baharini na phytoplankton, ambao huishi kwenye magamba, mwamba wa matope, na miamba mingine iliyo wazi ambayo huzalisha halijoto na mgandamizo. Miamba inapoundwa na angalau 2% ya viumbe hai vilivyooza, inachukuliwa kuwa bora kwa uzalishaji wa mafuta na gesi.
Eneo la Ghuba lina idadi kubwa sana ya miamba ya aina hiyo, ambayo baadhi yake ni minene sana, imeenea na ina utajiri wa viumbe hai vilivyooza.
Mifano ni miundo ya milima ya Hanifa na Tuwaiq upande wa Ghuba ya Arabuni, ambayo iliundwa yapata miaka milioni 200 hadi milioni 145 iliyopita, na Kazhdumi nchini Iran, ambao uliundwa yapata miaka milioni 145 hadi 66 iliyopita. Miamba hii ina kati ya 1% na 13% ya viumbe hai vilivyooza, na hata zaidi katika baadhi ya maeneo.
Mafuta na gesi

Chanzo cha picha, : University of Texas Institute for Geophysics
Safu za miamba na mabonde katika eneo hilo, pamoja na kuba zake, zinafaa sana kwa kuhifadhi hidrokaboni.
Milima ya Zagros, ambayo ni maarufu kwa wanajiolojia kutokana na umbo lake la kuvutia kwenye picha za setilaiti, ina mabilioni ya mapipa ya mafuta na mita za ujazo za gesi asilia.
Kwenye Bamba la Arabia, miundo mikubwa ya kuba imeunda mkusanyiko mkubwa wa mafuta na gesi. Hizi ni pamoja na uwanja wa mafuta wa Ghawar huko Saudi Arabia, ambao ni mkubwa zaidi duniani, unaweza kutoa zaidi ya mapipa bilioni 70 ya mafuta ghafi.
Uwanja wa gesi wa South Pars-North Dome, wa Qatar na Iran, unaweza kutoa angalau futi za ujazo trilioni 1,300 (mita za ujazo bilioni 46) za gesi - sawa na kiwango cha nishati cha zaidi ya mapipa bilioni 200 ya mafuta.
Hakuna kitu kama hiki kilichopo mahali pengine popote duniani, pwani au nchi kavu, ni jiolojia ya kipekee ya mafuta ya eneo la Ghuba ya Uajemi.
Tathmini za Utafiti wa Jiolojia wa Marekani zinaonyesha kwamba, hata baada ya zaidi ya karne moja ya uchimbaji na uzalishaji, kiasi kikubwa cha mafuta na gesi bado hakijagunduliwa katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
Katika ripoti ya mwaka 2012 inayohusu Rasi ya Arabia na Milima ya Zagros, shirika hilo lilikadiria kuwa kunaweza kuwa na mapipa bilioni 86 ya mafuta na futi za ujazo trilioni 336 za gesi asilia kwenye miamba, lcha ya kiasi ambacho tayari kimegunduliwa.















