Kwa nini Iran haitaki kuachia udhibiti wa Mlango bahari wa Hormuz?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Kwa mtazamo wa wengi, mafanikio muhimu zaidi ya kimkakati ambayo Iran ilipata katika vita vya siku 40 ni kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz.

Tehran imeweza kutumia nafasi yake ya kijiografia kuhamisha gharama za vita kutoka uwanja wa mapambano ya kijeshi hadi kwenye soko la kimataifa la nishati, na kubadili mgogoro ambao awali ulikuwa kati ya Iran na Marekani kuwa suala linaloathiri mataifa yenye uchumi mkubwa duniani.

Uwezo wa Iran wa kushinikiza Washington kuafikia makubaliano na Tehran, licha ya Marekani kuwa na nguvu kubwa zaidi za kijeshi unasemekana uliafikiwa licha ya Marekani kushindwa kuafikia malengo yake.

Hata hivyo, makubaliano hayo hayakudumu kwa muda mrefu. Viongozi wa Jamhuru ya kiislamu ya Iran wamekuwa wakisisitiza kuhusu umuhimu wa kudhibiti utaratibu wa Mlango bahari wa Hormuz.

Lakini je Iran haishushi thamani ya eneo hilo la kimkakati ikiendelea kutegemea sana mlango bahari wa Hormuz?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa nini Mlango Bahari wa Hormuz ni muhimu sana kwa Iran?

Katika vita vya siku 40, malengo yaliyotangazwa na Marekani yalikuwa mengi. Hata hivyo, katika awamu mpya ya mzozo huo, sehemu kubwa ya operesheni zake imejikita kwenye lengo moja mahsusi: kuhakikisha Mlango-Bahari wa Hormuz unabaki wazi na kuizuia Iran kuimarisha udhibiti wake katika njia hiyo muhimu ya bahari.

Marekani sasa imelazimika kuelekeza sehemu ya nguvu zake za kijeshi na kisiasa kwenye suala ambalo kabla ya vita halikuwa miongoni mwa vipaumbele vyake vikuu.

Hamidreza Azizi, mtafiti wa masuala ya Iran na usalama wa kikanda, amesema katika mahojiano na BBC Persian kwamba, kwa mtazamo wa Tehran, udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz si chombo cha kuongeza bei ya mafuta au kukusanya ada kutoka kwa meli zinazopita pekee, bali ni sehemu ya juhudi pana za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kubadilisha mfumo wa usalama katika Ghuba ya Uajemi.

Kulingana na Hamidreza Azizi, ushindi wa kweli wa kimkakati unaweza kusemwa umefikiwa tu ikiwa vita vitasababisha kuongezeka kwa uwezo wa Iran kujizuia dhidi ya mashambulizi ya adui na kuimarisha usalama wake.

Tehran inaamini kuwa lengo hilo linaweza kuafikiwa kwa kupunguza uwezo wa Marekani katika kusimamia usalama wa Ghuba ya Uajemi na kwa kutambuliwa kwa nafasi ya Iran katika mipango na maamuzi yanayohusu Mlango Bahari wa Hormuz.

Iran inaona kuwa iko tayari kubeba gharama za kisiasa, kiuchumi na hata za kijeshi ili kudumisha ushawishi wake katika Mlango Bahari wa Hormuz, kwa kuwa inaamini kuwa udhibiti wa eneo hilo ni sehemu muhimu ya mkakati wake wa muda mrefu wa kuimarisha usalama wake na nafasi yake katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Kwa nini Iran iko tayari kulipa gharama kwa ajili ya Hormuz?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mgogoro kati ya Iran na Marekani sasa unaonekana kuzidi suala la kupita kwa meli chache au kutozwa kwa ada za usafirishaji. Iran inataka kudumisha na kuimarisha nafasi iliyoipata wakati wa vita, huku Washington ikitaka kuzuia udhibiti wa Iran juu ya mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa nishati duniani.

Hali hii pia inatafsiriwa kama juhudi za kila upande kujiweka katika nafasi nzuri zaidi kwa mazungumzo ya baadaye.

Wakati huo huo, baadhi ya wanaounga mkono sera ya kusimamia kile kinachoitwa "utaratibu wa Iran" katika Mlango-Bahari wa Hormuz wanaamini kuwa njia hiyo ya maji inaipa Iran uwezo wa kuhamisha gharama za shinikizo la kijeshi la Marekani kwa uchumi wa dunia, kwa kuongeza hali ya kutokuwa na uhakika katika soko la nishati, Iran inaweza kuzihusisha nchi za Ghuba ya Uajemi na mataifa yanayotegemea mafuta katika athari za vita.

Wanaounga mkono sera hii nchini Iran wanasema kuwa Tehran ikiacha madai yake kuhusu Mlango-Bahari wa Hormuz, haitakuwa imeacha tu chombo cha kawaida cha kutoa shinikizo, bali itakuwa imepoteza mafanikio yake makubwa zaidi ya kimkakati yaliyopatikana wakati wa vita.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hatari ya kupungua kwa nguvu ya nyenzo muhimu zaidi ya Iran

Wachambuzi wengi wanaamini kuwa kwa sasa Iran inamiliki moja ya nyenzo zake muhimu zaidi za kimkakati. Hata hivyo, wanaonya kwamba kufungwa kwa muda mrefu kwa Mlango Bahari wa Hormuz si suluhisho la kudumu. Ingawa Tehran inaweza kuusababishia uchumi wa dunia kupanda kwa gharama kubwa, kuendelea kwa hali hiyo pia kunaweza kuiletea Iran yenyewe hatari kubwa.

Ikiwa mgogoro huo utaendelea kwa muda mrefu kiasi kwamba nchi zitaanza kuzoea kutokuwepo kwa njia hiyo badala ya kusubiri ifunguliwe tena, basi eneo hilo linaweza kupoteza nguvu yake ya kimkakati.

Katika hatua za mwanzo za mgogoro, nchi hujaribu kukabiliana na hali hiyo kwa kutumia akiba za mafuta, kubadili njia za meli na kupunguza mshtuko wa soko kupitia hatua za muda. Lakini mgogoro ukidumu, hatua hizo za dharura hubadilishwa na uwekezaji wa muda mrefu unaolenga kupunguza utegemezi wa Mlango-Bahari wa Hormuz.

Mbali na mabomba ya kusafarisha mafuta kama yaliyojengwa na Saudi Arabia, miundo mbinu ya nchi kavu, bandari mbadala na uwezo wa kuhifadhi mafuta yanaweza pia kuharakishwa kujengwa ili kupunguza utegemezi wa Mlango bahari wa Hormuz.

Baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa kupungua kwa utegemezi wa dunia kwa njia hiyo kunaweza kupunguza sehemu ya nguvu ya kimkakati ya Tehran.

Aidha, matumizi ya mara kwa mara ya Mlango-Bahari wa Hormuz kama chombo cha shinikizo yanaweza kuongeza motisha kwa wapinzani wa Iran kushirikiana zaidi katika masuala ya usalama.

Nchi za Ghuba ya Uajemi, ambazo kabla ya vita zilikuwa na mitazamo tofauti kuhusu kutegemea Marekani katika usalama wa eneo hilo, shinikizo la sasa zinaweza kuongeza ushirikiano katika kulinda usalama wa baharini, kuondoa mabomu ya majini, kulinda miundombinu muhimu na kuanzisha mifumo ya pamoja ya tahadhari na ulinzi.

Mgogoro wa Hormuz si tena suala linalohusu Tehran na Washington pekee. Kuendelea kwa hali hii kunaweza kuyasukuma mataifa mengine kuwekeza zaidi katika kupunguza utegemezi wao wa njia hiyo muhimu ya bahari.

Historia ya Urusi: Je, hali hiyo inaweza kujirudia?

Moja ya mifano ya wazi zaidi ya kihistoria katika suala hili ni ni Urusi. Kwa miaka mingi, utegemezi wa Ulaya kwa gesi ya Urusi ulikuwa mojawapo ya nyenzo muhimu zaidi za Moscow za kushinikiza mataifa mengine.

Hata hivyo, Kremlin ilipoanza kutumia nyenzo hiyo kwa kiwango kikubwa, nchi za Ulaya zililazimika kubeba gharama kubwa ili kuanzisha vyanzo na njia mbadala za kupata nishati.

Urusi iliweza kuchochea shinikizo kubwa kwa muda mfupi, lakini wakati huohuo ikapoteza sehemu ya nguvu yake ya kimkakati kwa muda mrefu kutokana na kupungua kwa utegemezi wa Ulaya kwa gesi yake.

Hali ya Iran si sawa na ile ya Urusi, kwani kutafuta mbadala wa Mlango-Bahari wa Hormuz ni jambo gumu zaidi kuliko kubadilisha sehemu ya gesi ya Urusi. Hata hivyo, kimkakati zinafanana. Chombo cha ushawishi kinavyotumiwa mara kwa mara, ndivyo wahusika wengine wanavyopata sababu zaidi za kupunguza utegemezi wa sehemu hiyo.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Je, nyenzo hii ya ushawishi inaweza kuigeukia Iran yenyewe?

Mlango-Bahari wa Hormuz hauonekani tu kama chombo cha kushinikiza wengine, bali pia kama sehemu ya udhaifu wa Iran yenyewe.

Uchumi na biashara ya Iran pia hutegemea usafiri wa baharini, ambao umeathirika kwa kiasi kikubwa baada ya Marekani kurejesha mzingiro wa kijeshi wa baharini dhidi ya Iran.

Hatua yoyote inayofanya iwe vigumu kwa wengine kutumia njia hiyo ya maji inaweza hatimaye kuathiri pia mapato ya fedha za kigeni ya Iran, uagizaji wa bidhaa kutoka nje na uwezo wake wa kujenga upya uchumi wa taifa hilo.

Hamidreza Azizi anaeleza hali hii kupitia aina mbili za kutokuwiana: kutokuwiana kwa uwezo na kutokuwiana kwa uwezo wa kubeba gharama.

Akizungumzia kutokuwiana kwa uwezo, anasema:

"Iran bado inaweza kushambulia kambi na maslahi ya Marekani katika eneo hilo kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani, na wakati mwingine kufanya mashambulizi ya kulenga shabaha maalumu. Lakini mashambulizi ya Marekani ndani ya Iran yataendelea kudhoofisha uwezo wa ulinzi wa nchi hiyo, pamoja na miundombinu yake ya makombora na jeshi."

Kwa mujibu wake, katika hali hii, eneo la bara la Marekani halilengwi moja kwa moja, na Iran haina uwezo wa kuzuia kikamilifu mashambulizi dhidi ya ardhi yake. Hivyo, hata kama pande zote mbili zinaweza kusababishiana gharama, aina na athari za gharama hizo si sawa.

Aina ya pili ya kutokuwiana, kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa sera za kikanda za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni kiwango cha uwezo wa kila upande kuvumilia gharama za vita.

Azizi anasema kuwa mashambulizi dhidi ya vituo vya Marekani yanaweza kusababisha vifo, gharama za kisiasa na kuathiri taswira ya Washington, lakini mradi mashambulizi hayo yanasalia katika kiwango cha chini, hayawezi kuwa tishio la moja kwa moja kwa uwepo wa Marekani.

Mchezo hatari wa Tehran

Hatari nyingine kwa Iran ni kwamba Marekani inaweza kukubali kuwa haiwezi kumaliza udhibiti wa Iran katika mlango bahari wa Hormuz bila hata kuongeza shinikizo la kijeshi.

Ikifikia hapo, hatua ambazo hazikuchukuliwa awali zinaweza kurejelewa tena kama oparesheni ya vikosi vya ardhini au mashambulizi ya visiwa vinavyodhibitiwa na Iran katika ghuba ya Uajemi.

Wakosoaji wanasema iwapo hatua hizo zitachukuliwa zinaweza kuvuruga shughuli katika mlango bahari wa Hormuz, na kuifanya hali hiyo kuwa ya kudumu na kuwalazimu wanaotegemea eneo hilo la bahari kutafuta njia mbadala ya usafiri wa baharini na kupunguza utegemezi wa mlango huo wa bahari.

Azizi anaonya kuwa Iran imeweza kuhimili na kushinda vitisho vikubwa katika vita viwili vilivyopita. Hata hivyo, anaamini kuwa kuendelea na mkakati huu kunaweza kubadilisha mkakati wa Marekani.

Swali kuu ni kuwa kwa kiwango gani Iran inaweza kutumia mlango huo wa bahari kama kishawishi, bila kuisukuma dunia kupunguza utegemezi wake kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, na kuifanya Iran kubeba gharama kubwa ya vita hivyo.

Thamani kubwa zaidi ya Mlango-Bahari wa Hormuz kwa Iran ilikuwa pale ambapo mataifa mengine yaliogopa uwezekano wa kufungwa kwake, kuliko wakati ambapo dunia inaanza kuzoea kutokuwepo kwa njia hiyo muhimu ya usafirishaji.