Kenya yapokea vifaa vya matibabu kutoka India kuimarisha mapambano dhidi ya Ebola

Chanzo cha picha, Getty Images
Kenya imepokea shehena ya kwanza ya tani 4.5 za vifaa vya matibabu kutoka kwa serikali ya India ili kuimarisha uwezo wa nchi hiyo wa kujiandaa na kukabiliana na uwezekano wa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, The Star imeripoti.
Shehena hiyo ilikabidhiwa rasmi na Kamishna Mkuu wa India nchini Kenya kwa Waziri wa Afya, Aden Duale, katika hafla iliyofanyika siku ya Jumatano.
Msaada huo ni sehemu ya jitihada pana za India kusaidia nchi za Afrika kuimarisha uwezo wa kuzuia na kukabiliana na milipuko ya Ebola.
Vifaa vya matibabu vilivyotolewa vinajumuisha vifaa vya kujikinga binafsi (PPE), vifaa vya kusafirisha sampuli za vipimo, vipima joto vya infrared, kinga za uso, viatu vizito za kujikinga, pamoja na vifaa vingine vya kuzuia na kudhibiti maambukizi.
Shehena ya pili ya msaada wa matibabu inatarajiwa kuwasili Kenya ndani ya siku chache zijazo.
Wakati wa hafla ya makabidhiano, maafisa walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuimarisha mifumo ya afya na kuboresha maandalizi ya kukabiliana na dharura zinazotokana na vitisho vya magonjwa ya kuambukiza.
Msaada huo unakuja wakati Kenya ikiendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, maandalizi, na hatua za haraka za kukabiliana na dharura ili kujikinga dhidi ya hatari ya kuenea kwa Ebola kuvuka mipaka na magonjwa mengine mapya ya kuambukiza.
Unaweza kusoma;






















