Kenya inavyopambana kudhibiti "wahuni na silaha" huku hofu ya vurugu za kisiasa ikiongezeka

Muda wa kusoma: Dakika 6

Siku ya Jumatano tulivu mwezi uliopita, mwanasiasa mmoja nchini Kenya alisimama kunywa kahawa baada ya kukata nywele katika jiji la magharibi la Kisumu.

Dakika chache baadaye, kundi la vijana waliovaa kofia lilimvamia ghafla Seneta Godfrey Osotsi, wakimpiga ngumi na mateke, wakimuacha na majeraha makubwa, kisha wakamnyang'anya simu na vitu vyake vya thamani kabla ya kutoweka mitaani.

Shambulio hilo lilinaswa na kamera za CCTV, na ndani ya saa chache video hiyo ilisambaa kwa kasi kubwa.

Polisi bado wanaendelea na uchunguzi, lakini seneta huyo amesema tukio hilo halikuwa ujambazi wa kawaida. Badala yake, alidai lilikuwa na msukumo wa kisiasa, akisema washambuliaji walimuuliza kwa nini haungi mkono juhudi za rais kugombea tena.

Hasira za kitaifa zilizofuata zililazimisha bunge la Kenya kuwaita wakuu wa vyombo vya usalama kueleza hali hiyo.

Kwa Wakenya wengi, tukio hilo halikuonekana kama la kushangaza pekee, bali lilithibitisha hofu iliyokuwepo kwa muda mrefu, kwamba nchi inaelekea tena kwenye enzi ya vurugu kali za kisiasa.

Historia ya Kenya ya kutumia makundi ya kihalifu yaliyoungwa mkono kisiasa inaanzia miaka ya mapema ya 1990, wakati mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa.

Tangu wakati huo, vijana wasiokuwa na ajira wamekuwa wakiajiriwa na baadhi ya wanasiasa na kutumika kama zana za vitisho wakati wa uchaguzi.

Makundi hayo yalikuwa kichocheo kikubwa cha machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi mwaka 2007 , ambapo takriban watu 1,500 walipoteza maisha.

Na sasa dalili zinaonesha kuwa mazingira yanaanza kuwa magumu kuelekea mzunguko mwingine wa uchaguzi wenye mvutano mkubwa, licha ya ukweli kwamba uchaguzi mkuu ujao bado uko mbali kwa takribani miezi 15.

Akiwa bado na chuki kubwa kufuatia kuondolewa madarakani kupitia mchakato wa kura ya kutokuwa na imani naye, mwaka 2024, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua anapanga kugombea urais. Wakati huohuo, kuna mgawanyiko wa wazi ndani ya moja ya vyama vikuu vya siasa nchini.

Hali hii inaongeza joto la kisiasa, huku mashambulizi dhidi ya wanasiasa yakifanywa na vijana walioajiriwa, wanaojulikana kama "wahuni", yakizidi kuwa ya wazi na ya kuthubutu.

Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen alikiri mbele ya kamati ya bunge kwamba serikali inapata ugumu kudhibiti makundi hayo, akisema yamebadilika kutoka makundi ya kawaida ya mitaani hadi kuwa "mitandao ya kisasa na iliyosambaa".

Murkomen, aliyefika pamoja na wakuu wa vyombo vya usalama, alifichua kuwa kuna zaidi ya makundi 104 ya uhalifu yanayofanya kazi nchini Kenya, mengi yakidaiwa kuwa chini ya ufadhili wa wanasiasa.

"Makundi haya yanamilikiwa na viongozi wa kisiasa ambao wana jukumu kubwa katika kuhamasisha watu. Ni hali ya vurugu. Kiongozi asiye na uwajibikaji ni tishio kwa usalama wa taifa," alisema, bila kutaja majina.

Takribani washukiwa 300 walikamatwa mwezi uliopita huku mamlaka zikiongeza msako dhidi ya makundi ya uhalifu, ambapo polisi walipata silaha na vifaa vya mawasiliano wakati wa operesheni hizo. Hata hivyo, hakuna mwanasiasa aliyekuwa miongoni mwa waliokamatwa.

Serikali tofauti nchini Kenya zimejaribu kupiga marufuku makundi hayo kwa miaka mingi, lakini tatizo limeendelea kuwepo huku magenge yakibadilika, kujipa majina mapya na kujitokeza upya kila kipindi cha uchaguzi.

Chanzo kimoja cha usalama kiliiambia BBC kuwa makundi hayo sasa yamekua na kuwa mashirika yaliyojipanga vizuri, yenye muundo wa uongozi na operesheni zilizoratibiwa.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua anaonekana kuwa mmoja wa walengwa wa mashambulizi hayo.

Tangu kuondolewa kwake madarakani, Gachagua ameripoti kukumbwa na mlolongo wa mashambulizi ya mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na kuvamiwa na makundi yenye silaha makanisani zaidi ya mara 20.

Yeye pamoja na washirika wake wanadai kuwa mashambulizi hayo yanafadhiliwa na mitandao ya uhalifu inayoungwa mkono na baadhi ya vyombo vya dola, kwa lengo la kudhoofisha azma yake ya kugombea urais.

Kwa miezi kadhaa, viongozi wa upinzani na makundi ya kiraia nchini Kenya wamekuwa wakiishutumu polisi kwa ama kushirikiana na makundi ya uhalifu au kupuuza vitendo vyao.

Wanasema kuwa makundi hayo hupanga mashambulizi katika mikutano ya kisiasa yakiwa na silaha za jadi kama rungu na mapanga, na mara nyingi hufanya hivyo hadharani.

Katika visa vingi, wanadai kuwa vurugu hizo hutokea mbele ya macho ya polisi bila hatua madhubuti kuchukuliwa, jambo linalozidisha wasiwasi kuhusu usalama na uwajibikaji wa vyombo vya dola.

Kifo cha mwanasiasa mkongwe Raila Odinga mwezi Oktoba mwaka jana pia kimechochea mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini Kenya, ambapo chama chake cha upinzani, ODM, kimegawanyika katika makundi mawili yanayokinzana kuhusu kumuunga mkono Rais William Ruto au la.

Mvutano huo uliongezeka mwezi Februari baada ya kijana mwenye umri wa miaka 28 kuuawa kwa kupigwa risasi wakati polisi walipokabiliana na wafuasi wa kundi linalompinga Ruto katika mkutano wa kisiasa. Kundi hilo lililaani tukio hilo likisema ni "vitendo vya vurugu vinavyofadhiliwa na dola, vikihusisha polisi na makundi ya wahuni waliolipwa".

Hata hivyo, msemaji wa serikali Isaac Mwaura alikanusha vikali madai kwamba baadhi ya makundi hayo yanafadhiliwa na serikali. Alisema: "Matumizi ya makundi ya kihalifu kutisha au kunyamazisha watu yanadhoofisha demokrasia yetu na hayatakubalika. Yeyote atakayepatikana akifadhili au kushiriki vitendo hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria."

Si viongozi wa upinzani pekee wanaolengwa. Mnamo Februari, mgombea wa useneta aliyeegemea upande wa muungano tawala wa Kenya Kwanza alivamiwa baada ya kundi la watu kuvamia ibada ya kanisani katika mji wa Kakamega na kumtoa kwa nguvu ndani ya jengo.

Aidha, uchaguzi mdogo uliofanyika Novemba mwaka jana katika maeneo ya magharibi na katikati mwa Kenya ulitawaliwa na vurugu, ambapo mawakala wa vituo vya kupigia kura walishambuliwa, makundi yenye silaha yalipigana wakati wa kuhesabu kura, na polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wapiga kura.

Mchambuzi wa masuala ya usalama Robert Chege alisema: "Matukio haya yanaonesha picha ya kutia wasiwasi ya nchi ambapo ushindani wa kisiasa unazidi kushika kasi mitaani kwa njia ya vurugu zilizopangwa, zikitekelezwa na makundi yaliyoajiriwa na yanayofanya kazi kwa ustadi na bila kuwajibishwa."

Kila tukio la shambulio, likichukuliwa peke yake, linaweza kuonekana kama la kawaida au kuelezeka kwa urahisi. Lakini yakichunguzwa kwa pamoja, wachambuzi wanaonya kuwa yanaonesha nchi ya Kenya ikielekea kwenye hatari kubwa ambayo tayari iliwahi kuikumba na kupona kwa tabu.

Profesa Makau Mutua, mtaalamu wa sheria na mshauri wa Rais William Ruto, alisema: "Tatizo la kutisha nchini Kenya ni kwamba hili sasa limekuwa jambo la kawaida karibu kwa vyama vyote vikuu vya kisiasa. Kwa kifupi, limekuwa kama utamaduni wa Kenya, janga linalosambaa."

Ripoti ya mwaka jana kutoka National Crime Research Centre ilibaini kuwa kuna mamia ya makundi ya kihalifu yanayofanya kazi nchini, huku zaidi ya 120 yakihusishwa na wanasiasa. Ripoti hiyo iliongeza kuwa makundi hayo hayakuwa tena ya muda mfupi, bali yamejikita kama taasisi ndani ya jamii zao.

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja aliwaambia wabunge kuwa jeshi la polisi linachukulia suala hilo kwa uzito mkubwa, akiongeza kuwa vyombo vya usalama tayari vimewatambua wanaohusika na machafuko hayo.

"Tatizo hili la 'wahuni na silaha' litaisha hivi karibuni. Tumechunguza kwa kina. Tumeona wanapotoka, nani anafadhili, nani anafanya nini, nani ni waandaaji wa ngazi ya chini na kadhalika," alisema Kanja.

Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen pia alijibu malalamiko kuhusu polisi kushindwa kuchukua hatua dhidi ya magenge. Alikiri kuwa kuna changamoto katika baadhi ya matukio, akitaja "matatizo ya kiutendaji" kama vile rushwa na uvujaji wa taarifa, huku akisisitiza kuwa wizara inachukulia kwa uzito tuhuma zote za ushiriki au uzembe wa polisi.

Hata hivyo, wakosoaji wanasema hatua za serikali zimekuwa hazina uthabiti, zikiwa kali kwa maneno lakini dhaifu katika utekelezaji.

Mchambuzi wa usalama Robert Chege anaeleza mgogoro wa usalama nchini Kenya kama tatizo lililojitengeneza lenyewe, linaloendelezwa na mitandao ya ufadhili wa kisiasa na mifumo ya dola "inayostawi kupitia vurugu na ukosefu wa usawa".

Aliongeza: "Swali si tena hawa 'wahuni' ni kina nani, bali ni nani anayewatuma, anayewafadhili na anayewalinda? Wapangaji wakuu wa wimbi hili la vurugu zilizopangwa bado wako gizani."

Wananchi wa kawaida wanatumaini kuwa mamlaka husika zitatoa majibu na kuchukua hatua madhubuti kabla hali haijazidi kuwa mbaya kuelekea uchaguzi mkuu unaopaswa kufanyika ifikapo Agosti mwaka ujao.