Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump: Vita na Iran vimekwisha, lakini hatutaondoka haraka

Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa anafuatiliwa na viongozi mbalimbali wa Iran wanaotaka makubaliano, huku Washington ikijitahidi kubainisha upande unaofaa wa kufanya nao mazungumzo.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Rais wa Namibia Netumbo Nandi - Ndaitwah amaliza kulipa deni lote la IMF

    Rais wa Namibia, Netumbo Nandi‑Ndaitwah, ameiongoza nchi yake kufikia hatua muhimu ya kiuchumi kwa kukamilisha malipo ya deni la Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

    Namibia imelipa jumla ya dola milioni 23.9, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa madeni ya nje na kuimarisha uthabiti wa uchumi wa taifa hilo.

    Kukamilika kwa deni hili kunatajwa kuongeza uhuru wa kifedha wa Namibia na kuipa serikali nafasi pana zaidi ya kuelekeza rasilimali zake katika miradi ya maendeleo ya ndani.

    Hatua hii imepokelewa kama ushindi mkubwa katika usimamizi wa fedha za umma chini ya uongozi uliopo, ikionyesha uthabiti wa kiuchumi wa nchi hiyo katika ukanda wa Kusini mwa Afrika. Kwa mujibu wa takwimu hadi Machi mwaka huu, malipo hayo yamefikia jumla ya dola milioni 23.8875.

    Namibia sasa imejiunga na mataifa mengine ya Afrika, ikiwemo Msumbiji, ambayo yamefanikiwa kufuta madeni yao kwa IMF, ikifuata mwenendo wa kupunguza mikopo ya nje na kuimarisha nidhamu ya kifedha.

    Akiwa na umri wa miaka 72 rais wa kwanza mwanamke Namibia alishinda uchaguzi kwa 57% ya kura huku mpinzani wake wa karibu Panduleni Itula akipata 26% ya kura, kulingana na tume ya uchaguzi nchini humo.

    Netumbo Nandi-Ndaitwah ameingia madarakani mwezi Disemba 2024.

  2. Marekani yauza silaha zenye thamani ya dola bilioni 8.6 kwa washirika wake wa kikanda

    Marekani imeidhinisha mauzo ya silaha zenye thamani ya jumla ya dola bilioni 8.6 kwa washirika wake katika Mashariki ya Kati, uamuzi uliotolewa zaidi ya wiki tatu baada ya kusitishwa kwa mapigano kati ya Marekani, Israel na Iran.

    Nchi zitakazonufaika na silaha hizo ni Israel, Qatar, Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu.

    Kwa mujibu wa mpango huo, Qatar itapatiwa mfumo wa ulinzi wa anga na makombora wa Patriot pamoja na vifaa husika, wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 4.

    Aidha, mauzo ya mifumo ya silaha za mashambulizi ya usahihi wa hali ya juu pia yameidhinishwa, yakiwa na thamani ya dola milioni 992.4.

    Kuwait imeidhinishwa kupokea mfumo jumuishi wa amri ya vita wenye thamani ya dola bilioni 2.5, huku Israel ikiruhusiwa kununua mifumo hiyo hiyo ya silaha za mashambulizi ya usahihi yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 992.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia imeidhinisha mauzo ya mfumo huo huo kwa Umoja wa Falme za Kiarabu, wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 147.

    Soma zaidi;

  3. Uhaba wa vileo washuhudiwa Saudi Arabia kutokana na vita mashariki ya kati

    Duka pekee la serikali la pombe nchini Saudi Arabia linakabiliwa na upungufu wa bidhaa mbalimbali, kuanzia bia na mvinyo hadi tequila, huku wateja wakiiambia Reuters kuwa usambazaji umechelewa kutokana na athari za vita vya Iran.

    Duka hilo lililopo katika eneo la kidiplomasia mjini Riyadh linafanya kazi bila jina wala bango la kunadi biashara.

    Lilifunguliwa mwaka 2024 kuhudumia mabalozi wasio Waislamu, na mwaka uliopita likapanua huduma zake kwa wafanyakazi matajiri wasio Waislamu kutoka nje ya nchi.

    Hata hivyo, marufuku kamili ya matumizi ya pombe iliyoanza kutumika mwaka 1952 bado yanaendelea nchini Saudi Arabia. Licha ya msimamo wake wa kihafidhina, taifa hilo limeruhusu duka moja lenye leseni kwa lengo la kuvutia wafanyakazi wa kigeni.

    Kwa mujibu wa Reuters, watu watano waliolitembelea duka hilo siku za hivi karibuni walisema rafu zake zilikuwa na bidhaa kidogo za pombe, ambazo ni ghali na zingine za kampuni zisizojulikana sana.

    Unaweza kusoma pia:

  4. Marekani kuondoa wanajeshi 5,000 Ujerumani kufuatia mvutano na Merz

    Idara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetangaza kuondoa takriban wanajeshi wake 5,000 nchini Ujerumani.

    Hatua hiyo inaonekana kama ujumbe wa kisiasa kwa mshirika wake wa NATO, huku mvutano kati ya Rais Donald Trump na mataifa ya Ulaya ukiongezeka kufuatia vita vya Iran.

    Trump alikuwa ametishia mapema wiki hii kupunguza uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Ujerumani.

    Kauli hiyo ilijiri baada ya mzozo wa maneno kati yake na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, ambaye alisema "Wamarekani hawana mkakati" na hangeweza kuona "ni njia gani ya kutoka" ambayo wanaweza kuchagua.

    "Wairani ni wazi wana ustadi mkubwa wa kufanya mazungumzo, au tuseme, ni wastadi sana wa kutofanya mazungumzo, kuwaruhusu Wamarekani kusafiri hadi Islamabad na kisha kuondoka tena bila matokeo yoyote," alisema. Akaongezea kuwa "taifa zima" akirejelea Marekani ilikuwa "linafedheheshwa" na uongozi wa Iran.

    Msemaji wa Pentagon Sean Parnell amesema mchakato wa kuondoa wanajeshi hao unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi sita hadi kumi na mbili.

    Trump pia amependekeza kuwaondoa wanajeshi wa Marekani kutoka Italia na Uhispania.

    "Italia haijatusaidia chochote na Uhispania imekuwa ya kutisha," aliongeza, akiwakosoa kwa majibu yao kuhusu vita nchini Iran. "Katika hali zote walisema, 'Sitaki kujihusisha.'

    Soma Pia:

  5. Trump asema ataongeza ushuru kwa magari yanayoagizwa kutoka Ulaya hadi asilimia 25

    Rais wa Marekani Donald Trump ameongeza ushuru unaotozwa magari na malori yanayoagizwa kutoka Umoja wa Ulaya hadi asilimia 25, hatua inayoongeza kwa kasi mvutano wa kibiashara kati ya Washington na Brussels.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump ameshutumu Umoja wa Ulaya kwa kile alichokiita kutotekeleza makubaliano ya biashara ambayo tayari yalikuwa yameafikiwa, ingawa hakutoa maelezo ya kina.

    “Nimefurahi kutangaza kwamba… wiki ijayo nitaongeza ushuru unaotozwa Umoja wa Ulaya kwa magari na malori,” alisema Trump Ijumaa.

    Tume ya Ulaya imejibu kwa kusema itaendelea kuweka chaguo zote mezani ili kulinda maslahi ya Umoja wa Ulaya.

    Tume hiyo imesema EU inatekeleza wajibu wake katika makubaliano hayo, lakini pia inatafuta ufafanuzi zaidi kutoka Marekani kuhusu upande wake wa utekelezaji.

    Hatua ya Trump kulenga sekta ya magari imechukuliwa kama pigo kubwa, ikizingatiwa sekta hiyo ni mhimili muhimu wa uchumi wa Ulaya.

    Hatua hiyo inakuja chini ya mwaka mmoja tangu EU na Marekani zikubaliane makubaliano katika uwanja wa gofu wa Turnberry nchini Scotland, yaliyopunguza ushuru wa bidhaa nyingi za Ulaya hadi asilimia 15.

    Makubaliano hayo yalionekana kuiletea EU nafuu baada ya Trump kutishia ushuru wa hadi asilimia 30 chini ya mpango wake mpana wa kile alichokiita “Siku ya Ukombozi.” Kwa upande wake, Ulaya ilikubali kuwekeza Marekani na kufanya mabadiliko yaliyotarajiwa kuongeza mauzo ya bidhaa za Marekani.

    Alipoulizwa ni kwa namna gani EU imekiuka makubaliano hayo, Trump hakutoa ufafanuzi.

    Alisema: “Tuna makubaliano ya biashara na Umoja wa Ulaya. Hawakuyazingatia ipasavyo, ndiyo maana nimeongeza ushuru kwa magari na malori.”

    Soma zaidi:

  6. Trump: Vita na Iran vimekwisha, lakini hatutaondoka haraka

    Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza mbele ya Bunge la Marekani kuwa vita na Iran “vimekwisha,” huku akisisitiza kuwa hana nia ya kusitisha mzozo huo kwa haraka.

    Rais huyo pia amejaribu kuimarisha hoja yake kwamba hahitaji idhini ya wabunge kuendelea na operesheni hiyo ya kijeshi.

    Katika barua aliyowasilisha kwa viongozi wa Bunge Ijumaa, Mei mosi, wakati ukikaribia mwisho wa muda wa kuwasilisha taarifa kuhusu vita hivyo, Trump alisema hakuna mapigano yoyote yaliyotokea kati ya pande hizo mbili tangu kusitishwa kwa mapigano.

    Ameiambia Congress kuwa “mapigano yaliyoanza Februari 28, 2026 yamekamilika.”

    Kwa mujibu wa Sheria ya Madaraka ya Vita ya mwaka 1973 nchini Marekani, rais anaweza kutumia nguvu za kijeshi bila idhini ya Bunge kwa siku 60 pekee. Baada ya hapo, anatakiwa kusitisha operesheni, kupata idhini ya Bunge, au kuomba nyongeza ya siku 30 endapo kuna dharura ya kijeshi inayohusiana na usalama wa majeshi ya Marekani wakati wa uondoaji.

    Trump pia amesema Marekani haina mpango wa kusitisha mapambano na Iran mapema, akionya kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha “tatizo lilelile kujirudia baada ya miaka michache.”

    Wakati huohuo, shirika la habari la IRNA liliripoti kuwa Tehran imewasilisha pendekezo jipya la mazungumzo na Marekani kupitia wapatanishi wa Pakistan, lakini Trump alilikataa haraka pendekezo hilo.

    Soma zaidi:

  7. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ya Jumamosi ya tarehe 2/05/2026.