Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Zijue faida nne za kiafya za kutoka nje wakati wa mvua
Kuanzia harufu yake ya kipekee hadi chembechembe hasi inazoachilia hewani, mvua ina manufaa yanayovutia kwa mwili wa binadamu, hasa katika kuboresha hali ya hisia.
Mvua si tu huleta nafuu ya joto, bali tafiti zinaonyesha pia inaweza kuboresha hali ya moyo, kusafisha hewa, kuchochea kumbukumbu na kusaidia mwili kupumzika.
Ilikuwa siku ya sita mfululizo kwa kiwango cha joto kuhisiwa kuzidi nyuzi 38 za selsiasi mjini New Milford, Connecticut, pale anga lilipoanza kubadilika na kuwa na rangi ya zambarau ya kutisha.
Nilikuwa ninaongoza warsha ya maigizo ya nje, ndipo nikawaona washiriki wakitazama kwa mshangao wingu refu la kutisha lililokuwa likisogea juu yetu.
Ghafla, radi zilitetemesha ardhi na umeme ukasambaa angani kama mtandao usio sawa wa nyuzi za buibui.
Tuliisikia mvua kabla hatujaigusa.
Kisha kwa ghafla, tukajikuta tumelowanishwa kabisa na manyunyu mazito yaliyotushukia kwa nguvu. Hakuna aliyeweza kumsikia mwenzake, hivyo nikaonyesha jukwaa lililokuwa karibu lenye paa, ambako mifuko ya nguo za kufuliwa ilikuwa imehifadhiwa, na mimi pamoja na wanafunzi wangu tukakimbilia huko.
Tukiwa tumelowa na kucheka, tukajitupa juu ya rundo la nguo chafu na kuendelea kulitazama dhoruba ikifoka. Baada ya takriban dakika 30, anga lilitulia na hewa ikawa safi na nyepesi kwa namna ya kushangaza.
Harufu kali na ya kipekee ya mvua ilitanda kila mahali.
Tulipokuwa tukirejea eneo la mazoezi, nyasi na miti vilionekana kuwa vya kijani zaidi na vyenye uhai mpya. Kila mmoja alionekana mwepesi zaidi, tabasamu likawa rahisi usoni, nami nikahisi kana kwamba ukungu mzito uliokuwa umefunika akili ulikuwa umetoweka.
Je, ilikuwa ni kwa sababu wimbi la joto lilikuwa limepungua, au msisimko wa kukimbilia mafichoni? Au huenda mvua yenyewe ilikuwa imechangia kuboresha hali yetu ya hisia?
Inaonekana kwamba baada ya miongo kadhaa ya utafiti kuhusu uwezo wa mvua kuboresha hisia, wanasayansi sasa wamepata ushahidi wa kuunga mkono wazo hilo.
Na hiyo si faida yake pekee. Tafiti zinaonyesha mvua pia husaidia kuondoa chembe hatari hewani, huku harufu yake ikisemekana hata kuchochea kumbukumbu.
1. Huchochea kemikali ya furaha mwilini
Moja ya sababu kuu ni kwamba mvua huongeza chembechembe hasi hewani. Hizi ni molekuli za oksijeni zenye elektroni ya ziada zinazozalika matone ya mvua yanapogongana au kupasuka yanapogusa ardhi.
Wataalamu wanasema chembechembe hizi zinaweza kuchochea uzalishaji wa serotonini katika ubongo, kemikali inayohusishwa na furaha, utulivu na kupungua kwa msongo wa mawazo.
Kwa mtazamo mpana, kutembea wakati wa mvua kunaweza kusaidia kuboresha hali ya moyo na akili. Hata hivyo, tahadhari inahitajika iwapo kuna radi au umeme.
Baadhi ya wanasayansi wanaeleza kuwa athari hizi chanya huenda zinasababishwa na chembechembe hasi hewani kuongeza kiwango cha oksijeni katika damu, jambo ambalo linaweza kuboresha hali ya hisia kwa namna inayofanana na athari ya mazoezi makali ya mwili.
Hata hivyo, bado hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoeleza kwa uhakika mfumo wa kibaolojia unaosababisha athari hizo.
Pam Dalton, mwanasayansi wa utambuzi katika Kituo cha Monell cha Sayansi ya Hisia za Kemikali nchini Marekani, anasema bado haijaeleweka kikamilifu kwa nini chembechembe hasi huathiri hali ya hisia, uchovu, afya ya moyo na mishipa pamoja na shinikizo la damu.
"Ingawa jambo hili linavutia, bado hakuna mwafaka mpana wa kisayansi kuhusu manufaa yake ya kibaolojia. Na hata zaidi, bado haijulikani kwa uhakika ni mifumo gani inayofanya chembechembe hasi kuleta athari hizi," anasema Dalton.
End of Pia unaweza kusoma:
Utafiti kuhusu athari za chembechembe hasi kwa hali ya hisia ulianza miaka ya 1950. Hata hivyo, matokeo yake yaliendelea kuwa ya kutatanisha hadi miaka ya 1990, wakati vifaa vya kisasa zaidi vya kuzalisha chembechembe hasi vilipoanza kupatikana.
Katika utafiti muhimu uliofanywa mwaka 1995, watafiti walibaini kuwa watu waliokuwa wakisumbuliwa na mfadhaiko wa msimu walionyesha uwezekano mkubwa zaidi wa kupungua kwa dalili zao baada ya kupata tiba ya kila siku kwa kutumia vifaa vya nguvu ya juu vinavyozalisha chembechembe hasi, ikilinganishwa na waliopata matibabu ya kiwango cha chini.
Kwa mujibu wa Michael Tehan, profesa katika Chuo Kikuu cha Columbia na kiongozi wa utafiti huo, mvua kubwa huzalisha kiwango cha chembechembe hasi hewani kinachokaribiana na kile kinachozalishwa na vifaa hivyo vya nguvu ya juu.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa hadi sasa hakuna utafiti uliothibitisha moja kwa moja uhusiano huo, wala kuonyesha kwa uhakika kuwa muda anaokaa mtu kwenye mvua una uhusiano wa moja kwa moja na mabadiliko ya hali ya hisia.
2. Husafisha hewa na kurahisisha kupumua
Mvua pia husaidia kusafisha hewa kwa kuondoa chembechembe zinazoelea kama vumbi, uchafuzi wa mazingira na vichochezi vya mzio.
Chembechembe hasi zinazozalishwa wakati wa mvua huvuta chembe hizi ndogo na kuzishusha ardhini, hivyo kufanya hewa iwe safi zaidi na rahisi kuvuta.
Wataalamu wanasema hali hii inaweza kusaidia afya ya mfumo wa upumuaji na pia kupunguza msongo wa mawazo, kwa kuwa hewa chafu imehusishwa na wasiwasi na matatizo ya afya ya akili.
"Kuna ushahidi wa kuridhisha unaoonyesha kuwa chembechembe hasi zina uwezo wa kuondoa vumbi, bakteria, vichochezi vya mzio na chembe nyingine kutoka hewani, jambo ambalo linaweza kuwa na manufaa kwa afya ya mfumo wa upumuaji kwa watu wengi," anasema Dalton.
Hadi takriban muongo mmoja uliopita, haikuwa wazi kikamilifu chembechembe hasi zina ufanisi kiasi gani katika kusafisha hewa.
Katika utafiti uliofanywa mwaka 2015, watafiti waliiga uwezo huo kwa kiwango kidogo kwa kuingiza aina mbalimbali za chembe ndani ya chumba cha kioo kilichotengenezwa mahsusi kuunda matone ya mvua.
Baada ya matone hayo kuyeyuka, watafiti walikusanya chembe zilizobaki na kurekodi zilipokuwa ili kubaini iwapo zilikuwa zimevutwa na matone hayo.
Waligundua kuwa matone madogo ya mvua yalikuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuvuta chembechembe hizo kutoka hewani.
Dan Cziczo, mmoja wa waandishi wa utafiti huo na profesa wa Sayansi ya Dunia, Anga na Sayari katika Chuo Kikuu cha Purdue nchini Marekani, anasema matone ya mvua yanapoanguka ardhini, kwa asili huwa kama yanazoa chembechembe ndogo zinazozunguka hewani zinazokutana nazo.
Chaji ya umeme iliyomo ndani ya tone la mvua hufanya kazi kama sumaku kwa chembechembe hizo, na kusababisha mchakato wa kuzivuta na kuziunganisha unaojulikana kama mgandamizo wa chembe.
Cziczo analinganisha hali hiyo na kinachotokea katika eneo la ujenzi pale maji yanaponyunyizwa juu ya vumbi. Vumbi lililokuwa likielea hewani husukumwa chini na kutua ardhini, na hivyo kuifanya hewa kuwa safi zaidi.
Nguvu ya mvua pia ina mchango wake.
"Kadri mvua inavyokuwa kubwa, ndivyo uwezo wake wa kusafisha hewa unavyoongezeka," anasema Cziczo. Hali hiyo pia husaidia kupunguza chembechembe chanya hewani, ambazo zimehusishwa na kuongezeka kwa hasira na msongo wa mawazo.
Mvua kubwa ikinyesha tena, unaweza kufikiria kufungua madirisha mara tu baada ya mvua kukoma.
Huenda ukagundua kuwa hewa inaonekana safi zaidi, na ikiwa mvua hiyo imefuatia upepo wa baridi, kama ilivyo kawaida kwa mvua kubwa, upepo huo unaweza kuingiza hewa safi zaidi ndani ya nyumba na kuboresha ubora wa hewa unayovuta.
3. Harufu ya mvua huchochea kumbukumbu
Harufu ya mvua inayojulikana kama Petrichor ni miongoni mwa harufu zinazotambulika kwa urahisi zaidi.
Harufu hii hutokea mvua inapogusa ardhi kavu na kuachilia chembechembe kutoka kwenye udongo, mimea na bakteria wa asili.
"Perichor hutokea wakati mvua inapotoa erosoli kutoka kwenye udongo," anasema Phil Stevenson, profesa wa kemia ya mimea katika Chuo Kikuu cha Greenwich na mkuu wa utafiti kuhusu sifa za mimea na kuvu katika bustani ya Kew nchini Uingereza.
"Wakati wa ukame, molekuli za kikaboni kutoka kwa mimea, wanyama, na udongo wenyewe hujilimbikiza kwenye nyuso. Matone ya mvua yanapoathiri, molekuli hizi - ikiwa ni pamoja na mafuta ya mimea tete - kipande, na kuwa chembe zinazoning'inia hewani."
Wanasayansi wanasema harufu hii inaweza kuamsha kumbukumbu za zamani na hisia za ndani kwa sababu harufu ina uhusiano wa karibu na sehemu ya ubongo inayoshughulikia hisia na kumbukumbu.
Ndiyo maana mara nyingi harufu ya mvua huibua hisia za utulivu, kumbukumbu za utotoni au hali ya faraja isiyoelezeka kwa urahisi.
Hivyo, mvua itakapokunya tena, angalia kupitia dirisha lililo wazi au tembea nje baada ya mvua kukatika na unusie harufu yake. Zingatia ni kumbukumbu gani za mbali zinazojitokeza akilini mwako kutoka matukio ya zamani.
Sauti ya mvua hutuliza akili
Mbali na harufu yake, sauti ya mvua pia ina athari ya kutuliza akili. Sauti ya mvua ya taratibu imeonekana kupunguza kiwango cha homoni ya msongo wa mawazo mwilini na kusaidia mwili kupumzika.
Wataalamu wa afya ya sauti wanasema sauti ya maji huamsha mfumo wa mwili unaosaidia kupumzika, kupunguza mapigo ya moyo na kushusha msongo wa mawazo.
Hii ndiyo sababu sauti ya mvua hutumika mara nyingi katika vifaa vya kusaidia usingizi na kutuliza akili.
Mvua si tukio la kawaida tu la hali ya hewa
Kwa mujibu wa sayansi, mvua ni zaidi ya tukio la kawaida la hali ya hewa. Inaweza kuboresha hali ya hisia, kusafisha hewa, kuamsha kumbukumbu na kutuliza akili.
"Iwapo mtu anasikiliza sauti hizi kwa makusudi kama sehemu ya utaratibu wa kujituliza, uzoefu huo unaweza kuanza kufanana na mazoezi ya umakini au tafakuri, ambapo sauti hutumika kama kiungo cha kuelekeza umakini na kuleta utulivu wa akili."
Ingawa mvua niliyoishuhudia haikunipeleka moja kwa moja kwenye hali ya utulivu wa kina wa kiakili, ilinisaidia kujihisi nafuu zaidi na kuwa karibu zaidi na wakati wa sasa.
Sasa, kila mvua inaponyesha, hujaribu kutenga muda zaidi wa kujizamisha kikamilifu katika uzoefu huo. Wakati mwingine utakapoona mvua katika utabiri wa hali ya hewa, fikiria kuutazama na kuuhisi kwa makini. Huenda ukapata mshangao wa kupendeza.
Kwa hiyo, mvua inayonyesha huenda isiwe sababu ya kujifungia ndani pekee, bali pia fursa ya kuipa akili na mwili nafuu ya asili.