Mkurugenzi wa zamani wa shirika la upelelezi la Marekani, FBI, James Comey, amejisalimisha kwa mamlaka ili kukabiliana na mashtaka yanayodai kuwa picha aliyosambaza kwa muda mfupi kwenye mitandao ya kijamii ilikuwa tishio kwa maisha ya Rais wa Marekani Donald Trump.
Kesi hiyo inatokana na chapisho la mwaka 2025 kwenye Instagram lililowekwa na Comey, lililokuwa na picha ya magamba ya baharini yaliyopangwa kuunda maneno “86 47”. ni istilahi ya mtaani inayomaanisha “kuondoa”, na waendesha mashtaka wanadai kuwa inahamasisha vurugu dhidi ya Trump, rais wa 47.
Comey alikanusha mashtaka akisema hakujua maana ya namba hizo, na ameshutumu upande wa mashtaka kwa kuwa na nia za kisiasa.
Hii ni mara ya pili kwa Wizara ya Sheria kumfungulia mashtaka ya jinai Comey, ambaye ni mkosoaji wa muda mrefu wa Trump.
Comey hakuweka ombi la kujitetea wala kuzungumza wakati alipofikishwa mahakamani kwa muda mfupi katika jimbo la Virginia.
Wakili wake, Patrick Fitzgerald, alisema mkurugenzi huyo wa zamani atataka kesi ifutwe kwa misingi ya mashtaka ya kuchagua na yenye nia ya kulipiza kisasi — akidai alilengwa kwa sababu ya kuzungumza dhidi ya Trump.
Jaji Fitzpatrick alikataa juhudi za Wizara ya Sheria kuweka masharti ya kuachiliwa kwa Comey, akisema hayakuwa ya lazima, kwa mujibu wa CBS News.
Waendesha mashtaka wamemshtaki Comey kwa kujua na kwa makusudi kutoa tishio la kuondoa maisha ya — na kusababisha madhara ya kimwili kwa — rais, na pia kusambaza tishio hilo kati ya majimbo.
Kila shtaka lina adhabu ya juu ya hadi miaka 10 jela.
Katika taarifa ya video Jumanne, Comey alisema ana nia ya kupambana na mashtaka hayo.
Chapisho lake la awali la Mei 2025 lilikuwa na picha ya magamba ya baharini ufukweni yaliyopangwa kuonyesha “86 47”, likiwa na maelezo: “Mpangilio mzuri wa magamba ya baharini wakati wa matembezi yangu ufukweni.”
Comey alifuta picha hiyo baada ya malalamiko ya umma.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mashtaka dhidi ya Comey Jumatano, Trump alimuita “mtu fisadi”.
“Niseme yeyote anayejua kuhusu uhalifu, anajua 86. Ni istilahi ya magenge ya uhalifu inayomaanisha muue. Magenge hutumia neno hilo wanapotaka kumuua mtu, wanasema ‘86 huyo’.
Watu kama Comey ni tishio kubwa sana, nadhani, kwa wanasiasa na wengine,”
Baadhi ya wataalamu wa sheria — pamoja na wabunge — wamehoji uzito wa mashtaka hayo.
Comey alifutwa kazi na Trump katika muhula wake wa kwanza baada ya kuanzisha uchunguzi kuhusu uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi wa urais wa Marekani wa 2016.
Tangu wakati huo, Trump amekuwa akitaka mara kwa mara kufunguliwa mashtaka dhidi yake — na mashtaka ya sasa ni jaribio la pili la utawala kufanya hivyo.