Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Majengo 8 yenye rangi za kuvutia zaidi duniani
Kwa muda mrefu, wabunifu wa majengo wamekuwa wakitumia rangi kama nyenzo muhimu ya kuongeza mvuto na ubunifu katika kazi zao.
Matumizi ya rangi kuwasilisha hisia za furaha na uzuri yamekuwepo kwa maelfu ya miaka.
Jamii za kale za Neanderthal zilipamba kuta za mapango kwa rangi zilizotengenezwa kutoka kwenye udongo na madini mbalimbali.
Baadaye, ustaarabu wa Misri na Ugiriki ya kale ulijenga mahekalu yenye rangi ang'avu, huku Waroma wakitumia marumaru za rangi tofauti kupamba majengo yao makubwa.
Katika vipindi vyote hivyo vya historia, rangi ilikuwa sehemu muhimu ya usanifu na ilionekana karibu kila mahali.
Rangi ilitekeleza jukumu muhimu katika madirisha ya vioo vya makanisa ya enzi za kati, pamoja na dari na kuta zilizopambwa kwa michoro ya fresco wakati wa kipindi cha Renaissance nchini Italia.
Pia imekuwa sehemu muhimu ya majengo ya kisasa yenye nyuso angavu na zinazong'aa katika karne ya 20 na 21. Mfano mmoja ni lango lenye umbo la mchemraba la Kituo cha Pompidou mjini Malaga, lililobuniwa na Daniel Buren, ambalo linajulikana kwa matumizi yake ya kipekee ya mwanga na rangi.
Mbunifu Adam Nathaniel Furman na mwandishi Kate Mazade, katika kitabu chao Chromatic Architecture: The Craft of Colour in Design, wanaeleza kwamba rangi ni "kipengele muhimu kinacholiinua jengo na kulifanya livutie na kuleta furaha kwa namna ambayo haiwezi kufanikishwa kwa njia nyingine."
Majengo haya manane yanadhihirisha jinsi rangi zinavyoweza kubadilisha sura na hisia za majengo, huku zikiwapa wasanifu majengo msukumo wa kutumia rangi kwa ujasiri zaidi katika kazi zao.
Hekalu la Sri Ranganatha Swamy, Tamil Nadu, India
Hekalu la Sri Ranganatha Swamy huko Tamil Nadu ni miongoni mwa majengo yanayotambulika zaidi nchini India.
Mchanganyiko wake wa rangi angavu za bluu, kijani, njano, nyekundu na zambarau hulifanya kuwa mfano bora wa jinsi rangi zinavyoweza kutumika kuonyesha utamaduni, imani na utambulisho wa eneo husika.
Muonekano wake wa kuvutia umeifanya hekalu hilo kuwa moja ya alama maarufu za usanifu wa Kihindu duniani.
Ujenzi wa Hekalu la Sri Ranganatha Swamy ulianza katika karne ya kwanza BK na kuendelea kupanuliwa na tawala mbalimbali kwa muda wa karne nyingi, hadi kufikia mwishoni mwa karne ya 20.
Leo, ni moja ya majengo makubwa zaidi ya kidini duniani, likiwa na eneo la zaidi ya hekta 60.
Eneo hilo limezungukwa na malango 21 ya kuingilia yanayojulikana kama gopuram, ambayo yamepambwa kwa mamia ya sanamu za rangi angavu na za kuvutia. Mapambo hayo ya pande tatu huifanya hekalu hiyo kuwa moja ya mifano maarufu zaidi ya usanifu wa jadi wa Kihindu.
2. Palau de la Musica Catalana, Barcelona, Hispania
Uzuri wa ukumbi wa tamasha wa Palau de la Música Catalana, uliojengwa mwaka 1908, umekuwa ishara ya utambulisho wa Catalonia, eneo la Uhispania lenye utajiri wa kitamaduni na historia ya maendeleo ya viwanda.
Jengo hilo, lililobuniwa na mbunifu Lluís Domènech i Montaner, linaunganisha mitindo mbalimbali ya usanifu ikiwemo Art Nouveau, Romanesque na Neo-Gothic, pamoja na athari za usanifu wa Mudéjar na mila za Valencia.
Kwa mwanahistoria wa usanifu Geoffrey Furman, kila sehemu ya Palau de la Música imejaa ishara na alama zinazolipa jengo hilo sura ya ulimwengu wa hadithi za kichawi.
"Kila jiwe, nguzo, ukingo na mapambo ya jengo hili yamepambwa kwa rangi na maumbo ya kuvutia yanayoonekana kuyaingiza maisha kwa namna ya ajabu na ya kichawi," anaeleza Furman.
3. Jengo la Guardian, Detroit, Michigan, Marekani
Jengo hili la ofisi lililojengwa mwaka 1929 na kubuniwa na mbunifu Wirt C. Rowland linajulikana miongoni mwa wakazi wa eneo hilo kama "Kanisa Kuu la Fedha" kutokana na muonekano wake wa fahari na umuhimu wake wa kihistoria.
Pia linahesabiwa kuwa miongoni mwa majengo muhimu zaidi duniani yaliyobuniwa kwa mtindo wa usanifu wa Art Deco.
Akizungumza na BBC, Mazade anasema Rowland alitumia rangi kuonyesha ustadi wa hali ya juu wa mafundi wa eneo la Maziwa Makuu nchini Marekani mwanzoni mwa karne ya 20.
Sehemu ya nje ya jengo hilo imefunikwa na karibu matofali milioni mbili pamoja na vigae vya terracotta vyenye rangi ya chungwa, vinavyolipa mwonekano wake utambulisho wa kipekee.
Ndani, ukumbi mkuu una dari yenye matao ya viwango vitatu, iliyopambwa kwa vigae vya rangi za msingi vilivyopangwa katika muundo unaofanana na blanketi la viraka.
"Jengo hili lilikuwa alama ya mafanikio makubwa ya kibiashara ya Detroit katika enzi yake, na hadi leo linaendelea kuwa kumbukumbu hai ya kipindi hicho cha ustawi," anaongeza Mazade.
4.Duka la De Bijenkorf, Eindhoven, Uholanzi
Inasemekana mbunifu, msanifu na msanii wa Italia, Gio Ponti, alipata msukumo wa kubuni jengo hili mwaka 1969 kutokana na mandhari ya mashamba ya Uholanzi yenye gridi za kijani kibichi alizoziona kutoka dirishani mwa ndege.
Kuipa mvuto wa kipekee jengo kubwa lisilo na madirisha kungekuwa changamoto kwa wasanifu wengi, lakini si kwa Ponti, ambaye anahesabiwa kuwa mmoja wa waanzilishi muhimu wa usanifu wa kisasa pamoja na majina makubwa kama Le Corbusier na Mies van der Rohe.
Kwa mujibu wa Geoffrey Furman, Ponti alilibadilisha jengo hilo kuwa "mandhari kubwa ya kuvutia yenye mng'aro wa zumaridi", lililoonekana tofauti kabisa na majengo mengine ya wakati huo.
Kwa kufanya hivyo, aliubadilisha uso wa kawaida wa zege uliotawala katika enzi hiyo na kuugeuza kuwa kazi bora ya sanaa ya kisasa iliyotoa sura mpya kwa jiji hilo.
5. Reversible Destiny Lofts, Tokyo, Japan
Mradi huu wa nyumba za kupangisha wa mwaka 2005 ulianzishwa kwa ajili ya kumuenzi Helen Keller, mwandishi na mtetezi wa haki za watu wenye ulemavu nchini Marekani.
Kitabu kinaelezea vyumba hivyo tisa vya aina ya 'loft'—kazi ya Shusaku Arakawa na Madeline Gins—kama mchanganyiko wa kipekee na wa kisasa (bricolage) unaoundwa na maumbo ya silinda, prismu za mstatili, tufe, na vipengele vya usanifu wa kisasa vyenye rangi angavu.
Vipengele hivi vyote vimeunganishwa ili kuunda mazingira mbadala na ya kipekee ya kuishi, ambapo kila sehemu ya uso na kipande cha samani kinajaa msisimko wa rangi nyingi na kali.
Msanii Arakawa na mshairi Gins walilenga kuwatoa wakazi katika hali yao ya kawaida ya utulivu na kuwafanya wahisi mabadiliko kupitia uchaguzi wao wa rangi.
"Waliamini kuwa ikiwa mazingira yangefanikiwa kuwatoa watu katika mtindo wao wa maisha ya kukaa tu ndani na kuwapa nguvu mpya, wangeweza kuishi muda mrefu zaidi," anaeleza Mazade.
Walichanganya sakafu zenye mawimbi na vyumba vya umbo la tufe, kisha wakavipamba kwa mchanganyiko wa rangi unaoleta hisia kali na tele—yote haya yakilenga, kinadharia, kuwanufaisha wakazi wake, anaongeza.
6. Kiwanda cha Kuchoma Taka cha Maishima, Osaka, Japan
Msanii na mbunifu wa Austria Friedensreich Hundertwasser alifariki dunia mwaka 2000, mwaka mmoja kabla ya jengo hili kukamilika.
Kwa mujibu wa kitabu hicho, Hundertwasser alijulikana kwa kupinga mtindo wa kisasa wa usanifu (modernism) uliosisitiza miundo yenye nyuso tambarare na inayofanana. Badala yake, aliamini kwamba majengo yanapaswa kuonekana kama viumbe hai vinavyoendelea kukua na kubadilika, si mashine zilizoundwa kutekeleza kazi maalumu pekee.
Kwa Hundertwasser, falsafa hiyo ilipaswa kutumika kwa aina zote za majengo, kuanzia makazi ya watu hadi majengo ya viwandani.
Kiwanda cha Maishima kinafananishwa na kasri la kufikirika kutoka katika hadithi za watoto, kiasi kwamba mara nyingi hukosewa kuwa ni sehemu ya bustani ya burudani iliyo karibu.
Mistari ya njano inayofanana na michoro ya mkono huonekana ikiteremka kwenye sehemu za chini za jengo, huku mnara wake mrefu wa mviringo ukiwa umepambwa kwa mistari kama hiyo ya rangi nyekundu.
Majengo yote ndani ya eneo hilo, yakiwemo sehemu zilizojengwa kwa mtindo wa kutokeza nje ya nguzo zake, yamesimama juu ya nguzo fupi za mviringo zilizopambwa kwa vitalu vya rangi mbalimbali.
Kwa mujibu wa mwandishi Kate Mazade, kila sehemu ya muundo huu ni ishara ya uasi dhidi ya kanuni za kawaida za usanifu.
"Kiwanda cha kuchakata taka chenye bomba la moshi la rangi ya buluu ya kijani, kuta zenye michoro ya visanduku vya mraba na mistari ya rangi ya manjano na nyekundu angavu; ni nini kingeweza kuwa kitendo cha uasi zaidi ya hicho?" anasema Mazade.