Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran yalipiza kisasi baada ya mashambulizi ya Marekani kuua watu wanne katika harusi

Vikosi vya Marekani vilianza tena mashambulizi dhidi ya Iran siku ya Jumanne, kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom).

Muhtasari

  • Trump: Sijaribu kuileta Iran kwenye meza ya mazungumzo
  • Ujerumani yaishutumu Urusi kwa shambulio la uwanja wake wa ndege Leipzig
  • Iran yalipiza kisasi baada ya mashambulizi ya Marekani kuua watu wanne katika harusi

Moja kwa moja

Na Abdalla Seif Dzungu

  1. Jeshi la Jordan ladai "kuzuia na kuharibu makombora 10 kati ya 13" yaliyofyatuliwa na Iran

    Katika taarifa iliyothibitisha shambulio la makombora dhidi ya nchi hiyo usiku wa Jumanne, jeshi la Jordan lilidai kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga iliweza "kuzuia" na kuharibu "makombora 10 kati ya 13 yaliyofyatuliwa kutoka ardhi ya Iran," na kwamba makombora mengine matatu yaliangukia "maeneo ya mbali yasiyo na makazi ya watu."

    Saa moja iliyopita, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi kilitangaza mashambulio ya makombora dhidi ya kambi za Marekani nchini Jordan na kutoa picha zinazohusishwa na mashambulio hayo pamoja na mwendo wa makombora angani juu ya Jordan.

    Katika taarifa yake, Walinzi wa Mapinduzi walidai kuwa "makombora ya balistiki yalilenga kambi ya Jeshi la Majini la Marekani nchini Jordan, inayojulikana kama Camp Titin, iliyoko kwenye mwambao wa Ghuba ya Aqaba."

    Wakati huo huo, jeshi la Kuwait lilitangaza asubuhi ya Jumatano kuwa limewasha mifumo yake ya ulinzi wa anga ili kukabiliana na kile ilichokiita "vitu vinavyorushwa vyenye nia ya uhasama" na kuwataka wananchi kuzingatia maelekezo ya usalama yaliyotolewa.

  2. Trump: Sijaribu kuileta Iran kwenye meza ya mazungumzo

    Rais wa Marekani Donald Trump, katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social usiku wa Jumanne, alikanusha ripoti ya ABC News kwamba utawala wake ulikuwa ukijaribu kuilazimisha Iran kufanya mazungumzo, akisema hajali kuhusu kufikia makubaliano na Tehran.

    "Kinyume na kile ambacho ABC ambayo (yeye huiita) Habari za Uongo imeiripoti, sijaribu kuileta Iran kwenye meza ya mazungumzo. Sijali hata kidogo kama watatia saini makubaliano ambayo hayana thamani kwao," Bw. Trump aliandika.

    "Napendelea zaidi hali ya sasa, ambapo tuna udhibiti karibu kamili wa Mlango-Bahari wa Hormuz na uchumi wa Iran unaporomoka kabisa. Wanachelewesha tu mchakato ambao hauepukiki," aliongeza.

    Rais wa Marekani aliandika mwishoni mwa ujumbe huu: "Ni lini watu wa Iran watainuka na kupambana?"

    Kauli hizi zilitolewa saa chache baada ya Trump kuelezea mashambulizi mapya ya Marekani dhidi ya maeneo karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz kuwa ya "haki" na kuonya kwamba Washington ingefanya mashambulizi makali zaidi iwapo Iran ingechukua hatua yoyote ya kulipiza kisasi.

    Iran inasema mashambulizi hayo yalilenga raia katika sherehe ya harusi katika kijiji cha Kohstak Sirik, na kuua angalau watu watano, akiwemo mtoto mmoja. Vyombo vya habari vya Iran vinaripoti kuwa zaidi ya watu 60 walijeruhiwa katika tukio hilo.

  3. Ujerumani yaishutumu Urusi kwa shambulio la uwanja wake wa ndege Leipzig

    Ujerumani imesema Urusi ilihusika na shambulio la ndege zisizo na rubani mwezi uliopita katika uwanja wa ndege wa Leipzig.

    Droni iliobeba kilipuzi iligunduliwa katika Uwanja wa ndege wa Leipzig/Halle mashariki mwa Ujerumani, karibu na ndege za mizigo za Ukraine, mnamo tarehe 4 Agosti.

    Ilishindwa kulipuka kwani kipuzi hicho kilikuwa na hitilafu, na wachunguzi wanashuku kuwa ndege ya pili isiyo na rubani iligongana na ndege ya mizigo iliyokuwa karibu.

    Ndege ya tatu isiyo na rubani iliripotiwa kupatikana karibu na uwanja wa ndege siku 10 baadaye.

    Waziri wa mambo ya ndani Alexander Dobrindt alisema shambulio la uwanja wa ndege wa Leipzig lilifuata "mfumo uliowekwa vizuri wa shughuli mseto za Urusi barani Ulaya" na dhana ilikuwa kwamba Ujerumani ingelengwa tena.

    Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Jumanne aliishutumu Ujerumani kwa kuweka ushahidi wa kulaumu Moscow kwa jaribio la shambulio la ndege zisizo na rubani katika uwanja wa ndege wa Leipzig.

    Putin hakutoa ushahidi wa shutuma hiyo.

    Wakati huo huo, ubalozi wa Urusi huko Berlin ulisema madai kwamba Urusi ilihusika yalikuwa "ya kipuuzi".

    Dobrindt alisema uchunguzi wa vifaa vilivyotumika pamoja na matokeo ya kijasusi ulithibitisha kuhusika kwa Urusi katika shambulio hilo.

  4. Iran yalipiza kisasi baada ya mashambulizi ya Marekani kuua watu wanne katika harusi

    Vikosi vya Marekani vilianza tena mashambulizi dhidi ya Iran siku ya Jumanne, kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom).

    Centcom ilisema mashambulizi hayo ya Marekani yalifuatia "jaribio la hivi karibuni la mashambulizi" lililofanywa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) dhidi ya meli za kibiashara katika Mlango-bahari wa Hormuz.

    Shirika la Red Crescend la Iran lilisema watu wanne, akiwemo mtoto mdogo, waliuawa na zaidi ya 50 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya Marekani, baada ya vipande vya kombora la Marekani kugonga nyumba ambamo sherehe ya harusi ilikuwa ikiendelea huko Sirik, kusini mwa Iran.

    Kama jibu, Iran ilianzisha mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq na Jordan, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya eneo hilo na Jeshi la Jordan. Mashambulizi pia yaliripotiwa Kuwait na Bahrain.

    IRGC ilisema Marekani "itajutia" mashambulizi hayo. Kufikia mapema Jumatano, ilikuwa imerusha mfululizo wa makombora ya balistiki kuelekea kambi ya Jeshi la Majini la Marekani (Marines) huko Aqaba, Jordan, ikiwa ni kulipiza kisasi kwa shambulio la Sirik, kulingana na shirika la habari la Iran lisilo rasmi kikamilifu, Tasnim.

    Jeshi la Jordan lilisema lilizuia makombora 13 ya balistiki; 10 kati yake yaliangamizwa, huku matatu yakiangukia maeneo ya mbali. Hakukuwa na vifo wala majeraha kutokana na shambulio hilo la Iran.

    Mtandao huo pia ulisema kuwa kituo cha usalama wa taifa cha nchi hiyo kilikuwa kimetoa tahadhari kwa wakazi wa mikoa ya Aqaba na Mafraq kuhusu vipande vinavyoanguka kutoka angani, na kuongeza kuwa tahadhari hiyo imeondolewa.

  5. Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja