Mji wa kale wa chini ya ardhi unaobaki na ubaridi wakati wa joto na joto wakati wa baridi

d
    • Author, Selin Ugurtash
    • Akiripoti kutoka, BBC News
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Karne nyingi zilizopita, wakazi wa Kapadokia nchini Uturuki walilazimika kujificha chini ya ardhi ili kujikinga na maadui waliokuwa wakiivamia jamii yao. Lakini waligundua pia kuwa makazi hayo yaliwapa kinga dhidi ya hali mbaya ya hewa.

Leo, dunia inapokabiliwa na ongezeko la joto na athari za mabadiliko ya tabianchi, wataalamu wanajiuliza iwapo makazi hayo ya kale yanaweza kutoa suluhisho kwa changamoto za kisasa.

Kwa mamilioni ya miaka, upepo na mvua vimekuwa vikichonga miamba katika eneo la Kapadokia, katikati mwa Anatolia, na kuipa maumbo ya kipekee yanayoinuka kutoka ardhini. Maumbo hayo yanafanana na minara mirefu ya mawe.

Zamani, kabla sayansi haijatoa maelezo kuhusu jinsi yalivyoundwa, wenyeji waliamini kuwa yalitokana na nguvu za kimiujiza. Ndiyo maana wakayapa jina la fairy chimneys, yaani minara ya mawe ya majini.

Lakini chini ya mandhari hiyo ya kuvutia kuna kitu kingine cha kushangaza zaidi: mji wa kale uliojengwa chini ya ardhi, unaojulikana kama Derinkuyu.

Unapoanza kushuka katika vichuguu vyake vyenye giza, hisia zako hubadilika mara moja. Hewa baridi inagusa ngozi yako huku kuta za miamba zikikuzunguka kwa karibu. Njia hizo ni nyembamba na zina mwanga hafifu kiasi kwamba sauti nyingi hazisikiki, isipokuwa mwangwi wa hatua zako.

Huenda umetoka nje wakati wa dhoruba ya theluji. Au labda ni mwezi Julai na eneo hilo linakabiliwa na joto kali. Juu ya ardhi unaweza kuwa umevaa glavu kujikinga na baridi au unafuta jasho kutokana na joto. Lakini ndani ya Derinkuyu, jina linalomaanisha kisima kirefu kwa lugha ya Kituruki, halijoto hubaki kati ya nyuzi joto 15 na 17 za Selsiasi mwaka mzima.

Awali, mji huo ulijengwa kama hifadhi ya kujikinga na mashambulizi ya majeshi ya Waarabu yaliyokuwa yakivamia eneo hilo kati ya katikati ya karne ya saba na mwanzoni mwa karne ya 11.

Sasa, karne nyingi baadaye, mji huo unawafanya wataalamu kutafakari upya umuhimu wa usanifu wa chini ya ardhi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Watafiti na wapangaji wa miji wanachunguza iwapo mbinu zilizotumika kujenga makazi hayo zinaweza kusaidia kubuni maeneo salama ya kujikinga na joto kali na hali nyingine mbaya ya hewa.

Makazi yanayokinga dhidi ya hali mbaya ya hewa

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kundi la Obrek Cave Research Group ni jumuiya ya wapenda mapango na vichuguu ambao wamekuwa wakichunguza na kuchora ramani za baadhi ya miundo muhimu ya chini ya ardhi nchini Uturuki.

Miongoni mwa maeneo waliyoyachunguza ni vichuguu vilivyokuwa chini ya Hagia Sophia, jengo maarufu linalojulikana kama mojawapo ya makanisa makubwa zaidi duniani.

Ali Yamac, mmoja wa waanzilishi wa kundi hilo, amekuwa akichunguza mapango na miundo ya chini ya ardhi ya Kapadokia kwa miaka 15. Ni vigumu kupata watu wengi wanaoifahamu dunia hiyo ya chini ya ardhi kama yeye.

Kwa Yamac na wenzake, kuingia pangoni wakati wa hali mbaya ya hewa ni kama kupata mahali pa kujisitiri.

Anaeleza kuwa katika mapango yote, yawe ya asili au yaliyochimbwa na binadamu, halijoto hubaki karibu na wastani wa halijoto ya juu ya ardhi katika kipindi chote cha mwaka.

"Mapango hubaki na ubaridi wakati wa kiangazi na kuwa na joto wakati wa baridi. Hilo ni jambo lenye manufaa makubwa," anasema.

Anakumbuka safari moja ngumu ya uchunguzi wakati wa kiangazi, ambapo yeye na timu yake walikuwa na matumaini ya kugundua makazi mengine ya chini ya ardhi.

d

"Nilikuwa nikisali nikisema, Mungu tafadhali tuonyeshe makazi ya mapangoni, hifadhi ya chini ya ardhi au kitu chochote kitakachotuwezesha kujisitiri ndani ya mwamba," anasema.

Huenda ombi lake lilikuwa na maana kubwa zaidi kuliko alivyofikiria wakati huo.

Kwa mujibu wa baadhi ya makadirio, halijoto nchini Uturuki tayari imeongezeka kwa nyuzi joto 2.1 za Selsiasi ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya mapinduzi ya viwanda.

Mabadiliko hayo yanafanya mawimbi ya joto kuwa makali zaidi na ukame kujitokeza mara nyingi zaidi. Wakati huohuo, mifumo ya mvua inabadilika na hatari ya mafuriko inaongezeka.

Utafiti mmoja wa hivi karibuni unakadiria kuwa vifo vinavyotokana na joto kali mjini Istanbul vinaweza kuongezeka mara kumi ifikapo mwisho wa karne hii.

Lakini joto kali si changamoto pekee inayowakabili wakazi wa Uturuki.

Katika majira ya baridi, Kapadokia hukumbwa na kipindi kirefu cha baridi na theluji. Wakati mwingine halijoto hushuka chini ya nyuzi joto sifuri, na kuwalazimu wakazi kutegemea mifumo ya kupasha joto ambayo ni ghali na hutumia nishati kwa wingi.

Hivyo, wakati mabadiliko ya tabianchi yanapoendelea kuleta changamoto mpya, huenda makazi ya chini ya ardhi yakawa na nafasi muhimu katika maisha ya baadaye.

Ugunduzi wa bahati nasibu

Kwa muda mrefu, makazi mengi ya chini ya ardhi yaliyochimbwa na binadamu katika eneo la Kapadokia yalikuwa hayajulikani kwa watafiti.

Hali hiyo ilibadilika mwaka 1963, wakati mji wa Derinkuyu ulipogunduliwa kwa bahati nasibu.

Mwananchi mmoja aliyekuwa akikarabati nyumba yake alibomoa ukuta na kukutana na mtandao wa vichuguu vilivyoenea chini ya eneo hilo.

Ugunduzi huo haukumletea tu mji wa kale ambao haukujulikana. Pia ulimsaidia kuelewa kilichokuwa kikiwatokea baadhi ya kuku wake waliokuwa wakipotea.

Kilichomshangaza zaidi kuhusu Derinkuyu ni ukubwa wake.

Makadirio kuhusu idadi ya ngazi na kina cha mji huo hutofautiana. Baadhi ya vyanzo vinataja ngazi sita hadi 12, huku vingine vikikadiria kuwa zinaweza kufikia 18. Kina chake kinatajwa kuwa takribani mita 85.

Mji huo unaenea kwa urefu wa takribani kilomita 2.5 na unakadiriwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi watu hadi 20,000. Pia una takribani visima na mifumo 53 ya kupitisha hewa.

Kwa watu waliokuwa wakiishi katika mazingira ya hatari, uwezo wa mji huo kudumisha halijoto inayofaa mwaka mzima ulikuwa faida nyingine kubwa. Wakiwa chini ya ardhi, waliweza kujikinga na wavamizi huku wakiepuka pia athari za hali mbaya ya hewa.

Ingawa maeneo hayo hayatumiwi tena kama hifadhi dhidi ya hali mbaya ya hewa, wataalamu wanaona kuwa miundo kama hiyo katika sehemu nyingine za dunia inaweza kuwa na manufaa makubwa.

Miji inaanza kuangalia chini ya ardhi

"Tumezoea kupanua miji yetu kwa kujenga majengo marefu juu ya ardhi. Lakini nafikiri sasa tunapaswa kuanza kuona maeneo ya chini ya ardhi kama rasilimali pia. Hilo litahitaji mabadiliko katika namna tunavyofikiri kuhusu miji," anasema Francesco La Vigna.

La Vigna ni mtafiti katika Taasisi ya Italia ya Ulinzi wa Mazingira na Utafiti (ISPRA), na pia mwenyekiti wa kundi la wataalamu wa jiolojia ya miji katika EuroGeoServices (EGS).

Baadhi ya watafiti wenzake katika ISPRA wameanza kuchora ramani za maeneo ya chini ya ardhi ya mji mkuu wa Italia, Roma. Timu yake nayo inasaidia kutathmini ni maeneo gani yanaweza kubadilishwa kuwa hifadhi za kujikinga na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wazo lao ni kupanua dhana ya maeneo yanayoweza kutumika kwa makazi na shughuli za binadamu, kama walivyofanya wakazi wa Derinkuyu karne nyingi zilizopita.

La Vigna anaelezea hatua hiyo kuwa ni hatua muhimu katika historia ya makazi ya chini ya ardhi.

Hadi sasa, zoezi la kuchora ramani limebaini zaidi ya maeneo 7,000 ya chini ya ardhi katika jiji hilo. Maeneo hayo yanajumuisha machimbo ya zamani na vichuguu vya maji, na yana ukubwa wa jumla wa takribani kilomita za mraba 350.

Anasema ni muhimu kuyatambua maeneo hayo kwa usahihi na kuyajumuisha katika mpango mkuu wa maendeleo ya jiji.

n

Mji wa Helsinki nchini Finland tayari umeweka mfano wa namna maeneo ya chini ya ardhi yanavyoweza kutumika katika maisha ya kila siku.

Chini ya jiji hilo kuna mtandao wa miundo ya chini ya ardhi yenye urefu wa takribani kilomita 200. Ndani yake kuna maeneo ya kuchezea watoto, kumbi za sanaa, mabwawa ya kuogelea, jumba la makumbusho na hata kanisa.

Kama ilivyo Kapadokia, maeneo mengi ya chini ya ardhi ya Helsinki yalijengwa awali kwa ajili ya kujilinda wakati na baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Hili linaonyesha kuwa miundombinu inayojengwa kukabiliana na changamoto fulani inaweza kupata matumizi mapya pale changamoto nyingine zinapojitokeza.

Lakini si kila eneo la chini ya ardhi huanza kutumika kwa sababu ya mpango rasmi wa serikali au mamlaka za miji.

Katika mji wa Coober Pedy nchini Australia, unaojulikana kwa uchimbaji wa madini ya opal, wakazi waligundua kuwa kuchimba miamba laini na kujenga makazi ndani yake kunawasaidia kujikinga na hali mbaya ya hewa. Mbinu hiyo pia imepunguza kwa kiasi kikubwa gharama zao za nishati.

Changamoto na hatari za makazi ya chini ya ardhi

La Vigna anasema kubadilisha maeneo ya chini ya ardhi kuwa hifadhi zinazoweza kutumiwa na umma kutahitaji mchakato wa makini na wa hatua kwa hatua.

Hii ni kwa sababu maeneo hayo yana miundo tofauti. Baadhi ni machimbo ya migodi, huku mengine yakiwa ni bunkers za kisasa zilizojengwa kwa ajili ya vita.

Kwa upande wa maeneo ya kujihifadhi, kazi inaweza kuwa rahisi zaidi. Mara nyingi wataalamu huhitaji tu kuthibitisha uimara wa zege na kuhakikisha kuwa mifumo ya uingizaji hewa inafanya kazi ipasavyo.

Lakini hali huwa tofauti katika maeneo kama machimbo ya migodi na mapango ya Kapadokia, ambako kuta na paa zake zinaundwa na miamba ya asili.

Changamoto kuu ni kuhakikisha kuwa miundo hiyo haitaporomoka na kwamba watu watakaokuwa ndani yake watapata hewa safi ya kutosha.

Kapadokia iko katika eneo la mpasuko wa kijiolojia wa Egemish, unaoenea kwa zaidi ya kilomita 64 katika eneo hilo.

Ingawa hakuna matetemeko ya ardhi yaliyorekodiwa katika eneo hilo maalumu la mpasuko kwa miaka 17,000 iliyopita, Uturuki ni nchi inayokabiliwa na hatari ya matetemeko ya ardhi. Hivyo, usalama wa miundo hiyo hauwezi kuchukuliwa kirahisi.

Yamac anasema Kapadokia iliundwa kutokana na shughuli za volkano na mmomonyoko wa miamba, lakini michakato hiyo hiyo inaendelea kuibadilisha hadi leo.

Watafiti wanaonya kuwa hatari ya mapango na vichuguu kuporomoka ipo wakati wote.

La Vigna anakubaliana na tahadhari hiyo. Anasema wataalamu wanapaswa kuchunguza uimara wa kila eneo na kuruhusu matumizi yake pale tu wanapothibitisha kuwa hakuna dalili za kutokuwa salama.

Changamoto nyingine ni upatikanaji wa hewa.

Derinkuyu inajulikana kwa mfumo wake mzuri wa kupitisha hewa, lakini teknolojia ya kisasa inaweza kufanya mfumo huo uwe bora zaidi.

Kwa kutumia feni na vifaa vya kupima ubora wa hewa, mifumo hiyo inaweza kuondoa hewa iliyochakaa na kuingiza hewa safi kutoka nje.

Huko Helsinki, mifumo kama hiyo hutumika kudumisha ubora wa hewa katika hifadhi za chini ya ardhi. Maeneo hayo sasa yanaweza kuwahifadhi watu hadi 6,000 kwa usalama, hata pale milango inapolazimika kufungwa wakati wa shambulio.

Kubadili namna tunavyoyaona makazi ya chini ya ardhi

Kwa mujibu wa Yamac, kwa sasa mapango mengi ya Kapadokia ambayo hayana wakazi hutumiwa kuhifadhi viazi na ndimu.

Kwa kweli, kukodisha mapango hayo kwa ajili ya kuhifadhi mazao katika mazingira ya baridi kumekuwa chanzo cha mapato kwa baadhi ya wakazi.

Kwa mfano, mji wa Ortahsar, wenye wakazi zaidi ya 3,000, una takribani mapango 1,000 yanayokodishwa kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa. Mapango hayo yana uwezo wa kuhifadhi hadi makasha milioni tano ya matunda jamii ya machungwa.

Hata hivyo, Yamac anaamini kuwa mapango hayo yanaweza kuwa na matumizi mengine muhimu zaidi, hasa kwa watu wanaokabiliwa na joto linalozidi kuongezeka.

Anasema: "Badala ya kununua nyumba ambayo nitahitaji kuwasha kiyoyozi katika kila chumba, ningependelea kuishi katika nyumba iliyochongwa ndani ya mwamba, ambako halijoto ni nzuri na ya kustarehesha."

Hilo ndilo wazo ambalo watafiti kama La Vigna wanataka liingizwe katika mipango ya maendeleo ya miji. Wanataka maeneo ya chini ya ardhi yasichukuliwe tena kama sehemu zilizopuuzwa, bali kama sehemu ya miundombinu inayoweza kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa karne nyingi, miji ya kale ya chini ya ardhi ya Kapadokia imeonyesha kuwa binadamu tayari ana maarifa ya kujenga makazi yanayoweza kudumisha halijoto inayofaa bila kutegemea mifumo mikubwa ya kupasha au kupoza hewa.

Huenda sasa ni wakati wa kuanza kuangalia chini ya ardhi ili kupata baadhi ya majibu ya changamoto zinazotukabili juu yake.