Moja kwa moja , Putin awasili China kabla ya mkutano wa kihistoria na Trump na Xi

Rais wa Urusi Vladimir Putin awasili China kushiriki mkutano wa kihistoria wa pande tatu na Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa China Xi Jinping pembezoni mwa mkutano wa APEC.

Muhtasari

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Faidha Ngaga

  1. Nvidia yakataa kumrejesha Jensen Huang huku ikitangaza faida kubwa

    .

    Mauzo ya kampuni ya teknolojia ya Nvidia yameongezeka mara mbili na kuvuka dola bilioni 100 kwa mara ya kwanza, huku kampuni hiyo ikisisitiza kuwa haina mpango wa kumrejesha mwanzilishi mwenza wake aliyeondoka, Jensen Huang.

    Katika matokeo yake ya kwanza ya kifedha tangu kuondoka kwa Huang, kaimu mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, Colette Kress, amesema shughuli za kampuni zinaendelea kama kawaida na kuwaambia wawekezaji: "Tunaweza kulimudu hili."

    Mauzo ya kampuni hiyo kwa robo ya mwaka yameongezeka mara mbili ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita, na kufikia dola bilioni 115.8 (pauni bilioni 86.9). Hali hiyo imesababisha hisa za kampuni hiyo kupanda kwa asilimia 4.8 katika biashara baada ya soko kufungwa.

    Mapema siku ya Jumanne, Huang alisema angeheshimiwa kurejea na kuiongoza Nvidia, baada ya kuondoka kufuatia madai ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa, yakiwemo uhusiano na mtu anayeshukiwa kuwa jasusi wa China.

    Hata hivyo, mwenyekiti wa bodi ya Nvidia, Harvey Jones, amesema katika mazungumzo na wachambuzi wa masuala ya fedha siku ya Jumanne kuwa: "Bodi haina nia ya kumrejesha katika nafasi hiyo."

    Faida ya kampuni hiyo pia imeongezeka mara mbili ikilinganishwa na mwaka uliopita. Katika robo ya mwaka iliyoishia Oktoba 25, faida ilifikia dola bilioni 65.

    Mapato ya Nvidia kutoka katika biashara ya vituo vya kuhifadhi na kuchakata data (data centres), ambayo ni sehemu muhimu ya shughuli zake, pia yaliongezeka mara mbili na kufikia dola bilioni 107 katika kipindi hicho.

    Kampuni hiyo imesema ukuaji wake wa haraka unatarajiwa kuendelea, huku mapato yakitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 13 katika robo inayofuata.

    Unaweza pia kusoma:

  2. Rubio asema Marekani haikabiliwi na mashambulizi ya kimfumo

    .

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amekanusha madai na hofu zilizoenea mitandaoni kuwa mfululizo wa hitilafu za mifumo ya teknolojia zilizotokea katika wiki iliyopita zina uhusiano, akisema hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa matukio hayo yanahusiana.

    Rubio amekiri kuwa watu wana hofu kutokana na mfululizo wa hitilafu hizo, zilizojumuisha kusimamishwa kwa safari zote za ndege nchini Marekani na kuvurugika kwa huduma za benki pamoja na mifumo ya kampuni za Apple na Microsoft.

    Hata hivyo, amewaambia waandishi wa habari kuwa: "Marekani haikabiliwi na mashambulizi ya kimfumo. Matukio haya hayahusiani kwa namna yoyote, kila moja lina chanzo chake."

    Wataalamu wa usalama wa kimtandao wamesema hakuna ushahidi unaounganisha hitilafu hizo, huku matatizo mengi yakionekana kusababishwa na masasisho ya mifumo ya zamani ya teknolojia.

    Katika wiki iliyopita, kumekuwa na hitilafu kubwa katika mifumo ya Microsoft, tatizo la kiufundi lililosababisha safari zote za ndege nchini Marekani kusimamishwa kwa saa kadhaa, pamoja na matatizo katika mifumo ya Shirika la Ujasusi la Marekani (NSA), benki kadhaa na kampuni ya Apple.

    Kila kampuni na taasisi iliyoathirika imesema kuwa tukio lililoikumba halikuhusiana na shambulizi la kimtandao.

    Kauli ya Rubio imekuja saa chache baada ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa wa Marekani, Jay Clayton, pia kuzungumzia suala hilo katika mahojiano na kituo cha Fox News, akisema hitilafu hizo hazikusababishwa na mashambulizi ya kimtandao.

    Alieleza kuwa taasisi nyingi zinafanya marekebisho na kuboresha mifumo yao, jambo ambalo limesababisha baadhi ya huduma kuvurugika.

    Rubio aliulizwa iwapo utawala wa Rais Donald Trump una wasiwasi kuwa hofu ya umma inaweza kusababisha watu kuhifadhi bidhaa kwa wingi au kukimbilia kutoa fedha zao benki kwa kuhofia usalama wa fedha zao.

    Akikiri kuwepo kwa hofu hizo, Rubio amesema njia bora ya kukabiliana nazo ni serikali ya Marekani kuwaeleza wananchi kile inachokifahamu kuhusu matukio hayo.

    "Viashiria vyote tulivyonavyo vinaonyesha kuwa kila moja ya matukio haya lina maelezo au chanzo chake ambacho hakihusiani na wahalifu wa kimtandao, mtu mwenye nia ya uhasama au nchi nyingine," amesema.

    Hitilafu za mifumo ya teknolojia zimekuwa zikiripotiwa kila siku tangu Alhamisi, wakati hitilafu ya Microsoft ilipovuruga huduma zake mbalimbali, ikiwemo barua pepe.

    Unaweza pia kusoma:

  3. Mapigano mashariki mwa DRC yalazimisha wagonjwa kuhamishwa kutoka hospitali ya Bunyakiri – MSF

    .

    Mapigano katika eneo la Bunyakiri, wilayani Kalehe, mkoani Kivu Kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), yamevuruga huduma za afya na kuwalazimisha raia kukimbia makazi yao, kwa mujibu wa shirika la kutoa misaada ya kitabibu la Médecins Sans Frontières (MSF).

    Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, MSF imesema mapigano kati ya kundi la waasi la FRN, ambalo awali lilijulikana kama AFC/M23, na majeshi ya serikali (FARDC) yameongezeka tangu Novemba 6.

    MSF imesema hali ilizidi kuwa mbaya Ijumaa kufuatia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani karibu na Bulambika, eneo lililo karibu na hospitali kuu ya Bunyakiri. Hospitali hiyo huhudumia wagonjwa kutoka maeneo mengi ya vijijini ambako upatikanaji wa huduma za afya za kawaida ni mdogo.

    Wafanyakazi wa hospitali hiyo wamehamisha huduma za matibabu pamoja na wagonjwa 76 kwenda katika kituo cha afya cha Maibano kilicho karibu. Hata hivyo, sehemu kubwa ya dawa, vifaa tiba na mahitaji mengine ya hospitali yamebaki katika jengo hilo.

    MSF imesema hatua hiyo ya kuhamisha wagonjwa na huduma za afya inaweza kuwaathiri maelfu ya watu ambao hutegemea hospitali hiyo kupata matibabu.

    Shirika hilo pia limesema baadhi ya wafanyakazi wake wamelazimika kuyahama makazi yao na linaendelea na juhudi za kuwatafuta wafanyakazi wengine ambao halijafanikiwa kuwasiliana nao.

    MSF imepunguza shughuli zake katika eneo hilo, huku baadhi ya wafanyakazi wake wakihamishiwa Bitale na Bukavu, maeneo ambayo tayari yamekumbwa na milipuko ya magonjwa ya kipindupindu na malaria.

    Shirika hilo limesema mzozo huo kwa ujumla unafanya juhudi za kutoa misaada katika maeneo ya mashariki mwa DRC kuwa ngumu zaidi.

    Mashirika ya Umoja wa Mataifa na serikali ya DRC yanasema mkoa wa Kivu Kusini ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ukosefu wa chakula, huku watu milioni 1.1 wakikabiliwa na njaa kali.

    Vita hivyo pia vimepunguza idadi ya watu wanaoweza kufikia mashamba yao na shughuli nyingine muhimu za kujipatia kipato.

    MSF imeonya kuwa iwapo huduma za afya zitaendelea kukatizwa kwa muda mrefu, maelfu ya watu wanaweza kukosa huduma za matibabu katika eneo ambalo tayari linakabiliwa na kuenea kwa magonjwa, watu kuhama makazi yao na uhaba mkubwa wa chakula.

    Unaweza pia kusoma:

  4. Iran yashambulia Kuwait na Bahrain

    .

    Maafisa wa jeshi la Kuwait wametangaza muda mfupi uliopita kuwa mifumo ya ulinzi wa anga imewashwa, wakisema kuwa mifumo hiyo kwa sasa inazuia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani zinazochukuliwa kuwa za uhasama.

    Kamandi kuu ya jeshi la Kuwait imesema kuwa milio ya milipuko iliyosikika nchini humo imesababishwa na makombora au mashambulizi mengine yaliyonaswa na mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo.

    Wakati huohuo, vyombo vya habari vya Iran, vikirejea vyanzo vya Kiarabu, vimeripoti kuwa milipuko kadhaa imesikika ndani ya Kuwait.

    Katika siku za hivi karibuni, Iran imesema imeshambulia vituo vya rada vya Marekani nchini Bahrain, ikiwa ni kujibu mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya maeneo mbalimbali katika Ghuba ya Uajemi, yakiwemo visiwa vya Qeshm na Sirik.

    Iran pia imetoa onyo kuwa iwapo nchi hiyo itashambuliwa, inaweza kulenga kambi za kijeshi za Marekani katika eneo hilo na hata nje ya eneo hilo.

    Unaweza pia kusoma:

  5. Mtandao wa siri wa Shirika la Ujasusi la Marekani (NSA) wakumbwa na hitilafu ya muda

    .

    Mtandao wa siri wa kiwango cha juu unaotumiwa na Shirika la Ujasusi la Marekani (NSA) kwa mawasiliano ya ndani ulipata hitilafu na kusitisha kufanya kazi kwa muda usiojulikana siku ya Jumanne, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani.

    NSA, ambalo ni shirika kubwa zaidi la ujasusi nchini Marekani, limesema hitilafu hiyo ya muda ilitokea katika utendaji wa baadhi ya mifumo yake wakati wa matengenezo ya kawaida yaliyokuwa yamepangwa. Hata hivyo, limeeleza kuwa huduma muhimu kwa shughuli zake hazikuathirika.

    Taarifa zinasema hitilafu hiyo iliathiri mtandao wa NSANet, ambao maafisa wa shirika hilo hutumia kutuma na kupokea taarifa za siri za kiwango cha juu.

    Kukatika kwa mtandao huo kunajiri wakati kukiwa na mfululizo wa hitilafu za kiufundi zilizoripotiwa nchini Marekani katika siku za hivi karibuni, zilizoathiri mifumo ya mashirika ya ndege, benki na miundombinu mingine.

    Katika matukio yote hayo, mamlaka zimekanusha kuwa hitilafu hizo zilisababishwa na mashambulizi ya kimtandao au sababu za nje.

    Msemaji wa NSA aliiambia BBC kuwa: "Ingawa hitilafu hiyo iliathiri baadhi ya mifumo ya ndani, huduma zetu muhimu kwa utekelezaji wa majukumu ya shirika zinaendelea kufanya kazi kikamilifu, na uwezo wetu wa kulinda usalama wa taifa letu haujaathirika."

    Aliongeza kuwa miundombinu ya kiteknolojia ya shirika hilo imeundwa kuhakikisha shughuli zinaendelea wakati wa matengenezo yaliyopangwa au hitilafu zisizotarajiwa, huku kukiwa na mifumo mbalimbali ya akiba.

    Shirika hilo halikueleza tatizo hilo lilianza lini wala linatarajiwa kutatuliwa lini.

    Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa hitilafu hiyo haikusababishwa na shambulizi la kimtandao. Hata hivyo, kutokea kwa hitilafu hiyo wakati kukiwa na mfululizo wa matatizo yaliyoathiri mifumo ya mashirika ya ndege na benki nchini humo kumeibua maswali.

    Unaweza pia kusoma:

  6. Putin awasili china kabla ya mkutano wa kihistoria na Trump na Xi

    .

    Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amewasili mjini Shenzhen, China, usiku wa kuamkia leo majira ya saa 2:00 asubuhi kwa saa za huko (18:00 GMT), kabla ya mkutano unaosubiriwa kwa hamu kubwa utakaowakutanisha kwa mara ya kwanza viongozi watatu wenye ushawishi mkubwa duniani.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya China, Putin alipokelewa na Cai Qi, mmoja wa viongozi wa juu wa Chama cha Kikomunisti cha China na mkuu wa watumishi wa Rais Xi Jinping.

    Kiongozi huyo wa Urusi pia alipewa mapokezi rasmi yaliyohusisha gwaride la heshima la wanajeshi wa China pamoja na burudani ya ngoma za kitamaduni alipowasili katika uwanja wa ndege wa Shenzhen.

    Ziara ya Putin imefanyika kuelekea mkutano wa kihistoria unaotarajiwa kufanyika Alhamisi pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC), ambapo atakutana kwa mara ya kwanza na Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa China Xi Jinping.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilithibitisha Jumatatu kufanyika kwa mkutano huo, kufuatia matangazo yaliyotolewa pia na Ikulu ya White House pamoja na Kremlin.

    Mkutano huo utakuwa wa kwanza kuwahi kuwakutanisha Trump, Xi na Putin katika meza moja ya mazungumzo, hatua inayotajwa kuwa ya kihistoria kutokana na ushawishi wa viongozi hao katika masuala ya siasa, usalama na uchumi wa dunia.

    Kwa mujibu wa gazeti la The Wall Street Journal, Putin alipendekeza mazungumzo hayo kama sehemu ya juhudi za kutafuta suluhu ya vita vya Urusi nchini Ukraine.

    Trump, ambaye mwezi Oktoba alieleza kuunga mkono mazungumzo ya pande tatu kuhusu kupunguza silaha za nyuklia, hivi karibuni aliwaambia waandishi wa habari kuwa viongozi hao watakuwa wakijadili masuala mbalimbali ya kimataifa.

    Hata hivyo, China haijatoa maelezo zaidi kuhusu ajenda rasmi ya mkutano huo, ambao tayari umevutia hisia za jumuiya ya kimataifa kutokana na matarajio ya maamuzi na majadiliano yatakayoweza kuathiri mwelekeo wa siasa za dunia.

    Unaweza pia kusoma:

  7. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 18/11/2026.