Sababu 5 zilizomfanya Trump na chama cha Republican kushindwa vibaya

.
    • Author, Jake Lapham
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Chama cha Democratic kimepata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, na kufanikiwa kuchukua udhibiti wa Bunge la Congress.

Kwa kawaida, chama cha rais aliyeko madarakani huwa katika wakati mgumu kwenye uchaguzi wa aina hii. Hata hivyo, ukubwa wa 'kichapo' cha chama cha Republican safari hii unatazamwa kama ishara ya kutoridhishwa kwa Wamarekani na uongozi wa Donald Trump katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Kuanzia kupanda kwa gharama za maisha hadi kutopendwa kwa rais, zipo sababu kadhaa zilizopelekea chama hicho kupoteza viti vingi. Hizi hapa tano kuu.

1. Gharama za maisha mzigo kwa Wamarekani

.

Kupanda kwa bei za bidhaa na huduma muhimu kumekuwa miongoni mwa mambo yanayowasumbua Wamarekani katika maeneo mbalimbali ya nchi. Hasira za wananchi kuhusu hali hiyo zilionekana wazi katika majimbo ambako ushindani wa uchaguzi ulikuwa mkubwa.

"Bei ya mafuta, vyakula, kila kitu kinapanda," alisema mpiga kura mmoja katika jimbo la North Carolina alipozungumza na BBC kabla ya uchaguzi. Alisema hali hiyo imemfanya abadili msimamo wake na kuamua kuipigia kura Democratic badala ya Republican.

Katika mwaka ulioishia Septemba, bei ziliongezeka kwa asilimia 3.7, huku gharama za mafuta na nishati zikichangia kupanda huko.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa mwanzoni mwa Oktoba, bei ya wastani ya rejareja ya dizeli nchini Marekani ilikuwa karibu kufikia rekodi ya dola 6.52 kwa galoni, iliyowahi kurekodiwa Septemba.

Athari za mfumuko wa bei zimekuwa kubwa kwa familia nyingi. Utafiti wa wapiga kura unaonyesha kuwa karibu watu wanane kati ya 10, sawa na asilimia 79, walisema kupanda kwa bei kumeisababishia familia yao changamoto kubwa katika mwaka uliopita.

Zaidi ya asilimia 60 ya waliohojiwa walimtupia lawama Trump, wakiamini kuwa sera zake ndizo zilizosababisha bei kuwa juu kuliko kawaida.

2. Vita vya Iran

.
Maelezo ya picha, a
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Februari vimekuwa miongoni mwa sababu zilizochangia kupanda kwa gharama za maisha.

Baada ya mashambulizi hayo, Iran ilichukua hatua ya kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz, hatua iliyovuruga usafirishaji wa mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) kupitia njia hiyo muhimu duniani.

Matokeo yake yalionekana haraka kwenye bei za mafuta. Mbali na athari za kiuchumi, vita hivyo pia havikupata uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa Wamarekani. Hata baadhi ya wafuasi wa vuguvugu la MAGA waliviona kama usaliti wa ahadi ya Trump ya sera ya "America First" (Marekani Kwanza), ambayo ilijumuisha kutoiingiza nchi katika vita vingine.

Katika utafiti wa wapiga kura, asilimia 63 walisema Marekani ilifanya uamuzi usio sahihi kuanzisha operesheni za kijeshi dhidi ya Iran.

Wengine, sawa na asilimia 74, walisema vita hivyo vilikuwa na mchango mkubwa au wa msingi katika uamuzi wao wa kumpigia kura mgombea wa Congress.

Siku iliyofuata baada ya uchaguzi, Trump alikiri kuwa vita vya Iran vilichangia kushindwa kwa chama chake. Hata hivyo, katika mahojiano na kituo cha Fox News, alitetea uamuzi wake wa kuingilia kati, akisema hakuwa na njia nyingine ya kuzuia Iran kumiliki silaha ya nyuklia.

3. Democrats walikuwa na ujumbe ulioeleweka kwa wapiga kura

Abdul El-Sayed stands at a podium with a finger up and in front of a lectern that has a sign reading: "Thank you Michigan"
Maelezo ya picha, Abdul El-Sayed akizungumza na wafuasi wake baada ya ushindi

Ushindi wa Democrats katika maeneo mbalimbali ya Marekani haukutokana na wimbi la mabadiliko pekee. Wagombea wake, wakiwemo waliokuwa wakigombea katika maeneo ambayo kwa kawaida huungwa mkono na Republican, waliweza kuwafikia wapiga kura kwa ujumbe uliowagusa.

Badala ya kusambaza hoja zao katika masuala mengi, walijikita zaidi katika changamoto za gharama za maisha na upatikanaji wa huduma za afya.

Aliyekuwa mwalimu James Talarico na mchungaji Adam Hamilton, kwa mfano, walizungumzia imani yao ya kidini kwa namna iliyowavutia wapiga kura katika majimbo ya Texas na Kansas.

Huko South Carolina, Annie Andrews, daktari wa zamani wa watoto, alipata ushindi ambao wengi hawakutarajia. Ujumbe wake kuhusu umuhimu wa kufanya huduma za afya ziwe nafuu ulionekana kuwagusa wananchi wanaoamini kuwa mfumo wa afya nchini humo una matatizo.

Naye Abdul El-Sayed, aliyewahi kufanya kazi katika sekta ya afya ya umma, alishinda Michigan na kukiwezesha chama chake kuendelea kushikilia kiti hicho. Katika kampeni yake alisisitiza umuhimu wa kuondoa ushawishi wa fedha katika siasa na kuhakikisha wananchi wanabaki na fedha zaidi mifukoni mwao.

Katika jimbo la Georgia, Seneta Jon Ossoff alifanikiwa kuchaguliwa tena kwa kutumia gharama za maisha na ufisadi kama ajenda kuu ya kampeni yake. Ushindi wake wa wazi katika jimbo ambalo Trump alishinda mara mbili unaweza kuongeza uvumi kwamba anajiandaa kuwania urais mwaka 2028.

Hata Trump mwenyewe alionekana kukiri uimara wa kampeni za wapinzani wake. Katika mahojiano na Fox News, aliwasifu Democrats akisema "walifanya kazi nzuri".

Kwa upande wa Republican, baadhi ya wagombea, akiwemo Ken Paxton wa Texas, walikosolewa kwa kushindwa kuendesha kampeni zilizozingatia ipasavyo mambo yaliyokuwa yakisumbua wananchi.

4. Mvuto wa mashaka wa Trump ndani ya chama chake

Masuala mawili yaliyowakera zaidi wapiga kura ni kupanda kwa bei na vita vya Iran yalihusishwa moja kwa moja na maamuzi ya Trump.

Hali hiyo ilizidi kuwa changamoto kwa Republican baada ya kiwango cha kumuunga mkono rais kupungua hata miongoni mwa baadhi ya wapiga kura wa chama chake.

Matokeo yake, majimbo yaliyomuunga mkono Trump katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2024 yalikuwa katika hatari ya kukigeuka chama hicho.

Katika jitihada za kuwahamasisha wafuasi wake, Trump aliwataka wapiga kura wafikirie kana kwamba yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa akiwania nafasi katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, baada ya kuwa mhimili mkuu wa siasa za Marekani kwa zaidi ya muongo mmoja, matokeo haya yanaibua maswali kuhusu kama mvuto wake kwa wapiga kura unaanza kupungua.

Kumweka Trump katikati ya kampeni ya Republican kulionekana kuwa mkakati wenye hatari, hasa wakati hasira za wananchi kuhusu hali ya maisha zilipokuwa zikiongezeka.

Tafiti za maoni zilizofanyika katika miezi ya kabla ya uchaguzi zilionyesha kuwa Wamarekani wengi walitaka rais ajikite zaidi katika kutatua changamoto ya kupanda kwa gharama za maisha.

Hata katika hotuba yake ya mwisho ya kampeni Jumatatu mjini Washington DC, Trump alitumia muda mwingi kuzungumzia mradi wake wenye utata wa ukarabati wa bwawa la Reflecting Pool badala ya maisha ya watpiga kura.

5. Msimamo wa wapiga kura wenye asili ya Hispania na Wamarekani weusi

.

Katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2024, Trump alipata ongezeko la uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya wapiga kura wenye asili ya Hispania na Wamarekani weusi. Mabadiliko hayo yalichangia ushindi wake mkubwa.

Lakini matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula yanaonyesha kuwa sehemu ya wapiga kura hao wameanza kurejea upande wa Democrats.

Katika jimbo la Texas, Democrats walishinda viti vyote vitatu vya Baraza la Wawakilishi katika majimbo ya uchaguzi yaliyopo kwenye maeneo ya mpakani na Mexico, ambako wakazi wengi wana asili ya Hispania.

Uchambuzi wa gazeti la New York Times unaonyesha kuwa kaunti zenye wakazi wengi wenye asili ya Hispania zilihama kwa zaidi ya asilimia 22 kuelekea kwa wagombea wa Democratic katika uchaguzi wa Seneti, ikilinganishwa na uchaguzi wa urais wa 2024.

Kwa mujibu wa mchambuzi wa takwimu za habari Jeff Adelson, mabadiliko hayo yalikuwa makubwa kuliko yaliyorekodiwa katika kundi jingine lolote kubwa la kijamii nchini Marekani.

Miongoni mwa mambo yanayoweza kueleza mabadiliko hayo ni kuongezeka kwa hasira kuhusu namna sheria za uhamiaji zinavyotekelezwa. Utafiti wa Kituo cha Utafiti cha Pew unaonyesha kuwa asilimia 56 ya Wamarekani wana mtazamo hasi kuhusu ICE, taasisi inayosimamia utekelezaji wa sheria za uhamiaji na forodha.

Mabadiliko kama hayo pia yalionekana katika maeneo yenye wakazi wengi weusi, ambako uungwaji mkono kwa wagombea wa Democratic katika uchaguzi wa Seneti uliongezeka kwa kiwango kikubwa.

Huko Mississippi, ambako takriban asilimia 37 ya wapiga kura ni Wamarekani weusi, sehemu kubwa zaidi ikilinganishwa na majimbo mengine, ushindani wa kiti cha Seneti ulikuwa mkali.

Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu na kuhaririwa na Ambia Hirsi