Moja kwa moja , Matokeo ya uchaguzi Marekani: Democrat washinda udhibiti wa Seneti na Bunge la Wawakilishi

Chama cha Democratic kimefanikiwa kupata udhibiti wa Seneti na Bunge la Wawakilishi la Marekani, hatua inayokipa mamlaka ya kuongoza Bunge la Congress kwa kipindi kilichosalia cha urais wa Donald Trump.

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Trump akiri vita ya Iran imechangia matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula

    n

    Rais wa Marekani Donald Trump amekiri kuwa vita dhidi ya Iran imechangia matokeo mabaya ya chama chake cha Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula.

    Akizungumza na kituo cha televisheni cha Fox News, Trump alizungumzia taarifa kwamba Marekani inapanga kushambulia baadhi ya maeneo nchini Iran.

    Amesema Marekani inapaswa kuchukua hatua kubwa, akiongeza kuwa huenda hatua hiyo ikahusisha shambulizi kali.

    Trump pia amesisitiza kuwa Iran haitaruhusiwa kamwe kumiliki silaha za nyuklia.

    Aidha, amekiri kuwa kupanda kwa bei ya mafuta pia kuliathiri chama cha Republican katika uchaguzi huo, akisema wapiga kura hawakufurahishwa na kulazimika kulipa zaidi kwa ajili ya mafuta ya magari.

    Trump amehitimisha maoni yake kuhusu matokeo ya uchaguzi katika mahojiano na Fox News kwa kusema haoni matokeo hayo kama pigo kwa urais wake, licha ya chama chake cha Republican kutarajiwa kupoteza udhibiti wa pande zote mbili za Congress.

    Amesema chama cha Democrat kimekuwa kikilenga kupata ushindi huo mkubwa kwa miaka mingi na hatimaye kimefanikiwa. Hata hivyo, amewapongeza kwa kile alichokiita kazi nzuri.

    Katika mahojiano hayo, Trump pia ametumia nafasi hiyo kueleza mafanikio ya utawala wake katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, akitaja ukuaji wa uchumi na usalama katika mpaka wa kusini mwa Marekani kuwa miongoni mwa mafanikio makuu.

  2. Trump alaumu wanachama wa Republican na Fox News kwa kushindwa uchaguzi wa muhula

    b

    Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea kutoa maoni yake kuhusu matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula kupitia mtandao wake wa Truth Social, akiwalaumu baadhi ya wanachama wa chama chake na kituo cha televisheni cha Fox News kwa kushindwa kwa wagombea wa Republican.

    Trump amesema ataanza kutoa uchambuzi wa kisiasa, akieleza sababu zilizowafanya baadhi ya wagombea kushinda au kushindwa.

    Akimtaja Gavana wa Texas, Greg Abbott, Trump amesema asingeshindwa kama asingekuwa kile alichokiita RINO katika miezi sita iliyopita ya maisha yake ya kisiasa.

    RINO ni kifupisho cha maneno ya Kiingereza yanayotumiwa na baadhi ya Republican kuwakosoa wanachama wanaowaona kuwa hawafuati misimamo ya chama, licha ya kujiita Republican.

    Trump pia amechapisha picha ya kofia nyekundu yenye neno "Veto", ishara inayoonekana kurejelea uwezo wake wa kupinga miswada itakayopitishwa na Congress itakayokuwa chini ya udhibiti wa chama cha Democrat.

    Aidha, amekikosoa kituo cha Fox News kwa kumwalika aliyekuwa meya wa New York, Bill de Blasio, ambaye ni mwanachama wa Democrat, katika jopo lake la wachambuzi wa kisiasa.

    Amedai Fox News inachangia kushindwa kwa Republican kwa kuwapa nafasi mara kwa mara wawakilishi wa chama pinzani kueleza misimamo yao.

    Mapema usiku huo, Trump alikuwa ameandika kuwa chama chake kingeshinda kwa kishindo kama yeye angekuwa mmoja wa wagombea katika uchaguzi huo.

  3. Tetesi za Soka Jumatano: Man Utd wamfukuzia beki wa Man City Ait-Nouri

    b

    Manchester United wanafikiria kufanya usajili wa kushtukiza wa beki wa kushoto wa Manchester City, Rayan Ait-Nouri, mwenye umri wa miaka 25. Masharti binafsi ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Algeria hayatarajiwi kuwa kikwazo katika kukamilisha usajili huo. (Florian Plettenberg)

    Kocha msaidizi wa timu ya taifa ya England, Anthony Barry, ameibuka kuwa mmoja wa wanaowania nafasi ya kuinoa Crystal Palace iwapo klabu hiyo itaamua kumfuta kazi kocha wake Mfaransa, Pierre Sage.(Mirror)

    Mkurugenzi wa michezo wa Barcelona, Deco, amemuweka beki wa kati wa Arsenal na timu ya taifa ya Ecuador, Piero Hincapie, mwenye umri wa miaka 24, kwenye orodha ya wachezaji anaowafuatilia kwa ajili ya kuimarisha safu ya ulinzi.(Sport - in Spanish)

    Bayern Munich wanaendelea kumfuatilia nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard, huku kukiwa na sintofahamu kuhusu mkataba mpya wa kiungo huyo wa Norway mwenye umri wa miaka 27.(Caughtoffside)

    Kiungo wa Arsenal na timu ya taifa ya Hispania, Martin Zubimendi, mwenye umri wa miaka 27, yuko tayari kutafakari uwezekano wa kuondoka klabuni hapo katika dirisha la usajili la Januari.(Team Talk)

    Klabu ya Al-Hilal ya Saudi Arabia haitampa kiungo wa Manchester United na timu ya taifa ya Ureno, Bruno Fernandes, mwenye umri wa miaka 32, nafasi ya kuondoka Old Trafford. Hii ni licha ya klabu hiyo ya Saudi Pro League kuwa karibu kumsajili mwanzoni mwa msimu.(Talksport)

    Tottenham Hotspur haitaruhusu kuondoka kwa kiungo wake wa Sweden, Lucas Bergvall, mwenye umri wa miaka 20, licha ya kuvutia nia ya Barcelona na Napoli.(Football Insider)

    Kocha wa Aston Villa, Unai Emery, yumo kwenye orodha ya makocha watano wanaozingatiwa na Manchester United kuchukua nafasi ya Michael Carrick. Hata hivyo, ripoti zinaeleza kuwa mfumo wa sasa wa uongozi wa masuala ya michezo ndani ya klabu hiyo huenda usimvutie kocha huyo raia wa Hispania.(Daily Mail - subscription required)

    Mshambuliaji wa Minnesota United, Kelvin Yeboah, mwenye umri wa miaka 26 na mpwa wa nyota wa zamani wa Leeds United na Ghana, Tony Yeboah, anafuatiliwa na klabu kadhaa za Ligi Kuu England. Everton, Crystal Palace na Sunderland zote zinatajwa kuwa kwenye soko la kutafuta mshambuliaji.(Talksport)

    Wachezaji wa Newcastle United wanaamini kuwa maamuzi ya hatari yaliyofanywa na klabu hiyo katika usajili wa wachezaji wakati wa dirisha la majira ya kiangazi ndiyo sababu kuu ya timu hiyo kufanya vibaya msimu huu.(Telegraph - subscription required)

    Soma pia:

  4. Matokeo ya uchaguzi Marekani: Democrat washinda udhibiti wa Seneti na Bunge la Wawakilishi

    d

    Chama cha Democrat kimefanikiwa kupata udhibiti wa Seneti na Bunge la Wawakilishi la Marekani, hatua inayokipa mamlaka ya kuongoza Bunge la Congress kwa kipindi kilichosalia cha urais wa Donald Trump.

    Chama hicho kimepata ushindi kadhaa uliotarajiwa kwa kiwango kidogo katika maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa ngome za Republican, yakiwemo majimbo ya Texas, Kansas na Ohio.

    Kwa mujibu wa makadirio ya kituo cha televisheni cha CBS, Democrat wanatarajiwa kudhibiti Seneti baada ya kuiondoa mikononi mwa Republican.

    Hii inafuatia makadirio ya awali yaliyoonyesha kuwa chama hicho kingeshinda pia udhibiti wa Baraza la Wawakilishi.

    Katika Bunge la Wawakilishi, Democrat wanatarajiwa kupata angalau viti 229, huku Republican wakitarajiwa kupata angalau viti 161.

    Baadhi ya matokeo yaliyotangazwa ni pamoja na:

    • Adam Hamilton wa Democrat anatarajiwa kushinda kiti cha Seneti katika jimbo la Kansas.

    • Bill Hegarty wa Republican amehifadhi kiti chake cha Seneti katika jimbo la Tennessee, kama ilivyokuwa kwa Tom Cotton katika jimbo la Arkansas.

    • Deb Haaland amechaguliwa kuwa gavana mpya wa New Mexico.

    • Sarah Huckabee Sanders wa Republican amechaguliwa tena kuwa gavana wa Arkansas.

    • Democrat wameongeza viti viwili vipya katika Bunge la Wawakilishi katika jimbo la Pennsylvania, kupitia ushindi wa Paige Cognetti katika wilaya ya nane na Janelle Stelson katika wilaya ya kumi.

    • Vincente Gonzales wa Democrat amehifadhi kiti chake katika wilaya ya 34 ya Texas.

    • Greg Landsman wa Democrat pia amehifadhi kiti chake katika wilaya ya kwanza ya Ohio.

  5. Mkuu wa MONUSCO akutana na Kabila huku juhudi za amani DRC zikiendelea

    n

    Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), James Swan, amekutana na rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila, mjini Goma. Huo ni mkutano wao wa kwanza kuripotiwa hadharani tangu Kabila achukue uongozi wa vuguvugu la Front for the Refoundation of the Nation (FRN).

    Kwa mujibu wa MONUSCO, mazungumzo hayo yalijikita katika juhudi zinazoendelea za kurejesha amani, kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano na kutafuta suluhu ya amani kwa mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC.

    MONUSCO imesema Swan pia alikutana na wawakilishi wa utaratibu wa ufuatiliaji na uhakiki wa utekelezaji wa usitishaji mapigano, unaojulikana kama MCVE+, na kuthibitisha tena uungaji mkono wa ujumbe huo kwa mchakato huo kwa mujibu wa mamlaka yake.

    Akizungumza na vyombo vya habari vya ndani baada ya mkutano huo, makamu wa rais wa FRN, Bertrand Bisimwa, amesema vuguvugu hilo linaendelea kuunga mkono mchakato wa amani wa Doha. Hata hivyo, ameeleza wasiwasi kuhusu utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo.

    Bisimwa pia amehoji mipango ya kuongeza muda wa mamlaka ya MONUSCO, akisema kundi lake linaunga mkono kuendelea kwa mpango wa ujumbe huo kujiondoa nchini hatua kwa hatua. Hata hivyo, amesema linaunga mkono kuendelea kwa jukumu lake la kuhakiki utekelezaji wa usitishaji mapigano.

    Aidha, amedai kuwa mapendekezo ya kufanya mabadiliko ya katiba yanaweza kuathiri makubaliano yaliyofikiwa kupitia mchakato wa Doha.

    Serikali ya Congo haikuwa imetoa majibu ya haraka kuhusu kauli hizo.

    Mkutano huo wa Jumanne unafanyika wakati wapatanishi wa kikanda na wa kimataifa wakiendelea na juhudi za kudumisha usitishaji mapigano na kuendeleza mazungumzo ya amani yanayolenga kumaliza miaka kadhaa ya mzozo mashariki mwa DRC.

    Unaweza pia kusoma:

  6. 'Sikuwa mgombea'- Trump ajitenga na chama chake cha Republican

    c

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ametoa kauli yake ya kwanza baada ya chama chake cha Republican kupata matokeo mabaya katika uchaguzi wa katikati ya muhula.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema: “Sikuwa mgombea katika uchaguzi huu. Kama ningekuwa mgombea, tungeshinda kwa kishindo!”

    Kwa mujibu wa wachanganuzi wa siasa za Marekani, kauli hiyo huenda isipokelewe vizuri na wanachama wa Republican kote nchini.

    Mchambuzi wa siasa Daniel Bush amesema kwa kauli hiyo, Trump anaonekana kujitenga na chama chake na kuelekeza lawama za matokeo mabaya kwa wagombea wa Republican.

    Bush ameongeza kuwa kauli hiyo haitasaidia kupunguza mgawanyiko ndani ya chama hicho, wakati wanachama wake wakianza kukabiliana na matokeo ya kupoteza udhibiti wa Baraza la Wawakilishi na uwezekano wa kupoteza pia Seneti.

    .

    Soma zaidi:

  7. Matokeo ya uchaguzi Marekani: Democrat washinda udhibiti wa Bunge la Wawakilishi, macho yaelekezwa Seneti

    d

    Chama cha Democrat kinaendelea kupata viti zaidi katika Bunge la Wawakilishi la Marekani, ambako chama kinahitaji viti 218 kati ya 435 ili kuwa na wingi wa wabunge.

    Bunge la Wawakilishi ni chombo cha chini cha Bunge la Congress. Wajumbe wake huchaguliwa kwa vipindi vya miaka miwili. Kwa kawaida, miswada ya sheria huwasilishwa na kujadiliwa katika baraza hilo kabla ya kupelekwa kwenye Seneti.

    Katika saa moja iliyopita, Democrats wanaonekana kupata viti vingine viwili kutoka kwa wapinzani wao wa Republican.

    Zach Dembo wa Kentucky na Rebecca Bennett wa New Jersey wanatarajiwa kushinda viti hivyo kwa tiketi ya chama cha Democrat.

    Katika Bunge la Wawakilishi, Democrats wanapigiwa upatu kushinda viti 218 na Republicans wanatarajiwa kushinda viti 160.

    .
  8. Wamarekani wakipiga kura, Trump asema Marekani itasitisha msaada kwa Israel

    d

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Jumanne kuwa amefikia makubaliano na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ya kusitisha ufadhili wa kila mwaka wa dola bilioni 4 kwa Israel kuanzia mwakani, ingawa Washington itaendelea kuiuzia silaha mshirika wake huyo wa karibu katika Mashariki ya Kati.

    Tangazo hilo la kushtukiza limetolewa wakati Wamarekani wakipiga kura katika uchaguzi wa katikati ya muhula, ambao utaamua iwapo chama cha Republican cha Trump kitapoteza udhibiti wa Bunge la Congress.

    Trump amesema hatua hiyo inalenga kwa kiasi fulani kuwaondolea wapinzani wa Republican hoja wanayoitumia kuikosoa serikali kuhusu uungaji mkono wa kijeshi kwa Israel. Amevituhumu vikundi vya mrengo wa kushoto ndani ya chama cha Democrat kwa kutumia suala hilo kuikosoa Republican.

    Hata hivyo, Trump hakutoa maelezo zaidi kuhusu namna msaada huo utakavyositishwa mwishoni mwa mwaka huu. Hii ni licha ya makubaliano ya maelewano yanayoipa Israel msaada wa kijeshi wa dola bilioni 3.8 kila mwaka kutoka Marekani kutarajiwa kumalizika Septemba 2028.

    Kauli yake inaonekana kuashiria kuwa msaada wa Marekani kwa Israel, ambao kwa miongo kadhaa ulikuwa suala lililoungwa mkono na vyama vyote vikuu vya kisiasa, sasa umeanza kuwa mzigo wa kisiasa kwa Trump miongoni mwa baadhi ya wapiga kura.

    Wachambuzi wamependekeza kuwa tangazo hilo lilitolewa kwa wakati maalumu, likiwa sehemu ya mkakati wa kisiasa siku ya uchaguzi.

    Mazungumzo kuhusu mustakabali wa msaada wa Marekani kwa Israel baada ya mwaka 2028 yamekuwa yakiendelea. Netanyahu tayari alikuwa amesema anatarajia msaada huo kupunguzwa hatua kwa hatua kadiri muda unavyosonga.

    Hata hivyo, kauli ya Trump imeashiria kuwa tayari amefanya uamuzi kuhusu mabadiliko makubwa yanayoweza kutokea katika uhusiano wa Marekani na Israel. Hii ni licha ya nchi hizo mbili kuendelea kukabiliana na Iran, zaidi ya miezi minane baada ya kufanya mashambulizi ya pamoja dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

    Akizungumza katika kipindi cha Fox & Friends cha televisheni ya Fox News, Trump alisema Israel haihitaji tena fedha hizo. Alidai kuwa baadhi ya wanasiasa wa mrengo wa kushoto ndani ya chama cha Democrat wanatumia msaada wa kifedha wa Marekani kwa Israel kuikosoa Republican.

    Kura za maoni zinaonyesha kuwa uungwaji mkono wa jumla wa Wamarekani kwa Israel umepungua, hasa kutokana na vita vya Gaza.

    Trump alisema: “Kuhusu kuifadhili Israel, mimi na Bibi Netanyahu tumefikia makubaliano. Tunaipa Israel dola bilioni 4 kila mwaka, lakini tulikubaliana miezi kadhaa iliyopita kusitisha msaada huo. Tayari tumekubaliana kuwa kufikia mwisho wa mwaka huu hatutaendelea kuilipa Israel.”

    Aliongeza: “Hata hivyo, tutaendelea kuisaidia Israel iwapo itahitaji msaada wetu.”

    Mustakabali wa uongozi wa Israel bado haujulikani baada ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 27, ambapo Netanyahu, ambaye amekuwa na uhusiano wa karibu na chama cha Republican nchini Marekani, alipoteza wingi wa viti vya kumuunga mkono katika serikali yake. Hata hivyo, wapinzani wake hawakupata nafasi ya wazi ya kumwondoa madarakani.

    Matokeo hayo yanatarajiwa kufungua kipindi cha mazungumzo marefu kuhusu kuunda serikali mpya.

    Ofisi ya Rais wa Marekani na ofisi ya Netanyahu hazikujibu maombi ya BBC ya kutoa maoni kuhusu suala hilo.

    Soma Pia:

  9. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 04/11/2026.