'Mwajiri wangu alinielekezea bunduki kichwani'

.
Maelezo ya picha, Stephanie alifanikiwa kutoroka baada ya kudaiwa kupigwa vibaya na mwajiri wake alipokuwa akifanya kazi za ndani nchini Iraq.
    • Author, Na Komla Adom
    • Nafasi, Mwandishi Mwandamizi, BBC Pidgin
    • Akiripoti kutoka, Ghana
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mwanamke kijana kutoka Ghana ambaye video yake ya kunyanyaswa na mwajiri wake nchini Iraq ilisambaa kwa kasi mitandaoni, ameeleza kwa kina mateso aliyopitia akiwa mfanyakazi wa ndani katika taifa hilo la Mashariki ya Kati.

Stephanie Nkrumah aliondoka Ghana akiwa na matumaini ya kupata maisha bora. Kupitia wakala wa ajira, aliahidiwa kazi nzuri ambayo ingemwezesha kujikimu na kusaidia familia yake. Hata hivyo, ndoto yake iligeuka kuwa jinamizi mara tu alipowasili Iraq.

Anasema alipelekwa kufanya kazi za ndani katika mazingira magumu, akilazimishwa kufanya kazi kwa saa nyingi bila mapumziko na chini ya vitisho na manyanyaso ya mara kwa mara.

"Nilikimbia kwa sababu nilihofia maisha yangu. Nilihisi kama ningebaki kule, ningekufa," alisema Stephanie.

Ahadi zilipogeuka mateso

.

Kabla ya kusafiri, Stephanie aliahidiwa kuwa angefanya kazi kwa saa nane kwa siku na kupata muda wa kupumzika. Pia aliambiwa kuwa sehemu ya mshahara wake ingetumika kulipa gharama za wakala aliyemtafutia kazi.

Lakini hali halisi ilikuwa tofauti kabisa.

Alisema alikuwa akifanya kazi kuanzia alfajiri hadi usiku wa manane bila muda wa kupumzika. Katika baadhi ya nyakati alihamishwa kutoka nyumba moja kwenda nyingine na kulazimishwa kuhudumia familia tofauti bila malipo ya ziada.

"Sikuwahi kufanya kazi kwa saa nane nilizoahidiwa. Kazi iliendelea hadi kila mtu ndani ya nyumba alipolala. Hakukuwa na muda wa kupumzika."

Stephanie alisema katika wiki zake za kwanza Iraq alifanya kazi katika nyumba mbili tofauti bila kulipwa mshahara wowote.

Kipigo kilichomnusuru na dunia kufahamu mateso yake

.

Kisa chake kilivuta hisia za watu wengi baada ya video kuonekana ikimuonyesha akishambuliwa na mwanaume aliyedaiwa kuwa msimamizi wa shirika la ajira lililompeleka kufanya kazi.

Katika video hiyo, mwanaume huyo anaonekana akimpiga makofi mara kadhaa, akimvuta kwa nguvu kutoka kwenye kiti, kumsukuma ukutani na kumshambulia mbele ya kamera.

Stephanie anasema tukio hilo lilitokea baada ya kuomba apelekwe hospitalini kwa sababu alikuwa mgonjwa.

"Nilimweleza mwajiri wangu kuwa nilikuwa najisikia vibaya na nilihitaji matibabu. Baadaye walizungumza wao kwa wao kwa lugha yao, kisha nikapelekwa kwenye chumba cha shirika la ajira."

Alisema mara baada ya kuingia humo alianza kupigwa.

"Aliniuliza kwa nini nilisema ninaumwa. Kisha akaanza kunipiga na kuniambia kuwa nililetwa Iraq kufanya kazi, si kuugua."

Kulingana na Stephanie, tukio hilo lilifikia kiwango cha kutisha zaidi pale mwanaume huyo alipotoa bunduki.

"Alinielekezea bunduki kichwani na kuniambia kwamba kama sitafanya kazi angenipiga risasi. Alisema ameninunua kwa fedha alizomlipa wakala wangu, hivyo sikuwa na haki ya kuumwa wala kulalamika."

Baada ya kipigo hicho, anasema alifungiwa ndani ya chumba hadi siku iliyofuata.

Mpango wa kutoroka

.

Kisa hicho kilimfanya aamue kuwa ilikuwa lazima atoroke ili kuokoa maisha yake.

Kwa miezi kadhaa alikuwa akizungumza kwa siri na wazazi wake kuhusu namna ya kurejea nyumbani. Baba yake, ambaye anaishi Canada, alimnunulia tiketi ya ndege na kusaidia kuratibu safari yake ya kutoroka.

Stephanie alisema siku ya safari alihofia mpango huo ungegundulika.

"Mwajiri wangu alisema tunakwenda sehemu fulani. Nilikuwa na hofu kubwa lakini tayari nilikuwa nimewasiliana na dereva wa teksi ambaye alikubali kunichukua na kunipeleka moja kwa moja uwanja wa ndege."

Hatimaye alifanikiwa kuondoka Iraq na kurejea Ghana salama.

Tofauti na wafanyakazi wengi wa ndani wanaonyang'anywa hati zao za kusafiria, Stephanie alibaki na pasipoti yake kwa sababu kazi yake ilimlazimu kusafiri kati ya miji mbalimbali na kupitia vituo vya ukaguzi vinavyohitaji kitambulisho rasmi.

Anasema hilo ndilo lililomsaidia kutekeleza mpango wake wa kutoroka.

Serikali ya Ghana yaingilia kati

.

Baada ya kurejea nyumbani, serikali ya Ghana ilichukua hatua rasmi kuhusu suala hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, alisema serikali imewasilisha malalamiko rasmi kwa mamlaka za Iraq na inataka waliohusika wawajibishwe.

"Tunataka haki itendeke kwa Stephanie. Tunahitaji wahusika watambuliwe na sheria ichukue mkondo wake."

Waziri huyo alisema serikali pia inatafakari uwezekano wa kusitisha usafirishaji wa wafanyakazi wa ndani kwenda Iraq kutokana na ongezeko la malalamiko ya unyanyasaji.

Aidha, Stephanie amepewa huduma za matibabu na msaada wa kisaikolojia ili kumsaidia kuanza tena maisha yake.

Serikali pia imemsaidia kifedha kuanzisha shughuli ndogo za kujipatia kipato na kumuahidi msaada wa masomo ili aweze kuendelea na elimu yake.

Wito wa kusaidia Waafrika wengine

Licha ya kuepuka mateso, Stephanie anasema bado kuna mamia ya Waafrika wanaopitia mateso kama yake katika nchi mbalimbali za Mashariki ya Kati.

Anasimulia kuwa akiwa Iraq alishuhudia visa vya kusikitisha vya wafanyakazi wengine waliopoteza maisha au kujeruhiwa vibaya.

"Ninajua watu ambao walipitia mateso makubwa kuliko yangu. Wengine hawakurudi nyumbani. Wengine walifariki bila familia zao kujua kilichowapata."

Kwa sababu hiyo, anasema anataka sauti yake iwe chachu ya mabadiliko.

"Tuliondoka nyumbani tukiamini tunaenda kutafuta maisha bora na kusaidia familia zetu. Lakini kwa wengi wetu, hali halisi ni tofauti kabisa na ahadi tulizopewa."

Stephanie sasa anatoa wito kwa serikali za Afrika, mashirika ya haki za binadamu na jumuiya za kimataifa kuongeza ulinzi kwa wafanyakazi wa ndani wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.

Anasema anaishukuru Ghana kwa kusaidia kurejesha matumaini yake, lakini anataka juhudi hizo ziwafikie pia wale ambao bado wamekwama katika mazingira ya unyanyasaji na hofu mbali na nyumbani.