Moja kwa moja , DR Congo yataka maelezo kuhusu vitisho vya jenerali Muhoozi wa Uganda

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imemtaka balozi wa Uganda kutoa maelezo kuhusu machapisho ya mkuu wa jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, yaliyotafsiriwa kama kuunga mkono waasi na kutoa vitisho kuhusu eneo la Walikale mashariki mwa Congo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula, Faidha Ngaga & Asha Juma

  1. Matumaini kwa Mamilioni: Sindano ya kuzuia HIV yenye ufanisi wa karibu asilimia 100 yafika Afrika

    .

    Uganda inatarajiwa kupokea shehena yake ya kwanza ya toleo nafuu la sindano ya mapinduzi ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (HIV), hatua inayotoa matumaini ya kupanua upatikanaji wa dawa hiyo barani Afrika ambako maambukizi ya HIV bado ni makubwa kuliko maeneo mengine duniani.

    Shehena ya kwanza duniani ya dawa hiyo ya bei nafuu, inayojulikana kama lenacapavir, iliwasili nchini Zambia Jumatano, huku usambazaji nchini Uganda ukitarajiwa kuanza katika siku chache zijazo, kwa mujibu wa shirika la Global Fund.

    Dawa hiyo hutolewa kwa njia ya sindano mara mbili tu kwa mwaka na imeonekana kuwa na ufanisi wa karibu asilimia 100 katika kuzuia maambukizi ya HIV. Inatarajiwa kugharimu takribani dola 40 za Marekani kwa mtu mmoja kwa mwaka.

    Zimbabwe nayo inatarajiwa kupokea shehena yake mwanzoni mwa mwaka ujao, huku nchi nyingine kadhaa zikitarajiwa kufuata.

    Kuwasili kwa dawa hiyo ya bei nafuu kunakuja mwaka mmoja tu baada ya toleo la awali lililotengenezwa na kampuni ya dawa ya Marekani ya Gilead Sciences kuanza kupatikana katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

    Toleo hilo la awali lilikuwa likigharimu karibu dola 28,000 kwa mwaka nchini Marekani, gharama iliyokuwa kubwa mno kwa watu wengi katika nchi zinazoendelea.

    Mkataba wa kihistoria wafungua njia

    Lenacapavir hufanya kazi kwa kushambulia ganda la kinga la virusi vya HIV, jambo linalovuruga uwezo wa virusi hivyo kuongezeka na kuanzisha maambukizi mwilini.

    Katika utafiti mkubwa wa kimatibabu uliohusisha zaidi ya wasichana balehe na wanawake vijana 5,000 nchini Uganda na Afrika Kusini mwaka 2024, hakuna hata mshiriki mmoja aliyepokea sindano hiyo aliyeambukizwa HIV.

    Wataalamu wa afya wanasema sindano hiyo ina faida kubwa ikilinganishwa na dawa za kila siku za kuzuia HIV zinazojulikana kama PrEP (Pre-Exposure Prophylaxis), ambazo zinahitaji kumezwa kila siku na wakati mwingine huambatana na unyanyapaa wa kijamii.

    Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipendekeza rasmi matumizi ya lenacapavir kwa ajili ya kuzuia HIV mwezi Julai 2025.

    Global Fund imeeleza kuwasili kwa dawa hiyo barani Afrika kama "hatua kubwa ya mafanikio" katika mapambano dhidi ya HIV, ikisema upatikanaji wa toleo nafuu utasaidia kuwafikia mamilioni zaidi walio katika hatari ya kuambukizwa.

    Katika taarifa yake, shirika hilo limesema:

    "Usambazaji huu unaashiria kasi na upanuzi ambao haujawahi kushuhudiwa wa upatikanaji wa dawa bora, salama na nafuu za kuzuia HIV katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati."

    Kwa mujibu wa Global Fund, zaidi ya watu 189,000 katika nchi 10 tayari wamepokea sindano yao ya kwanza ya lenacapavir.

    Shirika hilo linatarajia nchi 24 zitakuwa zimepokea dawa hiyo kabla ya mwisho wa mwaka huu. Kwa kushirikiana na serikali ya Marekani, lina mpango wa kuwafikia angalau watu milioni tatu ifikapo mwisho wa mwaka 2028.

    Hatimaye, dawa hiyo inatarajiwa kupatikana katika nchi 120 zenye kipato cha chini na cha kati duniani.

    Afrika bado inaathirika zaidi

    Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zinachangia karibu theluthi mbili ya watu wote wanaoishi na HIV duniani, huku wasichana balehe na wanawake vijana wakibeba mzigo mkubwa zaidi wa maambukizi mapya.

    Afrika Kusini ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaoishi na HIV duniani, ikiwa na karibu watu milioni nane wenye maambukizi ya virusi hivyo. Nchi hiyo ni miongoni mwa zinazotarajiwa kupokea sindano hiyo nafuu.

    Kwa mujibu wa WHO, watu milioni 41 duniani waliishi na HIV mwaka jana, huku watu 570,000 wakifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na Ukimwi.

    Hofu ya kupungua kwa misaada

    Usambazaji wa lenacapavir unafanyika wakati kukiwa na wasiwasi kuhusu kupunguzwa kwa misaada ya kigeni ya Marekani chini ya utawala wa Rais Donald Trump.

    Wataalamu wanaonya kuwa hatua hizo zinaweza kudhoofisha mafanikio yaliyopatikana kwa miongo kadhaa katika mapambano dhidi ya HIV barani Afrika, ambapo mataifa mengi bado yanategemea kwa kiasi kikubwa ufadhili wa kimataifa kwa ajili ya huduma za kinga na matibabu.

    Umoja wa Mataifa umeweka lengo la kutokomeza Ukimwi kama tishio la afya ya umma duniani ifikapo mwaka 2030.

    Soma Pia:

  2. Ajali ya Anthony Joshua: Kesi yaahirishwa

    .

    Kesi inayomkabili dereva wa gari lililombeba bondia wa Uingereza Anthony Joshua wakati lilipopata ajali katika jimbo la Ogun, Nigeria, Desemba mwaka jana na kusababisha vifo vya marafiki zake wawili wa karibu, imeahirishwa hadi tarehe 1 Desemba.

    Adeniyi Mobolaji Kayode anakabiliwa na mashtaka ya kuendesha gari kwa hatari na kusababisha vifo, kuendesha kwa uzembe na bila tahadhari, kusababisha majeraha na uharibifu wa mali, pamoja na kuendesha gari bila leseni halali ya taifa.

    Kwa upande mwingine, Abubakar Adamu, dereva wa lori lililohusika katika ajali hiyo, anakabiliwa na shtaka moja la kuzuia mtiririko huru wa magari barabarani.

    Wakili wa Kayode, Otunba Abiodun Olalekan, aliiambia mahakama Alhamisi kuwa mteja wake alikuwa mgonjwa na hakuweza kuhudhuria kikao hicho cha usikilizwaji wa kesi.

    Unaweza pia kusoma:

  3. Uturuki yalaani vikali mashambulizi katika pwani ya Libya

    .

    Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imeeleza kuwa mashambulizi ya Ukraine dhidi ya meli za Urusi katika maji ya Libya ni "ukiukaji wa sheria za kimataifa."

    Wizara hiyo imezitaka pande zinazohusika kwenye vita hivyo kujiepusha na mashambulizi dhidi ya meli za kiraia na kuheshimu sheria za kimataifa.

    "Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, vitendo vya kivita vinavyofanyika katika maji ya nchi isiyoegemea upande wowote ni kinyume cha sheria. Kwa upande wa Libya, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama tayari yamearifiwa kuhusu mashambulizi yaliyolenga meli katika bandari ya Benghazi na maeneo ya maji yanayoizunguka," msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Uturuki amesema katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari mjini Ankara.

    Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine alisema Jumanne kuwa shambulio la ndege zisizo na rubani lililofanywa wiki iliyopita dhidi ya meli ya kijeshi ya Urusi na meli ya mizigo katika maji ya Libya lilikuwa "halali," akisisitiza kuwa Ukraine ilichukua hatua hiyo kwa kujilinda.

    Unaweza pia kusoma:

  4. Dkt. Rioba kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mwana FA ateuliwa Waziri wa Uvuvi

    .

    Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Dkt. Ayub Rioba kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali katika mabadiliko mapya ya uongozi yaliyotangazwa Jumatano.

    Kabla ya uteuzi huo, Dkt. Rioba alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) aliyestaafu. Uteuzi wake unamweka katika nafasi ya kusimamia mawasiliano ya serikali na utoaji wa habari kwa umma.

    Katika mabadiliko hayo, mwanamuziki na mwanasiasa Hamis Mohamed Mwinjuma, maarufu kama Mwana FA, ameteuliwa kuwa Waziri wa Uvuvi baada ya Rais Samia kugawa iliyokuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kuunda wizara mbili tofauti.

    Mabadiliko hayo yamezaa Wizara ya Uvuvi na Wizara ya Mifugo, kila moja ikiwa na uongozi na muundo wake wa kiutawala.

    .

    Mwana FA amehamishiwa Wizara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambako alikuwa Naibu Waziri. Sasa atasimamia sekta ya uvuvi iliyokuwa ikiongozwa chini ya wizara iliyounganisha mifugo na uvuvi.

    Wakati huo huo, Rais Samia amemteua Dk Bashiru Ally Kakurwa kuwa Waziri wa Mifugo, hatua inayotenganisha rasmi usimamizi wa sekta za mifugo na uvuvi.

    Mabadiliko hayo ya uteuzi na uhamisho wa viongozi yametangazwa katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka.

    Unaweza pia kusoma:

  5. DR Congo yataka maelezo kuhusu vitisho vya jenerali Muhoozi wa Uganda

    .

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) imemwita mwanadiplomasia mkuu wa Uganda mjini Kinshasa kufuatia machapisho ya mitandao ya kijamii ya mkuu wa jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mwana wa rais wa nchi hiyo.

    Katika mfululizo wa machapisho kwenye mtandao wa X, Jenerali Kainerugaba alionekana kuunga mkono uwezekano wa waasi kuiteka Walikale, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa DR Congo. Hata hivyo, alisisitiza kuwa uwepo wa jeshi la Uganda nchini humo unalenga masuala ya usalama pekee.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya DR Congo ilimwita balozi wa Uganda kueleza matamshi hayo, ikiyataja kuwa "ya hatari sana" na yanayoweza kuathiri uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.

    Serikali ya Uganda haikuwa imetoa majibu yoyote kufikia sasa.

    Mvutano huu wa kidiplomasia umeibuka licha ya ushirikiano wa karibu wa kijeshi kati ya nchi hizo jirani.

    Tangu mwaka 2021, majeshi ya Uganda na DR Congo yamekuwa yakifanya operesheni za pamoja dhidi ya kundi la Allied Democratic Forces (ADF), lenye uhusiano na kundi la Islamic State, mashariki mwa DR Congo.

    Uganda pia imekuwa ikihusika katika juhudi za upatanishi kati ya serikali ya Congo na kundi lenye silaha linaloongozwa na aliyekuwa mbabe wa vita, Thomas Lubanga, katika jimbo la Ituri.

    Katika machapisho yake, Jenerali Kainerugaba aliishutumu Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), kundi lenye silaha linalofanya shughuli zake mashariki mwa DR Congo, kwa kuwalenga watu wa jamii ya Bahima.

    Wabahema ni jamii ya wafugaji wa jadi inayopatikana zaidi katika jimbo la Ituri kaskazini mashariki mwa DR Congo. Jamii hiyo ina uhusiano wa kihistoria na kitamaduni na Wabahima wa Uganda.

    Jenerali huyo pia alitoa vitisho vya kuungwa mkono kwa utekaji wa Walikale na waasi, huku akitetea uwepo wa jeshi la Uganda nchini DR Congo.

    Walikale ni eneo lenye utajiri mkubwa wa madini, likiwemo baadhi ya machimbo makubwa ya bati na dhahabu nchini humo.

    Akaunti ya X ya Jenerali Kainerugaba, iliyokuwa na karibu wafuasi milioni 1.4, baadaye haikuweza kupatikana.

    Haijulikani iwapo aliifunga mwenyewe kama alivyowahi kufanya hapo awali au kama jukwaa hilo liliisimamisha.

    Katika wiki hiyo hiyo, alitangaza:

    "Machapisho yangu kwenye X nchini Uganda ni maagizo ambayo lazima yatekelezwe."

    .

    Unaweza pia kusoma:

  6. Mwanzo mgumu wa Pochettino wazidi kuwaumiza United

    ,

    Mechi mbili, bila ushindi wowote. Kadi mbili nyekundu, mabao mawili ya kufunga. Bao moja lilikataliwa, mabao sita yakafungwa dhidi yao. Je, inawezekana kwa Mauricio Pochettino kujifunza lolote kutokana na wiki yake ya kwanza ya vurugu kama kocha wa Manchester United?

    Manchester United na Pochettino walionesha wazi kutoridhishwa kwao kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Sporting, wakikasirishwa na kutolewa nje kwa Leny Yoro katika mchezo dhidi ya Liverpool, wakiamini uamuzi huo haukuwa wa haki na ulichangia kipigo cha mabao 4-0.

    Viongozi wa klabu pia walikuwa na hasira kubwa baada ya sare ya 2-2 mjini Lisbon.

    Safari hii, lawama zilimwelekea mwamuzi wa fainali ya Kombe la Dunia 2022, Szymon Marciniak. Kupuliza filimbi kabla ya kichwa cha Amad kuingia wavuni kulimaanisha VAR haikupata nafasi ya kuchunguza iwapo mwamuzi huyo wa Poland alikuwa sahihi kudai kuwa Youri Tielemans alimfanyia madhambi Goncalo Inacio kabla ya kumpasia mpira Mivory Coast huyo.

    Aliyekuwa winga wa United, Ashley Young, hakukubaliana na uamuzi huo. Alielezea uchezeshaji wa Marciniak kuwa "aibu".

    Tielemans pia alipata kadi ya njano ambayo baadaye ilipelekea kadi nyekundu mwishoni mwa mchezo. United sasa wamepoteza wachezaji kwa kadi nyekundu mara nne katika michezo yao mitano iliyopita, jambo litakalomfanya Mbelgiji huyo kuukosa mchezo dhidi ya RB Leipzig huko Old Trafford tarehe 8 Disemba.

    Kisha, ndani ya dakika chache, Marciniak aliamua kwamba walinda mlango wa Manchester United, Senne Lammens, na mwenzake wa Sporting, Kaique, hawakuwa wamechezewa vibaya katika mabao yaliyofungwa dhidi yao. Safu zao za ulinzi zililalamika vikali.

    VAR ilimtaka Marciniak kwenda kuangalia tukio la Kaique kwenye skrini ya pembeni mwa uwanja, na baada ya kulitazama upya, alibatilisha uamuzi wake wa awali.

    Watu wa ndani wa United wanaamini tukio la Tielemans halikuwa faulo na kwamba bao la Amad lilipaswa kukubaliwa. Pia walihisi kuwa kama kulikuwa na madhambi yoyote dhidi ya Kaique yaliyofanywa na Patrick Dorgu, yalikuwa madogo na hayakustahili kufanya bao lao lifutwe.

    Pochettino alilazimika kuwa mwangalifu katika kauli zake, akijua kwamba matamshi ya ukosoaji mkali dhidi ya waamuzi yangeweza kumletea adhabu ya fedha.

    Alipoulizwa katika mkutano wake wa baada ya mchezo iwapo alihisi Marciniak alikosea, jibu lake la kwanza lilikuwa ni kutikisa kichwa kuashiria kukubaliana.

    Dakika chache kabla ya hapo, alipokuwa akizungumza na TNT Sports, alikuwa wazi zaidi:

    "Ni vigumu kupata mchezo ambao unaadhibiwa kwa kiasi hiki katika matukio muhimu ndani ya dakika 90," alisema.

    "Tumeadhibiwa sana katika matukio muhimu ya mchezo."

    .

    Unaweza pia kusoma:

  7. Mahakama Kenya yaamuru kusitishwa kwa ujenzi wa kituo cha Ebola cha Marekani

    .

    Mahakama nchini Kenya imesema kuwa serikali ya taifa hilo, ilikiuka baadhi ya vifungu vya Katiba katika ujenzi wa kituo cha karantini ya Ebola kilichofadhiliwa na Marekani.

    Mahakama pia imeamuru kusitishwa kwa kazi zozote zaidi za ujenzi wa kituo hicho, hadi serikali itakapotekeleza masharti iliyowekwa, ikiwemo kuweka wazi maelezo yaliyomo katika makubaliano yaliyoafikiwa kati ya Marekani na Kenya kabla ya ujenzi huo kuanza.

    Soma pia:

  8. Wasiwasi waongezeka kuhusu mlipuko wa Ebola DRC

    .

    Idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) sasa imezidi 12,000, kulingana na takwimu za serikali zilizotolewa hii leo, huku juhudi za kudhibiti mlipuko huo zikiendelea kukabiliwa na changamoto.

    Takwimu hizo zinaonyesha kuwa jumla ya watu 12,021 wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo, huku watu 5,904 wakifariki dunia.

    Mlipuko huo, unaosababishwa na aina adimu ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo, ulitangazwa katikati ya mwezi Mei katika jimbo la Ituri, kaskazini mashariki mwa Congo. Tangu wakati huo, umeenea katika majimbo 8 kati ya 26 ya nchi hiyo.

    Hakuna matibabu wala chanjo zilizoidhinishwa kwa ajili ya aina hii ya virusi vya Ebola.

    Kuchelewa kugunduliwa kwa maambukizi, migogoro na huduma duni za afya zimechangia kuenea kwa kasi zaidi kwa ugonjwa huo ikilinganishwa na milipuko iliyopita.

    Soma pia:

  9. Trump na NATO zataka Urusi kusitisha kupanua vita vya Ukraine

    .
    Maelezo ya picha, Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte

    Rais wa Marekani Donald Trump na Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte wamesema kuwa Urusi inapaswa kuepuka kuchukua hatua zozote zinazoweza kupanua vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

    Kauli hiyo imetolewa katika taarifa ya pamoja baada ya mkutano wao uliofanyika Florida, ambapo pia walijadili vita vya Iran.

    Mkutano huo ulifanyika siku chache baada ya kiongozi huyo wa chama cha Republican, ambaye amekuwa akikosoa washirika wa Marekani wa Magharibi, kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin na kiongozi wa China Xi Jinping wiki iliyopita barani Asia, akiwataja kila mmoja kuwa "rafiki yangu".

    "Vilevile, tulijadili umuhimu wa Urusi kuepuka hatua zozote zinazoweza, kwa kukusudia au bila kukusudia, kupanua vita hivyo, pamoja na umuhimu wa kupata suluhu ya amani haraka iwezekanavyo," viongozi hao walisema katika taarifa yao ya pamoja.

    Mkutano wa Trump na Putin uliibua upinzani kutoka kwa wanasiasa wa chama cha Democratic nchini Marekani na washirika wa Ulaya, ambao wamekuwa wakishinikiza kujumuishwa katika mazungumzo yanayoungwa mkono na Marekani ya kutafuta njia ya kumaliza vita nchini Ukraine.

    Rutte, ambaye mara kadhaa amejaribu kupunguza mvutano ndani ya NATO na kudumisha uhusiano mzuri na Trump, amesema kuwa ni jambo la kawaida kwa mataifa makubwa yenye silaha za nyuklia kukutana.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Trump na Rutte pia walijadili namna ya kuongeza matumizi ya fedha katika sekta ya ulinzi pamoja na uwekezaji nchini Marekani na katika nchi wanachama wa NATO.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye amekuwa akikosolewa na Trump, amesema kuwa Ulaya lazima ihusishwe katika mazungumzo ya kutafuta amani.

    Soma pia:

  10. Marekani yaipa SpaceX idhini ya kurusha satelaiti milioni moja angani

    .

    Marekani imeipa kampuni ya SpaceX idhini ya kurusha satelaiti milioni moja katika angani ili kusaidia kujenga vituo vya kuhifadhi na kuchakata data angani.

    Hii ni idhini ya kwanza ya aina yake.

    Kampuni hiyo inayomilikiwa na Elon Musk inataka kutumia nishati ya mwanga wa jua kuendesha satelaiti hizo zitakazochakata data kwa ajili ya akili unde (AI) na kutuma matokeo yake kurejea duniani.

    Tume ya Mawasiliano ya Marekani (FCC) ilisema kuwa mradi huo unaojulikana kama Starmind utasaidia katika "ukuaji wa uchumi wa Marekani unaotokana na teknolojia ya akili unde."

    Idhini hiyo imetolewa wakati jamii mbalimbali nchini Marekani zimekuwa zikipinga upanuzi wa vituo vya kuhifadhi na kuchakata data vinavyojengwa ardhini.

    SpaceX inaamini kuwa "vituo vya kuchakata data vilivyo angani" ndiyo njia yenye gharama nafuu zaidi na inayotumia nishati kwa ufanisi kukidhi ongezeko la mahitaji ya uwezo wa kompyuta unaohitajika kuendesha teknolojia ya akili unde (AI), mahitaji ambayo kwa mujibu wa kampuni hiyo yanazidi uwezo wa miundombinu iliyopo duniani.

    Akijibu tangazo hilo, Musk aliandika kwenye mtandao wa X "Tunashukuru sana. Huu utakuwa mchango mkubwa kwa Marekani na dunia nzima."

    Soma pia:

  11. Tetesi za Soka: Liverpool yafikiria kumrejesha Quansah, PSG ikimuwinda nyota wa Chelsea

    .
    Maelezo ya picha, Jarell Quansah

    Liverpoolhaijaondoa uwezekano wa kutumia kipengele cha mkataba kinachoiruhusu kumnunua tena beki wa Bayer Leverkusen, Jarell Quansah, mwenye umri wa miaka 23.

    Hatua hiyo itaiwezesha Liverpool kumsajili beki huyo wa timu ya taifa ya England mwaka 2027 kwa ada ya zaidi ya pauni milioni 50.

    Chelsea inakabiliwa na uwezekano wa kumpoteza mshambuliaji wake kutoka Brazil, Estevao Willian, mwenye umri wa miaka 19, ambaye analengwa na Paris Saint-Germain (PSG). Klabu hiyo ya Ufaransa inamtafuta mshambuliaji kutokana na baadhi ya wachezaji wake kuumia.

    Arsenal imemuongeza winga wa Club Brugge na timu ya taifa ya Ureno, Carlos Forbs, mwenye umri wa miaka 22, kwenye orodha ya wachezaji inayowalenga kuwasajili katika dirisha la usajili la Januari.

    Liverpool imekubali kumsajili winga wa Diambars FC, Sidy Barhama Ndiaye, Januari 2028. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 16 alivutia baada ya kufanya vizuri akiichezea Senegal katika Kombe la Dunia la vijana wasiozidi miaka 17.

    Beki wa kati wa England, Fikayo Tomori, mwenye umri wa miaka 28, huenda akaondoka AC Milan na kujiunga na Atletico Madrid huku mkataba wake wa sasa ukitarajiwa kumalizika ndani ya miezi sita ijayo.

    Everton haitafanya jaribio la kumsajili mshambuliaji wa Senegal anayeichezea Cagliari, Paul Mendy, katika dirisha la Januari, lakini bado inaendelea kumfuatilia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 kwa ajili ya usajili wa baadaye.

    Kipa wa Arsenal, Kepa Arrizabalaga, hajapokea ofa yoyote kutoka Valencia licha ya taarifa zilizomuhusisha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 na kurejea nchini kwao Hispania.

    Bayern Munich ina nafasi nzuri ya kumshawishi winga wa Ufaransa, Michael Olise, mwenye umri wa miaka 24, kuongeza muda wa mkataba wake ambao kwa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.

  12. Saudi Arabia na waasi wa Kihouthi washambuliana, milipuko yasikika Riyadh

    .

    Milipuko mikubwa ulisikika katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, jana jioni, baada ya kundi la Wahouthi kutangaza kuwa lilikuwa limelenga bandari za Jeddah na Jazan, kwa kile walichokiita, kujibu mashambulizi ya Saudi Arabia katika bandari ya Hodeidah, inayodhibitiwa na kundi hilo magharibi mwa Yemen.

    Saudi Arabia imesema kuwa imefanikiwa kuzuia shambulio la ndege isiyo na rubani la wahouthi lililolenga kiwanda cha kusafisha mafuta cha Ras Tanura. Picha za satelaiti, hata hivyo, zilionyesha moshi mwingi ukitanda juu ya eneo hilo.

    Wakati huohuo, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulitangaza kuwa umedungua ndege isiyo na rubani ya Wahouthi karibu na bandari ya Jeddah, katika pwani ya Bahari Nyekundu.

    Mapigano kati ya pande hizo mbili yameongezeka katika siku za hivi karibuni.

    Soma pia:

  13. Watu 31 wafariki baada ya lori ya mafuta kupata ajali mjini Cairo

    .

    Watu 31 wamefariki na wengine 21 kujeruhiwa baada ya moto mkubwa kuzuka kwenye barabara moja kuu mjini Cairo, Misri.

    Ajali hiyo ilitokea baada ya lori ya mafuta kupenduka na kusababisha ajali, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya nchi hiyo.

    Hospitali zilizo karibu zilipokea majeruhi waliokuwa na majeraha ya kuungua na matatizo ya kupumua kutokana na kuvuta moshi baada ya tukio hilo lililotokea jana jioni, katika barabara iliyoko eneo la Warraq.

    Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha miale mikubwa ya moto na moshi mweusi ukipaa juu angani, huku magari kadhaa yaliyokuwa karibu yakiteketea.

    Maafisa hawajatoa maelezo rasmi kuhusu chanzo cha moto huo. Hata hivyo, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali vimeripoti kuwa lori hilo la mafuta lilipinduka na kumwaga petroli kwenye magari yaliyokuwa karibu.

    Mwendesha mashtaka mkuu wa eneo hilo ameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo na kuagiza sampuli za vinasaba (DNA) zichukuliwe kutoka kwa miili ya waliofariki.

    Gazeti la serikali la Al-Ahram limeripoti, likinukuu vyanzo vinavyofahamu uchunguzi huo, kuwa lori hilo lililokuwa likimilikiwa na kampuni binafsi lilikuwa likisafiri kwenye barabara hiyo, wakati nyaya za umeme zilianguka mbele yake na kumfanya dereva ashindwe kulidhibiti gari hilo.

  14. Trump atangaza ushuru mpya kwa bidhaa zinazoingia Marekani

    .
    Maelezo ya picha, Donald Trump

    Marekani imetangaza ushuru mpya, dhidi ya bidhaa zinazoingia nchini humo.

    Ushuru huo mpya unatarajiwa kuathiri washirika wakubwa wa kibiashara wa nchi hiyo, wakiwemo China, Umoja wa Ulaya na maeneo mengine 12, yakiwemo Japan, Korea Kusini na Taiwan.

    China inakabiliwa na kiwango cha juu zaidi cha ushuru, cha hadi asilimia 40, ikifuatiwa na Vietnam ambayo inaweza kutozwa hadi asilimia 35. Nchi nyingine zitatozwa ushuru wa asilimia 20 au 25.

    Mwakilishi wa Biashara wa Marekani alitangaza mapendekezo hayo ya ushuru pamoja na ripoti za kina zinazoeleza jinsi sera za biashara za kila eneo husika zinavyodaiwa kuathiri biashara ya Marekani.

    Ushuru huo mpya utaanza kutekelezwa mwaka ujao baada ya mashauriano.

    Mapendekezo hayo ya ushuru yataathiri bidhaa kutoka mataifa yafuatayo: China,Umoja wa Ulaya,Singapore,Uswisi,Indonesia,Malaysia,Cambodia,Thailand,Korea Kusini,Vietnam,Taiwan,Bangladesh,Japan, India

    Soma pia:

  15. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Alhamisi ya leo