Je, NATO inaweza kuwa nguvu ya kuaminika bila Marekani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahusiano ya kuvuka Atlantiki (kati ya Marekani na Ulaya) yameingia kwenye mvutano mpya baada ya mataifa ya Ulaya kukataa kushiriki kikamilifu katika mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Rais wa Marekani, Donald Trump, mara kadhaa ametumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuonyesha kukerwa kwake na washirika wa Ulaya, na hata kutishia kujiondoa katika muungano wa kijeshi wa muda mrefu, North Atlantic Treaty Organization (NATO).
Marekani ndiyo inayochangia sehemu kubwa ya matumizi ya ulinzi na teknolojia ya kisasa ya kijeshi ndani ya NATO. Ikiwa ingeondoka, swali linabaki: Je, mataifa ya Ulaya yangekuwa na uwezo wa kutoa ulinzi wa kuaminika (deterrence) bila msaada wa kijeshi wa Marekani?
NATO ni nini, na ilianzishwa lini?
North Atlantic Treaty Organization iliundwa mwaka 1949 na nchi 12, zikiwemo Marekani, Uingereza, Canada na Ufaransa. Wanachama wake wanakubaliana kwamba ikiwa nchi moja itashambuliwa, nyingine zinapaswa kuisaidia kujilinda.
Lengo kuu la NATO lilikuwa kuzuia upanuzi wa Muungano wa Kisovieti barani Ulaya, muungano wa jamhuri za kikomunisti uliotawaliwa na Urusi.
Baada ya muungano huo kuvunjika mwaka 1991, nchi nyingi za Ulaya Mashariki zilijiunga na NATO, zikiwemo Albania, Bulgaria, Hungary, Poland, Jamhuri ya Czech, Slovakia, Romania, Lithuania, Latvia na Estonia.
Nchi za Sweden na Finland, ambazo zilikuwa hazijiingizi katika miungano ya kijeshi kwa miongo kadhaa, ziliomba kujiunga mwezi Mei 2022 kufuatia uvamizi mkubwa wa Urusi dhidi ya Ukraine.
Kwa sasa, muungano huu wa kijeshi una wanachama 32 kutoka Ulaya na Amerika Kaskazini.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
NATO haina jeshi lake la kudumu, lakini nchi wanachama zinaweza kuchukua hatua za pamoja za kijeshi kukabiliana na migogoro ya kimataifa.
Kwa mara ya kwanza, vikosi vya NATO vilishiriki mapigano mwaka 1994, wakati ndege za kivita za Marekani zilipodungua ndege za Serbia zilizokuwa zikishiriki mashambulizi ya mabomu nchini Bosnia kama sehemu ya Operesheni Deny Flight.
Operesheni zinazoendelea ni pamoja na Operation Sea Guardian, inayolenga kulinda Bahari ya Mediterania, pamoja na ujumbe wa NATO nchini Iraq (ambao kwa sasa unaendeshwa kutoka Naples kutokana na hali ya usalama katika eneo hilo).
Ombi la Ukraine kujiunga na NATO bado limesitishwa kwa sasa.
Muungano huo haujatuma wanajeshi nchini Ukraine wala kuanzisha eneo lisiloruhusiwa ndege kuruka (no-fly zone), kwa kuhofia kuingia moja kwa moja katika vita na Urusi, taifa lenye silaha za nyuklia.
Hata hivyo, nchi wanachama mmoja mmoja zimetoa silaha na vifaa vya kijeshi kusaidia Ukraine.
Ulinzi wa Ulaya

Chanzo cha picha, Getty Images
Kama muungano wa kijeshi, wa NATO una nguvu kubwa sana. Hata hivyo, wataalamu wanasema kuwa bila ushiriki wa Marekani, uwezo wa NATO wa kuzuia adui mwenye nguvu utapungua kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, takribani wanajeshi 68,000 wa Marekani walikuwa wamewekwa katika kambi mbalimbali za kijeshi barani Ulaya kufikia Desemba 2025.
Wanajeshi hawa wanasambazwa katika kambi 31 za kijeshi pamoja na maeneo mengine 19 ya kijeshi.
Dkt. Torrey Taussig, Mkurugenzi wa mpango wa usalama katika taasisi ya Atlantic Council, anasema:
"Kwa sasa, kujitolea kwa Marekani ndani ya NATO ni muhimu sana, katika nyanja za kijeshi za kawaida na pia silaha za nyuklia."
Ameeleza kuwa bila msaada wa Marekani, Ulaya itapata ugumu mkubwa kuziba mapengo katika maeneo muhimu kama:
Usafirishaji wa kijeshi wa masafa marefu, Ujasusi, Ufuatiliaji na uchunguzi, mifumo ya ulinzi dhidi ya makombora.
Kwa upande mwingine, Dkt. Gavin Hall kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde anakubali kwamba kujiondoa kwa Marekani kutakuwa pigo kubwa kwa usalama wa Ulaya.Anasema:
"Marekani bado ndiyo nguzo kuu inayobeba uwezo wa wanachama wengine wa NATO."
Hata hivyo, anaongeza kuwa nchi za Ulaya zinaelewa kwamba hatua za awali za kuhamasisha na kupeleka vikosi vitani tayari zinategemea wao wenyewe, na baadhi ya uwezo wa kijeshi unadumishwa hata bila msaada wa Marekani.
Kwa mfano, operesheni nyingi za NATO kama: ulinzi wa anga katika eneo la Balkan, doria za baharini katika Bahari ya Mediterania zinafanyika kwa kiasi kikubwa bila ushiriki wa moja kwa moja wa Marekani.
Wanachama wa NATO hutumia kiasi gani kwenye ulinzi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Donald Trump ana wasiwasi mkubwa kuhusu muungano huo na kile kinachoonekana kuwa kushindwa kwake hapo awali kuongeza matumizi ya ulinzi.
Wakati wa kampeni yake ya kugombea muhula wa pili wa urais mwaka 2024, Trump alitoa kauli tata akisema kwamba, akiwa rais, atahimiza Urusi kushambulia nchi wanachama wa NATO ambazo hazijatenga zaidi ya 2% ya pato lao la taifa (GDP) kwa ajili ya ulinzi.
Mnamo 2014, NATO iliomba wanachama wote kutumia takribani 2% ya GDP yao kwa ulinzi. Kufikia mwaka 2025, nchi zote wanachama zilikuwa zimefikia lengo hilo.
Lengo la hivi karibuni ambalo wanachama wamekubaliana nalo ni kuongeza matumizi ya ulinzi hadi kufikia 5% ya GDP ifikapo mwaka 2035.
Kulingana na taasisi ya kimataifa, Stockholm International Peace Research, Marekani ilichangia asilimia 66 ya jumla ya matumizi ya ulinzi ya nchi za NATO mwaka 2024.
Taussig anaeleza kwa nini kuongeza bajeti ya ulinzi ya Ulaya ni jambo lisiloepukika.
"Marekani pia huchangia takribani asilimia 15 ya bajeti ya pamoja ya NATO kufadhili makao makuu ya NATO, amri za kijeshi na miundombinu. Ingawa washirika wanaongeza matumizi ya ulinzi, fedha nyingi zaidi zingehitajika iwapo Marekani ingepunguza mchango wake wa kifedha."
NATO imekuwa ikiimarisha ulinzi wake dhidi ya tishio la Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo mwaka 2023, makamanda wa NATO walikubaliana mipango ya kina ya kukabiliana na mashambulizi yanayoweza kufanywa na Urusi katika eneo la Aktiki na Kaskazini ya Bahari ya Atlantiki, Ulaya ya kati, au ukanda wa Mediterania.
Mwaka uliotangulia, NATO pia ilitangaza mipango ya kuongeza idadi ya wanajeshi wake walioko katika hali ya tahadhari ya juu barani Ulaya kutoka 40,000 hadi zaidi ya 300,000. Aidha, imeimarisha ulinzi wake katika upande wa mashariki unaopakana na Urusi kwa kuunda vikosi vinane vya mapambano, ambavyo hutofautiana kwa ukubwa na muundo kulingana na mahitaji ya kijeshi.
Kila baada ya miaka mitatu, NATO hufanya mazoezi yake makubwa ya kijeshi yanayoitwa Steadfast Defender, yanayohusisha wanajeshi 90,000 kutoka nchi zote 32 wanachama wa NATO. Zoezi lijalo limepangwa kufanyika mwaka 2027.
Nchi za Ulaya tayari zinafanya mipango ya kijeshi ili kustahimili mashambulizi ya awali na kuwezesha uhamasishaji wa haraka wa majeshi, lakini Hall anasema hana uhakika kama hali hii inaweza kudumishwa kwa muda mrefu.
'Kuvunjika kwa uhusiano'
Jeshi la Marekani hufanya mara kwa mara mazoezi ya kijeshi ya pande mbili na ya pamoja na washirika wa Ulaya, jambo linalosaidia kuboresha mbinu za kivita na kuimarisha uwezo wa majeshi kufanya kazi pamoja.
Kuwa mwanachama wa NATO kunaipa Marekani ufikiaji rahisi wa vituo vingi vya kijeshi barani Ulaya.
Taussig anasema: "Bila NATO, Marekani ingelazimika kusaini mikataba ya ushirikiano wa ulinzi na nchi moja moja ili kuweza kufanya operesheni katika nchi hizo."
Anaeleza kuwa Marekani tayari ina makubaliano tofauti na nchi nyingi za Ulaya, lakini huenda ikalazimika kusaini mikataba mipya na zile ambazo haina nazo ushirikiano wa ulinzi. Hata hivyo, anakubali kwamba hatua yoyote ya Donald Trump ya kutekeleza tishio lake la kujiondoa NATO itakuwa na madhara ya kijeshi pamoja na kisiasa.
"Kisiasa, kuvunjika kwa uhusiano kati ya Marekani na muungano huo kutakuwa janga kwa umoja wa pande za Atlantiki na kwa uwezo wa NATO kuzuia Urusi na wapinzani wengine," Taussig anaonya.
Mbali na kutoa dhamana ya usalama, muungano huo pia umeiletea Marekani heshima na uhusiano mzuri mkubwa barani Ulaya.
"Tusisahau kwamba mara pekee ambapo Kifungu cha 5 cha ulinzi wa pamoja cha NATO kilitumika ilikuwa ni kuilinda Marekani, hasa kutokana na uaminifu wake kama mshirika thabiti ndani ya NATO."
Kifungu hicho cha 5 kilitumika baada ya mashambulizi ya kigaidi ya September 11 nchini Marekani.
Hall anahisi kuwa Trump anaweza kutumia tishio la kujiondoa NATO ili kupata makubaliano katika maeneo muhimu kama Greenland (ambayo amesema anataka kuipata kwa sababu za usalama wa taifa) au biashara. Anaongeza kuwa kujiondoa huko kutakuwa na madhara kwa pande zote mbili.
"Itavunja kabisa makubaliano ya baada ya Vita Kuu vya Pili vya Dunia kuhusu kutogawanyika kwa usalama wa eneo la Euro-Atlantiki. Itakuwa ishara kwamba usalama wa Ulaya si muhimu tena kwa Marekani, na kwamba mabadiliko katika hali ya usalama wa Ulaya hayaathiri tena maslahi ya Marekani."














