Kwa nini ujenzi wa msikiti nchini Japan umezua utata?

Eneo ambalo leo limejaa nyasi, hivi karibuni litakuwa makazi ya msikiti wa kwanza katika Jiji la Fujisawa, nchini Japan.
"Hali hii inanifanya niwe na wasiwasi kuhusu jinsi jamii yetu inaweza kubadilika," anasema Noriko Izumizawa, mkazi wa muda mrefu wa eneo hilo.
Mipango ya kujenga kituo cha Kiislamu katika Fujisawa, mji tulivu wa pwani ulio takribani saa moja kwa gari kusini mwa Tokyo, imeibua hisia tofauti miongoni mwa wakazi.
Hasira na hofu ni baadhi ya hisia zilizooneshwa, huku pia kukiwa na matumaini na kukubalika kutoka kwa wengine. Suala hili linaangazia wasiwasi unaoongezeka kuhusu uhamiaji na mabadiliko ya kijamii, wakati Japan ikikabiliwa na upungufu wa wafanyakazi kutokana na kupungua na kuzeeka kwa idadi ya watu.
Ingawa uhamiaji bado ni suala nyeti lenye vikwazo vya kisiasa, Japan imeendelea kutegemea wafanyakazi kutoka nje ya nchi ili kuziba nafasi za ajira zinazokosekana.
Hii inamaanisha kuwasili kwa wahamiaji wenye tamaduni, lugha, dini na mitindo ya maisha tofauti.
Kwa hiyo, mjadala unaoendelea katika miji kama Fujisawa na kote nchini Japan unahusiana moja kwa moja na swali la msingi kuhusu utambulisho wa Wajapani.
Izumizawa si yeye pekee mwenye hisia hizo.
Yeye ni miongoni mwa wakazi wa Fujisawa ambao wana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa uwepo wa jamii ya Waislamu katika jiji hilo na jinsi inavyozidi kuonekana wazi.
Anasema kuwa mijadala yenye mgawanyiko kuhusu uhamiaji nchini Marekani na barani Ulaya pia imeongeza hisia zake za wasiwasi.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwanzoni mwa mwaka huu, maandamano yalizuka kupinga ujenzi wa msikiti karibu na kituo cha treni cha eneo hilo, huku maelfu ya watu wakijitokeza barabarani kupinga mradi huo.
Baadhi ya watu wanaamini kuwa kujenga msikiti ambao ni mkubwa zaidi kuliko hekalu la Kijapani la Shinto lililo karibu kunachukuliwa kuwa ni kukosa heshima.
Pia kumekuwa na ripoti kuhusu kusambaa kwa matamshi ya chuki na taarifa potofu kwenye mitandao ya kijamii nchini Japan.
Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kuwa baadhi ya misikiti imepokea simu na barua pepe za matusi, jambo lililosababisha makundi yanayopinga chuki.
Hiroki Suzuka, msimamizi wa duka la kahawa lililo mkabala na eneo ambalo Msikiti wa Fujisawa unatarajiwa kujengwa, anatoa wito wa kuwepo kwa uelewano na mazungumzo zaidi kati ya pande zote.
"Sipingi moja kwa moja ujenzi huo, lakini pia siwezi kusema kuwa ninaunga mkono kwa nguvu," anasema.
"Nadhani hatua ya kwanza ni kujifunza zaidi kuwahusu; Uislamu ni nini, wao ni akina nani, na maadili pamoja na mitazamo yao ni ipi. Kila kitu huanza kwa kuwa na fikra zilizo wazi na nia ya kujenga uelewano wa pande zote," aliongeza.
Kuwa Muislamu nchini Japan
Mohammad Mohiuddin, mfanyabiashara, ameishi Osaka kwa miaka 39.
Alihamia Japan kutoka Sri Lanka mwaka 1987, wakati wa kipindi cha ustawi wa uchumi, akitafuta fursa bora za ajira.
Mwanzoni alifanya kazi katika biashara ya vito vya thamani, kisha akaingia katika biashara ya kusafirisha magari yaliyotumika kwenda nchi kama Sri Lanka na Pakistan.
Anasema alifika Japan wakati ambapo idadi ya wakazi wa kigeni ilikuwa ndogo zaidi kuliko ilivyo sasa.
Lakini, kulingana na Mohiuddin, siku hizi wenyeji wanaonyesha uadui zaidi kuliko ilivyokuwa wakati huo, na wanatoa kauli nyingi za kukera dhidi ya Waislamu, mtandaoni na hata katika maisha ya kila siku.
Anasema:
"Kuna maoni mengi sana kwenye mitandao ya kijamii yanayosema, 'Ondokeni Japan' au 'Rudini nchini kwenu.' "
"Baadhi ya watu hata huja msikitini na kuanza kupiga kelele na kutoa matusi."
Mohiuddin huenda katika Msikiti wa Osaka kila siku kwa ajili ya kuswali na kutekeleza majukumu yake mengine kama mwanachama wa jamii ya Kiislamu ya eneo hilo.
Anasema hajawahi kuhisi kwamba maisha yake yako hatarini.
Licha ya kuwa na uhusiano mzuri na majirani zake kwa miaka mingi, amegundua kuwa katika miaka ya hivi karibuni mitazamo ya watu dhidi ya Waislamu imebadilika.
"Sasa nahisi watu wanatuogopa," anasema.
Kwa mujibu wake, matusi ya maneno yameongezeka na kuwa makali zaidi katika miaka ya karibuni.
Anakumbuka kwamba wanajamii wa Kiislamu waliitwa mara kwa mara "magaidi," wakatuhumiwa kutengeneza mabomu, na kuambiwa waondoke Japan.
"Mambo kama haya yanapotokea, tunachoweza kufanya ni kuwa wavumilivu," anaeleza. "Wanataka kuanzisha ugomvi au kuleta mvutano. Wanataka kuona tunaweza kuvumilia kwa muda gani."
"Kwa hiyo tunabaki watulivu, tunazungumza kwa upole na tunawatendea kwa wema, kwa sababu kwa ujumla Wajapani hawajui mengi kuhusu Uislamu."
Hata hivyo, anaamini kuwa sehemu ya jukumu la kuziba pengo hili pia iko kwa Waislamu wenyewe.
"Tulijikita zaidi katika kazi zetu, na kwa muda mrefu hatukujitahidi vya kutosha kuwaonyesha watu sisi ni akina nani. Pia hatukufanya juhudi za kutosha kuwa sehemu ya jamii inayotuzunguka," anasema.
"Kuanzia sasa, nataka kujitahidi zaidi kuongeza mazungumzo na kujenga uelewano wa pande zote."

Mvutano kati ya uhamiaji na utambulisho wa taifa
Japan inakabiliana na swali kuhusu utambulisho wake huku ikikumbwa na mabadiliko makubwa ya idadi ya watu.
Kwa mujibu wa takwimu za Hirofumi Tanada, profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Waseda na mtafiti wa masuala ya Uislamu nchini Japan, idadi ya Waislamu nchini humo, wakiwemo wahamiaji na Wajapani Waislamu, inatarajiwa kufikia takribani watu 420,000 ifikapo mwisho wa mwaka 2024.
Mwaka 2019, idadi hiyo ilikuwa takribani 230,000.
Kuongezeka kwa idadi ya Waislamu kunaakisi mwenendo mpana unaoonekana kote nchini.
Idadi ya wakazi wa kigeni nchini Japan, wengi wao wakitoka China, Vietnam, Korea Kusini na Ufilipino, ilizidi milioni nne mwaka 2025.
Kwa mujibu wa takwimu za serikali, idadi ya wafanyakazi wa kigeni nchini Japan pia ilifikia rekodi ya watu milioni 2.57.
Katika mwaka huo huo, idadi ya watu nchini Japan ilipungua kwa karibu watu milioni moja.
Kwa miaka mingi, maafisa wa serikali wamekuwa wakiepuka kuitaja Japan kuwa ni "nchi inayokaribisha wahamiaji," lakini wakati huohuo wameendelea kuunga mkono utoaji wa visa vinavyochukuliwa kuwa vya muda badala ya vya kudumu.
Wakosoaji wanaelezea sera hiyo kama "mfumo wa siri wa uhamiaji."
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Japan, Sanae Takaichi, amechukua msimamo wa kihafidhina dhidi ya uhamiaji wa watu wengi.
Mnamo Juni 2026, serikali ya Japan iliamua kuongeza ada za visa kwa raia wa kigeni mara tano, baada ya ada hizo kutobadilishwa kwa karibu miaka 50.
Serikali ya Japan pia inapanga kuongeza idadi ya wafanyakazi wa Wakala wa Huduma za Uhamiaji kwa takribani watu 230, ili kuimarisha ufuatiliaji na kushughulikia wageni wanaokaa nchini baada ya visa zao kuisha.
Vilevile, mamlaka za Japan zinazingatia hatua za kudhibiti na kusimamia idadi ya raia wa kigeni wanaoishi nchini humo.
Kadiri uwepo wa jamii za wahamiaji unavyozidi kuonekana wazi, Japan imelazimika kukabiliana na swali ambalo kwa muda mrefu imekuwa ikilikwepa:
Je, Japan inaweza kuwa jamii yenye watu wa tamaduni mbalimbali huku ikiendelea kudumisha utambulisho wake wa kitaifa na mshikamano wa kijamii?
Huko Fujisawa, Izumizawa anakiri kwamba hajawahi kuwa na uzoefu wowote mbaya binafsi na jirani yake Mwislamu.
"Ukweli ni kwamba, labda ninaogopa tu jambo nisilolijua," anasema huku akiinua mabega.















